Tafakari Jumapili 14 ya Mwaka B wa Kanisa: Kashfa ya Kristo Yesu
Na Padre Gaston George Mkude, -Roma
Amani na Salama! Mcheza kwao utunzwa! Ni msemo wa Wahenga wa Kiswahili kutuonesha kuwa mtu anakubalika na kupokelewa vema anapocheza nyumbani kwao, ni hapo anapata watu wa kumshangilia na hata kumtia moyo katika lile analolifanya au kulitenda. Hii ni kawaida sana hasa katika uwanda wa michezo mbalimbali duniani. Lakini hata katika maisha ya kawaida inategemewa mmoja kutiwa moyo na watu wa kwao au kwake, lakini katika somo la Injili ya leo, tunaona msemo huu hauna nafasi. Yesu leo anacheza kwao, ndio kusema anafundisha na hata kutenda miujiza nyumbani kwao, katika nchi ya kwao. Mwinjili katika sehemu ya kwanza si tu anatuonesha mahali alipo Yesu, yaani katika nchi yao, bali pia alifundisha katika Sinagogi siku ya Sabato, na hata waliomsikiliza au hadhira yake walipomsikia walibaki na mshangao mkubwa, na walijiuliza, huyu ameyapata wapi haya? Pamoja na kuwa na mshangao mwanzoni, tunaona hali ile haidumu sana kwani mwinjili Marko anatuonesha pia watu wale wale walijikwaa.
Kujikwaa ni neno zuri kabisa linalotumika katika Somo la Injili ya leo, kwani linakaribiana kabisa na maana kusudiwa tangu awali. Mwinjili Marko anatumia neno la Kigiriki “skandalon”, ndio jiwe linakuwa njiani na kumsababisha mpita njia au msafiri kujikwaa. Ni kikwazo au makwazo kwa lugha rahisi na inayoeleweka na wengi. Ni jambo au kitu kinachomfanya mtu kupoteza imani yake, ni kitu kinachomtoa mtu katika mstari au msimamo wake, ni mtanziko katika maisha. Kwa kweli tunaposoma na hata kutafakari somo la Injili ya leo, tunabaki na maswali mengi, kwanza kwa nini walijikwaa kwa Yesu badala ya kuona fahari kuwa hata kati yao yao watu waliodharaurika kati ya Wayahudi kuwa ametokea mwalimu mwenye uwezo hata wa kutenda miujiza. (Yohane 1:46) Natanieli alihoji Je, kitu chema kinaweza kutoka Nazareti? Na hata Yesu tunaona mwinjili Marko anamalizia sehemu ya Injili ya leo akionesha pia mshangao kwa upande wa Yesu: “Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.” Yesu anashangaa hata kama kabla anasema pia; “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.”
Yafaa katika kutafakari sababu zilizowapelekea watu wa nchi yake kujikwaa au kukwazika, kuangalia pia nafasi ya Yesu katika jamii ile. Ndio kusema kwa maneno mengine, mwinjili Marko anataka tuangalie kwa kutafakari zaidi kitambulisho au “CV” ya Yesu. Yesu hakuwa msomi kwa maana ya elimu ya enzi zile, na wala hakutokea katika familia yenye sifa za kipekee au ya daraja au hadhi ya juu kijamii. Hivyo tunaweza kuona japo sababu ya wao pamoja na kustaajabu uwezo wake wa kufundisha na kuponya, bado walikuwa na haki ya kubaki na maswali na hata mwishoni kujikwaa kwake. Watu wa nchi wake, si tu walimfahamu vema Yesu bali hata tunaona wanajaribu kutuonesha “CV” ya Yesu akitanabaishwa pamoja na mama yake, na ndugu zake wengine na hata wanawataja kwa majina, kutuonesha wanamzungumzia mtu wanayemfahamu vema kabisa pasi na mashaka yeyote.
Huyu si yule Seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simon? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Mwinjili Marko anatumia neno la Kigiriki “teknon”, kuonesha aina ya kazi aliyokuwa anaifanya Yesu, ndio kusema si tu kazi yake bali kitu pekee walikuwa na hakika nacho kuwa Yesu alifahamu ni kazi yake hiyo ya kutumia mikono, ambayo leo wengi wanaitambua kama Useremala, lakini maana hasa ya neno hilo ingeweza kuwa kazi nyingine yeyote ile ya kutumia nguvu na mikono. Ndio kusema kazi ya hadhi na hali ya chini, sio kazi ya maana sana si tu nyakati za Yesu bali hata katika ulimwengu wa leo. Leo kazi ya maana sio tena ya kutumia nguvu bali akili na ujuzi na utaalamu zaidi. Wanamtambua Yesu sio tu kwa majina yake bali kwa kazi yake, ndio kusema mbele ya macho yao alikuwa ni mtu wa hadhi ya chini kabisa, asiyekuwa na elimu wala ujuzi wa pekee bali alifanyakazi ya mikono na nguvu zaidi.
Wanamtaja hata na mama yake pamoja na ndugu zake, ni familia iliyofahamika na kujulikana vema na wengi katika nchi ile. Kwa wayahudi tunaposikia kaka na dada zake kwa kweli ni karibu sawa na familia zetu za Kiafrika. Kaka na dada sio lazima wale wa kuzaliwa pamoja bali wanaweza kuwa hata binamu, au watoto wa mama au baba mdogo/mkubwa. Hivyo mwinjili anapotutajia hata na majina yao ndio kusema familia yake Yesu ilijulikana vema kuwa ni familia ya aina gani na ndio maana watu wale wanabaki na mshangao na hata kujikwaa kwa Yesu, ndio kukwazika. Lakini hata tunabaki na maswali zaidi kuhusu kujikwaa kwa hawa watu wa nyumbani au nchini kwake, Kapernaumu Yesu aliiingia katika mgogoro na viongozi wa kidini na kisiasa lakini leo na watu wa kawaida kabisa. Yesu baada ya kuzunguka kwa miezi kadhaa katika nchi ya ugeni kule Kapernaumu na hata katika Galilaya, akihubiri Injili na hata kuponya wenye magonjwa mbalimbali, sasa anarejea katika nchi yake mwenyewe, ndio kijijini kwake Nazareti.
Mwanzoni tunaona hata ndugu zake wa familia walijaribu kumshawishi na hata kumkamata kwa nguvu ili aweze kurejea katika maisha yake ya awali, ndio maisha ya kuendelea na kazi yake ya useremala. (Marko 3:31-35). Ni hapo Yesu anatambulisha familia na ndugu zake, kuwa ni wale wanaosikiliza Neno lake na kutimiza mapenzi ya Mungu. Leo tunaona anarejea mwenyewe kijijini kwao, sio kwa kulazimishwa na ndugu au jamaa zake bali kwa hiari yake mwenyewe, na safari hii anarejea nyumbani akiambatana na kikundi cha wanafunzi wake wa kwanza. Hivyo tunaweza kuona nia ya safari yake sio ya kifamilia, yaani kurejea ili kuwaona na kusalimia mama na kaka na dada zake, bali anarejea akiwa na nia ya kutimiza utume wake wa kuutangaza na kuuneza Ufalme wa Mungu. Anarejea kuja kuitambulisha rasmi familia yake mpya, ndio ile inayoundwa na wale wote wanaokuwa tayari kulisikiliza na kulipokea Neno lake; ndio wale walioacha nyavu zao, baba na hata wafanyazi nyuma yao ili kumfuata Yesu. (Marko 1:16-20), wakaacha kazi zao za awali na maisha yao ili kuwa wafuasi wake. (Marko 2:13)
Watu wale hawakujikwaa kwa Yesu mara baada ya kuwasili kwake, bali ilipofika siku ile ya Sabato. Ndio kusema hakukuwa na makwazo yeyote Yesu alipobaki katika mazingira ya familia yake ya mwanzo, yaani akishika na kuenenda kadiri ya mapokeo yao ya kiimani na kidini. Lakini wanajikwaa mara pale anapowaalika kubadili namna zao za awali, mapokeo na tamaduni zao nyingine nyingi za kidini na kiimani na kuwa na vichwa vipya na kuingia katika familia mpya, ndio familia ya wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo. Watu wale pamoja na kustaajabia mafundisho na miujiza aliyoitenda huko, lakini bado walibaki na maswali mengi vichwani mwao yaliyotokana na utambulisho wa Yesu, ndio leo naomba tuiite “CV”, au Kitambulisho cha Yesu. Kwao Yesu alipaswa kuwa ni mmoja wao, ni yule wanayemfahamu vema na vizuri lakini iweje leo anajitambulisha kwa “CV” tofauti, kwa nini leo anafundisha na kutenda kinyume na “CV” yake, kinyume na ujuzi na utaalamu wake walioufahamu kabla?
Yesu akiwa Kapernaumu anamponya mlemavu, aliyeletwa akibebwa na watu wanne, na kwa sababu ya msongamano makubwa wa watu ikiwapasa kuezua dari kwa juu ili wamteremshe mahali aliposimama Yesu. Mwinjili Marko kwa kitendo kile anatuonesha kuwa nyumba ya Israeli, yaani dini na mapokeo yao lazima kuezuliwa, lazima kuruhusu kuingia hata wale waliokuwa hawana nafasi kijamii na kidini, wale wote waliojisikia kutengwa na kusetwa na jamii. Na ndio tunaona Yesu akila na wadhambi, akiwagusa wakoma na kuwatakasa, na kuwafanya wote hawa kuingia katika familia yake mpya, katika nyumba yake mpya. (Marko 2:15-17 na 1:41). Ndio kusema lango lile la nyumba ya Israeli, Yesu amekuja na kulifungua kwa watu wote na sio tu kwa Wanawaisraeli, na hii inakuwa ni jiwe la kujikwaa kwa hata watu wa kijiji chake cha Nazareti. Ni katika muktadha huu tunaona watu wa nchi yake wanashindwa kumwelewa Yesu na hivyo kugeuka kuwa jiwe la kujikwaa kwao. Wanajisikia kusalitiwa na hata kuangushwa na kijana aliyekulia katika kijiji chao, kijana ambaye alirithishwa mapokeo ya dini na imani yao ya Kiyahudi. Leo Yesu anawaalika kuingia katika familia yake mpya, katika nyumba yake mpya, ndio ya wale wanaokuwa tayari kubadili vichwa vyao na kuanza kufuata mantiki na aina mpya ya maisha na mtazamo, ni kuwa na mwelekeo mpya kinyume na tofauti kabisa na ule waliouzoea wa kimapokeo.
Na ni hapo tunaona wanakuwa na maswali mengi juu ya Yesu na mwaliko wake. Si huyu mseremala, mwana wa Maria. Ni wapi anatoa mafundisho haya na uwezo wa kuponya pia unatoka wapi? Mashaka yao sio mafundisho yak eau miujiza bali ni nini chanzo cha mafundisho yale na uwezo ule wa ajabu wa kuponya? Ni kwa kukosa majibu ya maswali yao wanaona uamuzi sahihi ni kuacha kumsikiliza na kumwamini, hivyo kwao Yesu anakuwa ni jiwe la kujikwaa au “skandalon”, “Scandal”. Na ndio tunaona hata Yesu naye anakwazika na kutokuamini kwao, kuona hata watu wa nyumbani kwao wanashindwa kulipokea Neno lake, kushindwa kumpokea na kumkubali kuwa kweli ni Mwana wa Mungu. Wanakosa imani kwa Yesu, kwani kwao Yesu waliishia kumwona ni kijana au mtoto waliyemfahamu kwani amekua wakimuona na kumfahamu yeye pamoja na wazazi na hata ndugu na jamaa zake. Kwao Yesu ni mwanakijiji tu mwenzao, ni mmoja kati yao hivyo hapaswi kuwaalika katika familia yake mpya, kwani kwao familia ya Yesu ni ile aliyozaliwa na kukulia. Yesu pia anatualika nasi leo, kubadili vichwa, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, ni kwa namna hiyo kwa kulisikiliza na kulishika Neno lake, tunaingia katika familia yake na nyumba yake, ni kwa kukubali kuwa watu wapya, hapo tunakuwa kweli watu wa imani, maisha yetu kila siku hayana budi kubadilishwa na Neno lake tunalolisikia na kulisoma. Ukristo ni safari ya kutaka kufanana na Yesu mwenyewe, kwa kulipokea Neno lake na kuyafananisha maisha yetu na Neno lake. Niwatakie Dominika na tafakari njema.