Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Mungu ni chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Mungu ni chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 13 Mwaka B: Uhai na Haki Msingi

Dominika hii yanatutafakarisha juu ya Mungu aliye chanzo cha uhai na uzima. Aidha, tunapewa mwaliko kupitia masomo haya kujiaminisha kwa Mungu kwa imani kuwa kwake tutauhisha maisha yetu na kuwa na uzima tele. Yeye aliyetuumba ametushirikisha zawadi ya uhai na hata baada ya kuanguka dhambini hakutuacha katika mauti bali anatuita kwake tupate kupokea uzima tele.

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 13 ya mwaka B wa Kanisa. Pamoja na mengine mengi, Masomo ya Dominika hii yanatutafakarisha juu ya Mungu aliye chanzo cha uhai na uzima. Aidha, tunapewa mwaliko kupitia masomo haya kujiaminisha kwa Mungu kwa imani kuwa kwake tutauhisha maisha yetu na kuwa na uzima tele. Yeye aliyetuumba ametushirikisha zawadi ya uhai na hata baada ya kuanguka dhambini hakutuacha katika mauti bali anatuita kwake tupate kupokea uzima tele. TAFAKARI: Katika somo la kwanza kutoka Kitabu cha Hekima ya Sulemani, tunakumbushwa ya kwamba maisha ni zawadi ya Mungu. Kuwa na uhai na uzima ni zawadi itakayo kwa Mungu mwenyewe. Mungu ndiye muumbaji na ndiye chanzo cha kila kilicho hai na kilichopo. Kwa Mungu kuna uzima katika ukamilifu wake. Hivyo ni haki kabisa kusema kuwa Mungu hawezi kuwa asili ya mauti. Lakini uzima huu utokao kwa Mungu unaambatana na dhana ya haki. Kwa kuwa katika haki hakuna uharibifu, Mungu wa uhai na wa haki hawezi kuwa chanzo cha mauti.

Hivyo basi, pamoja na zawadi ya uhai, Mungu ameweka ndani yetu zawadi ya haki ambayo inatufanya tuishi kadiri ya mpango wake. Mungu hakutuumba ili kutuangamiza kwa kifo. Kifo kimekuja duniani kama matokeo ya uamuzi wa makusudi kufanya dhambi. Palipo na haki pana uhai na uzima na palipo na wivu na uchu pana kifo na mauti. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatambua mchango wa waamini Wakristo wa Korinto waliojitoa kusaidia jumuiya ya Wakristo kule Yerusalemu. Kwa sababu hiyo anawatia moyo wadumu katika huduma hii ya upendo. Walikubali kutoa sehemu ya mali walionayo ili wapate kuishirikisha kwa wengine. Walitenda jambo jema la haki na la upendo. Waliiga mfano wa upendo wa Yesu mwenyewe. Na kwa kitendo hicho wakawa sababu ya uhai kwa wahitaji waliokuwa Yerusalemu. Haki inayojengwa juu ya msingi wa upendo ni haki inayoleta uhai kwa wengine.

Katika Injili tunasimuliwa matukio mawili ya kimuujiza ambapo Yesu anauhisha tena maisha na kuleta uzima. Anamponya mwanamke mwenye kutoka damu na anamuuhisha tena binti Yairo. Mwinjili anatuonesha wema wa Yesu. Ni Yesu anayejali na anayelinda zawadi ya uhai. Ni Yesu anayetoa uzima. Nguvu ya kimungu ya uponyaji itokayo kwa Yesu inamponya mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka mingi na anamwambia wazi kuwa kupona kwake kumechochewa pia na imani yake. Na kwa yule afisa wa Sinagogi, aitwaye Yairo, Yesu anamsihi akisema “Usihangaike, amini tu.” Imani ni hatua muhimu katika kuonja nguvu ya Mungu ya kuponya na kuleta uzima. Kumbe, imani ni nyenzo anayoitumia Mungu kuganga, kuponya na kupyaisha maisha!

KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Dominika hii tunakumbushwa ya kwamba mauti ya mwanadamu si sehemu ya mpango asilia wa Mungu kwa sababu Mungu ni chanzo cha uhai na uzima. Mauti ilikuja kwa njia ya wivu wa Shetani, na hivyo kwa njia ya dhambi. Ikiwa tutaridhia ubaya wa Shetani katika maisha yetu wenyewe kwa kutenda dhambi tunajitamkia kifo juu yetu wenyewe. Aidha, tunaalikwa kujiaminisha kwa Mungu, kuwa tayari kujikabidhi akili, mwili na roho kwa Mungu aliye chanzo cha uzima. Tazama alivyofanya yule mwanamke na alivyofanya yule afisa wa sinagogi aitwaye Yairo. Hakukuwa na mashaka ndani yao bali waliamini. Walijisemea moyoni kuwa hakuna kitakachoshindikana kwa Yesu na ndivyo ilivyo kuwa. Walionja matunda ya kuamini kwao. Na Yesu anasema wazi kuwa imani inaokoa. Je, sisi tunayo imani inayotuokoa?

Tunayo imani thabiti isiyotilia mashaka uweza wa Mungu wa kutuokoa na kutujalia uzima? Tusiogope kuamini, tusiogope kujikabidhi kwa Mungu, naye atatujalia uzima. Kumbuka kuwa haitoshi tu kuwa sehemu ya kundi kubwa linalomfuata Yesu, kama walivyofanya watu wengi waliokuwa pamoja na Yesu alipofanya miujiza hii. Wewe fanya maamuzi ya kutoka ndani ya moyo wako useme kuwa nitagusa pindo la vazi lake; amua kuwa utakwenda kwake na utajikabidhi kikamilifu pasipo kuhofu kitu au kuwa na mashaka yoyote. Fanyia kazi kile unachoamini. Usibaki tu kuwa sehemu ya kundi la watu wanaomfuata Yesu na hata kama wanamgusa hawaonji mabadiliko kwa sababu hawanuii kumgusa. Amua kumfuata Yesu na kuguswa nae na hakika atauhisha tena ndani yako uzima.

Tunayo mambo mengi yanayohitaji kuponywa na Yesu. Tunao udhaifu wa namna nyingi ambao unahitaji nguvu ya Mungu ya kuuhisha na kufanya hai tena. Tuna udhaifu katika kuamini na kuiishi imani; tuna udhaifu katika kutenda haki; tuna udhaifu katika kutimiza wajibu wetu na katika kujali na madhaifu mengine mengi ya mwili na roho. Tukumbuke kwamba kukutana na Yesu na kuunganika naye kutaponya madhaifu haya yote. Tutafute kukutana naye katika Neno lake, katika Sakramenti zake, na katika historia na maisha yetu ya kila siku. Yeye ndiye anayetupatia utimilifu wa uhai. Zaidi ya hayo, tuwe chachu ya uhai ambao ni zawadi ya Mungu. Tuwe sababu ya kuleta uhai kwa wengine kwa kuwa mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Liturujia J13
25 June 2021, 16:19