Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili Na Roho! Injili
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Amani na Salama! Mama Kanisa katika Dominika tarehe 15 Agosti 2021 anatualika kufanya sherehe ya kupalizwa mbinguni Mama yetu Bikira Maria mwili na roho. Fundisho hili la imani lilitangazwa rasmi na Papa Pio XII hapo tarehe 01, Novemba, 1950. Mwanzoni kabla ya sherehe hii, Mama Kanisa kwa uchaji mkubwa na kwa karne nyingi lilikuwa likiadhimisha sherehe ya “Dormitio Maria”, yaani “Kulala kwa Maria”. Kanisa liliamini kuwa Maria aliye mkingiwa wa dhambi ya asili, kifo chake baada ya maisha yake ya hapa duniani ilikuwa ni usingizi wa milele. Na ndio tunaona hata Kanisa la Mashariki lilibaki kuamini na kufundisha kuwa baada ya kukamilisha maisha yake ya hapa duniani, Bikira Maria anazaliwa upya mbinguni, anazaliwa katika maisha ya utukufu wa milele, anashirikishwa katika utukufu ule wa Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo.
Kupalizwa mbinguni mwili na roho, ni vema tukaelewa sio katika maana ya kutoka ulimwengu huu na kwenda mahali pengine, kwani mbinguni sio mahali, ni hali ya kushiriki utukufu wa milele, ni kuunganika na Mungu. Hivyo, Bikira Maria baada ya maisha yake ya hapa duniani, anaingia katika utukufu wa milele mbinguni, ndio maisha ya kutokubanwa tena na mahali wala muda, na ndio Maria baada ya kufa kwake, anakuwa sasa Mama wa Kanisa zima, mama wa kila kila mmoja wetu. “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.” Mtakatifu Yohane Paulo II anatuambia katika barua yake ya “Redemptoris Mater”, yaani, “Mama wa Mkombozi”, kuwa kwa maneno hayo tunaonja maisha ya kiroho ya Mama yetu Bikira Maria, kuwa ni maisha ya imani. Hivyo kumzungumzia Maria daima anakuwa ni kielelezo cha imani ya kweli na ya kina kwa kila mfuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo.
Katika somo la Injili ya leo tunakutana na wanawake hawa wawili, Mariamu na Elisabeth. Tunaona na kushangazwa kuwa wanapokutana akina mama hawa wawili mazungumzo yao, sio yale ya kawaida, sio salamu ya kawaida wanapokutana akina mama, bali ni mazungumzo ya kitaalimungu na tena Taalimungu ya hali ya juu kabisa. Ndio kusema hayakuwa mazungumzo ya kawaida, ya wanawake wa kawaida katika ukawaida wao, bali wakiwa wamejawa na Roho Mtakatifu, wanaingia katika mazungumzo ya kiimani na kitaalimungu, yenye kuonesha ukuu na uweza wa Mungu katika maisha yao. Ni akina mama wanaoshirikishwa kwa namna ya pekee kabisa kazi ile ya ukombozi wa mwanadamu.
“Mariamu aliondoka, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji wa Yuda.” Mariamu anafanya sio safari ya kawaida bali ni safari ya imani na ya kimisionari, ni safari ya kuanza kumpeleka Yesu kwa nafasi ya kwanza kabisa katika mji ule wa Yuda, mji wenye hekalu la Yerusalemu, makao ya kidini na hata kisiasa kwa taifa lile la Israeli. Na Mariamu analifanya hilo kwa haraka, sio kwa kusuasua au kwa kujishauri, bali anaonesha utayari wake wa kushiriki katika safari ya imani, safari ya kimisionari, safari ya kumpeleka Yesu Kristo katika familia ile ya Zakaria na Elisabeth. Na ndio tunaweza kuona sherehe ya Kupalizwa mbinguni Mama yetu Bikira Maria, ni sherehe ya kimisionari kwa nafasi ya kwanza, ni sherehe inayotualika nasi kuwa kama Mariamu, kuwa wajumbe wa kumpeleka Yesu kwa ushahidi wa maisha yetu kwa wengine.
“Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.” Ni maneno ambayo Elisabeth anayatamka sio kwa akili na uwezo wake bali akiwa anaongozwa na Roho Mtakatifu. Na ndio maneno yanayomtambulisha Mariamu kuwa si mama wa kawaida bali ni mama ambaye hata uzao wake umebarikiwa. Ni kutokana na salamu hii ya Elisabeth tunaona Mama Kanisa katika Mtaguso ule wa Efeso wa mwaka 431, unamtambulisha Bikira Maria kama “Theotokos”, yaani, “Mama wa Mungu”. Ni kwa njia ya Maria, Mungu anaingia ulimwenguni. Bikira Maria anakuwa ni Sanduku lile la Agano kati ya Mungu na wanadamu, anakuwa ni Hekalu la Mungu, na ndio pia Sayuni mpya. Mtakatifu Ambrosi anaandika akisema; “Maria ni hekalu la Mungu, lakini sio Mungu wa hekaluni”, Ndio kusema kwa njia ya Maria, Mwenyezi Mungu anajifunua sura yake halisi kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa njia ya Maria, mwanadamu anapata nafasi nzuri kabisa ya kukutana na kumfahamu Mungu, sio tena kama Mungu yule wa hekalu la Agano la Kale, bali Mungu anayejifunua katika ukamilifu wake kwa njia ya Mwana pekee, yaani Bwana wetu Yesu Kristo.
Wazo hili la Maria kuwa ni Hekalu jipya la Mungu, tunaweza kuliona tunapojaribu kutafakari kwa makini somo la Injili ya leo. Sanduku la Agano liliingia tena Yerusalemu na kubaki katika nyumba ile ya Obedi-Edomu kwa miezi mitatu, na Mariamu leo nabaki nyumbani mwa Zakaria kwa muda wa miezi mitatu. Maneno ya Elisabeth pia; “Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?”, pia ndio maneno ya Mfalme Daudi kuwa imemtokeaje hata sanduku la Agano likamjia? (2 Samweli 6). Kuhusu Bikira Maria, jambo moja kubwa na la msingi tunaloliona ni kwa njia yake, mbingu inakutana na ulimwengu. Ni kwa njia ya Maria, Mungu anajimwilisha na kufanyika mwanadamu na kukaa kati yetu. Mwanafalsafa Jean Paul Sartre anasema; “Maria anajitambua kwa wakati mmoja kuwa Kristo ni mwanae, ni mtoto wake lakini pia ni mwana wa Mungu”. Ndio kusema Maria anapomwangalia mtoto Yesu anakiri kuwa kweli ni mwanae, lakini Maria haishii hapo tu bali pia anapiga hatua kiimani, kwa kumwona Yesu ni Mwana pekee wa Mungu. Ndio kusema kwa wakati uleule Maria anatambua kuwa Yesu ni mwanaye na pia sio mwanaye kwani ni Mwana pekee wa Mungu. Sio rahisi hili, yahitaji kama tulivyoanza tafakuri yetu ya leo; Naye heri aliyesadiki. Kumzungumzia Maria, ni kuzungumzia imani kama anavyotuambia Mtakatifu Yohane Paulo II.
Sartre anaendelea kusema; “Maria anamwangalia Yesu na kusema moyoni mwake: Huyu ni Mungu ni mwanangu. Huyu mtoto aliye Mungu anapata mwili kutokana na mwili wangu. Amezaliwa na mimi, ametapa macho kwangu, kinywa chake kimetokana na mimi, na anafanana na mimi kama mama yake. Ni Mungu anayefanana na mimi. Hakuna mwanamke mwingine yeyote aliye na bahati na kuwa mtoto aliye Mungu pia, Mwana wa Mungu ambaye anaweza kumchukua na kumbeba mikononi mwake na kumbusubusu, Mungu anayepata joto langu na kutabasamu, Mungu unayeweza kumshika na akacheka”. Ni maneno ya mwanafalsafa huyu kuonesha nafasi na hasa mahusiano ya kipekee kabisa anayokuwa nayo Mama yetu Bikira Maria. Kwa nafasi ya kwanza tumeona Maria kama Mama wa Mungu, ndio kusema ni zawadi na upendeleo wa Mungu kwa Maria. Lakini Elisabeth leo anatuonesha sio tu Bikira Maria alipokea upendeleo huo wa Mungu bali; “Naye heri aliyesadiki”. Maria pamoja na kujaliwa na kupata upendeleo huo wa Mungu, kwa upande wake naye anasadiki. Ndio ile kupiga hatua katika safari yake ya imani. Ndio safari ya imani ya Bikira Maria inaanzia pale alipokubali mpango wa Mungu katika maisha yake kwa maneno yale ya “fiat”, atendewe kama atakavyo Mungu. Bikira Maria hatangulizi mambo yake bali anatambua kuishi kweli ni kumtanguliza Mungu, kutanguliza sio mipango na matakwa yake binafsi bali kuishi ni kuishi katika mpango wa Mungu.
Maria si kwamba alielewa yote, bali daima alisukumwa na kuongozwa na imani thabiti kwa Mungu. Maria hakuwa na mashaka katika uaminifu na wema wa Mungu kwake, hivyo anajiachia na kujikabidhi mzima mzima ili mapenzi na mpango wa Mungu utumie kupitia yeye. Maria aliyaweka yote moyoni, ndio kusema aliamini, hata kabla ya kuelewa nini hasa maana yake mambo yale. (Luka 2:50-51). Na ndio tumesoma katika somo la Injili ya jana, katika Misa ya Mkesha ya Sherehe yetu ya leo; Wana heri wanaolisikia neno la Mungu na kuliishi. (Luka 8:21) Ni safari ile ya amani ambaye inafika ukomo na kilele chake pale Kalvario, mahali pa usiku wa giza la imani ya Maria baada ya kuona Mwana wake akifa pale juu msalabani, lakini ni hapo Maria anakuwa sas asio tu Mama wa Yesu bali ni Mama wa Kanisa zima. (Yohane 19:26) Hivyo, Maria ni mwalimu na kielelezo cha imani kwa kila mmoja, ni muonesha njia kama anavyoitwa na Kanisa la Mashariki, “Odighitria”.
Sehemu ya kwanza ya somo la Injili ya leo, ni wimbo wa kitaalimungu wa Elisabeth, ni wimbo unaomtambulisha Maria kama Mama wa Mungu na Mama yetu pia. Na sehemu ya pili ya somo ya Injili ya leo, ndio wimbo wa Maria, yaani, “Magnificat”. Wakati wimbo wa Elisabeth ulikuwa na ni wa kubariki na kutangaza heri, kubariki katika lugha ya Kibiblia na hasa katika Zaburi, ni kutangaza matendo makuu ya Mungu, mintarafu maskini na wanyenyekevu. Elisabeth leo anambariki Maria pamoja na uzao wa tumbo la Maria. Umebarikiwa wewe kati ya wanawake na uzao wa tumbo lako amebarikiwa. Makuu ya Mungu yanaonekana na kutendeka leo kupitia mwanamke, tena aliye binti mdogo kabisa, kwa njia ya Maria, Mwenyezi Mungu anaufunua ukuu na uwezo wake, ni kwa njia pia ya mtoto mchanga na mdogo kabisa tena ambaye bado kuzaliwa, Mungu anaonesha ukuu wake kwa ulimwengu. Ndio kusema Mungu anatumia viumbe wadogo na duni kabisa katika kuufunua ukuu wake.
Elisabeth pia leo ndiye anayeitangaza “heri” ya kwanza kabisa katika Injili. Na ndio heri inayomwelekea Maria kama kielelezo chetu cha imani. Utambulisho wa Elisabeta kwa Maria, kama tulivyotangulia kusema haukuwa wa kaiwada na hivyo ilimpasa Maria kuipokea salamu ile alipaswa naye kuwa na imani. Maria anatambulishwa kuwa ni Mama wa Mungu. Maria naye anapokea salamu na utambulisho ule kwa wimbo ule wa “Magnificat”, ambapo anazidi naye kuonesha ukomavu wake wa imani. Ni wimbo unaoonesha mantiki ya Mungu, Mungu anayejifunua sio kwa kutumia wenye nguvu bali walio wanyonge na wanyenyekevu, wanyonge na wanyenyekevu ndio wale wanaokubali mpango wa Mungu katika maisha yao, ni wale wanaotoa “fiat” kwa kila mpango wa Mungu unaokuja mbele yao katika maisha yao, ni wale wasio na shaka katika mpango wa Mungu, ni wale wenye imani ya kweli kwa Mungu na hivyo kujiachia na kujikabidhi wazima wazima.
Wimbo wa sifa wa Maria ndio unatuonesha kiini cha sherehe yetu ya leo, na hasa namna na jinsi ya kutenda kazi ya Mungu. Ni mwaliko kwetu kuwa kama Maria katika safari yetu ya imani, katika maisha ya kimisionari na ushuhuda kuwa daima wanyenyekevu, kukubali daima mpango wa Mungu katika maisha yetu hata kama hatuelewi vema, au tunapopita katika nyakati ngumu na zenye majaribu na giza nene. Ukuu na uwezo wa Mungu utaonekana tu katika maisha yetu ikiwa nasi tunakuwa kweli wafuasi wa Yesu Kristo wenye imani ya kweli na thabiti. Maria amepalizwa mbinguni mwili na roho, ndio kusema habanwi tena na muda wala nafasi, hivyo anatamani kuwa mama wa kila mmoja wetu, kutembea na kila mmoja wetu katika safari yetu ya imani. Basi kwa maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, tuzidi kumuomba Mungu ili atujalia nasi neema ya ujasiri wa kusema “fiat” kwa mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Niwatakie Dominika na sherehe njema ya Kupalizwa Mbinguni Mama yetu Bikira Maria na tafakari njema.