Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 tya Mwaka B wa Kanisa: Furaha ya Uinjilishaji na Umuhimu wa Mapumziko ya Kazi. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 tya Mwaka B wa Kanisa: Furaha ya Uinjilishaji na Umuhimu wa Mapumziko ya Kazi. 

Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka B wa Kanisa: Furaha ya Uinjilishaji

Ni muhimu kila mara kurudi na kukaa miguuni pa Yesu, kujifunza tena ili tuweze sote kutoka na nguvu na ari mpya ya kueneza Neno lake duniani kote. Ni mwaliko kila siku kutenga muda wa kukaa miguuni pake, kujifunza kutoka shule yake, ndio kulisoma Neno lake kwa kutafakari na hata kukaa naye kwa ukimya na tafakari mbele ya Yesu wa Ekaristi na hatimaye, kuyamwilisha yote!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya leo linataja mara mbili maneno; faragha, mahali pasipokuwa na watu! Kwa haraka haraka inatuwia vigumu kwa nini Mwinjili Marko anakazia juu ya faragha na mahali pasipokuwa na watu, na wakati huo huo tunajua utume wa Yesu Kristo ni kuutangaza na kuusimika ufalme wa Mungu kati ya watu. Ni mara baada ya wanafunzi wake kurejea katika utume wao ule wa mwanzoni kabisa wa kutoka na kwenda kama tulivyosikia katika Injili ya Dominika iliyopita, leo wanakusanyika mbele ya Yesu, wanamzunguka Bwana na Mwalimu wao. Anayefanyakazi ana haki ya kupata wasaa pia ya kupumzika kama anavyoonesha Mtume Paulo kuwa kazi ya uinjilishaji si kazi nyepesi hata kidogo. (2Wakorintho 11:23) “Wao ni watumishi wa Kristo? Nasema kiwazimu, mimi ni mtumishi wa Kristo kupita wao, maana nilivumulia taabu nyingi zaidi, nilitupwa gerezani mara nyingi zaidi, nilipigwa kupita kiasi, nilikuwa katika hatari ya kufa mara nyingi.”

Ni katika muktadha huo basi, hata Yesu anaona ulazima wa kuwapa nafasi ya kupumzika, lakini sio mapumziko ya kwenda kulala na kula starehe, bali ni yale ambayo leo tungeweza kuyaita ni fursa ya kukaa na mwalimu wao kwa karibu zaidi, kumshirikisha Yesu kile walichotumwa kufanya, ni kufanya tathmini pamoja na Mwalimu wao. Ni kuangalia wapi walikosea na wapi walienenda kadiri ya Mwalimu wao, ndio fursa ya kupumzika miguuni na pamoja na Bwana na Mwalimu wao. Ni Yesu mwenyewe anayechukua usukani sasa wa kuwahubiri na kuwafundisha tena. Leo tunaishi katika ulimwengu ambapo ukimya ni bidhaa adimu kabisa, katika ulimwengu wa kidigitali, ulimwengu leo upo kiganjani mwa kila mmoja mwenye vifaa vya kisasa vya kielektroniki. Ni ulimwengu ambapo ukimya na faragha imekuwa ni ngumu kuvipata. Ndio uhalisia wa ulimwengu tunaoishi wengi wetu, ni nadra sana kupata wasaa na fursa ya kukaa faragha pamoja na Yesu mwenyewe aliye Bwana na Mwalimu wetu. Leo watu wengi ulimwenguni wamejikuta katika urahimu wa matumizi ya vyombo vya mawasiliano vya kisasa na mitandao ya kijamii.

Wengi wetu leo tumekuwa watumwa wa matumizi yaliyopitiliza ya simu au kompyuta au vifaa vya aina hiyo. Sehemu ya kwanza ya somo la Injili ya leo, tunaona Mitume wanarejea kutoka utume wao, na wanakusanyika wote wakimzunguka Yesu na hapo wanampa mshindo nyuma au mrejesho wa utume ule wa uinjilishaji. Ni mara baada ya Yesu kupokea mirejesho yao ya utume, anawaalika kwenda faraghani, sehemu isiyokuwa na watu. Katika Injili ya Marko, tunaona mara kadhaa Yesu akijitenga na wanafunzi wake wa karibu na hapo mara zote tunaona Yesu anatumia fursa hii kuwafunulia mengi zaidi na kuwafundisha. “Pasipo mifano hakusema nao. Lakini walipokuwa peke yao, aliwaeleza wafuasi wake yote” (Marko 4:34) Mara baada ya kumponya bubu-kiziwi alimtenga na watu. (Marko 7:33). Aliwachukua Petro na Yakobo na Yohane, akawapeleka juu ya mlima mrefu wawe peke yao. (Marko 9:2). Pia mitume watatu, Petro, Yakobo na Yohane walimuuliza kwa faragha juu ya mwanzo wa mwisho. (Marko 13:3). Na hata waliposhindwa kumponya mwenye pepo wanafunzi wake walimuuliza akiwa faragha. (Marko 9:28) Hivyo faraghani ni nafasi ambayo tunaona Yesu amefanya na hata kuwafundisha mengi.

Kama nilivyotangulia kusema hapo juu kuwa neno faragha, mahali pasipokuwa na watu limetumika mara mbili katika somo la Injili yetu la leo. Yesu anawaalika kuingia chomboni, ndio kusema faragha ya kweli sio mbali na jumuiya bali ndani ya jumuiya yake Kristo, yaani Kanisa na katika uwepo wake yeye mwenyewe. Mahali pasipokuwa na watu sio kujitenga tu kimwili na wengine bali kuingia katika muunganiko wa kweli na wengine kwa kukaa miguuni mwa Yesu. Ni kuingia katika muunganiko na Mungu, ni fursa na wasaa wa kusali. Yafaa kutambua kuwa kazi ya Uinjilishaji ni tofauti na kazi nyingine ambazo mwanadamu anaweza kuzifanya katika maisha yake. Kazi ya uinjilishaji kama tulivyosikia katika Injili ya Dominika iliyopita sio ya mwanadamu bali ni ya Yesu Kristo mwenyewe, ni ya Mungu na hivyo kila mara lazima kujitathmini na hasa kuchota nguvu ya kusonga mbele zaidi kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, ndio maana Yesu anawaalika leo baada ya misheni yao ile ya mwanzo kukaa miguuni mwake. Ni muhimu kila mara kurudi na kukaa miguuni pa Yesu, kujifunza tena ili tuweze sote kutoka na nguvu na ari mpya ya kueneza Neno lake duniani kote. Ni mwaliko kila siku kutenga muda wa kukaa miguuni mwake, kujifunza kutoka shule yake, ndio kulisoma Neno lake kwa kutafakari na hata kukaa naye kwa ukimya na tafakari mbele ya Yesu wa Ekaristi.

Uinjilishaji wa kweli unaanzia daima kwa Yesu mwenyewe na ili uweze kusonga mbele hatuna budi kila mara kurudi kwake ili tupate nafasi ya kujifunza tena na tena na kuchota nguvu ya kusonga mbele. Kuna kishawishi cha hatari kabisa cha wahubiri wa Injili kuishia kama wanaharakati wa kijamii kwa kukosa kujua ni wapi wanapaswa kujifunza na nani wanapaswa kufanya tathmini naye. Injili ya leo inatukumbusha sisi sote kama kweli tunataka kuwa wainjilishaji wa kweli, hatuna budi kutambua umuhimu na ulazima wa kurejea na kupumzika pamoja na Yesu mwenyewe, ni muhimu kusaka nafasi iwe katika familia zetu, makanisani na popote pale za kukaa pamoja na Yesu, na hasa kwa njia ya Neno lake na pia mbele ya Yesu wa Ekaristi Takatifu. Uinjilishaji wa kweli ni tunda la maisha ya sala. Hivyo kila mmoja wetu ili kuweza kutimiza wajibu wetu kama wabatizwa tunaalikwa leo kuwa watu wa sala. Kusali ni kukaa na kuzungumza pamoja na Yesu, ni kumshirikisha yote kuhusu maisha yangu na yako, hata madhaifu na mapungufu yetu, ni nafasi pia ya kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa pamoja naye, ni kukaa miguuni mwake na kuegama kifuani mwake, ni kumsikiliza pia ili tujue nini cha kufanya na kwa jinsi gani tunapaswa kutumiza utume wetu.

Uinjilishaji unageuka mkavu na hata hatarishi pale unapokosa kuwa ni matunda ya sala. Ni vema leo kukumbuka umuhimu wa kuwa watu wa sala, sala sio maneno yangu mbele ya Mungu bali ni upendo wangu kwake, ni kujaribu kuonja pia upendo wa Mungu kwetu, upendo usio na mfano. Kusali narudia ni kitendo cha upendo daima! Ni hapo Yesu anatualika kukaa naye faraghani, mahali pasipokuwa na watu, ni mahali ambapo tunaonja upendo kana kwamba ni mimi peke yangu tu ndiye ninayependwa na Mungu, ni hapo kila mmoja anaonja upekee wake mbele ya Mungu. Hatuwezi kuwa wajumbe wa upendo na huruma ya Mungu kama nasi haturudi na kuchota miguuni mwake huruma na upendo, kwani uinjilishaji ni kuwapelekea na kuwashirikisha wengine Habari njema, yaani upendo na huruma ya Mungu kwao. Kama tulivyoona hapo juu, leo tunaishi katika ulimwengu wenye makelele mengi na ya kila aina, ni ulimwengu unaokosa faragha, ni ulimwengu tunaouita kijiji kikubwa, kila mmoja anakutana na kila mmoja lakini pasipo kujali mahusiano ya upendo. Ni ulimwengu wenye ukame wa upendo wa kweli, ukame wa ukimya na faragha. Hatuna budi sisi wanafunzi na rafiki zake Yesu Kristo kuwa walimu wa faragha na ukimya, kuwa walimu wa maisha ya sala kwa wale wanaotuzunguka, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu, parokia zetu, mahali pakazi na kadhalika na kadhalika.

Mwanafalsafa Peter Kreeft katika Kitabu chake cha “Three Philosophies of Life” anasema; “But we need to hear that silence. We need it more than anything else in the world. Kierkegaard wrote, ‘If I would prescribe just one remedy for all the ills of the modern world, I would prescribe silence. For even if the word of God were proclaimed in the modern world, no one would hear it; there is too much noise. Therefore, create silence” Ndio ulimwengu wetu wa leo ambao kwa hakika umepungukiwa na jambo moja muhimu nalo ni faragha, ukimya, kuwa katika utulivu wa kuweza kuongea na kusikiliza ujumbe wa Mungu kwetu. Ni hitataji la muhimu na ndio leo Yesu Kristo anatualika sisi sote kuwa na wasaa wa kwenda faragha, ili hapo tuweze kuongea naye, tuweze kuimarisha mahusiano yetu naye na zaidi tuweze kujifunza na kupata nguvu za kuwa mashahidi wa Habari njema ya wokovu kwa watu wote. Mapumziko ya Yesu pamoja na wanafunzi wake tunaona hayadumu kwa muda mrefu, kwani ni mwendo wa kuvuka tu ziwa lile la Galilaya.  Sehemu ya pili ya Injili ya leo, Yesu anakutana tena na makutano. “Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia” Mwinjili Marko anatumia neno la Kigiriki “splagknizomai”, ndio kusema ni ile hisia kali kabisa anayokuwa nayo Yesu ya ndani kabisa, hisia ya upendo wa Kimungu kwa mwanadamu, ni hisia kuzidi hata upendo ule wa mama kwa mtoto wake, sio hisia ya nje nje au ya juu juu tu bali ni ya ndani kabisa. Ni hisia ya upendo na huruma ya Kimungu kwa mwanadamu, ni upendo usiokuwa na masharti, upendo mkamilifu na wa kweli kabisa.

Mwinjili Marko anatuonesha pia nafasi nyingine ambapo Yesu alikuwa na hisia kama hii ya Injili ya leo. Pale mkoma alipomwomba Yesu amtakase. (Marko 1:40-41). Pia Yesu alihurumia umati uliokuwa na njaa na hata kufanya muujiza wa kuongeza mikate. (Marko 8:2). Hi indio sura halisi ya Mungu anayetufunulia Bwana wetu Yesu Kristo kwa kila mmoja wetu anayekuwa katika hali duni na ya mateso makubwa, hali ya kuwa mbali na Mungu, hali ya kukosa machungo mazuri. Mwinjili Marko anatuonesha kuwa mchungaji wa kweli ni Yesu Kristo mwenyewe, anayewaona mkutano mkuu na kuwahurumia, kuwa na hisia kali ya upendo na huruma kwao. Ndio kusema kazi ya Uinjilishaji ni kazi ya Yesu mwenyewe na daima kila anayetaka kushiriki kazi au utume huo hana budi kusukumwa na huruma na upendo huu wa Kimungu. Ni kuwaangalia watu wa Mungu na kuwahurumia, kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu kwao. Ni kuwa daraja kati yao na Mungu ili waweze kuonja huruma na upendo wake. Kila anayetaka kushiriki utume huo anakubali kuwa daraja la huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Ni kwangu na kwako wengine wanapaswa kukutana na huruma ya Yesu Kristo mwenyewe na si vinginevyo. Kiu na njaa ya watu wengi leo ulimwengu ni kukutana na sura ya kweli ya Mungu, yaani upendo na huruma yake. Yesu anawahurumia na anabaki nao na kuwafundisha mambo mengi. Sifa ya kwanza ya mjumbe wa Injili au muinjilishaji ni upendo na huruma ya Mungu kwa watu anaowahudumia na kuwatumikia. Nitawakie Dominika na tafakuri njema.

                                     

15 July 2021, 15:14