Tafakari Jumapili 17 ya Mwaka B: Uweza wa Mungu katika Ukarimu!
Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.
UTANGULIZI. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 17 ya mwaka B wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani inayoadhimishwa Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Wazee ni amana na utajiri wa jamii, wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii. Wazee wamapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa mwaka 2021 anasema, Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani ni fursa kwa mababu, mabibi na wajukuu wao kudemka kwani maisha yataka matao! Upweke hasi, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; faraja kutoka kwa vijana na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake. Katika Dominika hii dhamira kuu katika Liturujia ya Neno la Mungu yahusu mamlaka na uweza wa kimungu unaojidhihirisha katika matendo ya huruma na wema kwa watu. Masomo yanatutafakarisha ya kwamba mamlaka na uweza wa Mungu haviko katika matumizi ya mabavu na nguvu bali vinajidhihirisha katika matendo mema, matendo ya ukarimu, matendo ya huruma na huduma kwa watu. Watu wanavutwa kwa Mungu kwa njia ya matendo yake ya huruma na upendo kwao. Mungu wetu ni Mungu anayewaleta watu wake pamoja.
TAFAKARI: Katika somo la kwanza 2 Wafalme 4:42–44. Nabii Elisha anashirikisha kwa watu chakula alichopokea kama zawadi na kwa tendo hilo la ukarimu alitendalo Mungu anaweka baraka yake na kudhihirisha uweza wake. Hicho kidogo alichokitoa nabii kinafanywa kuwa kikubwa na chenye kutosheleza mahitaji ya watu. Kwa mikate ishirini anawalisha watu mia moja. Nabii anafanikiwa katika hili kwa sababu anaongozwa na imani katika Mungu asiyeshindwa jambo na pia anaongozwa na nia njema ya kutenda jema kwa watu wa Mungu. Katika Somo la Pili: Waefeso 4:1–6. Mtume Paulo anahimiza umoja uwapasao wana wa Mungu. Huu ni umoja ambao ni tunda la ubatizo walioupokea kwa njia ya imani katika Mungu mmoja aliye Baba wa wote. Aidha, Mtume Paulo anakumbusha ya kwamba kwa njia ya ubatizo wamefanyika kuwa wana wa Mungu wanaoitwa kuwa watakatifu; wamepokea wajibu wa kutekeleza na wanapasika kuenenda kadiri ya wito wao. Ili kuweza kuufikia umoja ambao Mtume Paulo anausisitiza wanapasika kuishi maisha ya fadhila kama vile upendo, ukarimu na upole. Fadhila hizi ni kielelezo cha uwepo, uweza na mamlaka ya Mungu anayefanya kazi kati yao.
Katika Injili Yohane 6:1–15. Yesu anaona huruma kwa watu wake na anatenda muujiza na kuwalisha watu zaidi ya elfu tano akidhihirisha mamlaka yake na uweza wa kimungu. Kile kilichotendwa na nabii Elisha katika Agano la kale kinafanyika tena na Yesu katika Agano jipya kwa kiwango kikubwa zaidi. Yesu anawalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili tu. Muujiza huu mbali na kushibisha njaa ya mwili unawaandaa watu kwa kupokea chakula kinachoshibisha njaa ya kiroho. Anatulisha kwa neno lake na kwa Ekaristi Takatifu ambayo ni uwepo halisi wa Yesu mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai; ni mwili na damu yake Kristo.
KATIKA MAISHA. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, sisi sote ni wahitaji na tunao watu wenye huhitaji ambao wanaishi kati yetu. Tunawiwa kushughulikia mahitaji yao. Tunaiga mfano wa nabii Elisha na kielelezo bora cha upendo na ukarimu kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe ambaye anawaonea watu huruma na kuwalisha chakula. Wako wengi wenye kuhitaji huruma na ukarimu wetu. Ni wajibu wa kikristo kuwahudumia wengine na kuwasaidia katika mahitaji yao. Sisi tulio wafuasi wa Kristo tunapasika kuiga mfano huo wa Kristo mwenyewe ambaye daima hushughulikia mahitaji ya watu wake. Kwa kufanya hivyo tunamshuhudia Kristo na kumfanya awepo katika ya watu wake. Aidha, masomo yetu yanatukumbusha kwamba hakuna kilicho kidogo kwa Mungu. Mungu wetu ni mwenye enzi na muweza wa yote. Anao uwezo wa kugeuza kilicho kidogo na pungufu machoni pa mwanadamu na kukifanya kikubwa na chenye kutosheleza. Anao uwezo wa kukipa thamani kile ambacho ni dhalili. Anao uwezo wa kukiinua kilicho chini na kukiweka mahala pa juu zaidi. Anao uweza wa kukiheshimisha kilichodharaulika. Mikate mitano na samaki wawili ni kidogo machoni pa mwanadamu kuweza kulisha watu zaidi ya elfu tano lakini hicho hicho ni kikubwa sana kwa Mungu asiyeshindwa kitu. Kwa moyo wa shukrani tuwekeze tulivyo navyo kwa Mungu na yeye atavibariki.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunapotafakari ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika hii tunakumbushwa pia juu ya nguvu ya ukarimu. Tendo lako dogo la ukarimu lina uwezo wa kuweka tabasamu katika nyuso za wengine. Furaha yetu inatimia pale ambapo tunakuwa sababu ya furaha kwa wengine. Tusiruhusu uchoyo na ubinafsi vikatuelemea. Tuwe wakarimu na tujenge jumuiya ya kidugu. Mtakatifu Yohane Paulo II anatukumbusha ya kwamba: “Hakuna aliye maskini kiasi cha kushindwa kutoa kitu na wala hakuna aliye tajiri kiasi cha kushindwa kupokea kitu.” Labda tunaweza pia kujiuliza je wakati huu ambapo tunapitia kipindi kigumu wakati ulimwengu mzima unaathiriwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO- 19 ni mema gani tumetafuta kuyatenda kwa wenzetu wakati tunashughulikia hali zetu? Je, tunasaidiana vipi sisi kwa sisi katika kukabiliana na madhira ya tatizo hili? Je, tunashughulikiaje mahitaji ya wale walio wanyonge na dhaifu sana katika jamii zetu? Na kwenye familia zetu je tunaziishi fadhila za kikristo? Ndugu msikilizaji, Dominika hii ni nafasi ya kujitafakari na kuuisha ndani yetu maisha ya fadhila na matendo mema kwa wengine. Ninakutakia Dominika Njema na Mungu akubariki.