Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili Kumi na Moja ya Mwaka B wa Kanisa: Ukuaji wa Ufalme wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili Kumi na Moja ya Mwaka B wa Kanisa: Ukuaji wa Ufalme wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. 

Tafakari Jumapili 11 ya Mwaka B: Ukuaji wa Ufalme wa Mungu

Mhusika mkuu wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu ni Mungu mwenyewe anayepanda mbegu ya Neno lake katika nyoyo za waja wake. Neno hili linakuwa na kukomaa hatua kwa hatua hadi kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani toba na wongofu wa ndani. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anashiriki katika ujenzi wa Ufalme wa: haki, amani, upendo na udugu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ufalme wa Mungu ni uwepo wa Mungu katika mioyo na maisha ya mwanadamu. Ni Mungu akiwa kweli kiongozi wa kila hatua tufanyayo katika historia ya mwanadamu. Mwinjili Marko katika sehemu ya Injili ya leo anatupa mifano aliyotumia Yesu Kristo Mwenyewe katika kuulezea ufalme wa Mungu. Mwinjili Marko anatualika leo kutafakari haswa juu ya ukuaji wa ufalme wa Mungu katika maisha yetu, ni nani mhusika mkuu katika ukuaji na kuchanua kwa ufalme wa mbinguni katika nafsi za kila mmoja wetu? Yesu Kristo anatumia mifano ya kilimo, iliyojulikana na kueleweka vema na hadhira yake ya Kiyahudi na hasa kwa wakazi wa mkoa ule wa Galilaya ambako walikuwa wanajihusisha na kilimo na ufugaji.  Nyakati au hatua tatu muhimu kwa kila mkulima ni wakati wa kupanda, kukuza au matunzo ya mazao na wakati wa mavuno. Yesu Kristo katika Injili ya leo haweki mkazo sana katika hatua zile mbili yaani upandaji na mavuno na badala yake anasisitiza zaidi juu ya hatua ya matunzo na makuzi ya mazao.  Yesu Kristo anaelezea juu ya nguvu ya ile mbegu kukua na kuzaa matunda, hivyo mara inapopandwa ardhini inakua na kuzaa matunda.

Mpandaji na mvunaji hakika ni kazi ya mkulima mwenye shamba au watumwa wake, lakini kuota, makuzi na kustawi kwa mimea ni kazi inayokuwa nje ya uwezo wa mkulima. Hata hivyo tunaona Mwinjili Marko leo haoneshi hata hatua nyingine muhimu katika matunzo ya shamba kama kupalilia, kuweka mboleo au hata kumwagilia mimea ikibidi, ni na makusudi yake ya kutusaidia kupata ujumbe kusudiwa mintarafu ufalme wa Mungu kati yetu, katika maisha yetu. Labda tunaweza kuona ni mara ngapi kama wahubiri au wajumbe wa Injili tunajikuta tukiwa na mashaka na wasiwasi mwingi juu ya kuenea kwa Ufalme wa Mungu katika dunia yetu ya leo yenye changamoto mbali mbali? Tunaona leo Yesu anakazi juu ya nguvu ya ndani isiyozuilika ya mbegu ya Ufalme wa Mungu, ya kuku ana kustawi bila kutegemea juhudi na bidii kwa upande wetu. Ni kama asemavyo Nabii Isaya kuwa neno lake daima litazaa matunda. Isaya 55:11 “ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”

Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo tunaona Mwinjili hatumii neno kupanda na badala yake kusiha au kurusha zile mbegu ardhini. Ni mkulima anayekwenda shambani kwake na kuanza kurusha zile mbegu na ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopanda mbegu ya Habari Njema kwa ulimwengu mzima.  Ni Neno kwa kila kiumbe na hivyo halibagui yeyote ila linajumuisha wanadamu wote. Ni mkulima anayesiha mbegu kwa kuzirusha popote bila kujali wala kuangalia ni wapi zinadondokea hizo mbegu, ni mkono unarusha huku na kule katika shamba lile.  Ni mkulima anayesiha kwa furaha bila kujali maana ana hakika na matumaini ya kupata matunda mema na mazuri. Na ndio kazi ya kueneza Habari Njema inapaswa kufanyika kama mkulima anavyosiha mbegu zake ardhini kwa ukarimu, bila ubaguzi wala kujibakiza, bila upendeleo kwa kuangalia wapi litazaa matunda na wapi halitazaa, ni mwaliko kwetu sote kuwa na ujasiri na ukarimu wa kuwashirika watu wote popote Habari njema ya wokovu.

Baada ya kusiha mbegu, kinafika kipindi cha kukua kwa mimea, ni katika hatua hii mkulima hana tena maamuzi zaidi ya kuacha na kuona jinsi mimea inavyokua yenyewe kwa kupata mwanga na rutuba. Ni wakati wa kubaki na subira na matumaini kwa mkulima kuona mbegu ile ikiota, kukua na hatimaye kuweza kuzaa matunda tarajiwa. Mkulima analala na kuamka na kuendelea na majukumu yake mengine kwani hana tena uwezo wa kuyafanya yachipuke na kustawi. Kwa hakika mkulima hata kinachoendelea chini ardhini baada ya kusiha mbegu hana tena mamlaka wala uwezo wa kujua ni nini kinajiri.Na ndio hivyo hivyo Neno la Mungu ndani mwa kila mwanadamu, halina budi kukua kwa miaka na hivyo kuhitaji uvumilivu na subira kwa upande wa kila mmoja wetu. Ni mchakato unaochukua muda mrefu na si kitendo cha mara moja tu na kusema tumekamilika. Hata kama inachukua muda lakini daima Neno lazima likue na kuleta matunda katika maisha ya mwanadamu. Anayekuza mbegu ile njema sio mimi na wewe bali ni kwa neema na ndio nguvu za Mungu mwenyewe. Hatuna budi kutimiza wajibu wetu wa kulisiha Neno na kuacha neema za Mungu kufanya kazi yake.

Kishawishi kikubwa miongoni mwetu ni kukata tamaa hasa pale tunapokosa kuona matokeo chanya ya haraka katika maisha ya kiimani. Ni hakika kuwa Neno lake lazima liote na kuzaa matunda kwa kila anayefikiwa nalo. Hivyo muda usiwe sababu ya kutukatisha tamaa na badala yake uwe chanzo cha matumaini na faraja kwa kila mmoja wetu. Ni wazi ni vema kutambua kile kinachokuwa ndani ya uwezo wetu na hilo ndilo tunapaswa kulitimiza na mengine kumwachia Mungu ili akuze ufalme wake kati ya viumbe wake. Yafaa pia kukumbuka maneno ya Mtume Paolo katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 3:6 alipojitanabaisha kuwa yeye alipanda Neno na Apollo akamwagilia ila ni Mungu mwenyewe ndiye mkuzaji. Hivyo kila muhubiri wa Neno hana budi kukumbuka kuwa ni kwa Neema na Nguvu za Kimungu tu Neno lake litakua katika nafsi na maisha ya muumini. Mwinjili Marko anatuonesha jinsi mkulima, alilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo nchi ikazaa yenyewe; kwanza jani, tena suke na hatimaye ngano pevu katika suke. Na mkulima anakuja mwishoni kabisa wakati wa mavuno.

Ni Neno lenye nguvu hivyo lazima kuzaa matunda hata kama inachukua muda mrefu mbele ya macho ya mwanadamu. Ni Nguvu ya Kimungu iliyopo katika Neno lake, ni Mungu mwenyewe anayeikuza hiyo mbegu ya Neno lake katika nafsi zetu. Hivyo kututaka wajumbe wa Habari  Njema kutambua nguvu iliyomo katika Neno la Mungu, kila mahali tunaposiha Neno lake hakika litachipuka na kukua na kutoa matunda, muhimu kila mmoja wetu atimize wajibu wake wa kuwa mjumbe, wa kuwa msambazaji wa makuu ya Mungu kwa wengine, maisha yetu hayana budi kusiha Neno lake. Na kusiha Neno lake sio lazima kusimama mimbarini na kuhubiri bali tunaalikwa kwa nafasi ya kwanza kuhubiri kwa njia ya maisha yetu, maisha yangu yawe habari njema pale nyumbani, katika jumuiya, kazini, shuleni, shambani, sokoni, popote pale ninapokuwepo niwe sababu ya furaha na matumaini kwa wengine. Hakika hakuna mmoja anayekutwa na habari njema ya wokovu akabakia katika hali yake ya awali, hivyo hatuna budi kusonga katika kuwa wajumbe na waenezaji wa habari njema kwa kila kiumbe.

Muhimu ni kuhakikisha kuwa tumesiha Neno la Mungu n asio hekima na busara au mantiki ya dunia hii bali daima ile ya mbinguni, ile ya Kristo Mfufuka, hapo tunakuwa na hakika kuwa Neno la Mungu lina nguvu hata kama litakawiha lazima litazaa matunda mema mwishoni. Ni hatari ya wahubiri au waenezaji wa Habari njema badala ya kueneza Neno la Mungu katika ukamilifu wake, na kuanza kuingiza mantiki za ulimwengu huu, hapo kwa hakika tusitegeme hakika ya kukua na kustawi. Ujumbe wa leo hata unatutaka kutokutumia nguvu au mabavu na kukosa uvumilivu na subira katika kueneza ufalme wa Mungu kwa watu wake, iwe ni wahubiri au makatekista, au walimu na hata wazazi na walezi, kila mmoja wetu mwenye wajibu wa kueneza ufalme wa Mungu hana budi kukumbuka kuwa Neno lake lina nguvu na kamwe tusikate tamaa, hata kama tunakutana na changamoto mbali mbali katika kutimiza utume wetu. Leo Injili inatuambia hata kuna umuhimu wa mkulima kulala na kuondoka, ndio kusema kuwa na subira, kutokukata tamaa anaposubiri mbegu kuota na kuku ana kustawi mpaka wakati wa mavuno. Ndio kusema tunatakiwa kuwa na imani katika nguvu iliyopo katika mbegu ile, yaani Neno la Mungu, na ndio neema ya Mungu inayofanyakazi kwa namna isiyoonekana kwa macho yetu ya nyama.

Ndio namna Mungu pia anavyofanyakazi ndani ya mwanadamu, kwa namna ya ajabu na isiyojulikana machoni petu. Ni ujumbe wa kumuimarisha kila mjumbe wa Habari njema ya wokovu! Mfano wa pili pia unafanana na ule wa kwanza, yaani mkulima anayepanda mbegu ndogo zile za haradali na hatimaye kuota na kuwa mti mkubwa kabisa. Ni kuonesha kuwa Neno la Mungu daima lina nguvu na matokeo au matunda yake ni makubwa. Mbegu ya Ufalme wa Mungu daima inabaki kuwa ndogo kwa maana ya unyenyekevu wa Mungu mwenyewe na hivyo kutoonekana katika macho ya kiulimwengu. Ila matunda yake yanazidi kila aina ya ukubwa wa kiulimwengu. Ni nguvu iliyomo ndani ya Neno lake kuweza kukua na kustawi na kutoa matunda mengi na mazuri. Ni mbegu inayokuwa ndogo kabisa ndio kusema mbele ya mantiki ya ulimwengu huu si kitu cha maana lakini mara inapopandwa na kuchipuka na kukua hakika matunda yake yanastaajabisha wote. Na uwingi si katika idadi bali katika thamani na ubora wake.  Luka 17:21.

Ni Injili inayotualika na kututaka kuwa na mwono au mantiki mpya ya Mungu mwenyewe, kuangalia na kupima sio kwa vipimo vya ulimwengu huu bali kwa jicho na mantiki ya mbinguni. Kuwa na imani na hakika katika nguvu na uwezo wa Mungu hata kama wengine watatucheka na kutushangaa. Moja ya matokeo yake ni kuwa kimbilio la kila mmoja wetu. Hivyo kuwa kiota kwa kila anayelikimbilia na kuliamini. Zaburi 91:1; 84: 4; 1:3. Yesu Kristo anamalizia kwa kuwaelezea zaidi wanafunzi wake. Na ndio mwaliko pia kwetu kuwa ili kuelewa Neno lake hatuna budi kuwa na muda wa sala na tafakari ili Roho wa Mungu aliye mwalimu wetu apate kutufunulia siri kuu za Mungu na nguvu ya Neno lake. Ni mwaliko wa kutenga muda wa kutafakari Neno lake kila siku katika maisha yetu ili kuweza kuelewa ujumbe unaokusudiwa katika maisha yak ila mmoja wetu. Mungu ana ujumbe mahususi kwako na kwangu, kwa kila mmoja wetu. Nawatakia tafakari njema na Dominika yenye kila baraka zake Mwenyezi Mungu.

11 June 2021, 08:52