Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani inapaswa kuwa ni matunda ya upendo kwa Mungu na wala si hofu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani inapaswa kuwa ni matunda ya upendo kwa Mungu na wala si hofu! 

Tafakari Jumapili 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani Tunda la Upendo

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 12 ya mwaka B wa Kanisa ambapo masomo yanatualika kuutafakari uthabiti wa imani inayotokana na uhusiano wa kweli kati yetu na Mungu. Imani yetu kwa Mungu haipaswi kuwa tunda la hofu bali matokeo ya upendo wetu kwa Mungu ambaye hatuachi kamwe katika kila hali tunayopitia na kamwe halali wala kusinzia!

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 12 ya mwaka B wa Kanisa ambapo masomo yanatualika kuutafakari uthabiti wa imani inayotokana na uhusiano wa kweli kati yetu na Mungu. Imani yetu kwa Mungu haipaswi kuwa tunda la hofu na woga bali matokeo ya upendo wetu kwa Mungu ambaye hatuachi kamwe katika kila hali tunayopitia. TAFAKARI: Katika somo la kwanza, Mungu, kama alivyofanya mara nyingi katika Agano la Kale na watu wake, anaingia katika mdahalo na Ayubu. Ayubu alitamani kukutana na Mungu, aongee naye, ajadiliane naye akiwa na lengo la kutetea shauri lake. Hatimaye katika sura hii ya 38 Mungu anajitokeza na kuzungumza. Mungu anamkabili Ayubu kwa maswali mengi. Katika mdahalo wake na Ayubu, Mungu anajidhihirisha yeye kuwa ni Bwana wa ulimwengu unaonekana. Ayubu aliwaza tu kuhusu hali yake na madhira aliyopitia pasipo kutazama kwa mapana nafasi ya Mungu katika yote aliyopitia. Alihisi Mungu amemwacha kabisa lakini haikuwa hivyo na kwa sababu hiyo hata katika yote aliyopitia upendo wake kwa Mungu ulipasika kubaki moto moto.

Dhamira hii ya Mungu ambaye hatuachi kamwe katika hali zetu tunazopitia inaendelezwa tena katika Somo la Pili ambapo Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anawahakikishia ya kwamba wanabidishwa na upendo wa Kristo. Kule kujua kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya wote ni sababu tosha kwa Paulo kusonga mbele. Hii ni imani kubwa na Mtume Paulo anaamini kuwa imani na matumaini yake haviwezi kumdanganya. Ikiwa Kristo alikufa kwa ajili ya wote basi lipo tumaini hata katika magumu na changamoto na kwa tumaini hilo inawezekana kusonga mbele. Katika Injili Yesu anaonesha nguvu yake juu ya maumbile: anatuliza dhoruba. Mwinjili Marko anataka kukazia ukweli kwamba Yesu anajua majaribu ambayo wanafunzi wake wanayapitia na anataka wamwamini si kwa sababu ya hofu bali kwa sababu ya upendo na urafiki ambao tayari ameujenga kati yake na wao. Iwe ni katika usingizi wake, au ni katika utendaji wake, daima yuko pamoja nao na hatawaacha. Muhimu ni kukumbuka daima kuwa Bwana yu pamoja nao katika safari yao.

KATIKA MAISHA: Ni nini tunachoamini na tunachojua kumhusu Mungu? Yapo mambo lukuki tunayokiri kumhusu Mungu. Tunakiri ya kwamba Mungu ni mwenyezi, muumba wa mbingu na dunia, ajuaye yote yaliyopita, ya sasa na ya wakati ujao. Tunaamini kuwa hakuna linashindikana kwake. Je, haya yote tunayoyajua na kuyaamini kumhusu Mungu yana nafasi gani katika maisha yetu ya kila siku na katika hali mbalimbali tunazopitia? Kile tunachokifahamu kumhusu Mungu wetu kinatusaidia kumuamini zaidi? Mitume katika hali yao ya kibinadamu walifanya lile waliloamini kuwa ni muhimu kufanya ili kuokoa jahazi. Wanapotambua kuwa hali ni mbaya wanafanya tendo la imani la kumuamsha Yesu aliyelala na kumuomba awaokoe. Ni imani kuomba msaada kwa Yesu lakini ni imani changa itokanayo na hofu na woga wa kuangamia.

Je, ni mara ngapi tumekutana na dhoruba katika maisha yetu na tukadhani ya kuwa Mungu wetu amelala au tukahisi hayuko nasi kabisa? Dhoruba ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Tuwe na uhakika kwamba tutakutana na taabu na madhira mengi tu katika maisha yetu. Tendo kubwa la imani tunaloweza kufanya ni kumwambia Mungu na Bwana wetu: “Naamini kuwa hata katika hali hii ninayopitia wewe u pamoja nami. Najua ya kuwa unanipenda na huwezi kuniacha nikaangamia. Endelea kulala Bwana wangu maana hata katika usingizi wako wewe unanilinda.” Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Dominika hii iwe ni sehemu ya kutathimini maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu ili tuone kama tunakua kiroho ama tunadumaa. Tujiulize kwanini tunasali, kwanini tunafunga, kwanini tunatoa sadaka na kutenda matendo mema kwa jina la Mungu? Je ni kwa sababu ya hofu au ni upendo kwa Mungu? Tumuombe Mungu atujalie neema ya kuimarika kiimani; kutoka katika imani itokanayo na hofu na kukua katika imani ambayo ni tunda la upendo. Aidha, tumuombe Mungu atujalie utulivu hasa tunapokutana na magumu tukijua kuwa uwezo wake juu yetu ni mkubwa kuliko dhoruba zinazotusonga.

Liturujia Ok

 

18 June 2021, 16:27