Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka B: Yesu Kristo Ni Ufunuo Wa Huruma!
Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.
UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 16 ya mwaka B wa Kanisa. Dhamira msingi ya Dominika hii yahusu wokovu wa watu na wajibu wa wachungaji. Masomo yanatupatia nafasi ya kumtafakari Kristo Yesu aliye mchungaji mwenye huruma kwa kondoo wake, anayetafuta daima kuwaleta pamoja na kuwakomboa. Aidha, tunaalikwa nasi kukumbuka wajibu tulionao wa kushughulikia wokovu wetu na wa watu wote. Tunaalikwa kuiga mfano wa Kristo Yesu mwenyewe ambaye hachoki kamwe kushughulikia wokovu wa watu wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema likizo ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kujipatia tena nguvu za kuweza kusonga mbele katika mapambano ya maisha ya kila siku. Ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, ukuu na uweza kutokana na kazi kubwa ya uumbaji. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani mazingira bora na safi ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiikolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu kwa sababu mazingira bora ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Tutumie vyema likizo zetu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu katika maisha yetu!
TAFAKARI: Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha nabii Yeremia tunasikia unabii wa kimasiha unaohusu ujio wa Kristo Yesu. Nabii Yeremia anazungumzia kundi lililotawanyika kwa sababu ya kutokuwa na wachungaji wenye kujali na kukosekana kwa uongozi bora na adilifu. Kundi hili limetawanyika kujitafutia malisho lipate kuishi kwa sababu wale waliokabidhiwa jukumu la kulichunga na kuliongoza hawakulijali na waliliacha na hatimaye, likamegeka na kutawanyika kama umande wa asubuhi. Kwa upande mmoja nabii anatoa onyo kali kwa wachungaji na viongozi wa watu wa Mungu ambao hawajali: ustawi, maendeleo, mafao na maslahi ya kundi hili la Mungu. Kwa upande mwingine nabii analeta tumaini kwa kundi lililotawanyika. Mungu atalikusanya tena na kuliweka pamoja na atalipatia wachungaji bora watakaolichunga na kuliongoza vyema. Tumaini hili linatimia kwa ujio wa Kristo Yesu ambaye ni ufunuo wa huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia vultus” yaani Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa naye kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele. Katika somo la pili Mtume Paulo anazungumza juu ya kazi aliyoifanya Kristo Yesu ya kuwakusanya tena kundi la Mungu na kuliweka pamoja. Wale wote waliokuwa wamejitenga mbali na Mungu kwa sababu ya dhambi sasa wamekusanywa tena na kupatanishwa naye Mungu kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo Yesu.
Katika Injili wafuasi wa Yesu wanarejea kutoka katika safari ya kitume waliyotumwa na Bwana Yesu. Wanatoa mrejesho wa kazi waliyotumwa kuifanya na yale yote waliyoweza kuyatekeleza. Wanaripoti kile walichofundisha kwa watu na matendo makuu waliyoweza kuyatenda katika safari yao. Wanadhihirisha kuwa wajumbe waaminifu wa Injili ya upendo na matumaini ambao wanatambua kuwa hawakujituma wenyewe katika kazi hiyo bali walitumwa na Kristo Yesu, na hivyo wanao wajibu wa kutoa mrejesho kwa kazi na utume wao. Lakini zaidi ya kutoa mrejesho wanapata nafasi ya kujifunza tena kutoka Kristo Yesu mwenyewe ambaye hachoki kulihudumia kundi lake. Ni wazi Mitume walikuwa wamechoka na walihitaji kupumzika lakini katika kupumzika kwao wanapata fundisho la ziada ya kwamba kama wachungaji wanapasika kujitoa daima kwa kundi la Mungu kwa ajili ya kuwapatia Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na waja wake!
KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican tunapotafakari masomo haya tunajikumbusha juu ya ukweli kwamba wokovu wetu watoka kwa Mungu; yeye anataka sisi sote tuokoke na tubaki katika muunganiko na urafiki naye. Daima anatuhangaikia na anataka kutukusanya na kutuweka pamoja kama kundi lake chini ya wachungaji wema, watakatifu na waadilifu wanaoendana na moyo wake. Tumaini kubwa tunaloweza kuishi nalo katika maisha yetu ni ya kwamba Mungu hatatuacha kamwe tutangetange, wala hatatuacha kutushibisha kwa neno lake. Huruma yake kwetu ni kuu na daima anadhihirisha mapendo yake kwetu. Hatuna sababu ya kuogopa bali tunapasika kumtumainia yeye. Je, tunaishi tukiongozwa na tumaini hilo? Mama Kanisa anatumwa kueneza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu. Katika mafundisho yake Yesu akifuatwa na makundi kwa makundi, aliwalisha wenye njaa, aliwaponya wagonjwa, aliwaondolea dhambi zao, aliwafukuza pepo na kuwafufua wafu. Huu unaendelea kuwa utume wa kila Mkristo maana, kama anavyofundisha Baba Mtakatifu Francisko, “Yesu anathibitisha kwamba huruma siyo tendo la Baba tu, bali ni kigezo cha hakikisho la wana wake kweli.
Kwa kifupi tunaitwa kuonesha huruma kwa sababu tumeonewa huruma kwanza. Huruma ya Mungu kwetu inaonekana pia katika tunza yake kwetu, akitulinda na kutuneemesha, ili tuishi kwa furaha, amani na utulivu wa ndani. Kilele cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu ni tukio kuu la fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa sababu hiyo kila mdhambi amechangia katika mateso na kifo cha Kristo Yesu, na mateso, kifo na ufufuko wake ndio sababu ya wokovu wa kila mkosefu. Hivyo sura halisi ya upendo wa Mungu ni huruma yake, na huruma “ni jina la pili la upendo” na kwa hakika Mungu ni upendo zaidi ya hayo, tunakumbushwa kwamba, sisi sote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tunashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu mintarafu kazi ya uinjilishaji na uenezaji wa Habari Njema ya Ufalme wa Mungu. Sisi sote tumetumwa na tuna wajibu wa kushughulikia wokovu wetu na wa wenzetu. Kila mmoja kwa nafasi yake na kwa wito wa maisha yake amefanyika kuwa mchungaji pale alipo. Kristo Yesu anatupatia mfano na anatutaka tuige kwake kama vile alivyowafundisha Mitume wake.
Je, tunajitoa kwa dhati kuwaelekeza wengine katika njia ya Mungu? Je, tunajitoa kushibisha njaa na kuzima kiu ya watu wa Mungu. Tunatoa ushuhuda gani wa maisha ambao ni mfano kwa kundi la Mungu? Tumebatizwa na tumetumwa. Tunao wajibu wa kushughulikia wokovu wetu tena kwa hofu na tetemeko. Mwishoni, tunakumbushwa kwamba tutapasika kutoa hesabu au mrejesho wa kazi ambayo tumekabidhiwa kuifanya. Kama walivyofanya Mitume nasi tutawiwa kufanya hivyo. Tutapasika kutoa ripoti ya kazi ambayo Kristo ametukabidhi. Swali la kujiuliza ni Je, tunaitenda kazi hii kadiri ya maagizo ya Kristo Yesu mwenyewe au tunaifanya tunavyotaka sisi tukitafuta maslahi yetu. Kumbuka lazima kutoa hesabu. Basi tuombe neema ya Mungu katika Dominika itutegemeze katika kutimiza wajibu wetu wa kushughulikia wokovu wetu na wa watu wote. Tuwaombee wale ambao katika Kanisa wamepokea utume wa pekee wa kuwa wachungaji wa kundi la Mungu kwa njia ya sakramenti ya daraja ili wapate kuifanya kazi yao kwa uaminifu mkubwa na kulingana na mapenzi ya Kristo mwenyewe na kwa kuiga mfano wake. Wokovu wa watu wa Mungu ni wajibu wa kila mbatizwa. Ninakutakia Dominika njema na Mungu akubariki.