Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Pasaka: Upendo Kamili
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani ya Yesu Kristo Mfufuka iwe nanyi nyote! Sehemu ya Injili ya leo ni mwendelezo wa ile tuliyotafakari Dominika ya tano ya Kipindi cha Pasaka. Ni baada ya kusikiliza mfano wa mzabibu na matawi yake, Yesu Kristo leo anatueleza nini kinatokea kwa wale wanaobaki wakijishikamanisha naye, aliye mzabibu wa kweli. Sehemu ya Injili ya Dominika ya leo, ni mojawapo kati ya mazungumzo au wosia wa Yesu Kristo kwa wanafunzi wake kabla ya fumbo la ukombozi wetu, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Ni kati ya maagizo na maelekezo muhimu na ya msingi kabisa ambayo Bwana wetu anawaachia na hata leo anatuachia sisi wanafunzi na wafuasi wake, ambao leo anatutambulisha kama rafiki zake ikiwa kama tutazishika amri zake. Leo Yesu Kristo anazungumzia tena kwa kurudia rudia mara kumi na mbili, neno moja “UPENDO”, akiwaalika wafuasi wake “PENDANENI”, ni mwaliko kwetu tulio wafuasi wake kupendana. Zana au wazo la upendo ndio linalotawala sana mazungumzo ya mwisho ya Yesu na wanafunzi, ndilo neno kuu katika wosia wake kabla ya Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake.
Hivyo tunaweza kusema ujumbe mkubwa kabisa na wa muhimu kupita yote ni juu ya upendo. Labda kabla ya kuona zaidi sehemu ya Injili ya leo, tunabaki na swali na mshangao ni kwa jinsi gani upendo unakuwa ni amri, unakuwa ni sawa na maagizo? “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake…amri yangu ndiyo hii, mpendane kama nilivyowapenda ninyi”. Upendo anaotuagiza Yesu sio ule wa hisia bali ni kupenda kama anavyotupenda yeye bila mastahili yetu, sio kwa sababu sisi ni wema zaidi au wenye sifa za pekee, bali kwa kuwa kila mmoja anabeba sura na mfano wa Mungu. Ni upendo usio na masharti, ni upendo wa Kimungu maana haujitafuti wenyewe. Yesu leo anatuonesha amri ya muhimu kabisa katika maisha yetu, ni ile ya upendo, ndio mbegu ya Kimungu inayosiwa katika nafsi ya kila mmoja wetu. Sio amri inayozidi asili yetu bali ni sehemu ya asili ya maisha ya kila mwanadamu. Ni upendo unazaliwa na kutokana na Mungu mwenyewe, ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa kila mmoja wetu na unaoelekea pia kama hatima na lengo lake kwa Mungu mwenyewe.
Ni upendo wenye chimbuko na chemuchemu yake kutoka kwa Mungu mwenyewe; “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu”. Hivyo tunaalikuwa kuishi sio upendo mwingine wowote bali ule utokao kwa Mungu. Kwa kuwa chimbuko la upendo huo ni Mungu mwenyewe basi pia hitimisho lake halina budi kuwa Mungu mwenyewe. “Mpendane kama nilivyowapenda mimi”. Kipimo na kielelezo cha upendo wetu ni Yesu Kristo Mwenyewe, ni kwa namna na jinsi ile ile anayotupenda sisi nasi tunaalikwa kuwapenda wengine. Yesu anatupenda upeo, na ndio nasi tunaalikwa kupenda kwa namna hiyo hiyo! Labda tunaweza kujiuliza, je, tunaweza kweli kupenda kwa namna ile ya Yesu Kristo? Ni swali la haki, lakini kama tulivyotangulia kuona hapo juu, tunaweza hilo ikiwa nasi tutapiga magoti na kumuomba Mungu zawadi ya upendo huo wa Kimungu, hivyo kamwe hatuwezi tukibaki wenyewe bali kama anavyotualika na kurudiarudia Yesu Kristo, kukaa ndani mwake, kubaki pamoja naye, ni kwa njia hiyo pekee nasi tunaweza kupenda kama yeye.
Upendo unazaa wana wa Mungu, rafiki zake Kristo! Fumbo la Ukombozi wetu, ni fumbo la upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Ni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, sisi sote kwa njia ya kushiriki Fumbo hilo siku ile ya Ubatizo wetu, nasi sote tumefanyika kuwa wana wa Mungu, warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu. Ni kwa njia ya upendo nasi tumezaliwa na kufanyika kuwa wana wa Mung pamoja na kuwa rafiki zake Yesu Kristo Mfufuka. Kila anayependa amezaliwa na Mungu. Rej. 1Yohane 4:7. Yesu Kristo leo anatuita sisi rafiki, ni kwa njia ya upendo ule ule wa Kimungu, sisi sio watumwa tena, kwa fumbo la ukombozi wetu, sisi sote tumefanyika kuwa rafiki zake Kristo Mfufuka! Hakika kumpenda Mungu sio kuwa na Mungu mioyoni mwetu bali sisi tunaingia na kuishi katika Moyo wa Mungu Mwenyewe! Ni kuingia katika akili kamilifu ya Mungu, mawazo makamilifu ya Mungu, ni kuwepo katika Moyo wa Mungu! Hili ndio fumbo la upendo wa Mungu kwetu. Mtakatifu Katarina wa Siena alikuwa na msemo usemao, Mungu ni “Crazy of Love”, ndio jinsi Mungu anavyotupenda kila mmoja wetu, anakupenda wewe kama vile hakuna mwingine yeyote zaidi yako, ananipenda nami kama vile hakuna mwingine yeyote zaidi yangu!
Huu ndio upendo wa Kimungu na ndio upendo ambao leo tunaalikwa kuwa nao, kuwapenda wengine kama Mungu anavyotupenda. Neno upendo ni moja ya maneno tunayoyatumia sana katika maisha yetu ya siku kwa siku, yawezekana hata baadhi yetu hatuoni sababu kwa nini tutafakari kitu au neno ambalo hata watoto wadogo hulitumia wasemapo, mama au baba nakupenda. Na ndiyo Yesu Kristo analitumia mara nyingi mno leo hata karibu linachosha masikioni au kupoteza maana na uzito wake. Niwaalike japo kwa ufupi kutakatari nini maana ya “UPENDO”. Kabla hatujaingia kuona aina za upendo yatosha tena leo kuona Yesu Kristo anatumia tena kile kitenzi cha “kubaki”, au μενειν (menein) kwa Kigiriki. Labda tunakumbuka Dominika iliyopita tulijaribu kuona maana hasa ya neno hili KUBAKI au KUISHI NDANI YA. Ni mahusiano ya ndani kati ya Yesu Kristo na kila mmoja wetu kama mfuasi. Ni kubaki katika nafsi na rohoni na moyoni. Ni kumbeba Yesu Kristo katika hali zetu zote za maisha, hata katika nyakati za furaha na zile ngumu za huzuni na majonzi na mateso.
Ni kwa kubaki tu pamoja na Yesu Kristo nasi tunakuwa kweli wanafunzi wake, tunakuwa matawi yanayoweza kuzaa matunda mema, na leo anasema ni kubaki katika pendo lake nasi tunaweza kupendana. Hivyo kubaki na Yesu Kristo daima ni lazima na muhimu kwa maisha yetu ya kiroho na hata maisha yetu ya siku kwa siku. Rejea Yohane 14:23; 15: 9-10. Ni kubaki katika pendo lake hapo tunapata furaha ya kweli. Furaha ya kweli haipatikani kwa kuwa na mali au mambo mengine isipokuwa tu ni katika muunganiko huu na Yesu Kristo, ni katika kubaki na Yesu Kristo anatuhakikishia kuwa tunakuwa na furaha ya kweli na furaha ya kudumu. Furaha hapa sio tu kukosa matatizo au mateso au maumivu au hali ya hisia kimwili bali ni furaha ya kweli ipatikanayo kwa kuwa na amani ya kweli ya nafsi, ni uwepo wa Mungu katika maisha yetu na hivyo hata kama tunapitia magumu na mateso na shida kubwa kiasi gani, tukibaki pamoja na Yesu basi hapo hakika tunakuwa na furaha kwa maana ya amani ya kweli nafsini kwetu, ni hakika hata katika nyakati ngumu.
Amri zangu nawapa, ni kama vile Yesu Kristo anatupa amri nyingi zaidi ya moja, ila cha kustaajabisha mwishoni anasema amri yangu ni hii, pendaneni, kaeni katika pendo langu. Amri ya upendo ni ujumuisho wa amri nyingine zote za Mungu, ni ukamilifu wa amri zote za Mungu, ni kwa kumpenda mwingine hapo kweli nasi tunamjua Mungu kama asemavyo Mtume Yohane. Rejea 1Yohane 4:20 Mwinjili Yohane sehemu ya Injili ya leo anaandika baada ya tukio la ufufuko, na hivyo kipimo cha upendo siyo tena kama unavyojipenda mwenyewe, bali ni Yesu Kristo mwenyewe. Na ndio mwaliko wa KUBAKI ndani mwake na hapo kweli tunaweza tukapenda katika kweli, kwa maana kama Yeye aliyetupenda hata akawa tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Pamoja ya kuwa katika Maandiko Matakatifu tunaona pia sehemu kadhaa neno mtumwa linatumika likiwa na maana chanya, ila leo Yesu Kristo anatumia neno rafiki. Mtumwa ni yule anayetimiza tu anayoelekezwa au kuambiwa na bwana wake, ila rafiki ni msiri maana ni mahusiano yanayojengeka katika upendo na sio malipo au ujira. Hakuna mtu anayemlipa rafiki yake kwa kumtendea wema, ni tunda la upendo wa kweli ila kwa mtumwa uhusiano ni tofauti maana unajikita kati ya watu wawili wanaokuwa katika mizani miwili tofauti.
Rafiki ni mmoja sawa na wewe. Kwa kifo na ufufuko wake sisi tumepona, tumepata hadhi tena ya kuwa wana wa Mungu na ndivyo tulivyo, hivyo ni warithi pamoja na Mwana, ni rafiki zake Kristo Mfufuka kwa ubatizo wetu, na ndio tunaalikwa kubaki naye. Ni vema kusema japo kifupi maana na hasa aina ya upendo. Aina ya kwanza ni ile inayojulikana kwa Kigiriki kama ερος (eros), ni aina ile ya upendo wa kibailojia kati ya mtu mke na mtu mume, wawili wapendanao, ni upendo unaonza kwa mwonekano au uzuri wa nje, ni kama ule wa Adamu mara baada ya kumwona Eva. Ni upendo unaoona uzuri wa mwingine na kutaka mwingine awe wake wa daima. Ni upendo milikishi, mwingine awe sehemu ya mimi, ni upendo wa hisia za kibailojia kati ya mtu mume na mtu mke! Yesu Kristo anazungumzia tena upendo wa kimungu, kwa Kigiriki cha Agano Jipya neno linalotumika ni αγαπη (agape), ni upendo usio na masharti, ni upendo wa Kimungu, kujisahau mwenyewe kwa ajili ya mwingine. Sio upendo milikishi, bali kumpenda mwingine kwa kuwa anabeba sura na mfano wa Mungu.
Na neno Agape halitumiki katika Kigiriki cha kale ila kwa mara ya kwanza linaanza kutumika wakati wa Ukristo kumaanisha aina hii ya upendo wa kimungu ambao sisi wafuasi wa Kristo tunaalikwa kuuishi. Aina ya tatu ni ile inayojulikana kwa Kigiriki kama φιλια (filia) ndio ule upendo wa kirafiki baina ya marafiki. Ni upendo pia unaokuwepo baina ya wazazi na watoto pia. Ni upendo jumuishi sio milikishi kama ule wa aina ya kwanza eros. Ni upendo unaojengeka katika kuaminiana kati ya watu wanaokuwa na hadhi sawa au unasaba fulani. Kwa kweli aina ya upendo unaokamilisha aina nyingine mbili ndio huo wa agape, upendo wa kimungu usio na masharti, ni upendo wa kuwapenda hata maadui na watesi wetu au wanaotunenea na kututakia mabaya. Ni upendo usiokinzana na aina hizi nyingine bali unazipa hadhi ya juu kabisa. Ni kupenda kama Kristo anavyotupenda maana ni Yeye aliyetuchagua kwanza sisi. Ndio upendo wenye chimbuko na asili yake kwa Mungu mwenyewe, na tunaweza kuiishi ikiwa tu tunabaki ndani ya moyo wa Mungu, ndani ya Mungu mwenyewe! Nawatakia tafakuri na Dominika njema.