Tafakari Jumapili 15 ya Mwaka B wa Kanisa: Masharti ya Uinjilishaji
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama. Katika ulimwengu mamboleo, watu wakubwa na hasa wafanya biashara wakubwa wanaozunguka mahali pengi duniani wana falsafa yao ijulikanayo kama “travel light”, ndio kusafiri kirahisi bila kuwa na mizigo mingi na mizito. Na hii si tu falsafa ya kusafiri bila hata ya maisha ya ulimwengu wa leo wa kidigitali, ni teknolojia ya leo kujaribu kufanya kila kitu kuwa chepesi na chenye kubebeka kirahisi. Kifupi ni mwanadamu anayetaka kukwepa uzito mkubwa katika maisha yake, ili aweze kuwa huru na hata kuweza kupiga hatua kubwa zaidi katika maisha yake. Hii ni falsafa ya ulimwengu wetu wa leo, katika nyanja mbali mbali tunaona mwanadamu anapambana ili aweze kuwa huru zaidi na zaidi, ili aondokane na uzito mkubwa na hata kazi ngumu na zenye kutumia nguvu nyingi. Ni ulimwengu ambao mtaji mkubwa na wa uhakika haupo tena katika nguvu kazi, bali katika akili na utaalamu na ujuzi wa mwanadamu. Na ndio maana ulimwengu leo unatawaliwa na teknolojia ya kiganjani au kidoleni (Digital world and technology).
Somo la Injili ya leo, Yesu anatualika nasi wafuasi na rafiki zake kuongozwa na falsafa hiyo ya “travel light”, ili tuweze kuwa huru zaidi katika kutimiza utume wetu wa kimisionari, ili tusitingwe na uzito wa mambo mengi mengine, kwani la muhimu na la msingi mbele yetu, ni moja tu, kuenda kuutangaza na kuusimika Ufalme wa Mungu duniani. Ni kutoka na kwenda na kutimiza kile tu anachotualika yeye mwenyewe kukifanya katika maisha yetu. Injili ya leo, Yesu anawaita na kuwatuma wale Thenashara na kuwapa uwezo hata juu ya pepo wachafu. Kitendo cha kwanza ni kuitwa, hivyo hakuna anayejiita mwenyewe, bali sisi sote kama wabatizwa, tunaitwa na Yesu mwenyewe, na hatuiti na kuishia hapo bali anataka kutushirikisha utume wake, na ndio wa kwenda kuivunja ile himaya na utawala wa yule aliye mwovu ulimwengu. Muhimu ndugu zangu, lazima kila mara hatuna budi kutambua kuwa ni Mungu mwenyewe anayetuita, iwe ni katika maisha ya wakfu, maisha ya ndoa na kadhalika, na anatuita sisi sote kutoka na kwenda kutimiza utume ule ule wa kuusimika Ufalme wa Mungu hapa duniani.
Kila anayekutana na Yesu Kristo katika maisha yake, anajawa na hamu na shauku kuu ya kutobaki na furaha na amani ile peke yake, bali lazima kutoka na kuwashikirisha wengine. Na ndio hasa chanzo cha umisionari wetu, lazima kwa nafasi ya kwanza, mimi na wewe tukutane na Yesu Kristo, kuisikia Habari njema yake, na ndio hapo nasi tutajawa na shauku na nguvu ya kutoka na kuwashirikisha wengine, Habari njema tuliyoisikia na kuipokea kutoka kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Anawatuma wawili wawili, kwa kweli sio kwa sababu za kuwafanya japo wasiwe wapweke njiani au kuwa na mtu wa kuzungumza na kutimiza naye wajibu kama msaidizi, bali ni kwa sababu za kitaalimungu. Kutumwa wawili ndio kusema inatukumbusha na kutuhimiza kuwa Ukristo wetu sio maisha ya ubinafsi, bali tunaweza kuishi na kukua katika imani yetu kwa msaada na tukiwa ndani ya jumuiya. Utume wa Kristo kwa kila mmoja wetu tunaweza kuutimiza tukiwa wamoja katika jumuiya yake, yaani Kanisa lake. Na ndio maana lazima kutambua kuwa utume huo anaotupa Yesu Kristo daima na lazima tuwe wamoja katika jumuiya moja, na ndio Kanisa lake.
Zaidi sana, katika ulimwengu wa Kiyahudi, ushahidi ulipokelewa na kukubalika pale tu unapoletwa na mashahidi wawili. Ndio kusema kweli za Injili, za Habari njema ya wokovu, sio kweli za mtu binafsi bali daima zinasimamiwa na jumuiya, yaani Kanisa. Ni kweli zile zinazotunzwa na kufundishwa na Kanisa, ndio nasi tunaalikwa kutoka na kwenda kuwashirikisha wengine. Kamwe hatutumwi kuwapelekea wengine mawazo na fikra au falsafa zangu binafsi bali kweli zile za Injili kama zinavyofundishwa na Mama Kanisa. Yesu Kristo tofauti kabisa na muktadha wa dini ile ya Kiyahudi, Yeye anawaita na kuwatuma wanafunzi wake kwenda, angali katika dini ya Kiyahudi, marabi hawakutoka na kwenda kuhubiri, bali walisubiri wanafunzi kuwaendea na kujifunza Torati kutoka kwao. Kwa wanafunzi wa Yesu mtindo na aina yake ni ile ya kutoka na kwenda, siyo ya kubaki ndani na kusubiri, ndio mtindo unatutaka kuachana na yote ya kale, na hasa kuachana na ubinafsi na umimi wetu, ni kwa njia ya kutoka na kuwaendea wengine hapo kweli tunaishi amri ile ya mapendo. Anayependa daima anatoka ndani mwake, katika zoni ile anayojisikia salama na kutaka daima kumshirikisha mwingine hali ile njema na ya usalama, anayependa hajiridhiki na furaha na amani yake mwenyewe bali daima ya mwingine na hasa wale wanaomzunguka na hata wanaokuwa mbali naye.
Yesu anawatuma na kuwapa pia uwezo juu ya pepo wachafu. Yesu hawapi uwezo juu ya wale wanaokataa kuipokea Injili yake, bali kwa pepo wachafu. Yesu mwenyewe mara zote katika Injili tunaona aliwakemea na kuwatoa pepo wachafu watu mbali mbali, ndio kusema aliwatoa katika hali duni na mbaya za kuwa watumwa na kuwafanya watu huru, aliwafungua kutoka vifungoni ili waweze kuwa huru. Pepo wachafu hapa ni zile nguvu zote za giza zinazomfanya mwanadamu kuwa mbali na Mungu, kukosa uhuru na furaha ya kweli. Ni wajibu wa kila mbatizwa kwa njia ya Kanisa kutoka na kwenda kumkomboa mwanadamu kutoka katika nguvu na utawala wa yule mwovu, kuwafanya wengine waishi na watembee katika mwanga na uhuru wa wana wa Mungu. Ndio maisha kuendana na kweli za Injili. Sehemu ya pili ya Injili ya leo, Yesu anawaelekeza nini cha kuchukua njiani na nini wasibebe pamoja nao wakati wa kwenda kuipeleka Habari Njema ya wokovu. Ni hapa kama nilivyotangulia kusema mwanzoni Yesu anawataka wawe watu kama wafanyabiashara wakubwa wa leo na falsafa yao “Travel light”, wasibebe kitu kingine njiani isipokuwa, fimbo tu, viatu na kanzu moja tu.
Wanafunzi wale wanaonywa na kutahadharishwa kuepuka mizigo mizito pamoja nao, bali wachukue yale ya msingi na lazima tu. Kwa nini fimbo, wakati ilijulikana na kutumika kama silaha ya mtu maskini? Yesu tayari aliwakataza wanafunzi wake katika Injili ya Matayo wasibebe wala fimbo (Matayo 10:10). Kwa nini basi leo anaruhusu wanafunzi wake kubeba fimbo njiani? Maana tunajua kuwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu utume wao ni kuwa watu wa amani, na hivyo kujiepusha na kila aina ya maisha inayoweza kuleta magomvi na mafarakano. Katika Maandiko Matakatifu, fimbo pia ilikuwa na maana nyingine zaidi ya silaha ya mtu duni na maskini. Musa na Haruni wakiwa wawili kama anavyowatuma Yesu wale Thenashara leo, walitumia fimbo kuweza kuwapigani na kuwakomboa watu wa Israeli, hivyo fimbo ilikuwa ni ishara ya uwepo wa nguvu ya Mungu kati yao. Musa aliweza kufanya miujiza mbele ya Farao kwa kutumia fimbo yake (Kutoka 7:9-12 na 10:13) na hata aliigawa bahari ya Shamu (Kutoka 14:16) na hata kufanya maji kutoka katika mwamba wa jiwe kwa kutumia fimbo (Kutoka 17:5-6).
Hivyo hata wanafunzi wa Yesu katika kutimiza misheni yao ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika nguvu zote za yule mwovu, wanaalikwa kuwa na fimbo mikononi mwao, ndio nguvu itokayo kwa Yesu Kristo mwenyewe, na ndio Neno lake. Ni kwa njia ya Neno lake na masakramenti yetu, nasi tunajaliwa kama Kanisa nguvu ya Mungu ya kuweza kumshinda yule mwovu na utawala wake. Pia Yesu anawaambia wawapo njiani wasichukue; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za kibindoni. Yafaa hata hapa tuelewe kuwa Yesu hakuwa anapinga kumiliki au kuwa na vitu kwa ajili ya maisha ya kila siku. Lakini Yesu kama alivyowaonya na kuwataka wanafunzi wake wa enzi zile pia anatuonya nasi leo kwa maneno na ujumbe wenye uzito uleule. Ni tahadhari ya kuwa watumwa kwa kujishikamanisha na hata kuabudu vitu, mali au fedha katika maisha ya mfuasi wa Yesu Kristo. Ni tahadhari ya kujiangalia kila mmoja wetu kwani mali na vitu na pesa na mambo kama hayo mara nyingi yanatufanya kuwa watumwa na kukosa uhuru wa kweli wa kuwa mashahidi wa Habari njema ya wokovu kwa wengine.
Si tu wasichukue fedha bali hata mkate, mkate tunaoomba ni ule wa kila siku na sio wa kujilimbikizia na kuweka akiba ya kesho na keshokutwa, ndio kusema maisha ya mfuasi wa kweli ni yule anayeishi leo yake kama vile anaishi tayari katika maisha ya umilele. Ni maisha yanayoangaliwa kwanza ya muhimu na msingi, maisha ya kuwa huru ili kuweza kutimiza misheni yake Yesu Kristo. Leo duniani bado kuna watu wengi sana wanakufa njaa, lakini pia tunaona kuna watu wengi ambao wanakula na kusaza bila kujali hata mwingine anayekuwa jirani yake achilia mbali wanaokuwa mbali ya macho yake. Mkristo anaalikwa kutoka katika zoni yake ya usalama na kujitosheleza na kumfikiria mwingine anayekuwa muhitaji zaidi yake. Kuhubiri na kuutangaza ufalme wa Mungu si lazima tufanye salama ndefu kutoka nyumbani au kijijini kwangu au nchi yangu, itoshe kila mmoja wetu atoke ndani mwake, katika ubinafsi wake na kumwangalia yule ninayekutana naye kila siku, yule anayenizunguka katika maisha yangu.
Sehemu ya tatu ya Injili ya leo, Yesu anaonesha kuwa baadhi yao watapata mapokezi mazuri na wengine kukataliwa na hata kufukuzwa. Mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Kauli hii ya Yesu kamwe haina maana kuwa wanatumwa kutembelea au kupeleka ujumbe kwa familia moja tu inayowapokea na kuwakaribisha. Yesu tayari anaona hatari na kishawishi kinachokuwa mbele yao. Ndio kusema anayetangaza Habari njema atakutana na watu wema na wakarimu, watakaokuwa tayari kuwakaribisha katika nyumba na makazi yao. Lakini kama tujuavyo yawezekana kabisa nyumba au familia ile ya kwanza isiwe ni mahali au makazi bora zaidi au kukupa chakula bora zaidi. Ni hapa wanaweza kukutana na watu wengine wema pia na hata wenye nafasi inayokuwa bora zaidi na kuwakaribisha wajumbe wale wa Habari Njema.Wajumbe wa Injili hawatumwi kwenda kusaka fursa na nafasi za kuwafanya wao waishi vizuri zaidi, na ndio maana Yesu anawakumbusha kuwa wanatumwa kwenda kuwa mashahidi wa Habari njema, sio kwenda kutafuta nafuu au maisha yanayokuwa mazuri zaidi.
Hivyo kutokuwataka kuhamahama ni sawa na kuwaambia wasiangalie wapi panakuwa ni nafuu zaidi na pazuri na ambapo mmoja anaweza kupata mahitaji yake yote bila shida kubwa. Wanafunzi wanatumwa kwenda kupeleka Habari njema na sio masilahi binafsi. Lakini pia hata pale wasipokaribishwa, Yesu anawaalika hata kukung’uta vumbi za miguu yao ili kuwa ushuhuda kwao. Kwa desturi wayahudi walipoingia nchi ya wapagani, na saa ile ya kutoka walipaswa kukung’uta vumbi za miguu yao, kuonesha kuacha nyumba yale yote yanayokuwa kinyume na dini na imani yao. Ndio Yesu leo anawaalika wanafunzi wake kuacha nyuma yale yote wanayokutana nayo katika misheni zao kinyume na kweli za Injili, ndio mambo yale yote yanayoupinga ufalme wa Mungu, yanayokwenda kinyume na mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Leo duniani kuna itikadi na falsafa na mitindo ya maisha, inayokuwa sawa na vumbi, ambayo kila mfuasi wa Yesu Kristo hana budi kuepukana nayo, ndio kukung’uta vumbi za miguu ili iwe ushahidi kwao, sio dhidi yao bali maisha yao yaweze kuwa taa na nuru, yaweze kuwa chumvi yenye kukoleza na kuwavuta wengine kuishi kweli za Injili. Nawatakia Dominika na tafakuri njema!