Kardinali Polycarp Pengo: Jubilei ya Miaka 50 ya Ukasisi: PONTI!
Padre Gaston George Mkude, -Roma.
Hakika ni jambo jema na la kufaa sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Baba Mwadhama Polycarp Joseph Pengo, anaposherehekea miaka 50 ya ukasisi wake. Nikiri tangu mwanzoni kabisa mwa makala hii ugumu wa kuandika au kusema neno juu ya mtu mwenye haiba ya juu na kubwa kama Baba Mwadhama. Hivyo, ninachoenda kuandika sio tathmini au historia ya utume na utumishi wake, bali niwaalike tutafakari kwa pamoja juu ya jina ambalo tumezoea kumuita na yawezekana bila yeye mwenyewe kujua. Hivyo, nitangulie pia kumuomba msamaha kama hakuwa analijua jina hilo lakini lenye maana kubwa kabisa mintarafu ukuhani na ukasisi wake, na hasa leo tunapomshukuru Mwenyezi Mungu pamoja naye kwa miaka 50 ya ukasisi katika Shamba la Bwana. Kwa kuwa sina vigezo wala sifa za kumwongelea Baba Mwadhama, ni vema kusema mapema kuwa andiko hili sio la historia lenye kubeba wasifu wake wa maisha yake yote. Kwa msingi huo, ndio maana utaona kwamba nimejikita sio katika kumsemea ambaye anaweza kujisemea mwenyewe, au wale waliomfahamu kwa karibu na jirani zaidi yangu. Ni kweli wapo wengi kabisa ninaowafahamu na hata nisiowafahamu wenye kuwa na mengi ya kusema juu ya Baba Mwadhama. Hivyo, leo pamoja na kusema machache nitawaalika zaidi tuonje nini maana ya kuwa kuhani na nini hasa tunajifunza kutoka katika maisha ya ukuhani ya Baba Mwadhama.
Itoshe kama alivyopenda kusema Mt. Bernard wa Chartres, “Ili tuweze kuona mbali, basi hatuna budi kusimama juu ya mabega ya watu wakubwa kwa kimo,” - “Nanos gigantium humeris insidentes,”. Na ndio maana andiko hili sio tunda au matokeo ya ufahamu wangu peke yangu, bali nimejaribu kudadisi na kuuliza wengine wenye kimo kikubwa zaidi kunizidi ili wanisaidie nami kusimama juu ya mabega yao, ili kuweza kuona mbali zaidi. Ningebaki na kimo changu tu, hakika nisingeweza kuona mbali. Ni kwa msaada wao na kukubali kwao kukwea juu ya mabega yao, nami nimeweza kuona mbali kidogo na kupata cha kusema. Hivyo, nitangulize shukrani zangu kwa wale wote niliowaomba japo kunipa mang’amuzi na ushuhuda wao kumhusu Baba Mwadhama. Askofu na mhubiri mashuhuri Fulton Sheen aliwahi kusema; “Every priest is a Jacob’s ladder, that is to say, someone who connects heaven and earth,” yaani “Kila kuhani ni ngazi ya Yakobo, ndio kusema, ni ngazi inayounganisha mbingu na dunia.” Pia Mtakatifu Tomaso wa Akwino anasema; “The priest is a mediator, a bridge, between human beings and God.” “Kuhani ni kiunganishi, daraja, kati ya wanadamu na Mungu.” Ndio maana tunaona kwamba kila kuhani ni Kristo mwingine; ni Kristo anayejimwilisha ubinadamu wetu, anaunganisha Umungu na Ubinadamu wetu.
Kuhani daima ni kiungo kati ya Mungu na wanadamu. Kuhani sio tu Kristo mwingine bali ni Kristo mwenyewe na ndio maana anapotamka yale maneno, “Huu ni Mwili wangu,” na “Hii ni Damu yangu”, hasemi ni Mwili wa Kristo au Damu ya Kristo bali anasema wangu na yangu! Ni hakika ukuhani ni fumbo! Kwa kweli, sifa ya kuhani sio kuwa karibu na Mungu tu na mbali na watu, na vilevile, sio kuwa karibu na watu tu na mbali na Mungu, bali daima anakuwa jirani na karibu na Mungu na watu wake anaotumwa kuwahudumia. Kuna kishawishi kikubwa kabisa kudhani tumeitwa kuwa makuhani ili tuwe karibu na jirani na Mungu, na kuacha mambo mengine nyuma, hapana; kwani Kuhani ni yule anayetambua na kukumbuka kila siku kuwa wito wake ni kuwa jirani na Mungu na wakati huo huo pia jirani na watu. Kuhani anaitwa kuwa na harufu ya kondoo kwani ni kwa njia ya kuhani, kondoo hawa kila siku kupitia yeye kama ngazi wanaweza kwenda mbinguni, wanaweza kumkaribia na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. Kuhani ni ngazi ile ya Yakobo, ni ngazi inayoshika vizuri ardhi na pia kutufikisha wengine mbinguni. Baba Mtakatifu Fransisko anatukumbusha mara nyingi kuwa kila kuhani hana budi kuwa na harufu ya kondoo, ndio kusema ni mtumishi anayejihusisha daima na shida na matatizo ya wengine, kwani ana lengo moja la kuwahakikishia usalama wa maisha ya milele, ndio urafiki na Mungu. Kuhani anapaswa kuwa rafiki wa Mungu kwa nafasi ya kwanza ili aweze kuwaleta wengine katika urafiki na ushirika na Mungu mwenyewe. Ni rafiki wa wadhambi na watakatifu pia kwa wakati mmoja.
Waraka kwa Waebrania unatupatia kitambulisho cha kuhani ni nani. (Waebrania 5:1) “Maana kila kuhani mkuu anachaguliwa kutoka kati ya watu, na kuwekwa wakfu kwa ajili ya watu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atolee dhabihu na sadaka kwa ajili ya dhambi.” Ni hapa ninataka kusema kitu ambacho sina hakika sana kama Baba Mwadhama anajua hilo na kama alikuwa hajui basi leo ninaomba nimng’ate sikio, si tu yeye, bali na nyote mtakaotenga muda na kupitia makala hii kumuhusu. Kuna jina ambalo kwa muda mrefu sasa tunamtambua na kumuita “Ponti.” Na hata leo wengi wetu bado tunalitumia jina hilo tunapotaka kumzungumzia au kuulizana juu yake. Ni jina ambalo tumelikuta likitumika na kaka na wakubwa zetu katika ukuhani na hivyo sijui ni nani hasa alianza kumuita na kumtambulisha kwa jina la “Ponti.” Mimi sio mwanzilishi wa jina hilo lakini napenda kusema japo machache kumhusu kwani jina hilo lina mengi ya kututafakarisha katika fursa hii ya Jubileo ya miaka 50 ya ukuhani wa Baba mwadhama.
Ni kweli kabisa Baba Mwadhama ni “Ponti” na amelidhihirisha hilo katika maisha yake ya utume na utumishi uliotukuka wa miaka 50 ya ukasisi katika Shamba la Bwana. Labda msomaji utajiuliza nini maana ya jina hilo, na hata kushawishika kudhani makuhani wengi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wamepotoka kwa kuanza kumuita baba yao kwa majina yasiyofaa na kustahili kwa mtu mkubwa wa haiba ile. Niseme kwa kurudia kuwa, aliyempa jina hilo hakukosea hata kidogo na ndio maana nimeona andiko langu liguse hasa jina hilo la utani na yawezekana mwenyewe hakuwa anajua; maana hatungethubutu kumuita akitusikia au mbele yake! Neno “Ponti” ni kifupisho cha neno la Kilatini “Pontifex” na ndio maana Baba Mtakatifu ni “Pontifex maximus.” Hivyo neno “Ponti” ni kifupisho cha neno “Pontifex.” “Pontifex ni muunganiko wa maneno mawili ya Kilatini, yaani “Pons na facere”; yenye maana ya daraja na kutengeza, hivyo Pontifex ni mtengeneza madaraja, ni kiungo, ni ngazi ni kiunganishi. Na ndio maana hata katika dini za Kirumi walikuwa na kuhani mkuu waliyemuita na kumtambua kama “Pontifex maximus.” Ndio maana hata leo Kanisa linazidi kutumia neno hilo kumaanisha kuwa Baba Mtakatifu ni mtengeneza madaraja kwa nafasi ya kwanza, na kila askofu na kila kuhani pia ana wajibu huo.
Kila Padre anapaswa kuwa mtengeneza madaraja, kuwa kiungo kati ya Mungu na wanadamu. Na ndio maana ninarudia kusema jina hilo, ingawa kwa kweli ni la utani zaidi lakini lenye maana kubwa kiteolojia, mintarafu ukuhani katika Kanisa. Kila kasisi hana budi kuwa “Pontifex”, kuwa “Ponti” kwelikweli kwa kuwa karibu na watu ili kuwaongoza kwa Mungu. Mwadhama Polycarp Pengo kwa wengi wanaomfahamu na kuwa jirani naye, wanakiri kuwa ni mtu wa sala na tafakari za kina. Ni mtu anayetambua jukumu na wajibu wake wa kuwa “Ponti.” Ili kulifanikisha hilo la kuwa “Ponti” hana budi kwa nafasi ya kwanza kujishikamanisha na Mungu, anakuwa ngazi au daraja linalokuwa salama kwa neema na msaada wa Mungu pekee. Mwadhama anayejua vema, lazima kujishikamanisha kwa nafasi ya kwanza na Mungu ili kuweza kuwasaidia wengine kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu pia. Nguvu ya utume na utumishi wake hakika ni matunda ya neema za Mungu kwa miaka yote hiyo hamsini, na ndio maana leo tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja naye.
Maisha yake ya ukuhani hakika yanaakisi vema kabisa kuwa amekuwa daima mjenga madaraja katika ofisi zile tatu za Kristo Mwenyewe aliye kuhani wetu mkuu (Tria munera). Kila kuhani anashiriki katika ofisi zile tatu za Kristo kama kuhani, nabii na mfalme. Kama kuhani, kila kasisi anaitwa kutakatifuza watu kwa maadhimisho ya masakramenti; kama nabii, kila kuhani anaitwa kuwa mwalimu wa Neno la Mungu na pia kama mfalme, kila kuhani anaalikwa kuwaongoza na kuwachunga kondoo wa Bwana. Labda hapa chini niseme pia kidogo zaidi kuhusiana na hizo ofisi tatu kumuhusu Baba Mwadhama. Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, Baba Mwadhama ni mtu wa imani thabiti na pia mtu wa sala. Pamoja na kuwa mtu wa sala, kila mara Baba Mwadhama anatambua kuwa yeye ni “Ponti,” yaani mjenga madaraja kwa kuadhimisha matakatifu ya kuwapeleka wengine kwa Mungu. Ni mtu anayethamini sana na kuyapa nafasi ya kwanza kabisa Maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali, iwe maparokiani au popote pale anapokuwepo. Ni hakika na hata labda hatuna sababu ya kusema mengi kwani wengi wetu tumenufaika na huduma zake.
Kama Nabii, Mwadhama si tu amejaliwa kipaji cha ualimu bali pia kuhubiri. Na kama anavyotuasa Mtume Paulo kwamba kuhubiri iwe wakati wa kufaa na hata ule usiofaa, ndio kuwa wahubiri wenye ujasiri wa ndani kabisa (Parrhesia) (2Timoteo 4:2). Na ndio kitu tunachokionja kwa Baba Mwadhama kama nabii, na kama mwalimu mwenye ujasiri wa kushuhudia ukweli utokao kwa Mungu kwa watu wake. Mahubiri yake daima utapenda kuyasikiliza, si tu yanavyovutia bali zaidi yenye kuakisi ujumbe wa Mungu mwenyewe kwa watu wake. Baadhi yetu tuliopata japo bahati mara chache ya kumuuliza maswali kadhaa juu ya imani au maadili ya Kanisa, tulionja uwezo wake mkubwa wa kudadavua na kufafanua mambo hata magumu kwa lugha ya kueleweka na hata kuvutia. Ni mtu mwenye kina kabisa iwe katika mafundisho na hata mazungumzo yake. Sio mtu wa porojo, iwe mimbarini anapohubiri lakini hata katika mazungumzo yake ya kawaida. Unapoongea naye unaonja busara na hekima na hata maarifa mapana na yenye kina ndani mwake.
Mahubiri ya Baba Mwadhama ni matunda ya tafakari ya kina na sala. Ni kweli Baba Mwadhama ni mteolojia wa hali ya juu kabisa lakini kila unaposikiliza homilia na mafundisho yake, utang’amua kuwa sio matunda tu ya kusoma katika maktaba mbalimbali ya vitabu bali ni matunda ya tafakari za kina na sala pia. Ni mwalimu kwetu wahubiri pia kujifunza kwake kuwa hatuna budi kuwa watu wa tafakari, watu tunaotenga muda wetu na kukaa mbele ya Mwalimu wetu mwenyewe, yaani Bwana wetu Yesu Kristo, kupitia Neno lake. Huwezi kumsikia akihubiri vitu vya rejareja au kutumia mimbari kama jukwaa la kuburudisha kwa vichekesho na utani pamoja na kuwa mahubiri yake siyo makavu, kwani yamejaa ujumbe kusudiwa wa Neno la Mungu kwetu wanadamu. Baba Mwadhama ni shule na darasa zuri kwetu kuwa mahubiri hayana budi kuakisi Neno la Mungu kwa watu wake na sio porojo na hadithi za kuburudisha; sitaki kusema kuwa mahubiri yasiwe hai bali lazima kujua nini tuseme, ili Neno la Mungu ndio litawale na kuwasaidia wengi kumjua zaidi Mungu kusudi wampende na kumtumikia na mwisho sote tufike mbinguni. Mhubiri mzuri basi ni “Ponti” ni daraja linalounganisha na kuwaleta watu kwa Mungu. Mahubiri yetu hayana budi kuwa matunda ya tafakuri za kina kama wasemavyo katika moto wa Shirika la Wahubiri au Dominikani “contemplata aliis trader,” yaani kuwagawia wengine matunda ya tafakuri! Mahubiri yamsaidie mwingine kujenga urafiki wa karibu zaidi na Mungu na jirani, muhubiri mzuri ni “Ponti”.
Pamoja na kuwa mtu wa tafakari, lakini pia Baba Mwadhama ni mtu anayesoma na kujichotea maarifa mengi vitabuni na kusoma alama za nyakati; ndio kujua nini kinachojiri katika jamii inayomzunguka. Mwanataalimungu Karl Barth alipenda kusema, “Muhubiri anapaswa kushika Biblia mkono mmoja na mkono mwingine kushika gazeti.” Ndio kusema, mhubiri mzuri ni yule anayejibu maswali ya nyakati husika, ni mmoja anayejua kutumia Neno la Mungu kugusa maisha ya watu. Baba Mwadhama hachoshi kusikiliza wakati akitoa mahubiri yake kwani anajua kushika Neno la Mungu mkono mmoja na mkono mwingine akiwa ameshika gazeti. Huku ndio kusoma na kujua alama za nyakati, kuwasaidia wengine kupata majibu ya maswali na shida zao mbalimbali maishani. Mahubiri hayana budi kuakisi imani ya anayehubiri, na ndicho ambacho tunakionja katika mahubiri ya Baba Mwadhama, sio mmoja anayetushirikisha anayoyajua tu bali hasa imani na upendo wake kwa Mungu na kwa jirani. Mahubiri yetu hayana budi kutoa majibu ya maswali wanayokuwa nayo waamini. Kuwa mchungaji wa kweli ni kuwa “Ponti”, kuwa daraja daima kati ya Mungu na watu wake, ni kuwa mjumbe wa Mungu katika kuwatumikia wengine. Kuwa nabii au mwalimu ni kuwa kiungo muhimu wa kuwashirikisha wengine imani na urafiki wako na Mungu.
Mwadhama ni Nabii kweli kweli, kwani hakusita kutoa sauti yake kutetea jambo la haki na kweli hata kama lingewaudhi wakubwa na wengine. Ni mtu mwenye msimamo thabiti na anayesimamia ukweli, hata kama wengine wangekuwa kinyume na mtazamo au mwono wake. Niseme kwa uhakika kwamba, pale anapoujua ukweli pasipo shaka, Mwadhama atausimamia ukweli huo. Mwadhama sio mtu wa maadili ya kimachinga, maadili ya pungufu unaongea, ni mtu anayesimamia ukweli na kuuishi ukweli huo hata kama kwa upande wake itamgharimu na kumpunguzia marafiki. Maadamu anaujua ukweli, sio mwoga wa kuishi ukweli huo na kuwashirikisha wengine kile kilicho cha kweli. Leo duniani tupo katika mkwamo mkubwa wa maadili kwani mwanadamu anapomuweka kando Mwenyezi Mungu, aliye muasisi wa maisha yetu, hapo tunaangukia katika kapu la maadili ya kimachinga, pungufu unaongea, kila mmoja anakuwa ni muasisi wa maadili yake mwenyewe. Hakika Mwadhama amekuwa ni mwalimu wetu wa maadili ya kweli ni yale yanaoheshimu nafasi ya Mungu kama muumbaji wetu. Maadili ya kweli ni yale tu yanayoasisiwa na Mungu mwenyewe na hivyo mwanadamu hapaswi kamwe kuchukua nafasi ile ya Mungu na kuishia katika maadili ya mtumba, maadili ya pungufu unaongea, maana hayana kipimo cha kweli cha ubora na thamani yake.
Ni kiongozi kwa kuzaliwa; ni wale watu ambao tunasema kuwa ni; “Born to be a leader!” Amezaliwa hakika kuongoza, na sio uongozi wa maneno bali wa mifano kwa maisha yake. Mwadhama sio aina ya viongozi ambao wangehubiri maji na kunywa bia au mvinyo. Maisha yake ni darasa na shule zuri la jinsi ya kuwa kiongozi katika namna ile ya Kristo mwenyewe. Ni kielelezo kizuri kwa wengi wetu tuliobahatika kufaidi utume na utumishi wake, iwe jimboni kwake kwa kuzaliwa au kule alikotumwa kutoa huduma kwa kipindi chote cha miaka 50 ya ukuhani katika Shamba la Bwana. Unataka kujifunza kuwa kiongozi mzuri, basi nikualike uende katika darasa na shule ya Baba Mwadhama Kardinali Polycarp Joseph Pengo! Pamoja na kuwa kiongozi kwelikweli, bado Baba Mwadhama sio aina ile ya viongozi wanaoamini katika uwezo wao binafsi na hata kushawishika kudhani hawahitaji wengine. Ni mtu anayemtangulizi Mungu, lakini pia ni mtu shirikishi. Ni mwaka 2000 baada ya kutambua ukubwa na uzito wa kuhudumu jimbo kuu la Dar es salaam, akatambua kuwa ni muhimu kuomba kuwa na askofu msaidizi, na hata baadaye akawa pia na maaskofu wasaidizi wawili. Ni mtu anayetambua mafanikio yake kama kiongozi ni kuweza kushirikiana na wengine na ndio utaonja ni mmoja mwenye heshima kubwa kwa kila padre anayekutana na kufanyakazi naye. Ni mmoja anayetambua kuwa katika kila kuhani hapo unakutana na Kristo mwingine. Ni mmoja anayetambua kuwa sote kila mmoja kwa nafasi yake ni kiungo muhimu katika kulijenga Kanisa la Kristo.
Katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Baba Mwadhama si tu kwamba ameshirikiana vema na makuhani na watawa peke yao, bali pia alitoa nafasi kubwa ya utume wa walei katika Kanisa. Leo, jimbo lina mengi ya kujivunia na moja kati ya mengi ni utume wa walei, iwe katika vyama vya kitume na hata nafasi ya kila mlei katika Kanisa. Leo maparokia mengi yamejengwa na kukua chini ya uongozi wake, kwani alitambua na kuwaalika waamini walei kuwa ndio wajumbe na wadau wa kwanza katika kuhakikisha kwamba Injili inaenea. Leo walei wa Jimbo la Dar es Salaam, wanajua na kutambua wajibu wao katika kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Shukrani ni kwa Baba Mwadhama aliyetambua na kuhakikisha kuwa daima anakuwa kweli “Ponti,” yaani kiunganishi muhimu katika kuhakikisha kwamba kundi alilokabidhiwa kila mmoja anajua nafasi yake na kuicheza kwa haki. Ni kwa uongozi wake leo Kanisa la Jimbo kuu la Dar es salaam, tunajiona kuwa ni jumuiya au kundi moja chini ya mchungaji mmoja. Na ndio hasa maana ya Kanisa, kwa Kiebrania “Qahal”, ni kusanyiko, ni jumuiya inayojisikia kuwa moja bila kujali huduma au nafasi ya kila mmoja katika familia hiyo kubwa. Na ndio tunaona hata katika Agano Jipya, Kanisa linatambulika kama “ekklesia”, neno la Kigiriki la muunganiko wa maneno mawili, “ek na kalein” ya kimaanisha, “walioitwa kutoka”. Kanisa ni jumuiya au kusanyiko lililoitwa kutoka katika ulimwengu huu (kosmos), ili kufanya kwa pamoja “Mwili wa Kristo”, ndio jumuiya inayokuwa na namna mpya ya kufikiri na kutenda, inayoongozwa na mantiki ya mbinguni katika kutenda na katika kuona mambo. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi 2:5 “Muwe nao moyo aliokuwa nao Kristo Yesu” Na kwa kweli ni kwa msaada wa uongozi thabiti wa Baba Mwadhama leo, Jimbo kuu la Dar es salaam, linaweza kujivuna kwa kutembea kwa pamoja kama Kanisa.
Ni mtu anayeishi ukweli usemao; “Gloria Dei, vivens homo,” yaani, Utukufu wa Mungu ni pale mwanadamu anapopata maisha ya kweli. Utume wa kila kuhani ni kumsifu Mungu, na sifa ya Mungu ipo katika kumwokoa mwanadamu, katika kumsaidia mwanadamu kuingia katika mahusiano ya upendo na Mungu, ya kukubali daima kuishi maisha ya kuwa mwana; anayeisikiliza na kuitii sauti ya Mungu. Huo ndio utume wa kikuhani katika kufanya yote ili Mwenyezi Mungu apewe sifa, sio mimi na wewe bali Mungu! Utume wa kila kuhani ni katika kuhakikisha Mwenyezi Mungu anapewa sifa na mwanadamu anatakatifuzwa, anapata wokovu, ndio urafiki na Mungu na jirani. Mwadhama, pamoja na nafasi yake kama Askofu Mkuu na zaidi sana kama Kardinali pekee nchini, bado amebaki kuwa karibu na watu na hata wanyonge na duni kabisa. Injili ya Luka 22:24-26 inatuambia “…Lakini ninyi sivyo! Bali aliye mkubwa wenu awe kama mdogo wenu, na kiongozi awe kama mtumishi.” Na ndio maana, daima amebaki mtu mnyenyekevu na mtumishi wa wengine. Na ndio mwaliko kwetu wengine tunaotumikia kama makuhani kutambua tumeitwa, sio kuwa mabwana wakubwa na kutumikiwa, bali kuwa wadogo na watumishi. Ni udogo wake unaona sio mtu mwenye makuu bali anayeishi roho ya udogo na utumishi.
Leo tunaweza kusema urafiki na mapenzi yake makubwa kwa watoto wa Utoto Mtakatifu. Mwadhama ni mmoja anayetambua wajibu wa kuhani ni kuwapenda wadogo, ni kuwalinda na zaidi sana kuwarithisha Imani walio wadogo. Ni kwa njia ya kuwa jirani na karibu na watoto anatukumbusha iwe wazazi katika familia, makuhani, watawa, kila mmoja wetu kuona wajibu mkubwa tunaopewa na Kristo mwenyewe wa kuwapokea watoto wadogo na kuwalinda na kuwarithisha Imani. Tunasoma Injili ya Marko 10:13-16 “Watu walimletea watoto wadogo ili awaguse, wafuasi wake wakawakemea. Lakini Yesu alipoona hayo aliudhika akawaambia, “Waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto, hatauingia kamwe.” Kisha kawakumbatia na kuwawekea mikono, akawabariki.” Labda nimetaja kundi moja tu la Utoto Mtakatifu kwa leo, lakini Baba Mwadhama amedumu kuwa rafiki na jirani na makundi mengine yote, katika urika wa maaskofu wenzake, mapadre wa majimbo, mapadre na watawa wa mashirika mbalimbali ya kijimbo na yale ya kimisionari na zaidi pia makundi mbali mbali ya walei katika ngazi mbali mbali. Na ndio siri kubwa ya mafanikio makubwa ya utume na utumishi wake, ni katika kuhakikisha anajali na kuthamini mchango wa kila mmoja kwa nafasi yake. Na hata mahusiano yake na wale wanaokuwa nje ya waamini wa Kanisa Katoliki au Imani katika Kristo. Ni mtu anaheshimu watu wa imani nyingine na pia ni muekumene kweli kweli!
Mtakatifu Yohane Paulo II, wakati akiadhimisha miaka 50 ya ukuhani wake, aliwahi kusema; “Upadre ni zawadi na ni fumbo.” Ni zawadi kwani sio mastahili yetu, na basi inakuwa fumbo kwani tunafanyika kile ambacho kwa macho ya kawaida hatuwezi kukiona. Ni siku ile ya Upadrisho, kuhani husika anajaliwa kwa namna isiyoonekana kwa macho ya nyama, uwezo wa kumleta Mungu kwa watu wake kwa maadhimisho ya masakramenti na kuwa mhubiri wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Ni fumbo kwani kila kuhani sio tu ni “Alter Christus, yaani Kristo mwingine, bali pia ni “Ipse Christus”, ni Kristo mwenyewe na ndio maana narudia wakati ule wa mageuzi kuhani anatamka maneno yale yale ya Kristo. Askofu Fulton Sheen katika kitabu chake “Why I became a Priest?”, anatusaidia pia kuelewa hilo wazo analotuambia pia Mtakatifu Papa Yohane Paulo II, Upadre ni Fumbo na Zawadi. Anapojiuliza swali hilo anajibu mwenyewe kwa kusema; “Swali hili ambalo mara kwa mara najiuliza, halijaulizwa vizuri kwa sababu kwa swali hili inaweza kuonekana kuwa ni mimi niliyemchagua Bwana wetu, wakati ni yeye aliyenichagua. Mimi sikutaka kufanya lolote, ni Yeye aliyetaka mimi nifanye kitu fulani. Ni yeye aliyependa kunifanya niwe chombo, kama kalamu, ambayo kwa hiyo angetumia kuandika ndani ya mioyo ya watu shairi la upendo wake.
Kama nikisema, ‘Kwa nini nilikuwa padre’, ningekuwa nimesahau maneno ya Bwana: ‘Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi’ (Yohane 15:16°)” Kutoka Kitabu cha Pd. Raymond Saba “Wewe ni Kuhani Milele – Tafakari ya Mababa wa Kanisa juu ya Upadre. Hakika ukuhani ni zawadi kwani kila mara tunatambua kwa unyenyekevu mkubwa kuwa sio sisi tuliomtafuta Mungu kwa nafasi ya kwanza bali ni Yeye, na ametuita sio kwa sababu sisi ni bora na hivyo mastahili bali anatuita tulio duni na wadogo kabisa ili uweza na neema zake zipate kuonekana na wote. Ni nafasi nzuri kila mara kukumbuka kuwa tunaitwa kuwa watu wa shukrani, ndio watu wa Ekaristi, na ndio sala yetu kubwa kila siku mbele yake. Baba Mwadhama, si tu Mwanataalimungu wa Maadili kama nilivyoonesha hapo awali, bali pia alijua kufundisha wengine ili tutambue umuhimu wa kushika maadili katika maisha yetu. Maadili sio mzigo bali ni nyenzo ya kutusaidia sisi kuwa na kuishi kama watu kweli. Maadili ni msaada kwa mwanadamu na sio kikwazo kama wengi tunavyodhania. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kutumia mfano wa simulizi la paka na njiwa. Njiwa aliumbwa mwanzoni bila mabawa na hivyo aliishia kuwa chakula cha paka. Siku moja akamlilia na kumuomba Mungu, akilalamika kwa kushindwa kujitetea kwa haraka kutoka mikono ya adui yake mkubwa paka. Basi Mungu akamjalia mabawa. Lakini njiwa akarudi tena kwa Mungu na kuendelea kulalamika kuwa hali yake kwa sasa ni mbaya zaidi kwani mabawa yanazidi kumuongezea uzito na kumfanya akamatwe kwa haraka na rahisi na paka. Ndipo Mungu akamshangaa na kumuuliza mabawa yale amempatia ili aweze kuruka na kujilinda katika nyakati hatarishi. Na ndivyo ilivyo maadili katika maisha ya mwanadamu; ni msaada wa kutusaidia kuruka juu na kuishi kirahisi zaidi kama watu kadiri ya mpango wa milele wa Mungu kwetu.
Ukuhani ni kuwa mtu wa shukrani daima, ndio kuwa mtu wa Ekaristi, si tu katika Maadhimisho ya Misa Takatifu, bali hata kwa maisha ya siku kwa siku. Ni kuwa mtu wa shukrani ya daima, na ndicho kinachoadhimishwa katika Jubileo ya miaka 50; ni kile ambacho Baba Mwadhama amedumu kukiadhimisha kila siku katika maadhimisho ya Misa Takatifu. Ni kuwa na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa makuu aliyotenda na anayoendelea kutenda katika maisha ya Baba Mwadhama Kardinali Polycarp Joseph Pengo. Andiko hili siyo tathmini ya utume uliotukuka wa Baba Mwadhama bali ni kujaribu kutafakari kwa pamoja na kwa udogo kabisa maana ya ukuhani na nini wengine tunajifunza tunaposhirikiana na Baba mwadhama kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya fumbo la ukuhani kwa miaka hii 50 ya huduma na utumishi. Ni nafasi ya kutafakari pamoja naye kile ambacho Mungu mwenyewe amemstahilisha bila kuwa na mastahili ya kwake mwenyewe; ni kugeuka nyuma na kwa moyo wa mshangao kumwambia Mungu asante kwa mema yote; ni kuimba wimbo wa sifa pamoja naye katika maadhimisho haya ya miaka 50 ya huduma ya utumishi, ya kuwa daraja, yaani “Ponti” kati ya Mungu na watu wake!
Jubilei ni adhimisho sio tu la shukrani, bali zaidi sana la mshangao. Mshangao kwa wema na ukuu wake Mwenyezi Mungu kwetu wanadamu pasipo mastahili yetu. Kila mmoja katika maadhimisho haya ni vema kubaki mbele ya Mungu na kinywa wazi tukimwambia asante kwa zawadi ya Baba mwadhama katika Kanisa letu la Dar es salaam, Tanzania, Afrika na ulimwengu mzima! Jubileo ni adhimisho la mshangao kwa wema na ukarimu wake Mwenyezi Mungu kwetu watu wake. Motto ya uaskofu wa Baba Mwadhama ni maneno kutoka Injili ya Yohane 19:5 ἰδοὺ ὁ ἄνθρωπος – Ecce homo! “Mtazameni mtu!”, Ni maneno ya Pilato hata baada ya kumkuta Yesu bila hatia, bado anamtoa nje na kuwaambia Wayahudi tazameni mtu, ni mtu asiye na hatia wala kosa lakini bado mnataka asulubiwe. Ni mwaliko wa kuutazama upendo na huruma ya Mungu isiyo na mipaka wala maelezo. Si Yesu asiyekuwa na uwezo wa kujitetea wala kudai haki yake, bali anayeona fahari na utayari mkubwa kuyatoa maisha yake kuwa sadaka ya wokovu wetu. Ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu.
Na ndio Baba Mwadhama ameona aongozwe na maneno hayo sio ya Yesu bali ya Pilato, labda tunashangaa kwa nini hakuchagua misemo au maneno ya Yesu, na badala yake anaona aongozwe na maneno ya mtawala mpagani wa Kirumi. Si kwa bahati mbaya amechagua maneno yale na hakika ukiangalia maisha yake utaona ni kwa kiasi gani amejaribu kuyafananisha maisha yake na Kristo aliye kweli kuhani, altare na mwanakondoo. Ni kutaka kubaki katika hali ile ya kudogoshwa kabisa na kudharaulika, lakini kwa sababu iliyo kuu na njema kabisa na si nyingine bali wokovu wa wengine. Kuwa mtu kweli, kukubali mateso na hata kifo kwa ajili ya kitu chenye thamani kubwa kabisa, kutoa maisha yake kama kuhani ni kufananisha maisha yake na ya Kristo aliyekubali kuteswa na kufa kwa ajili ya wanadamu. Ni maneno yanayotualika kuona thamani nasi ya kuwa “Ponti”, kuwa daraja hata ikitupasa kuteseka na kudharaulika ili wengine wapate kumfikia Mungu, waupate wokovu, waupate uzima wa kweli na wa milele. Kuhani sio tu ni Kristo mwingine (Alter Christus) bali ni Kristo mwenyewe (Ipse Christus)!
Ukuhani kama asemavyo Mt. Augostino ni huduma ya hatari iliyo kubwa kabisa, ndiyo, “Periculosissimum ministerium”. Ndio maneno yenye kuakisi moto wa Baba Mwadhama, kukubali kuwa mtu kweli, kujivika hali duni na ya mateso na sadaka kubwa, kama ile aliyokuwa nayo Bwana wetu Yesu Kristo saa ile alipokusanywa nje kwa Mayahudi ili apokee kikombe kile cha mateso tena ya aibu kubwa. Ni kukubali kujivua heshima, na hata utu wako nyakati fulani kwa ajili ya kutimiza wajibu na kazi ya Kristo. Ni kujifananisha na Kristo kwa hali ya juu kabisa na hasa nyakati zile zinazokuwa ni ngumu na hatarishi katika maisha ya kikuhani. Mtazameni, na kwa kweli tukiangalia maisha ya Baba mwadhama si mtu wa maneno mengi, bali matendo yake, maisha yake yamekuwa ni Injili inayoishi na kutembea. Maisha yake kama kuhani ni shule na darasa kwa kila mmoja mwenye moyo wa unyenyekevu, anayehitaji kuchota na kujifunza maisha ya fadhila na utu wema na urafiki na Mungu na wengine. Hakika ukuhani na utumishi wake ni baraka si tu kwa familia na ndugu na jamaa au na jimbo lake la kuzaliwa, bali nathubutu kusema kwa Kanisa zima iwe Tanzania na hata nje ya nchi na Bara letu. Niseme nini basi zaidi ya kutamka maneno haya: Ad meliora et maiora semper! Deo gratias! Nihitimishe kwa maneno machache kwa Baba mwadhama, Pongezi! Pongezi! Pongezi nyingi! Asante! Asante! Asante sana! Ad maiora et ad multos annos!