Tafuta

Sherehe ya Bikira maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Imani, Matumaini na Mapendo ya Kanisa. Sherehe ya Bikira maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Imani, Matumaini na Mapendo ya Kanisa. 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili Na Roho! Imani!

Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria mwili na roho ni utimilifu wa neema alizojaliwa kwa kukingiwa dhambi ya asili. Kukingiwa kwake dhambi ya asili ni kwa sababu katika mwili wa Bikira Maria ndipo Yesu alipata umwilisho. Hivyo basi kupalizwa mbinguni Bikira Maria, ni moja ya mafundisho makuu ya imani ya Kanisa Katoliki. Tuombe neema ya imani, matumaini na mependo thabiti!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu katika sherehe ya kupalizwa mbinguni Bikira Maria mwili na Roho. Kila tarehe 15 Agosti ya kila mwaka Kanisa linaadhimisha sherehe ya kupalizwa mbinguni Bikira Maria Mama wa Mungu. Maria ameingia utukufu wa mbinguni, ameshirikishwa utukufu wa Mwanae kwani katika maisha yake alimfuata Mwanae bila kumwacha hata alipokuwa msalabani. Maria ni mama yetu. Kwa maisha yake alituonyesha jinsi ya kumfuata Kristo, tupate kufika mbinguni. Anatuonyesha ya kuwa hatuwezi kuiingia hali ya utukufu bila kupitia mateso na msalaba. Tumwombe yeye, aliye malkia wa mbinguni, atusaidie ili sisi nasi tushirikishwe utukufu wa Mwanae. Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria ni utimilifu wa neema alizojaliwa kwa kukingiwa dhambi ya asili. Kukingiwa kwake dhambi ya asili ni kwa sababu katika mwili wa Bikira Maria ndipo Yesu alipata umwilisho. Hivyo basi kupalizwa mbinguni Bikira Maria, ni moja ya mafundisho makuu ya imani ya Kanisa Katoliki. Licha ya kuwa Maandiko Matakatifu hayasemi moja kwa moja kuhusu kupalizwa mbinguni Bikira Maria mwili na Roho.

Kanisa kwa njia ya Mapokeo ambayo ni chanzo kimojawapo cha ufunuo wa kimungu limepokea na kufundisha habari ya kupalizwa Mbinguni Bikira Maria kuwa ni ufunuo wa kweli. Kanisa limefikia hatua hiyo baada ya tafakari na majadiliano ya kina na kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho ilitambuliwa na Kanisa rasmi na kuanza kuadhimishwa mwaka 1950 baada ya kutangazwa na Baba Mtakatifu Pio XII katika Barua ya kipapa inayoitwa Munificentissimus Deus yaani Mungu Mkarimu, tarehe 1 Novemba 1950 katika sherehe ya watakatifu wote. Baba Mtakatifu Pio XII akitoa tamko la kupalizwa mbinguni mwili na roho Bikira Maria, mama wa Mungu asiye na doa la dhambi alisema: “Kwa sababu hii baada ya kumtolea Mungu sala na maombi ya kudumu, na baada ya kuomba mwanga wa Roho wa kweli, tunaarifu, tunaadhimisha, tunaeleza wazi kabisa na kutangaza kuwa: ni ufunuo wa imani kwamba Mama safi wa Mungu, Maria Bikira daima, baada ya maisha yake hapa duniani alipalizwa mwili na roho katika utukufu wa mbinguni”.  

Kabla ya kutangazwa siku hiyo rasmi, tangu karne ya 5, kulikuwepo tayari na vikundi vya watu, na sehemu mbalimbali hasa Roma makao makuu ya Kanisa wakiamini kuhusu kupalizwa mbinguni Bikira Maria, na kwamba mwili wake haukuoza kaburini. Hivyo makanisa mengi yalijengwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa mbinguni, miji na sehemu mbalimbali za kuabudia ziliwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa mbinguni. Baada ya hali hiyo kuonekana miongoni mwa wakristo wengi, Papa Pio XII mwaka 1946, aliitisha mkutano wa Maaskofu na kuwaomba wafanye uchunguzi kuhusu swala hilo. Baada ya uchunguzi huo, maaskofu walitoa taarifa na kusema kwamba, inafaa kutamkwa rasmi kuhusu kupalizwa mbinguni Mama Bikira Maria. Kumbe, hata kama Biblia haisemi, waziwazi kuhusu kifo cha Bikira Maria wala kupalizwa kwake mbinguni, Kanisa haliachi kutoamini kuhusu kupalizwa kwake mbinguni kwani muunganiko wa Yesu Kristo Mkombozi wetu na Bikira Maria katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu hapa duniani ni sababu tosha ya kuamini.

Kunako tarehe 8 Desemba 1854 Papa Pio IX alitangaza rasmi, Bikira Maria ni mkingiwa dhambi ya asili toka siku ile ya kutungwa kwake mimba tumboni mwa mama yake kama matayarisho ya kuwa mama wa Mungu, alizaliwa akiwa na uzima wa neema ya utakaso na katika maisha yake Bikira Maria hakutenda dhambi wala hakuwa na doa lolote la dhambi hivyo mwili wake haukupaswa kuoza. Bikira Maria alibaki Bikira daima kabla na baada ya kumzaa mkombozi kwani alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mtaguso wa Efeso mwaka 431 ulitamka wazi kuwa Bikira Maria ni Mama wa Kristo kwa Kigiriki “Christokos” kwani mwili wake ulichukua mimba ya mkombozi wetu Yesu Kristo, na ni Mama wa Mungu Kigiriki “Theotokos”, maana fumbo la umwilisho yaani Mungu kujifanya Mtu ulifanyika mwilini mwake. Kumbe, Bikira Maria ameshiriki kikamilifu kazi ya ukombozi wetu na mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini bado pia maandiko matakatifu hayako kimya juu ya Bikira Maria. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1).

Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha ufunuo (11:19; 12:1-6, 10), mwanamke anayeongelewa ni mfano wa Bikira Maria tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu na ni mfano wa Kanisa, joka ni mfano wa shetani na mtoto wa mwanamke ndiye Masiya Yesu Kristo. Vita kati ya joka na mwanamke ni mapambano kati ya nguvu za giza na Kanisa. Liturujia humlinganisha Mama Maria na Kanisa kwa sababu ya kufaulu kumshinda shetani kwa nguvu ya Kristo. Mtume Paulo katika Somo la pili la Waraka wake wa kwanza wa Wakorinto (15:20-26), anatueleza kwamba, Yesu Kristo amemshinda shetani na ubaya wake yaani, dhambi na mauti. Ushindi huu umedhihirishwa katika ufufuko wa Yesu Kristo, na pia utadhirishwa zaidi nyakati za mwisho miili yetu itakapofufuliwa. Tunda lingine la ushindi wa Kristo ni kupalizwa Bikira Maria mbinguni. Injili ilivyoandikwa na Luka (1:39-56), yaeleza ndiyo ya Bikira Maria isiyo na mtikisiko wala manung’uniko kwa wito wa Mungu. Licha ya hatari na magumu ambayo angeyapata Bikira Maria anaitaka mwito wa Mungu akisema; Mimi ni mtumimishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema (Lk 1: 38).

Ndiyo yake, kukubali kwake fumbo la umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili ndani mwake na kukaa kwetu (Jn 1: 14), lilifumbatwa katika utii wake wa kimapendo na utayari wake wa kushirikiana na Mungu katika kutekeleza mpango wa ukombozi wa mwanadamu. Ndiyo yake ikamafanya awe mama wa Mungu. Ndiyo yake, imani yake, utii na utayari wake, vikawa sababu ya ukombozi wake yeye mwenyewe na ukombozi wetu sisi na hivyo kustahilishwa kupalizwa mbinguni mwili na roho. Tunajifunza nini kutokwa kwa Mama Bikira Maria? Kwanza kabisa ni utii. Tuwe na utii kwa wajumbe wa Mungu kuziishi ahadi zetu za ubatizo ili zitustahilishe tuzo la utukufu mbinguni. Pili uvumilivu katika mateso na kumtumainia Mungu nyakati zote za magumu kama Bikira Maria aliyekubali kubeba ujauzito bila kujali aibu na adhabu ya kifo ambayo angeipata kwa kutupigwa mawe kutokana na kukosa uaminifu mbele ya macho ya binadamu kama ilivyokuwa desturi ya wayahudi.

Bikira Maria alivumilia kuona na kushiriki mateso ya mwanae hata alipomwona anakata roho msalabani. Kuwa na moyo wa unyenyekevu na utumishi kwa Mungu na jirani kama Bikira Maria licha ya kuwa mjamzito alifunga safari na kwenda kwa Elizabeti kumhudumia naye akiwa katika kipindi cha kumzaa mtangulizi wa Yesu; Yohane mbatizaji, katika uzee wake. Ahadi ya kuwa Mama wa Mungu kwa kumzaa Kristo haikumfanya ajisikie kuwa yeye ni mtu wa kutumikiwa bali kwa unyenyekevu anajifanya kuwa mtumishi na hivyo anastahilishwa kupalizwa mbinguni mwili na roho. Basi na tufurahi sote katika Bwana, tunapoadhimisha sikukuu hii kwa heshima ya Bikira Maria, kwani hata Malaika nao wafurahia kupalizwa kwake, na wanamsifu mwana wa Mungu. Katika kufurahi huku, tumwombe Mungu atujalie tuyaelekee daima mambo ya juu tupate kustahili kuushiriki utukufu wake.

Bikira Maria
12 August 2021, 15:17