Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Furaha ya Uinjilishaji inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Furaha ya Uinjilishaji inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! 

Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka B: Huduma Kwa Watu wa Mungu!

Viongozi wa kiroho wanapaswa kujitoa kiaminifu, wakiwatumikia na kuwajali waamini wao na wasitafute maslahi binafsi. Wakimwiga Kristo, wanapaswa kuwa wajumbe wa amani na umoja katika Jumuiya walizokabidhiwa. Jumuiya ya Kikristo daima ilenge kudumisha amani na umoja baina yao na viongozi na jirani zao na kuwapa watu matumaini pale wanakumbwa na ugumu wa kimaisha.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 16 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya 15B yalitueleza wajibu wa viongozi wa kiroho wa kuihubiri Injili kwa uaminifu na pia wajibu wa waamini wa kusikiliza na kuyaishi yale wanayofundishwa ili waweze kuufikia uzima wa milele. Masomo ya dominika hii ya 16 B yanatueleza kuwa viongozi wa kiroho wanapaswa kujitoa kiaminifu, wakiwatumikia na kuwajali waamini wao na wasitafute maslahi binafsi. Wakimwiga Kristo, wanapaswa kuwa wajumbe wa amani na umoja katika Jumuiya walizokabidhiwa. Jumuiya ya Kikristo daima ilenge kudumisha amani na umoja baina yao na viongozi na jirani zao na kuwapa watu matumaini pale wanakumbwa na ugumu wa kimaisha.

Katika somo la kwanza la kitabu cha Nabii Yeremia (23:1-6); ni makaripio ya Mungu kwa viongozi wazembe wa Israeli. Uzembe wa viongozi hawa ulisababisha maadili ya watu kuporomoka na hivyo watenda dhambi na kumuasi Mungu. Matokeo ya dhambi zao ni mji wa Yerusalemu na Hekalu lililowakilisha uwepo wa Mungu kugeuzwa kuwa magofu na kuchukuliwa mateka Babiloni kwa watu wake na viongozi wao. Mungu kwa huruma yake kwa kinywa cha Nabii Yerehemia anatangaza kuwa: Wachungaji waovu na potofu waliopelekwa uhamishoni kama mateka, wataondolewa, watakufa huko kwa sababu ya dhambi zao. Lakini Mungu atawakusanya watu wake kutoka pande zote za uhamishoni na kuwarudisha katika nchi yao. Mungu anasema nitawarudisha kondoo zangu katika mazizi yao, nao watazaa na kuongezeka. Mungu anaahidi kuwapa watu wake wachungaji wapya, watakaowalisha na kuwaongoza katika malisho na maji, na kuwalinda kutokana na hatari zozote za adui. Wachungaji hao watachipuka kutoka shina la Daudi, na huko litatoka chipuki la haki, mwingi wa hekima, atakuwa mfalme wa haki na utakatifu. Wachungaji hao watakuwa na wasaidizi ambao watavikwa pia haki na utakatifu, na karama ya uongozi itakuwa mabegani mwao, ili amani, haki, upendo, na utakatifu vitawale huko Israeli.

Katika kutoa ahadi hii, Mungu anawafananisha watu wa Israeli kama kondoo ili waweze kuelewa vizuri ujumbe wake. Hii ni kwasababu miaka 400 kabla ya Waisraeli kuanza kuishi Palestina, wengi wao walikuwa wachungaji kama Maandiko Matakatifu yanavyoshuhudia: Mfano; “Yosefu mwana wa Yakobo, akimpa Farao habari za ndugu zake anasema: “Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa Baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kaanani, wamenijia, na watu hao ni Wachungaji…nao wameleta kondoo zao, ng’ombe zao na waliyo nayo” (Mwa 46:31-32). Hata walipotoka Misri kuelekea Kaanani chini ya uongozi wa Musa, pamoja nao walichukua kondoo, mbuzi, na ng’ombe wengi (Kut 12:38). Huko Palestina nako waliendelea na kazi ya ufugaji. Daudi kabla ya kupakwa mafutwa na Samweli kuwa mfalme alikuwa anachunga kondoo za Baba yake Yesse huko Bethlehemu (1Sam 16:11-13). Katika kuwahudumia wanyama wao wachungaji walionja adha nyingi; jua kali, mvua, baridi, wanyama wakali na hata majambazi. Wachungaji wema waliwafahamu wanyama wao kwa majina, rangi, umri, na mmoja alipougua walimhudumia na kumtibu kwa upendo mkubwa. Wachungaji, waliishi katika mahema, kwa kuwa walihamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta malisho, maji na mahali salama kwa ajili ya mifugo yao. Wachungaji waliishi nje ya miji na vijiji wakiwahudumia wanyama wao usiku na mchana. Mungu anatamadunisha hali hii ya uchungaji, anajilinganisha na kujiita “mchungaji mwema”, ili kuwafanya watu wa Israeli wauonje mapendo wake kwao.

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (2:13-18); linatueleza kuwa katika Agano la Kale kulikuwa na tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Katika Agano jipya watu wote tumeunganishwa na kifo cha Kristo. Sasa sote tunaweza kumfikia Mungu kwa njia ya Kristo mchungaji wetu mwema na mwaminifu aliyeutoa uhai wake kwa ajili yetu. Masimulizi yanasema kuwa Kanisa la Efeso, waamini wake wengi walitoka katika familia za watu wa mataifa wasio Waisraeli. Familia hizi ziliitwa familia za kipagani. Waamini hawa kutoka makabila mengine walionekana kuwa duni na wale waliotoka katika familia za Kiyahudi walionekana kuwa bora zaidi. Ndiyo maana katika Hekalu la Yerusalemu kulikuwa na ukumbi wa Wayahudi na ukumbi wa watu wa mataifa walioongokea uyahudi. Hawa watu wa mataifa hawakuruhusiwa kuvuka kwenda upande wa wayahudi. Kuvunja sheria hiyo kuliendana na adhabu kali hata ikibidi kifo. Paulo Myahudi, Mtume wa kimataifa anakemea tofauti hizi, akieleza kwamba; haijalishi unatoka katika kabila gani, unapoingia ukristo unakuwa kiumbe kipya. Kinachotuunganisha na maisha mapya ni Roho Mtakatifu, tunayempokea katika Ubatizo. Kwa ubatizo sote ni familia mpya ya Mungu: Kaka na Dada zake Yesu. Paulo anasisitiza kuwa; kwa kifo cha Kristo, ule ukuta uliowatenganisha Wayahudi na watu wa mataifa umebomolewa. Sisi sote ni familia ya Mungu, tunaounganishwa na upendo.

Roho Mtakatifu tuliyempokea anatufanya familia moja yenye haki sawa ya kumwabudu Mungu. Hekalu la Yerusalemu sio mahali pekee tena anakopatikana Mungu maana sote tunamwabudu Mungu katika roho na kweli tukisali kwa pamoja “Baba Yetu” (Mt 6:10). Kumbe, Roho Mtakatifu ametufanya kuwa siyo tu familia moja, bali mwili mmoja na roho mmoja katika Kristo (Efe 2:16). Kumbe mgawanyiko, chuki na vita baina ya Wakristo ni matokeo ya dhambi. Roho Mtakatifu zawadi ya Mungu kwetu anatufundisha kupendana, kusaidiana na kuimarishana katika madhaifu yetu. Kama vile wazazi wanavyosikitishwa wanapoona mgawanyiko na chuki baina ya watoto wao, Mungu kadhalika anahuzunishwa kuona sisi kama kaka na dada katika imani, tunachukiana, kusogoana na kutoshikamana. Tofauti zetu za kiumri, kihisia, kihistoria, kikarama au kimapato hazipaswi kutufanya tubaguane bali ni utajiri tunaojaliwa na Roho Mtakatifu ili tuweze kuhudumiana. Tofauti hizi ni zawadi, tulizopewa kama mawakili wema, ili tuzitumie kwa faida ya wote. Tunapotumia haya katika utofauti wake, tunakamilishana na kujengana. Mungu anamwokoa mtu mmoja mmoja, lakini siyo katika utengano, ila katika umoja kama familia ya kiimani.

Kinyume na maonyo na makaripio ya Nabii Yeremia kwa viongozi wazembe wa wa Taifa la Israeli, Injili ilivyoandikwa na Marko (6:30-34), inasimulia matunda ya kazi za Mitume 12 aliowachagua Yesu ili waendeleze kazi ya kuujenga na kuusimika ufalme mpya wa Mungu chini ya Kristo Mchungaji mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Sehemu hii ya injili inatoa taarifa za kurudi kwa Mitume kwa Yesu baada ya kuihubiri injili. Ingawa walikuwa wamechoka sana, walijawa na furaha kwani nguvu ya Kristo ilitenda kazi ndani yao. Yesu anawaambia wajitenge kidogo mahali pa faragha wapate kupumzika. Lakini watu wengi waliwatafuta ili waendelee kuwahudumia. Yesu anawaonea huruma kwa kuwa walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Hapa tunajifunza kuwa viongozi wa kiroho sharti wajisahau wenyewe, wawe tayari muda wote kuwatumikia wahitaji, hata ikibidi wao kukosa muda wa mapumziko. Wajibu wa waamini ni kuwaombea na kuwahudumia ili wawe na nguvu zaidi ya kuendelea kuwahudumia kwani wao katika hali ya ubinadamu wana mahitaji ya lazima yanayowawezesha kuwahudumia vyema watu waliokabidhiwa. Basi, tuombe neema za Mungu, tukimruhusu Roho Mtakatifu atuongoze vyema ili tuweze kuisha kwa upendo na umoja ili mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele Mbinguni.

Tafakari

 

15 July 2021, 15:53