Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 15 ya Mwaka B wa Kanisa. Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 15 ya Mwaka B wa Kanisa. Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. 

Tafakari Jumapili 15 ya Mwaka B wa Kanisa: Injili ya Matumaini!

Ujumbe wa Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Mwaka B ni imani na matumaini: Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni tumaini na tegemeo letu maana tu wateule wake hata kabla ya kuumbwa ulimwengu. Hivyo, tumtegemee yeye katika maisha yetu tukiziendea ahadi alizotupatia yaani kuurithi uzima wa milele. Kanisa linatumwa kutangaza na kuwaponya wanaosetwa!

Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 15 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii ni Mungu ni tumaini na tegemeo letu maana tu wateule wake hata kabla ya kuumbwa ulimwengu. Hivyo, tumtegemee yeye katika maisha yetu tukiziendea ahadi alizotupatia yaani kuurithi uzima wa milele. Somo la kwanza ni kutoka kitabu cha nabii Amosi (7:12-15). Ili kuulewa vyema ujumbe wake ni vyema kurejea mazingira yaliyopelekea ujumbe huu kutolewa. Baada ya kifo cha Mfalme Solomoni mwanae Rehoboamo akawa mfalme. Lakini  ni makabila mawili tu yaliyomtamua kama mfalme na yakabaiki kwake, makabila mengine 10  yaliunda ufalme wao tofauti. Kwa hiyo kukawa na falme mbili: Ufalme wa Yuda/Kusini chini ya Rehoboamo ukiwa na makabila mawili na mji wake mkuu ulikuwa ni Yerusalem. Ufalme wa Israeli/Kaskazini ukiwa na makabila 10 na mji wake mkuu ni Samaria. Falme hizi mbili daima ziligombana. Vita vilinukia kila wakati. Hata hivyo wakati wote Yerusalemu ilibaki kuwa ni kitovu cha ibada kwa falme zote mbili.

Lakini Mfalme wa Israeli upande wa kaskazini aliona kuwa watu wake kuendelea kwenda kuabudu Yerusalemu makao makuu ya ufalme wa Yuda upande wa kusini ni hatari kwa ufalme wake hivyo alijenga hekalu Betheli ili watu wa ufalme wake waabudu huko. Betheli maana yake ni Nyumba ya Mungu/mahali patakatifu pa ibada. Ibrahimu aliabudu pale alipofika nchi ya ahadi (Mwa 12:8). Yakobo aliabudu pale alipokuwa anamkimbia ndugu yake Essau (Mwa 28: 18). Yakobo aliabudu pale alipokuwa na familia yake akirudi nyumbani baada ya kupatanishwa na ndugu yake Essau (Mwa 35:3, 6). Kumbe Betheli ikawa mahali patakatifu kwa ajili ya ibada kwa makabila 10 ya Kaskazini. Makuhani katika Hekalu la Betheli walilipwa na Mfalme. Amazia Kuhani alikuwa mmoja wapo. Makuhani na Manabii hawa walikuwa ni wa uongo na matapeli maana walilifanya hekalu lao la Betheli kuwa mradi wao wa kujitajirisha. Mungu alimchagua Amosi kutoka Ufalme wa Yuda/kusini, na kumteua awe mhubiri katika Ufalme wa Israeli/kaskazini. Akiwa mtii kwa Mungu, Amosi hakusita kwenda katika Hekalu la Betheli.

Huko Amos alipata shida mbili. Kwanza alikuwa mgeni, mtu wa nje kutoka ufalme wa Yuda. Israeli ilikuwa katika kipindi cha mpito cha usitawi, kwa hiyo watu wake na viongozi hawakuwa tayari kuwasikiliza manabii waliotishia kwamba adhabu inakuja au majanga kutoka kwa Mungu. Makuhani walipingana na Amosi, kwa sababu waliona kibarua chao kiko hatarini. Ndiyo maana Amazia anamshambulia Amosi akimwambia; Wewe ni mgeni, ondoka hapa, kama una njaa katafute chakula kwa mfalme wako katika nchi yako, huna haki ya kuhubiri ugenini pasipo kuwa na ridhaa yetu; “Ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Amosi anamjibu kuwa yeye ametumwa na Mungu akisema; “Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.”

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (1:3-14); ni utenzi wa Mtume Paulo akimshukuru Mungu kwa sababu: Mungu alimtuma mwanae kwetu akatupasha habari za wokovu. Mungu ametutakasa kutoka dhambini kwa sakramenti ya ubatizo kwa zawadi ya Roho Mtakatifu anayetufanya kuwa wana na warithi wa uzima pamoja na Kristo. Kwa kutuwezesha kushiriki uzima huo tena tungali hapa duniani na baadaye katika ukamilifu wake huko mbinguni. Kwa zawadi ya wajumbe wake yaani, maaskofu, mapadre, watawa na makatekista ambao daima hawachoki kutushawishi kuijongea meza ya Bwana kwa njia ya Neno na Ekaristi Takatifu. Daima wanawajibika kutuonesha ile njia ya wokovu. Somo hili laonyesha pia aina sita za baraka itokayo kwa Mungu: wito wa wateule kushiriki uzima wa wenye heri, hali ya watu katika kufanywa watoto wa Mungu, wokovu ulioletwa na Kristo msalabani, ufunuo wa siri ya mapenzi ya Mungu, uteule wa Israeli na mwito wa wapagani wapate pia kushiriki wokovu.

Injili ilivyoandikwa na Marko (6:7-13) ni simulizi la kuitwa na kutumwa kwa Thenashara/mitume 12 wa Yesu. Mitume ndio msingi na nguzo za mafundisho ya Kanisa kwani wao ndio waliojifunza yote walioliachia kanisa kutoka kwa Yesu mwenyewe. Katika kuwatuma mitume, Yesu aliwapa uwezo wa kutenda miujiza kulikoambatana na kuhubiri Injili kwa watu wote. Katika kuwatuma Yesu alisisitiza mambo matatu katika kuenenda kwao; Kutangaza kuwa ufalme wa Mungu umekaribia, kuwaalika watu wafanye toba na kuachana dhambi, na kuukumbatia ufalme wa upendo wa Mungu. Katika utume wao, wasifungamane na watu au vitu. Katika hili anawaambia kwamba wasichukue mkate, wala fedha, nguo wala chochote, wamtegemee Mungu. Wanaalikwa kuwajali wagonjwa kwa namna ya pekee, wakiwaponya katika shida zao.

Maagizo haya ya Yesu ni fundisho kwetu kwamba; Mungu ndiye anayemchagua mhubiri wa Injili. Alimchagua Amosi, mchungaji asiyejua kusoma wala kuandika. Aliwachagua mitume, wavuvi na watoza ushuru, watu walioonekana kutokuwa na elimu au sifa nzuri katika jamii. Hakuwachagua matajiri na wasomi, ili hekima yake ing’ae katika utendaji wa wanyonge. Mtu asifanye kazi ya kuhubiri kama mradi au ajira ili apate kuishi. Mapadre na makatekista wetu ni wahudumu na siyo waajiriwa. Hata hivyo mtumishi anastahili posho yake. Ni wajibu wa wale wanaopokea huduma yao kuwategemeza ili nao waishi kama wanadamu wengine (Mt 10:10). Anayehubiri kwa ajili ya kupata fedha na kipato cha maisha huyo si mtenda kazi pamoja na Kristo bali ni Nabii wa Uongo. Mhubiri yeyote yule ni lazima awapende wagonjwa.

Wajibu wetu ni kuwapokea wale anaowachagua Mungu na kuwatuma kwetu kutuhubiria kwani kuwapokea wao tunampokea Kristo: “Anayewapokea ninyi, ananipokea mimi, na anampokea yule aliyenituma” (Mt 10:40). Paulo anatushauri akisema; “Lakini ndugu, tunataka muwatambue wanaojibidisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana na kuwaonyeni, mkawastahi sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Iweni na imani ninyi kwa ninyi” (1Thes 5:12-13). Tuwaombee wale wote wanaotetea wanyonge, wanaopigania haki na amani ya watu wote ili Mungu awazidishie matumaini wasikate tamaa wasonge mbele wasirudi nyuma. Tuwaombee Mapadre na viongozi wa Kanisa wawe tayari kutetea haki na ukweli na kuwaambia watu wanalopaswa kutenda. Mali na fedha visiwafunge midomo yao ili watufundishe kutenda haki na kuenenda katika upendo, umoja na amani.

J15 Mwaka B
09 July 2021, 09:10