Tafakari Jumapili 18 ya Mwaka B: Yesu Kristo Ni Chakula Cha Uzima!
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Amani na Salama! Hitimisho la sehemu ya Injili ya Dominika iliyopita kutoka katika sura ile ya sita ya Mwinjili Yohane, inaakisi mtazamo wa wengi katika ulimwengu wetu wa leo. Wengi leo wanamsaka Yesu mtenda miujiza, anayeweza kuwashibisha njaa zao za kila aina iwe ni mali, pesa, elimu, majumba, magari, na kadhalika na kadhalika. Yesu anayetenda miujiza ili kama ni mali basi nipate nyingi zaidi na zaidi. Na ndio tunaona utitiri wa madhehebu yanayozaliwa kila kukicha na wahubiri wanaohubiri miujiza ya mafanikio katika maisha ya watu, wahubiri wa utajiri, uponyaji, kuondolewa mikosi na laana na kadhalika na kadhalika. Na ndio umati ule baada ya kula na kushiba ile mikate ya shayiri na kusaza wakata kumkamata Yesu ili wamfanye awe mfalme wao. Ni hapo wanakosa kuelewa maana ya ishara ile, maana Mwinjili Yohane hauiti muujiza kama ni ishara, ndio kusema nyuma yake kuna katekesi, kuna kufundisho muhimu na la maana sana. Yesu hakutenda ishara zile kwa ajili ya kuwaadaha na kuwafanya watu wamstaajabie, bali watambue Umungu na ukuu na uwezo wake, ili wapate KUMWAMINI. Nia na shabaha ni kuwasadia watu wafike hatua muhimu kabisa ya kuamini, ya kuwa kweli wanafunzi wake, ya kuwa kweli wana wa Mungu, ya kukabidhi maisha yao bila kujibakiza katika kumpenda Mungu na jirani.
Umati ule unakosa kuelewa maana ya ishara ile, wao walibaki juu juu na kuona ni muujiza wa kulishwa mikate, na wakakosa kuona nia hasa ni ile roho na moyo wa kushirikisha kidogo wanachokuwa nacho, ule moyo wa upendo na kujali wengine, wa kuwa tayari kuwashirikisha wengine kile unachokuwa nacho hata katika uduni na udogo kama kijana yule mdogo aliyekuwa na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili. “Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?” Mkutano ule unajibidisha kumtafuta Yesu na hata wanaamua kupanda chomboni na kwenda ng’ambo ya pili ya ziwa lile la Galilaya, yaani Kapernaumu. Na cha kushangaza, Yesu hajibu swali lao, kwani mara moja anasoma mioyoni mwao na kutambua swali lao ni kweli si hilo. Bali ndio kusema utatenda tena muujiza ule wa kutulisha na kutushibisha? Utaendelea kutupatia mkate na samaki ili tule na hata kusaza? “Amini, amini, nawaambieni, ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele”.
Mkutano unamtafuta na kumwendea Yesu si kwa sababu walikuwa na njaa na kiu ya kweli ya kushibishwa na Neno lake, kupata ufafanuzi zaidi wa ishara ile aliyoitenda ya kuwalisha mikate na samaki, bali njaa na kiu yao ni mikate ya chakula, ni chakula cha dezo kwa lugha ya mtaani, chakula bila kutokwa na jasho, chakula cha bure bure. Ni kama wengi wetu wanaodhani Yesu anaweza kutenda miujiza ya kujaza mifuko yetu pesa bila ya kufanya kazi, nyumba zetu chakula bila shuruba yeyote ya kutoa jasho, ndio wale waokwenda kuombewa miujiza itendeke ya kupata magari na mali bila wao kujishughulisha na kazi ya kuwaweza kupata kipato chochote. Na ndio Yesu anatufundisha nasi leo, kuwa amekuja ili sisi tuweze kuishi na kuongozwa na mantiki ya mbinguni, ile ya Mungu mwenyewe. Katika ishara ile ya kuwalisha mikate, Yesu anatuonesha kuwa ni kwa kukubali kugawana kile kinachokuwa mbele yetu kwa upendo na kujali basi hakika muujiza mkubwa unatendeka kwani hakuna hata mmoja wetu atakayebaki katika njaa na dhiki kubwa. Ulimwengu wetu wa leo umetawalia sana na ubinafsi na umimi, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu na popote pale.
Ni ulimwengu ambao kila mmoja anajali mambo yake mwenyewe, hakuna mwenye muda na mwingine. Na ndio mwaliko wa Yesu katika ishara ile, ya kutusihi kubadili vichwa vyetu, namna zetu za kufikiri na kutenda katika maisha. Yesu hakutaka mkutano ule uishie katika ishara tu bali katika kupata maana ya ishara ile, na ndio hata kwetu leo, kila mara tunaposoma Injili ni vema tusibaki katika kustajabia makuu ya Mungu bali pia kuchota somo, ujumbe kusudiwa katika matendo makuu ya Mungu. Na ndio hata nasi leo, swali lile lile tunapaswa kujiuliza, kwa nini tunamtafuta Yesu katika maisha yetu, kwa nini tunasali, kwa nini tunashika amri na kuishi imani yetu? Yawezekana kabisa mimi na wewe tusiwe mbali sana na mkutano ule uliovuka na kumtafuta Yesu. Mkutano ulimtafuta kwa ajili ya chakula chenye kuharibika, ndio kuomba mathalani neema fulani maishani, muujiza, afya njema, mafanikio fulani, ulinzi wake na kadhalika na kadhalika, sio kwamba hatupaswi kumuomba Yesu atujalie hayo tunayoomba mara nyingi, lakini leo Yesu anatufundisha kuomba kile kinachokuwa bora kabisa, kile kinachodumu milele, n asio vile vya kuharibika, vile vya kupita vya dunia hii. Yesu anatutoa katika ngazi moja na kutupandisha ngazi ya juu kabisa katika maisha ya ufuasi. Mfuasi wa kweli ni yule ambaye anakua katika imani yake, katika kutambua kipi ni bora na chenye kudumu milele na milele.
Mwanamke msamaria pake kisimani hakutambua kuwa Yesu anamwalika kuomba sio maji ya kutuliza kiu na kisha kurudi tena na tena pale kisimani, bali maji ya uzima wa milele. Na ndio leo mkutano na hata sisi kutambua kutafuta sio mkate tu wa kula na kutuliza njaa zetu bali mkate wa uzima wa milele. Ndio kusema Yesu anatualika kukwea hatua moja juu zaidi, kukua katika safari yetu ya kumwamini Mungu, kukua katika kumpenda Mungu na jirani. Labda tunajiuliza chakuka kidumucho milele ni kipi hicho? Katika somo la Injili ya Dominika iliyopita tulisikia juu ya mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini tunaposoma zaidi hatusikii tena juu ya wala samaki na hata vikapu vya masalia tunasikia juu ya mikate tu na hakuna kinachosemwa zaidi juu ya wale samaki. Mkate katika lugha ya Biblia tunaona maneno ya Musa kwa Wanawaisraeli; “…kwamba mtu haishi kwa mkate tu, ila huishi kwa kila litokalo kinywani mwa Bwana” (Kumbukumbu 8:3). Pia mkate inaashiria wale waliokosa kujua hekima ya mbinguni; “Njoni mle mkate wangu, mnywe divai niliyochanganya” (Mithali 9:5). Pia tunaona kutoka kwa Nabii Isaya; “Kwa nini mnatoa fedha mpate kitu kisicho mkate, kwa nini mnachoka mpate kitu kisichoshibisha?” (Isaya 55:2) Hivyo tunaweza kuona mkate wa Bwana, ndio Neno lake, mafundisho yake, mikate mitano inayozungumziwa na Mwinjili Yohane inaakisi pia vitabu vitano vya Sheria ya Mungu, ndio Torati.
Na wale samaki wiwili Je ? Samaki wawili wanawakilisha makundi mawili ya Maandiko Matakatifu ambayo pamoja na Torati ndio ukamilifu wote, yaani Manabii na vitabu vingine vinavyosalia. Ni vyote kwa ujumla wake vinamsaidia mmoja kumuelewa Mungu na kuishi kadiri ya maagizo na amri zake. Na hapa tunaona hatusikii tena juu ya samaki, kama anavyotuonesha Mwinjili Marko ; « Walikuwa wamesahau kuchukua mikate, walikuwa na mkate mmoja tu chomboni mwao » (Marko 8 :14) Na mkate huo ndio Yesu Kristo mwenyewe, ambao Mungu leo ametupa sisi watoto wake, katika Kanisa lake na ndio Injili yake, Habari njema ya wokovu wetu. Mwenye kula Neno lake hakika huyo hataona njaa kamwe, na ndio fundisho ambalo Yesu anatualika kulitafakari katika maisha na safari yetu ya ufuasi. Mkutano walimwuliza Yesu ; « Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu ? » Na hapo Yesu anawaonesha ni ipi iliyo kweli kazi ya Mungu ; « Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye ». Katika Injili ya Yohane kamwe hatusikii neno « imani » bali kitenzi « kumwamini/kuamini ». Anayeimani ni yule anayelipokea Neno lake na kuongozwa nalo, anayelishika Neno katika maisha yake, anayefananisha maisha yake na hilo Neno, anayelipokea kama mkate wake wa uzima wa milele, anayejishibisha kwa Neno la Mungu.
Na ndicho Yesu anachosubiri kwa kila mmoja wetu, sio kumuona kama mtenda miujiza bali kuingia katika mahusiano naye kwa njia ya Neno lake, kulipokea na kulifanya Neno lake liwe taa ya maisha ya kila mmoja wetu. Ni mahusiano ya upendo usio na masharti hata kidogo, hi indio imani ya kweli, imani sio kitendo cha akili tu bali pia ni utashi kamili kwani inatuingiza katika mahusiano ya ndani na ya pekee kabisa katika maisha yetu. Kuamini ni kujikabidhi mzima mzima kwake Bwana wetu Yesu Kristo, ni kukubali kuongozwa na mantiki ya Neno lake la uzima wa milele. Ni maisha yetu yote bila kujibakiza au kugawanyika, tunabaki kuwa wenye mahusiano naye hata katika nyakati za dhiki na tabu na shida kubwa, ni kuwa na hakika ya uwepo wake pamoja nasi katika safari yetu nzima kuelekea uzima wa milele. “Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini?” Kwa Wayahudi ishara ile ya kuwalisha mikate na samaki haikutosha kwao kuamini, hivyo bado wanahitaji ishara iliyo kubwa zaidi. Maana hata babu zao walikula mana jangwani na Musa aliwalisha sio kwa siku moja tu kama walivyolishwa na Yesu Kristo bali kwa miaka arobaini.
Na ndio Yesu anachukua fursa ile kuwafundisha kuwa sio Musa aliyewalisha bali ni Baba yake aliye mbinguni. Na zaidi sana anatufundisha kuwa leo Mungu hatulishi tena kwa mana kwa chakula chenye uzima wa milele. Chakula kinachomaliza njaa na kiu yetu milele yote. Mkate anaotupa Yesu Kristo sio wa muda na kupita tu bali ni wa milele yote. “Bwana, siku zote utupe chakula hiki.” Ndio ombi la mkutano kwa Yesu leo. Ni sawa kama ombi lile la mwanamke Msamaria pale kisimani. (Yohane 4:15) Mwanamke yule hakuelewa ni maji ya aina gani hayo ya uzima na hivyo alibaki na picha ya maji yale yale ya kisimani. Na hata mkutano leo bado wanabaki katika ngazi ileile ya mkate wa kila siku, mkate wenye kuharibika, mkate usiodumu milele. Na ndio Yesu pia anatumia tena fursa ile adhimu kuwafunulia zaidi na zaidi. “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa naye aniaminiye hataona kiu kamwe”. Hivyo Yesu anawasaidia kuelewa mafundisho na maana ya ishara ile, ni Yeye mwenyewe aliye mkate wa kweli, ni Neno lake ndilo daima litamaliza njaa na kiu ya kila mmoja wetu. Ni kwa kumpokea yeye na kuongozwa na mantiki ya Neno lake, kila mfuasi wa Yesu anakuwa na hakika ya kusafiri kwa salama kumwelekea Mungu, ni Yeye anapaswa chakula chetu cha maisha ya siku kwa siku kwa njia ya Neno lake na pia katika masakramenti yake. Niwatakie Dominika na tafakuri njema.