Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa: Msikitendee kazi chakula kiharibikacho! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa: Msikitendee kazi chakula kiharibikacho! 

Tafakari Jumapili 18: Msikitendee Kazi Chakula Kiharibikacho!

Ujumbe wa Yesu katika dominika hii ni msikitendee kazi chakula kiharibikacho. Wayahudi wanamtafuta Yesu ili awape mikate washibe na pia wanadai ishara ili waweze kumwani. Lakini Yesu anawaambia kuwa wasihangaike sana, kilicho cha muhimu ni kumwamini Kristo na Mungu Baba aliyemtuma. Hiki ndicho chakula kisichoharibika maana kitawafikisha katika uzima wa milele.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa Yesu katika dominika hii ni msikitendee kazi chakula kiharibikacho. Wayahudi wanamtafuta Yesu ili awape mikate washibe na pia wanadai ishara ili waweze kumwani. Lakini Yesu anawaambia kuwa wasihangaike kushibisha matumbo yao tu; kilicho cha muhimu ni kumwamini Kristo na Mungu Baba aliyemtuma. Hiki ndicho chakula kisichoharibika maana kitawafikisha katika uzima wa milele.  Katika somo la kwanza la kitabu cha kutoka (16: 2-4, 12-15); Mungu anawalisha Waisraeli jangwani. Chakula hicho ni mfano wa Ekaristi takatifu, chakula cha roho. Baada ya kutolewa utumwani Misri waisraeli walisafiri safari ndefu ya kuchosha. Walipofika jangani, sehemu ambayo haikuwa na maji wala chakula, waliwanung’unikia Musa na Haruni wakawaambia; “Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula hata kushiba; kwani mmetutoa huko ili kutuua kwa njaa”. Mungu akayasikia manung’uniko yao akamwambia Musa; Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate na nyama kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku.

Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Njaa iliwafanya wana wa Israeli wakate tamaa na maisha, wakanung’unika sana huku wakitamani kurudi utumwani Misri. Hawakuthamini kukombolewa kwao kutoka utumwa wa Farao, wakaona ni aheri wangeendelea kuwa watuwa ili mradi tu waendelee kushibisha tumbo kwa nyama ili wazime njaa ya kimwili wakisahau njaa mbaya zaidi ni njaa ya kiroho. Sisi nasi hatuna fikra na mawazo kama haya ya kutafuta kuzima njaa ya tumbo hata katika dhambi? Katika somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (4:17, 20-24); Paulo anatufundisha kuwa kutenda dhambi ni kuvaa utu wa zamani akisema; “Nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao. Maana sivyo mlivyojifunza kwa Kristo, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudangaya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu upya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” Kuishi kitakatifu ni kuvaa utu upya. Wakristo tunajivika utu mpya katika ubatizo na hivyo tunapswa kuishi kadiri ya utu mpya, yaani tuishi kitakatifu.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:24-35); inatueleza mafundisho ya Yesu juu ya habari za chakula kiletacho uzima wa milele. Watu wanamtafuta Yesu kwa hamu kubwa kweli, wanamkuta ng’ambo ya bahari, wanamuuliza Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu anawaambia kwa sababu walikula mikate wakashiba. Yesu anawaonya wasikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele ndio kuzitenda kazi za Mungu. Na kazi ya Mungu ni kumwamini yeye aliyetumwa na yeye. Lakini watu hawa wanataka ishara ili waweze kumwamini. Kama vile Musa alivyofanya ishara jangwani kwa kuwapa chakula Waisraeli watu wakamwamini basi Yesu naye afanye ishara ili wamwamini kuwa ni Masiha. Yesu anawakumbusha kuwa sio Musa aliyewapa mana jagwani bali ni Mungu. Hata hivyo chakula hicho kilikuwa ni ishara tu na utabiri wa chakula kiletacho uzima wa milele ndiye Kristo mwenyewe kama anavyosema; “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa naye aniaminiye hataona kiu kamwe.”

Njaa, njaa ni mbaya sana. Njaa humfanya mtu alegee, mwili kudhoofika na mtu hukonda. Ndiyo maana waswahili husema njaa mwana malegeza na shibe mwana malevya. Njaa yawezakuwa ya kiroho, ya kimwili, ya kiakili hata ya kimaadili. Kuna njaa ya upendo, kuna njaa ya matumaini, kuna njaa ya msamaha, kuna njaa ya vitu, kuna njaa hata ya kuona mtu. Mama Teresa wa Calcutta aliwahi kusema; “Kuna njaa ya upendo na kuthaminiwa katika dunia hii kuliko njaa ya mkate. Njaa inawezakuwa ni upungufu wa chakula tumboni. Hii njaa ndiyo iliyowafanya watu wamtafute Yesu kwa sababu walikumbuka kuwa aliwalisha kwa mkate (Yohane 6:25–26). Hii ndiyo njaa iliyowafanya waisraeli wayakumbuke masufuria ya nyama ya utumwani Misri, wakanung’unika (Kutoka 16: 2-3). Njaa inawezakuwa pia ni ukosefu au upungufu wa chakula. Ni katika msingi huu tunazungumzia baa la njaa. Njaa hii ya ukosefu wa chakula ni silaha kubwa ya maangamizi na ukosefu wa amani. Baba Mtakatifu Benedict XVI akishutumu wingi wa fedha unaotumika katika kununulia silaha za kivita anasema; Si rahisi kuzungumzia amani pale ambapo watu wanateseka kwa sababu ya njaa.

Njaa ni kuwa na hamu, tamaa au shauku na neno, tendo, kitu au mtu. Kuna njaa ya kutenda mapenzi ya Mungu; Yesu akawaambia; “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake” (Yn 4:34). “Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa” (Mt. 5:6). “Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaondoa mikono mitupu” (Lk.1:53). Kuna njaa ya upendo. Mama Teresa wa Calcutta alisema; “Ni vigumu zaidi kumaliza njaa ya upendo kuliko njaa ya mkate.” Kuna njaa ya kupata mume au mke. Sara katika kitabu cha Tobiti alifikiria kujinyoga sababu ya kukosa mme. “Huyu Sara aliolewa mara saba na wanaume saba. Lakini jini Asmodeo lilimuua kila mume aliyemuoa Sara kabla hajalala naye (Tobiti 2: 8). Sara alitukanwa akiambiwa; “Ewe muuaji wa wanaume! Ona aibu! Umekwisha kuwa na wanaume saba, lakini hata mmoja wao hakukupatia mwana…Nenda zako, uwafuate wanaume zako marehemu. Heri tusione hata mtoto aliyezaliwa na wewe” (Tobiti 2: 8-9). “Sara aliposikia maneno hayo alihuzunika sana na kutoa machozi. Akataka kujinyonga.

Lakini alipotafakari, alisema; “La! Sitajinyonga! Watu wasije wakamdharau baba yangu na kusema; “Ulikuwa na mtoto mmoja tu, binti ambaye ulimpenda sana, lakini alijinyonga kwa sababu ya uchungu!” Jambo kama hilo litasababisha kifo cha baba yangu mzee, nami nitakuwa na hatia. Sitajiua mwenyewe, hasha; nitamwomba Bwana achukue roho yangu, nisisikie tena matusi kama yale!” (Tobiti 2: 10). Mungu alisikiliza kilio chake akampatia mume, kijana Tobia. Kuna hata njaa ya uvivu ambayo ni sababu ya matatizo. “Ewe mvivu, utalala hapo mpaka lini? Utaamka lini katika usingizi wako? Wasema: “Acha nilale kidogo tu, acha nisinzie kidogo! Niache nikunje mikono nipumzike kidogo!” Wakati huo umaskini, utakuvamia kama mnyang’anyi, ufukara utakufuata kama jambazi” (Methali 6: 9-10). Kuna hata njaa ya kumwona mtu. Zakayo alikuwa na njaa ya kumwona Yesu hata akapanda juu ya mti ili amwone. Yakobo, baba yake Yosefu alikuwa na njaa ya kumwona mtoto wake. Simeoni alikuwa na njaa ya kumwona mwokozi kabla ya kufa na baada ya kumwona akasema; sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani, maana macho yangu yameuona wokovu, uliowaahidia mataifa. Mtakatifu Augustino alisema; “Mwenyezi Mungu umetuumba kwa ajili yako mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia ndani mwetu.”

Katika njaa zote hizi, jjaa ya kiroho ni mbaya zaidi kwani roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu. Tujishughulishe basi kila mara kuzima njaa ya kiroho ili tupate uzima wa wa milele. Yesu ni Mkate wa uzima wa milele anayetulisha kwa neno lake na kwa Mwili na Damu yake. Tunaposoma na kusikiliza Neno la Mungu kama mtu binafsi na kama familia tunapata uzima wa milele. Tukishiriki Sadaka ya Misa Takatifu, tukasikiliza Neno la Mungu na kupokea Ekaristi Takatifu kwa mastahili tunapata amana ya uzima wa milele. Mara nyingi tunakuwa na woga au kukata tamaa katika maisha yetu, tunatamani kurudi katika masufuria ya nyama au kuenenda kama wengine wanavyofanya na kukishughulikia chakula cha mwili na kuziacha roho zetu zikizimia kwa njaa. Tukumbuke kuwa; “Mtu hataishi kwa mkate tu ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana”. Tuwe na hamu ya kupokea Ekaristi Takatifu. Katika maisha yetu ya kila siku tunakumbwa na vishawishi vya kutaka ishara. Wapo wanaoamini kuwa dini ya kweli ni ile yenye miujiza. Wapo wanaohama kanisa moja kwenda lingine wakitafuta miujiza ya uponyaji. Huko ni kutafuta mikate na sio kumtafuta Yesu Bwana wa uzima. Kwa ubatizo tumekuwa watu wapya, tumeuvua utu wa kale, tukauvaa utu mpya hivyo tusitamani kurudia hali yetu ya zamani. Katika taabu na mahangaiko ya kimaisha tusikate tamaa na kutamani kurudi katika hali yetu ya zamani, bali tumsikilize Yesu, tutweka mpaka kilindini tutafanikiwa.

J 18 Mwaka B
29 July 2021, 16:12