Tafuta

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo chakula cha uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo chakula cha uzima wa milele. 

Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka B: Fumbo la Mwili na Damu ya Yesu!

Kristo Yesu anajitambulishwa kwa kusema: “Ego eimi”, yaani, "Mimi ndimi". Ni utambulisho ambao wengi baada ya kumsikia wanakwazika nayo, kwani Yesu anajitambulisha juu ya Umungu wake, aliyetoka mbinguni, aliye kweli chakula na kinywaji cha uzima wa milele. Wayahudi wengi wanashindwa kulipokea Fundisho hili la uwepo wake endelevu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mama Kanisa katika Dominika hizi anatupa nafasi ya kuzidi kutafakari moja ya mafundisho magumu ya Bwana wetu Yesu akiwa katika Sinagogi la Kapernaumu, ni mafundisho ya utambulisho wake, ni moja ya mazungumzo ambayo Mwinjili Yohane anatuonesha kwa kutumia maneno yale ya Kigiriki “Ego eimi”, yaani, Mimi ndimi. Ni utambulisho ambao wengi baada ya kumsikia wanakwazika nayo, kwani Yesu anajitambulisha juu ya Umungu wake, aliyetoka mbinguni, aliye kweli chakula na kinywaji cha uzima wa milele.  Tangu mwanzoni tumeona kuna makundi matatu yanayopata shida kulipokea fundisho hili la Bwana wetu Yesu Kristo. Kundi la kwanza ni lile la makutano, kwani wao walikuwa wanamfuata Yesu kwa kuwa tu alitenda muujiza wa kuwalisha, hivyo wanashindwa kufika ukomo wa safari yao ya imani, kwao Yesu ni mtenda miujiza na hawaoni lingine lolote. Na kundi la pili ni lile tulilolisikia Dominika iliyopita, ndilo la Wayahudi, ndio wale wanaoshindwa kuipokea mantiki mpya, sura mpya na halisi ya Mungu kama anavyoifunua kwetu Bwana wetu Yesu Kristo. Na kundi la mwisho tutalisikia Dominika ijayo, ndio ya wale wanaokuwa karibu kabisa na Yesu, ni wanafunzi na wafuasi wake wa karibu.

Somo la Injili ya leo inaanzia na aya ile tuliyoisoma Dominika ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa ndio kusema inatupa utangulizi mzuri na pia kutusaidia katika kutoka Yesu Kristo kama mkate ushukao kutoka mbinguni, yaani kama Neno la uzima, kama hekima ya milele ya Mungu, na hivyo kutuingiza katika fundisho lingine la Ekaristi Takatifu. Wayahudi walielewa vema kabisa pale Yesu alipojitambulisha kuwa ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, alikuwa anamaanisha juu ya Injili yake, ujumbe wa Mungu ulioshuka kwa watu wake, na ndio hapo wakakwazika, walijikwaa kwa neno lile au utambulisho wake Yesu Kristo. Lakini tunaona pia leo Yesu Kristo anazidi kujitambulisha kuwa mkate wanaopaswa kuula sio tu Neno lake au Injili yake bali pia Mwili na Damu yake azizi. Na hata neno linalotumika na Mwinjili Yohane la kula halina maana ya kula ya kawaida au kula kistaarabu bali kula karibu sawa na Simba anaposhambulia mzoga, na neno la Kigiriki linalotumika hapa ni “troghein”, ndio kula na kutafuna kwa mtindo ule wa Simba au wanyama wa porini.

Na ndio hapo tunaona wasikilizaji wake wanazidi kujikwaa na kukwazika na fundisho hilo, na hasa Wayahudi ambao kwao ni haramu na hawakuruhusiwa sio tu kula nyama ya mwanadamu bali hata kugusana na damu. Damu ni chemchemi ya uzima, na mmiliki wa uzima ni Mungu pekee. Yafaa mara moja tuelewe kuwa kwa Wayahudi, mwili na damu haimaanishi tu nyama bali ni utambulisho wa mtu mzima na hasa udhaifu wake, mwanadamu ni mwili kwani ni kiumbe duni na hatima yake ni kifo au umauti. Hivyo Yesu leo anapotualika kula mwili wake na kunywa damu yake, ni sawa na kusema kufananisha maisha yetu na maisha yake, kuunganika naye, kuwa na mafungamano na mahusiano ya upendo na ya ndani kabisa kati yak ila mfuasi na Yesu Kristo mwenyewe. Na ndio tunaona hata katika tamaduni zetu, chakula sio tu kwa ajili ya kuijenga miili yetu bali pia ni kutuunganisha na kutufanya wamoja. Ni mwaliko wa Yesu Kristo kula mwili wake na kunywa damu yake, ni kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa naye, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda na kuishi na kuwa sawa naye katika kila kitu, kuongozwa daima na Neno lake katika nyanja zote za maisha yetu.

Kula mwili wake na kunywa damu yake, ndio pia kushiriki katika mateso na kifo chake, ni kuwa wamoja naye katika hali zote za maisha ya siku kwa siku kwa kila mfuasi wake. “Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” Ndio kusema wasikilizaji wake walielewa kuwa Yesu hakuwa tu anamaanisha kufananisha maisha yao na Neno lake bali pia anawaalika kuula mwili wake na kunywa damu yake, na ndio maana wanazidi kuulizana kwa kushindana kati yao. Na ndio hapo tunaona Yesu badala ya kujaribu kulainisha lugha yake anazidi kuwaalika sio tu mwili wake bali pia na kunywa damu yake. Ni ndio hapa tunaona wasikilizaji wake wanazidi kujikwaa katika fundisho hilo, wanakwazika kwa mafundisho haya ya Yesu kwani kama tulivyotangulia kuona kuwa kwa Myahudi ilikuwa ni mwiko na haramu kubwa sio tu kunywa bali hata kugusa damu. (Walawi 7:26-27; 17:10-11) Na hata leo Wayahudi wanapochinja mnyama kwa ajili ya kitoweo wanahakikisha kuitoa damu yote, na kuizika ardhini kwani hapo wanaamini ndio kuirudisha kwa Mungu mwenyewe, mtoaji wa uzima.

Kwenye damu ndiko ambako uhai unapatikana na ndio maana tunaona hata katika ibada nyingi za Agano la Kale, kunatumika damu kama mojawapo ya vitu muhimu kuwepo. Wanawaisraeli wanafanya agano na Mungu chini ya mlima Sinai kwa kutumia damu. (Kutoka 24:6-8) Na kwa ishara hiyo ya damu ni kama wameingia mahusiano ya ndani kabisa na Mungu, ni kama wanaunganishwa na ile damu, ile chanzo cha uhai na uzima. Ni kama ndugu wa damu wanavyohusiana basi ni kwa ishara ya damu nao wanaingia katika mahusiano mapya na ya ndani kabisa na Mungu. Na ndio katika muktadha huo pia Yesu leo anatualika kula mwili wake na kunywa damu yake, ndio kusema nasi tunaolikwa kushiriki meza ile ya Mwili na Damu yake, tunaalikwa kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa na Bwana wetu Yesu Kristo. Pamoja na kuwa Yesu Kristo tayari ametufundisha kuwa kila aaminiye huyo hakika ataokoka, ataupata uzima wa milele, lakini pia leo anazidi kutufundisha pia; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho.” Safari ya imani inatualika kufika pia kileleni na ndio kwenye kuunganisha maisha yetu na Yesu Kristo, ya kuwa wamoja naye, na ndio anatuonesha kuwa ili kuunganika naye kwa namna ile ya juu kabisa, anajitoa sadaka na kuwa chakula chetu cha kiroho.

Hivyo imani ni muhimu kabla ya kujongea meza ile ya Ekaristi Takatifu. Imani kama wasemavyo Walatini ni “Conditio sine qua non” ili kuweza kuijongea altare ya Ekaristi Takatifu na ndio maana katika Ibada ya Misa Takatifu tunakutana kwanza na Meza ya Neno na tunahitimisha na Meza ya Mwili na Damu yake Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya imani, haiwezi kuzaa matunda na wala kubadili maisha yetu ikiwa hatuipokei kwa imani kubwa. Ili kuwa kweli mwili mmoja na Bwana wetu Yesu Kristo hatuna budi kuyafananisha kwa nafasi ya kwanza maisha yetu na Injili yake, na Neno lake. Ni kama kusema hakuna anayeweza kuingia mkataba na mtu mwingine kabla ya kuusoma mkataba wenyewe, mkataba hapa ni Neno la Mungu, hivyo daima tunaalikwa kumsikiliza Yesu Kristo mwenyewe katika Injili yake kabla ya kuijongea meza ile ya Ekaristi Takatifu. Bila kuishi Neno lake basi maisha yetu yanakosa maana na hata kuijongea meza ile ya Ekaristi Takatifu inakuwa ni sawa na kufuru.

Ekaristi Takatifu ni Mwili na Damu yake Bwana wetu Kristo, hivyo sio mlo wa kawaida tu kama tunavyoweza kula milo mingine, ni mlo mtakatifu, ni mlo wenye madai, wenye kututaka kuyafananisha maisha yetu na yake Bwana wetu Yesu Kristo. Ni mlo unaotutaka kila mshiriki kuishi kweli za Injili, kuishi Neno lake Bwana wetu Yesu, na hivyo sisi washiriki wa meza ile kufananisha maisha yetu na kile tunachokiadhimisha. Wakristo wa kwanza walitambua umuhimu wa kukutana kila Dominika ili kama jumuiya kushiriki na kuadhimisha fumbo lile la mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Walikusanyika kama tufanyavyo nasi leo kusikiliza kwanza Neno la Mungu na pia kwa pamoja kushiriki katika meza na karamu ile ya upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu. Ni muhimu kwa kila mmoja tunaposhiriki Ibada za Misa Takatifu iwe kila siku au siku zile za lazima hasa Dominika kukumbuka na kuzingatia kuwa tunaalikwa kulisikiliza Neno lake ili tuweze kuliishi na katika meza ya Ekaristi Takatifu tunapata nguvu ya kuliishi na kulishika Neno lake, nguvu ya kufananisha maisha yetu na yake, kuwa Injili, au Habari njema inayotembea, kuwa mashahidi wa kweli za Injili kwa maisha yetu. Ninawatakia tafakuri na Dominika njema.

 

11 August 2021, 15:18