Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka B: Ekaristi Takatifu na Roho Mtakatifu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, leo ikiwa ni Jumapili ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa katika hekima na busara yake ya kichungaji, anaendelea kutupatia Katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ni Chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka, Shukrani, Kumbukumbu na Uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu na wafuasi wake. Huu ni uwepo wa Kristo Yesu kwa nguvu ya Neno na Roho Mtakatifu. Ekaristi Takatifu ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao! Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu Ekaristi takatifu kama chakula, neema na kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mwinjili Yohane kwa namna ya pekee kabisa, anaonesha uhusiano kati ya Ekaristi Takatifu na Fumbo la Utatu Mtakatifu. “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” Yn 6:32-33.
Chakula hiki cha uzima wa milele ni Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Hiki ndicho kielelezo cha Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele! Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa, imani thabiti kwa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu, ndicho kiini cha tafakari hii! Katika Somo la kwanza 1 Fal. 19: 4-8, linamwonesha Nabii Eliya, ambaye ni kati ya Manabii wanaoheshimiwa sana kwenye Agano la Kale. Hii ni kutokana na sababu kwamba, aliwasaidia Waisraeli kusimama imara katika imani kwa Mungu mmoja, licha ya “patashika nguo kuchanika” kutokana na madhulumu, nyanyaso na ukatili wa Yezebeli. Ndiyo maana Nabii Eliya alimkimbia na hatimaye, akajikatia tamaa na kuomba afunikwe na kifo! Lakini Mwenyezi Mungu akampatia chakula na maji yaliyomwezesha kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu hadi kuufikia Mlima Horebu, Mlima wa Mungu, mahali ambapo Mwenyezi Mungu alifunua ukuu na utukufu wake mbele ya Mtumishi wake mwaminifu Musa! Huu ulikuwa ni mpango mkakati wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaokoa waja wake kwa chakula kilichoshuka kutoka mbinguni!
Katika Somo la Pili Efe 4: 30-5:2. Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anawaangalisha Waefeso kamwe wasimsikitishe Roho wa Mungu waliyempokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa Kipaimara. Anawataka wawe ni watu wenye fadhila; vyombo vya huruma, upendo na msamaha, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Mababa wa Kanisa wanasema Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Utume huu wa pamoja toka hapo unawahusisha waamini wa Kristo katika ushirika wake pamoja na Baba ndani ya Roho Mtakatifu. Roho hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake, ili kuwapeleka kwa Kristo. Anamdhihirisha kwao Bwana Mfufuka, anawakumbusha neno lake, anafumbua akili zao kutambua kifo chake na ufufuko wake. Analifanya fumbo la Kristo liwepo kwao, juu ya yote katika Ekaristi, na mwisho kuwapatanisha na kuwaweka katika umoja na Mungu, ili wazae matunda mengi ya toba, wongofu wa ndani kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha! Rej. KKK 737.
Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, Yn 6:41-51 “Kashfa ya Fumbo la Umwilisho” inaendelea kujionesha kwa manung’uniko ya Wayahudi kwa sababu Kristo Yesu amesema kwamba, Yeye ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni! Wanamtambua kuwa ni Yesu, Mwana wa Yusufu! Watu hawa wana imani dhaifu kiasi cha kushindwa kumwona na kumtambua Mungu aliyejifunua kwao kwa njia ya Kristo Yesu. Kuamini ni kukubali kufungua macho ili kuona maajabu na matendo makuu ya Mungu katika maisha. Mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani anayo njaa na kiu ya maisha ya kiroho inayoweza kuzimishwa tu na chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti, Sala, Maisha adili na matendo ya huruma! Maisha ya kweli ni kumkubali na kumpokea Kristo Yesu, chakula chenye uzima wa milele!
Kama sehemu ya Katekesi endelevu na fungamani, Mwinjili Yohane katika sehemu hii, anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wakati wa Kipindi cha mageuzo, Padre anasali akisema hivi: Ee Bwana kweli u Mtakatifu na chemchemi ya utakatifu wote. Tunakusihi uzitakase kwa nguvu ya Roho wako dhabihu hizi ili ziwe mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo! Roho Mtakatifu analiwezesha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kuwa mwili mmoja na roho moja. Ekaristi Takatifu inajenga na kuliimarisha Kanisa. Waamini katika umoja wao na kwa mapaji na nguvu ya Roho Mtakatifu wanajenga Kanisa linalorutubishwa Neno la Mungu na kwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu na hivyo kushiriki pia maisha ya Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu inajenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Thoma wa Akwino anasema, uwepo wa Mwili kweli wa Kristo, na wa Damu yake Azizi katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hauwezi kufahamika kwa milango ya maarifa, bali kwa imani peke yake, ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mungu.