Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Kisima cha huruma na upendo wa Mungu. Siku ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa maisha ya Mapadre. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Kisima cha huruma na upendo wa Mungu. Siku ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa maisha ya Mapadre. 

Sherehe ya Moyo Mt. wa Yesu: Kisima Cha Huruma na Upendo!

Tunapoadhimisha Sherehe hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunakumbuka hasa mapendo yake kwetu sisi wanadamu. Yeye alitupenda sisi mpaka upeo, hivi hata akajitoa afe msalabani ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Msalabani moyo huu ulifunguliwa kwa kuchomwa mkuki; na kwa hiyo kwetu sisi moyo huu u-wazi na ni chemichemi ya neema kwa maisha yetu

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.     

Tafakari ya neno la Mungu katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu mwaka B wa kiliturujia. Sherehe hii huadhimishwa ijumaa ya dominika ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste yaani baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu tunayoisherehekea dominika ya kwanza baada ya Pentekoste na Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo/Ekaristi Takatifu tunayoisherehekea dominika ya pili baada ya Pentekoste. Ni sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo ni alama ya mapendo. Tunapoadhimisha Sherehe hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunakumbuka hasa mapendo yake kwetu sisi wanadamu. Yeye alitupenda sisi mpaka upeo, hivi hata akajitoa afe msalabani ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti na kuwahuisha wakati wa njaa” (Zab. 33:11,19). Katika Moyo Mtakatifu wa Yesu yamo mapendo yote ya Mungu anayotupenda nayo sisi wanadamu. Msalabani moyo huu ulifunguliwa kwa kuchomwa mkuki; na kwa hiyo kwetu sisi moyo huu u-wazi na ni chemichemi ya neema kwa maisha yetu ndiyo maana katika sala ya mwanzo katika Liturujia ya Sherehe hii Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka jinsi alivyotupenda kwa mapendo yake makuu. Tunakuomba utujalie kupata neema tele katika chemchemi hiyo ya Baraka za mbinguni. Kumbe katika sikukuu hii tunashukuru Kristo kwa mapendo yake. Lakini pia kutafakari pale tulivyoenda kinyume na mapendo hayo katika maisha yetu ili kuomba radhi, kutolea heshima ya ibada yetu na kufanya malipizi yatupasayo.

Katika somo la Kwanza la kitabu cha Nabii Hosea (11:1b, 3-4, 8c-9); tunajifunza kuwa mapendo ya Mungu kwa binadamu yanashinda hasira yake, kadiri ile mapendo ya mzazi yanavyoshinda hasira ya mwanae mkaidi. Mungu aliwachukua Waisraeli kama mama amchukuavyo mtoto wake, akiwafundisha kutembea, akiwalisha na kuwabeba katika mikono yake, akiwaponya na kuwahudumia kadiri ya mahusiano ya mama na mtoto. Lakini Israeli alikuwa mtukutu, mkorofi na mwasi. Pamoja na utundu na uasi wake na kukosa shukrani, Mungu alimpenda na hakumtenda kwa ujeuri kama alivyowatenda mataifa mengine katika miji ya Sodoma na Gomora (Mwa 10:19, 19:28). Upendo ulimzuia Mungu asiwake hasira kwasabau ya uvumilivu wake; “Mimi ni Mungu, siyo mwanadamu, Mimi ni Mtakatifu.” Ndiyo kusema upendo wa wanadamu una ukomo na moyo wake ni mdogo kiasi kwamba hauwezi kamwe kuchota na kuelewa upendo wa milele wa Mungu. Ingawa tu wakosefu kama Waisraeli, tusiogope kumrudia Mungu sababu moyo wake haumtupi mtu mwovu anapokiri na kutubu makossa yake na kuamua kuiacha njia yake ovu na mbaya.

Somo la Pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (3:8-12, 14-19); linatueleza kwa mhutasa mpango wa Mungu baada ya anguko la mwanadamu kwa kukaidi amri na maagizo yake, kwamba kisha binadamu kuanguka dhambini, Mungu Baba aliweka mpango wa kuwakomboa watu wote kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye angewarudisha watu wote katika mapendo yake. Tumekombolewa kwa sababu ya upendo usio na mipaka wa Mungu katika Utatu Mtakatifu. Paulo anatuasa tusali sana ili tupate ufahamu mkubwa wa mapendo ya Mungu kwetu. Na kwa njia ya ufahamu huo Kristo atakaa ndani yetu. Paulo anapowaeleza Waefeso matamanio ya moyo wake na sala zake za kila siku anatuasa tutambue upendo na utajiri wa Kristo usiopimika kwa ajili yetu. Paulo anatualika tumruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani mwetu ili tuuonje upendo wa Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo. Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane (19:31-37); tunafahamishwa utimilifu wa Agano la Kale katika Agano jipya na la milele.

Ukweli ya kwamba Agano jipya ni utimilifu wa Agano la kale unaonekana katika Nafsi ya Yesu. Yeye alitukomboa toka utumwani mwa dhambi na mauti bila kuvunjwa mfupa kama vile Waisraeli walivyokombolewa toka utumwani Misri bila kuvunja mfupa wa mwana kondoo wa Paska. Nasi tukisadiki katika Kristo aliyetobolewa ubavu wake na mara ikatoka damu na maji chemchemi ya neema zote tutaweza kuzipokea neema hizo zitokazo ubavuni pake na kuokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Moyo Mtakatifu wa Yesu ndio chanzo cha chemchem ya Upendo wa Mungu kwa watu wote. Neno Moyo linajitokeza kila wakati tunapoeleza hisia zetu mbalimbali. Katika lugha ya kawaida mtu anapokuwa na huzuni au masikitiko moyoni tunasema mtu huyu amevunjika moyo au amekufa moyo. Ni kusema kana kwamba moyo wetu wa nyama ni kama kinasa hisia. Tunapokuwa na wasiwasi, mashaka, au woga mapigo ya moyo yanaongezeka kuashiria kwamba kuna kitu si sawa. Mapigo ya moyo yakiwa dhaifu ni ishara kwamba wasiwasi unaongezeka na pengine kifo kinakaribia. Na moyo unaposimama ndiyo mwisho wa uhai wetu. Ndiyo kusema Uhai na Hisia zimefungwa katika Moyo. Hivyo kwa sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunaunganisha uhai ndani ya Mungu na Upendo wa Kristo kwa watu wote.

Kumbe basi, upendo wa Mungu umekuwa dhahiri katika Kristo Yesu. Agano la Kale ni hadithi ya Upendo wa Mungu kwa watu wake na jibizo hafifu la watu hao. Hata hivyo Mungu ni mkarimu na mpole tena mvumilivu. Tusingeelewa hili kama Kristo asingelikuja. Yesu alikuja duniani na ujumbe kuwa Mungu ni Baba yetu mwema na anatupenda upeo. Uthibitisho wa mwisho wa upendo wake kwetu ni huu; “Kumtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminiye aokoke. Alikuja siyo kuhukumu bali kuokoa” (Yn 3:16-17). Upendo wa Yesu unajidhihirisha kwa sadaka yake msalabani kwa kuutoa uhai wake kwa ajili yetu (Yn 15:13). Kumbe upendo wa Mungu kwetu sisi ulikuwa ukitiririka katika moyo Yesu uliokuwa wa kibinadamu. Kama binadamu aliwaonea huruma umati uliomfuata waliokuwa kama kondoo wasio na mchungaji (Mk 6:34). Alimwonea huruma yule Mkoma (Mk 1:41). Alimwonea huruma yule mjane wa Naim aliyefiwa na mwanae pekee (Lk 7:13). Alilia juu ya kifo cha rafiki yake Lazaro (Yn 11:41). Alisikitika na kulia kwamba mji wa Yerusalemu utabomolewa (Lk 19:41). Alihuzunika kiasi cha kutoka jasho la damu katika bustani ya Gethseman (Lk 22:44).

Kristo Yesu, alikuwa mwingi wa furaha alipoona maskini na watu wadogo wamepokea ujumbe wa Mungu (Lk 10:21). Upendo wa Mungu umewekwa bayana kabisa katika nafsi ya Yesu Kristo na kwa kupitia upendo huo tunajua Mungu alivyo maana Yesu anasema; “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yoh.14:9). Kumbe ndani ya moyo wa Yesu linatiririka pendo lisilojibakizi. Ndivyo unavyoimba utangulizi wa liturujia ya sherehe hii ukisema; “Yeye aliinuliwa msalabani, akajitoa mwenyewe kwa ajii ya kutupenda sisi. Alichomwa ubavu akamwaga damu na maji, zipate kutoka humo sakramenti za Kanisa. Nasi sote tuvutwe na huo Moyo wazi wa Mwakozi, na kuchota kwa furaha neema katika chemchemi ya wokovu.”

Moyo Mtakatifu

 

10 June 2021, 15:47