Tafakari Jumapili 18 ya Mwaka: Yesu Ni Utimilifu wa Upendo wa Mungu Baba!
Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.
UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 18 ya mwaka B wa Kanisa. Dominika hii inafanya mwendelezo wa dhamira ambayo tuliisikia Dominika iliyopita ya kuwa uweza wa Mungu unajidhihirisha katika matendo ya huruma, upendo, ukarimu na huduma makini kwa watu wake. Katika hali zote Mungu hachoki kamwe kuwatendea wema watu wake. Anatafuta daima kuwaleta pamoja apate kuwakomboa. Mwaliko wanaopewa wana wa Mungu ni kuyatumia mema ya dunia wanayopokea ili kuunganika na kushibana na Mungu mwenyewe. Urafiki wetu na muunganiko wetu na Mungu ni wa thamani kubwa zaidi kuliko wingi wa vitu vizuri tunavyoweza kupokea kutoka kwake. Kristo Yesu anawaalika waja wake kukuza na kudumisha mafungamano pamoja naye kwa njia ya upendo, ili hatimaye, waweze kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kristo Yesu ndiye utimilifu wa upendo wa Baba wa milele, anayeganga njaa ya binadamu na kuzima kiu ya utakatifu wa maisha!
TAFAKARI: Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka, (Kutoka 16:2–4, 12-15) mkutano mzima wa watu unawalalamikia Musa na Aroni kwa sababu wana njaa. Wanatamani wangalibaki watumwa na kuwa na wingi wa masufuria ya nyama kuliko uhuru ambao wameupata kwa mkono wa Mungu. Lakini pamoja na manung’uniko haya na mengine yaliyokuja baadae wema wa Mungu haukomi kwao. Mungu anabaki kuwa Mungu mwenye kuwapenda na kuwatendea wema watu wake. Anadhihirisha uweza wake katika matendo ya wema na ukarimu; ananyesha kutoka mbinguni mvua ya mikate na anawapatia nyama ili watu wapate kula. Naye Mungu anatenda haya akitazamia kuwa watu hawa wataenenda katisha sheria yake. Kunyesha mikate na kuwapa watu nyama ni jambo dogo sana kwa Mungu. Anachotaka ni kujenga urafiki na muunganiko nao. Badala ya kushikamana na vitu wanaaitwa kujenga urafiki na Mungu. Mtume Paulo katika Somo la pili (Waefeso 4:17, 20–24) anaendelea kuwambukusha Waefeso juu ya wito mkuu walioitiwa yaani utakatifu. Anawaonya dhidi ya tamaa zenye kudanganya na anawaasa wauvue utu wa kale na kuuvaa utu mpya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kwa maneno mengine Paulo Mtume anawaambia ya kwamba, imani waliyoipokea lazima ichochee: toba na wongofu wa ndani, ilete mabadiliko ndani yao na kunuia mambo yaliyo mema. Na hivyo, hawapaswi kubaki katika mwenendo wa zamani bali mwenendo mpya ambao unadai urafiki na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Neema wanayoipokea kutoka kwa Mungu haipaswi kupotea bure kama umande wa asubuhi!
Katika Injili Yohane (Yn 6:24–35) mkutano unamtafuta Yesu kwa sababu waliona ishara alizozitenda na jinsi alivyowalisha watu wengi kwa kubariki mikate mitano na samaki wawili, watu wakala na kushiba na hatimaye, kukusanya masalia ya vikapu kumi na viwili. Yesu anatumia nafasi hii kuwafungua macho wapate kuona mbali zaidi na kutamani kilicho bora zaidi. Anataka kuilekeza mioyo yao katika kuutafuta uzima wa roho zao na kuujenga urafiki na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Hivyo badala ya kukazia chakula kinachoshibisha mwili anawaalika kukifanyia kazi chakula kinacholeta uzima wa roho. Yesu anatumia fursa hii kuanza mafundisho juu ya Ekaristi Takatifu. Anaweka wazi kwamba yeye ndiye chakula cha uzima na anawaalika waende kwake. Anawapa mwaliko wa kujenga urafiki na muunganiko wa daima naye. “Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho!” Yn 6:33-39.
KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican sisi nasi ni watafutaji. Kila mmoja wetu anayo mahitaji katika maisha yake na angetamani ajitosheleze katika hayo. Lakini katika kutafuta lazima tukumbuke kuwa na hierakia ya thamani, yaani lazima tujue mambo gani ni ya muhimu na ya lazima, mambo gani ya muhimu lakini si ya lazima, na mambo gani si ya muhimu na wala si ya lazima. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuamua vizuri ni katika mambo gani tunawekeza akili, moyo, nguvu na muda tulio nao kuyatafuta. Hii ndio siri kubwa ya kufanikiwa katika jambo lolote. Tunapojiruhusu kuwa na hierakia ya thamani tunaepuka kutawanya nguvu zetu na tunajielekeza katika jambo moja lenye kuweza kuzaa matunda. Masomo ya Dominika hii yanatukumbusha ya kuwa maisha ni zaidi ya kula na kunywa. Ni wazi kuwa tunahitaji chakula cha mwili lakini tunahitaji zaidi kuwa warithi wa ufalme wa Mungu. Mtume Paulo katika waraka kwa Warumi anatukumbusha ya kuwa “Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.” (Rum 14:17). Kushusha mvua ya mikate ni jambo dogo sana kwa Mungu, na hilo halina uzito na umuhimu sana ukilinganisha na wokovu wa roho zetu.
Aidha, katika Dominika hii tunakumbushwa ya kuwa mema yote tuliyo nayo yatoka kwa Mwenyezi Mungu (Yakobo 1:17). Hivyo basi tunapoweka juhudi na tunapotafuta mahitaji yetu tunapaswa kukumbuka kumshirikisha Mungu katika hayo tunayoyatenda na tunapofanikiwa tutafute kumwona Mungu katika mafanikio yetu. Mara nyingine tunajisahau; tunakuwa wepesi wa kulalamika tunapokosa na tunasahau kushukuru tunapopata au kwa yale tuliyokwisha kupata. Tunakuwa wepesi wa kudai kuliko kuwa wepesi wa kushukuru. Tunataka kuongeza maradufu vitu tulivyo navyo na tunasahau kushukuru kwa vile tulivyokiwsha kupokea. Mkutano unawalalamikia Musa na Aroni kwa kidogo walichokosa na unasahau kushukuru kwa kikubwa walichopokea. Moyo usio na shukrani hukausha mema yote. Tujifunze kuwa watu wa shukrani maana kwa kushukuru tunajivunia baraka juu ya baraka. Na zaidi ya hayo tutatufe kumwona Mungu katika kila hali. Mungu yu nasi daima na hatuachi kamwe. Tuanze na yeye na tumalize naye.