Tafuta

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni changamoto kwa Wakristo kutoka katika undani wa maisha yao ili kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni changamoto kwa Wakristo kutoka katika undani wa maisha yao ili kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! 

Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Uinjilishaji na Ushuhuda

Mtakatifu Francisko wa Assisi alikuwa anawausia watawa waliomfuata kuwa hawana budi kwenda kuhubiri Injili kwanza kwa maisha yao, ila ikibidi hata pia kwa maneno yao. Ni mwaliko wa kuwa Injili iliyo hai, kuwa Habari Njema kwa kila kiumbe, si tu kwa wanadamu bali hata kwa kazi ya uumbaji kiujumla. Ni ndio kuwa na imani ya kweli, ni kuishi kadiri ya wito wetu kama Wakristo. Imani!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi nyote! Sehemu ya Injili ya leo, Mk. 16:15-20 ni hitimisho la Injili ilivyoandikwa na Mwinjili Marko. Katika hitimisho tunatarajia maneno au neno linaloashiria mwisho na tamati, ila kinyume chake katika hitimisho hili tunakutana na neno linaoonesha mwanzo mpya, yaani utume kwa wanafunzi wake Yesu Kristo kwa kila kiumbe. Ni mwaliko wa kwenda na kupeleka Injili, Habari Njema kwa kila kiumbe. Ni hitimisho la utume wa Bwana wetu Yesu Kristo hapa duniani, ila ni mwanzo wa utume wetu kama wafuasi wake. Kila mmoja wetu anatumwa na kupeleka Habari Njema (ευαγγελιον-eungelion) kwa viumbe vyote. Yesu Kristo baada ya kupaa mbinguni anabaki nasi katika Neno lake, Injili, Habari njema, nasi ndio wajumbe wa hiyo Habari Njema, kila mmoja wetu anaalikwa katika Dominika ya leo kuwa Habari Njema na kuwa mjumbe wa hiyo Habari Njema kwa wengine. Nendeni, ni kutoka katika hali zetu za awali, ni kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda na kuanza mwanzo mpya kwa kuongozwa na Neno la Kristo Mfufuka.

Ni kuanza mahusiano mapya na kila kiumbe, maana baada ya dhambi kuingia ulimwenguni, mwanadamu anakuwa na mwelekeo hasi si tu dhidi ya mwanadamu mwingine bali hata viumbe vingine vyote vilivyopo ulimwenguni. Hivyo utume wetu ni kwa kila kiumbe kama anavyosisitiza Mwinjili Marko katika Injili ya leo. Ni utume wa kuunda ulimwengu mpya, ulimwengu unaoongozwa na Neno lake Yesu Kristo Mfufuka. Kila aaminiye na kubatizwa ataokoka, ni hakika kutoka kwa Mwokozi wetu. Yafaa kutafakari pia imani inayozungumziwa hapa ni uamuzi na uchaguzi wa aina ya maisha utokanao na upendo wa kweli kwa Mungu. Ni kumfuasa huyu anayetuita kwa kuwa Yeye alitupenda kwanza sisi, akatufia pale juu msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Ni mwitikio wa upendo wake usio na mipaka. Ni kumchagua na kumwelekea Mungu badala ya kuelekea viumbe.  Neno kwenda ni mwaliko wa kuanza safari mpya, ni safari ya kumwelekea Mungu, kuisikia sauti yake, yaani Neno lake, na kuishi tukiongozwa nalo. Wito wa kikristo daima ni mwaliko wa kutoka na kwenda, kutoka katika ukale na kuanza maisha mapya, ni safari ya daima.

Ni safari ya toba na wongofu wetu ambayo hatuna budi kwa msaada wa neema zake basi tuweze kukua katika mahusiano yetu na Mungu na pili na kila kiumbe. Mtakatifu Francisko wa Assisi alikuwa anawausia watawa waliomfuata kuwa hawana budi kwenda kuhubiri Injili kwanza kwa maisha yao, ila ikibidi hata pia kwa maneno yao. Ni mwaliko wa kuwa Injili iliyo hai, kuwa Habari Njema kwa kila kiumbe, si tu kwa wanadamu bali hata kwa kazi ya uumbaji kiujumla. Ni ndio kuwa na imani ya kweli, ni kuishi kadiri ya wito wetu kama wakristo. Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo kuamini ni kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa na Mungu, ni kukubali kuongozwa na kutawaliwa naye, kuwaza, kufikiri na kutenda kama atakavyo Yeye na hivyo anachukua nafasi ya kwanza katika maisha yetu. Ubatizo ni kuzamishwa katika fumbo la Yesu Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Ni sakramenti inayotufanya kuwa wana wa Mungu, kuwa viumbe wapya, kuwa na mahusiano mema na Muumba wetu na kila kiumbe. Ni kuwa na kichwa kipya, ni kuvua ukale na kuuvaa utu mpya.  Ni kuishi kama Kristo na kuishi utakatifu.

Huo ndio wito wa kila mbatizwa, kila aliyejaliwa neema ya imani. Maana imani ni zawadi itokayo kwa Mungu, ni Mungu anayekuja kukutana na nafsi ya kila mmoja wetu. Mwinjili Marko anazidi kutuonesha kuwa anayeamini kweli basi matendo yake yataambatana na ishara kadha wa kadha. Ni kweli ishara hizi sio zile za kawaida lakini sio kwamba Injili inathibitishwa kwa ishara hizi, hivyo ishara hizi ni vema zikaeleweka kwa mwanga wa lugha ya picha katika Biblia. Rejea Isaya 11:6-8. Pepo wabaya hapa, wanaashiria zile nguvu zote za yule mwovu yaani maovu katika maisha ya mwanadamu. Pepo wabaya ndio ubinafsi, majivuno, tamaa ya mali na kila aina ya uovu. Ni kwa Nguvu ya Injili inafukuza kila aina ya uovu ndani mwetu na kutupa tena uzima wa Kimungu. Ni kwa kuamini Injili na kukubali kuanza maisha mapya kila mmoja wetu anakuwa huru na kila aina ya uovu. Lugha mpya ndio lugha ya upendo, lugha inayotuunganisha wanadamu badala ya ile ya kututenganisha na kutugombanisha na kutufarakanisha. Ni lugha ya upendo, amani, msamaha na huruma.

Ni lugha inayounda jumuiya moja yaani Fumbo la Mwili wa Kristo Mfufuka, ndilo Kanisa moja na takatifu la wote na la mitume, kundi moja chini ya mchungaji mmoja. Nyoka na sumu ni ishara zinazotumika katika Biblia kumaanisha adui wa mwanadamu na maisha. Rejea Zaburi 91:13 na Luka 10:19 Yafaa kutafakari hasa katika ulimwengu wetu wa leo ni kwa jinsi gani tunakunywa sumu kama ile ya mitandao na internet, ni nini tunasoma na kuona katika njia za kisasa za kimawasiliano? Kila mmoja wetu ajitafakari ni mara ngapi tumetumiana Habari Njema katika simu zetu au njia za mawasiliano au hata vitu tunavyotuma na kuweka mitandaoni. Ni aina gani ya vitu tunapenda kuangalia katika runinga zetu au mitandaoni? Hata pengine sasa tumefika mbali kutumia simu zetu badala ya kutujenga bali kutubomoa sisi au hata kubomoa wengine. Ni kwa nguvu ya Injili sisi tunaweza kuponywa kutoka sumu za umambosasa.

Maradhi yanatudhoofisha, kuna mambo mengi katika maisha yetu yanadhoofisha nguvu zetu za kiroho na hivyo kwa kupokea Injili tunaponywa, tunauishwa tena kwa kujaliwa neema na nguvu za kimungu ndani mwetu. Injili ni nguvu ya Mungu katika maisha ya kila kiumbe maana ni Mungu mwenyewe anayejimwilisha kwa njia ya Neno lake. Hivyo sherehe ya kupaa kwake Mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo ni mwanzo wa utume wetu maana kila mmoja wetu anaalikwa kuwa Habari Njema, kuwa Injili-eungelion kwa kila kiumbe iwe kwa maisha na hata kwa maneno pia. Uwepo wetu duniani uwe ni uponyaji kwa watu wanaotuzunguka, uwe ni Habari Njema kwa wengine na hivi kuweza kuwa ni ishara ya Nguvu za Mungu kati yetu. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema na maandalizi mema ya Sherehe ya Pentekoste.

13 May 2021, 08:08