Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 13 Mwaka B: Uhai Ni Zawadi!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 13 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatufundisha kuwa chanzo cha uhai ni Mungu. Uhai ni zawadi ya Mungu kwetu sisi. Mungu anapenda tuishi. Magonjwa, mahangaiko, mateso na kifo havitoki kwa Mungu bali ni kazi ya shetani mkuu wa giza na mauti. Mungu ni Bwana wa uhai na Yesu aliye nafsi ya pili ya Mungu alikuja kutudhihirishia hili ndiyo maana katika injili aliwahuisha/kuwarudishia uhai watu watatu; Binti Yairo (Mk 5:21-24, 35-43), Mtoto wa kiume wa mjane wa Naim (Lk 7:11-17) na Lazaro ndugu ya Maria na Martha (Yn 11:1-44). Kumbe Mungu daima yupo upande wa maisha, upande wa nuru ndiyo maana katika sala ya mwanzo Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akiomba; “Ee Mungu, umependa kutufanya sisi tuwe wana wa nuru kwa neema uliyotufadhili. Tunakuomba utujalie tusifunikwe na giza la udanganyifu, bali tukae daima peupe katika nuru ya ukweli.”
Somo la kwanza la kitabu cha Hekima ya Sulemani (1:13-15; 2:23-24); latueleza kuwa Mungu alikusudia heri kwa wanadamu alipowaumba. Mungu aliyetuumba na kutujalia zawadi ya uhai anapenda tuishi. Hivyo chochote kinachoangamiza maisha na uhai hakitoki kwa Mungu bali ni matokeo ya kukiuka misingi ya uhai na maisha aliyotujalia Mungu. Mateso, mahangaiko na kifo ni matokeo ya dhambi. Kwanza tunahanagaika na kufa kimwili na mwisho tunakufa kiroho na kuukosa ufalme wa Mungu. Biblia yafundisha kwamba taabu zote tupatazo ni mapato ya dhambi kwa kumtii shetani badala ya Mungu. Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakifa katika dhambi kwani kifo ni matokeo ya dhambi ambayo kwanza kabisa husababisha kifo cha kiroho. Dhambi inaharibu uzima wa Mungu ndani yetu, inaharibu mahusiano baina ya wanadamu. Na mwisho dhambi inatupeleka katika kifo cha mwili. Kifo cha roho kikishatokea, kifo cha mwili ni dhahiri. Kumbe kifo ni adhabu kwa sababu ya dhambi; “Kwa maana u-mavumbi wewe na mavumbini utarudi” (Mwa 3:19). Hili lilikuwa tangazo la huzuni itokanayo na madhara ya dhambi. Dhambi inatuondolea uzima wa kimungu ndani yetu. Dhambi ni sumu dhidi ya mwili, iingiapo mwilini, kifo hakiepukiki.
Somo la pili la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (8:7, 9:13-15); ni maonyo ya Mtume Paulo kwa Wakorintho kuhusu kushika ahadi wanazoziweka. Wakorinto waliahidi kuwasaidia fukara wa Yerusalemu kwa fedha. Hivi anawajulisha kuwa kuwasaidia fukara ni neema si hasara. Neema ya Yesu na iwabidishe kwa ajili ya manufaa ya walio wahitaji kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na kwa ajili ya wao kujipatia zaidi neema na baraka za Mungu zinazowawezesha kuurithi uzima wa milele. Injili ilivyoandikwa na Marko (5:21-43); inasimulia miujiza miwili aliyoifanya Yesu. Muujiza wa kwanza, ni wa kuponywa mwanamke aliyetoka damu, licha ya mahangaiko ya kutafuta tiba kwa waganga wengine wengi na kupoteza mali zake, hakuweza kupona. Muujiza wa wa pili ni wa kumfufua binti Yairo. Hapa tunaona jinsi Yesu anavyoshughulika na kuhaingaikia maisha ya wanadamu, anataka waendelee kuishi. Yesu ni Bwana wa uhai ndiyo maana anamrudishia uhai binti Yairo. Katika lugha ya kiyunani Yairo maana yake ni “Mleta mwanga/ anayeamsha. Huyu alikuwa mkuu wa Sinagogi. Yairo aliamini na kutumaini kwamba Yesu akimwekea binti yake mkono atapona na kuendelea kuishi.
Mara alipokea taarifa kwamba, binti yake amekwisha kufa naye akafadhaika sana (Mk 5:35). Yesu anaonja adha ile. Hivyo anamfariji akimwambia usiogope, jipe moyo tu (Mk 5:36). “Kijana hakufa, bali amelala tu” (Mk 5:39). Kisha akaandamana naye mpaka nyumbani kwake walikuta wakilia na kuomboleza. Baada ya kuwatoa watu nje. Akamshika mkono yule maiti akamwambia; “Talitha Kum” maana yake; “Msichana nakuambia inuka.” Yule msichana akainuka mara akatembea. Yesu akaamuru wazazi wake wampe chakula ishara kuwa sasa binti yao yu hai, yuko kati yao, wampe mahitaji muhimu ya kawaida, wamhudumie, watimize wajibu wao wa kibinadamu. Hapa tunaonja upendo wa Mungu na ukarimu wake kwa kuonja na kushirikia shida za wanadamu ili kuwapatia uzima. Hii ni kwasababu Mungu hakuifanyisha mauti wala hapendi kuona walio hai wakifa, bali waishi (Hek 1:13). Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutoharibika kwa mfano wake mwenyewe (Hek 2:23). Uhai ni zawadi na tuzo la thamani kubwa ambayo Mungu anampa mwanadamu na hajutii kumpa mwanadamu zawadi hiyo (Rum 11:29). Kifo kilimhuzunisha Kristo, alionja madhara ya dhambi kwa mtu kwani kifo si mpango wa Mungu.
Kristo Yesu alikuja duniani aingamize dhambi na kifo. Kwa fumbo la Umwilisho ameharibu kifo cha kiroho, na kuturudishia uzima wa kimungu tuliopoteza kwa sababu ya dhambi. Pia kwa umwilisho, miili yetu inapata hadhi mpya. Miili yetu sasa inakuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Kristo alikuja kuangamiza kifo cha mwili, kwani kwa kutusamehe dhambi sasa tuna amani rohoni, kwa kuwaponya wagonjwa tunapata amani mwilini, kwa kufufua wafu, ameumba vipya. Maandiko yanatuambia kwamba; “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti” (1Kor 15:26), maana kwa fumbo la Pasaka; mateso kifo na ufufuko wake Kristo aliishinda mauti. Kwa kifo chake, msamaha umepatikana kwa wote, uzima wa kimungu ni dhahiri kwa wote wanaopenda. Kwa kupata uhai wa kiroho, uhai wa mwili unafuata. Dhambi hupeleka mwili kifoni. Kristo anatupa uzima na amani ya kweli. Katika ubatizo tunapata uzima wa kiroho, tunafufuka kutoka dhambi na kuingia katika hali ya uzima. Kifo sasa ni njia tu ya kuingia katika uzima wa milele. Siku ya kifo cha mwili ndipo tunapoishinda dhambi kabisa. Kama tukifa katika Bwana, tuna uzima wa kimungu ndani yetu.
Siku ya kifo chetu, tusali pamoja na Kristo; “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu.” Kifo ni mlango wa kuingia katika uzima wa milele. Kifo ni mwisho wa malumbano. Maandalizi ya tuzo au hukumu. Kifo ni ushindi dhidi ya dhambi; “Mimi ni ufufuko na uzima, kila aniamiye, hata akifa, ataishi” (Yn 11:26). Ikiwa tunaamini kuwa Kristo alikufa na kufufuka, vivyo hivyo, na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye” (1Thes 4:14). Ili tuweze kuurithi uzima wa milele yatupasa kumpenda Mungu na jirani. Tukumbuke kuwa dhambi ni sumu ya upendo. “Anayempenda ndugu yake, anaishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani yake” (1Yn 4:16). Yeye asiyependa anaishi katika mauti (1Yn 3:14). Tukiwatendea wenzetu kadiri ya upendo, tunawaongezea uhai, na heshima ya utu, na tunashirikiana na Mungu katika kazi ya uumbaji na ukombozi. Tuombe neema za Mungu ili kwa kafara ya Yesu ambayo inatolewa kila katika adhimisho la Misa Takatifu nasi tunaoipokea itutie uzima wa kimungu ndani mwetu ili tuweze kuungana na Yesu Bwana na mwokozi wa maisha yetu hata ukamilifu wa maisha yetu huko mbinguni aliko yeye.