Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka A: Makwazo Kumhusu Kristo Yesu!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa naye aniaminiye hataona kiu kamwe.” Haya ndio maneno ya hitimisho la somo ya Injili ya Dominika iliyopita. Yesu anajitambulisha kwa wasikilizaji kwa namna ambayo iliwakwaza, ni maneno yaliyoweka imani yao njia panda, na hapo ndio tunaona wasikilizaji wake ambao Mwinjili anawatambulisha kama “Wayahudi” walimnung’unikia Yesu kutoka na maneno hayo. Wayahudi waliamini kuwa na ukweli wote, na ndio Torati na Manabii. “Atamlisha mkate wa ufahamu, na kumnywesha maji ya hekima.” (Yoshua bin Sira 15:3) Hivyo ndio kusema mkate wa uzima ni Neno la Mungu ambalo Wayahudi waliamini kuwa nalo katika ukamilifu wake, ndio Torati na Manabii na Vitabu vingine vya Maandiko Matakatifu. Kwao ilikuwa ni makwazo makubwa kwani Yesu leo anajitambulisha kuwa ni Yeye aliye mkate wa uzima wa milele, ni kwa kulisikiliza na kulishika Neno lake kila mwenye njaa na kiu atashibishwa na hataona njaa wala kiu tena. Wayahudi walishindwa kuupokea utambulisho wa Yesu kama chakula cha uzima na wakabaki kumwona kama Mwana wa Yusufu tu, na tena waliyemfahamu vema hata kazi na ujira wake kuwa ni ule duni kabisa na zaidi sana hata mama yake pia walimfahamu.
Ni watu waliomfahamu vema na vizuri na kwa nini basi anajitambulisha na kujifananisha kuwa ni Mungu, ni kutoka mbinguni? “Wakasema, huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, nimeshuka kutoka mbinguni?” Na tunasikia manung’uniko haya hawakumwelekezea Yesu bali yalikuwepo baina yao, miongoni mwao, kati yao wenyewe. Kunung’unika sio kitendo kile cha kulalamika tu, naomba kieleweke na Mwinjili anakitumia kitenzi hicho kuonesha mkwamo wao wa kiimani, kukwazika na kujikwaa kwao kwa fundisho lenye utambulisho mpya kumuhusu Yesu, utambulisho ambao unamfunua Yesu kuwa si tu mwanadamu kweli bali pia ni Mungu, ametoka kwa Mungu, amekuja kuifunua katika ukamilifu sura halisi ya Mungu. Kwao haikuwa jambo rahisi na lenye kueleweka kuwa kwa njia ya Yesu hekima ya Mungu imejimwilisha na kukaa kati yao, na kuwa katikati yao. Hakika muktadha wa somo la Injili ya leo, tunaona Yesu anatoa mafundisho haya akiwa Galilaya katika sehemu ile ya Kapernaumu, kama ndivyo basi kwa nini mwandishi anawataja wasikilizaji wake kama Wayahudi na sio Wagalilaya? Na zaidi sana swali lao linatusaidia japo kuelewa kwanini Mwinjili Yohane anawatamka kama Wayahudi; “Sasa asemaje huyu, nimeshuka kutoka mbinguni?”
Wayahudi waliamini kuwa hakuna mtu aliyemwona Mungu na kuishi, na hata hawezi kuonekana kwa macho ya nyama, kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale. “Akazidi kusema: Huwezi kuniona uso wangu, kwa maana mwanadamu hawezi kuniona akaishi.” (Kutoka 33:20) Ingawa ilikuwa ni hamu ya mwanadamu daima kuuona uso wa Mungu, kukutana naye ili kutambua mipango na mapenzi yake kwa mwanadamu. “Musa akamwambia, Nakuomba unioneshe utukufu wako.” (Kutoka 33:18) Ni wazi Mwenyezi Mungu amekuwa akijifunua na kujidhihirisha kwa namna mbali mbali kwa kupitia viumbe au katika uumbaji wake. “Lakini ama moto au upepo, ama hewa nyepesi au mzunguko wa nyota, ama maji ya kasi ay mianga ya mbingu, walihesabu kuwa ndiyo miungu, inayotawala ulimwengu.” (Hekima ya Sulemani 13:2). Si kwamba Mungu ni mmoja wa hivi viumbe bali walibaki na mshangao mkubwa wa uzuri wa uumbaji kiasi cha kuona lazima nyuma yake kuna Mungu mwenye ukuu na uweza na uzuri wote katika ukamilifu wake, na hivyo viumbe vingine vyote vulishirikishwa uzuri na ukuu na enzi ile kamilifu. Na ndio tunasoma pia katika Waraka kwa Warumi; “Kwa maana yajulikanayo katika Mungu yamefunuliwa ndani yao, kwani Mungu amewafunulia hayo. Tena, tangu kuumbwa ulimwengu, yale yasiyoonekana katika Mungu yanatambulikana katika matendo yake kwa wenye kutumia akili, yaani uwezo wake wa milele na umungu wake.” (Warumi 1:19-20).
Mungu si tu amejifunua kupitia uzuri na ukuu katika uumbaji wake, bali zaidi sana wakati wa neema ulipowadia, ndio “Kairos”, Mungu akajimwilisha, akautwaa ubinadamu wetu na kukaa kati kati yetu ulimwenguni, ndio Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu Hili ndilo Fumbo la Umwilisho. Sasa tunaweza kumwona, kumgusa na kumsikiliza katika nafsi ya Yesu wa Nazareti, ambaye ndiye sura halisi ya Mungu katika sura ya kibinadamu, na ndio maana Yesu anatukumbusha kila anayemwona yeye basi amemwona Baba. (Yohane 14:9-11) Wayahudi wananung’unika, ndio kusema wanakwazika na kujikwaa kwa fundisho hilo gumu la kumtambua Yesu kama Mwana pekee wa Mungu, kama sura halisi ya Mungu kwetu wanadamu. Wanakwazika kuona Mungu anayetwaa ubinadamu wetu na kukaa kati kati yetu, na kuwa mmoja baina yetu isipokuwa hakuwa na dhambi, na tena aliyezaliwa katika familia ya kawaida kabisa, na hata duni na wazazi waliojulikana hata kazi zao za hali ya chini kabisa. Kwao Mungu ni mwenyeenzi, yupo katika kiti chake cha enzi mbinguni na kamwe hawezi jirani au karibu na mwanadamu. Mungu hawezi kujifunua katika hali duni na nyonge kama ile waliyoiona na kukutana nayo, wanashindwa kumuona Mungu, kuiona sura halisi ya Mungu katika sura ile ya Yesu Kristo.
Yesu anawafundisha na kuwaambia leo Wayahudi; “Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.” Pamoja na kuwa hakuna aliyemwona Baba, lakini leo Yesu anatufundisha kuwa ni kwa njia yake nasi tunaweza kuutafakari ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Ikiwa kwa wengine, kwa njia ya ubinadamu wa Yesu, wanapata fursa ya kukutana na Mungu, kwa wengine ni makwazo ya kujikwaa na kuwakwamisha katika safari yao ya imani. Na hii si tu nyakati zile za Yesu bali hata katika ulimwengu wetu wa leo, wapo wengi wasioamini ufunuo huu wa sura halisi ya Mungu kupitia Mwana wa Mungu aliyefanyika mwanadamu na kukaa kati kati yetu, kuwa sawa nasi isipokuwa hakuwa na dhambi. Na ndio maana tangu mwanzoni niliwaalika kujua sababu za Mwinjili Yohane kuwatambulisha wasikiliza wa Yesu kama Wayahudi na si Wagalilaya. Iweje Yohane anawatambulisha wasikiliza wa Yesu kama Wayahudi na sio Wagalilaya kwani mafundisho haya Yesu anayatoa akiwa Kapernaumu, ndio mji mdogo katika mkoa ule wa Kaskazini, yaani wa Galilaya. Na kwa kweli ni Wagalilaya na hasa watu wa Nazareti waliomfahamu Yesu pamoja na wazazi na familia yake, haikuwa watu kutoka Yudea kwani walikuwa ni watu wa mbali kabisa na hata yawezekana hawakufahamu mengi kumuhusu au utambulisho wake na asili na familia yake.
Ndio tunaona Mwinjili Yohane anapotumia neno “Wayahudi”, hakuwa na maana ya kutambulisha watu wa eneo fulani la Kijiografia, bali alikuwa na nia na lengo la Kiteolojia. Myahudi au Wayahudi ni wale wote wanaoshindwa kumwamini Yesu, kuiona sura halisi ya Mungu kwa njia ya Yesu wa Nazareti, wanashindwa kuwa na imani kwa Yesu. Ndio kusema somo la Injili ya leo, halizungumzii Wayahudi wale walioshi miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, bali kwetu sisi tunaolisoma somo hili na kulitafakari. Ni mwaliko kwangu na kwako katika kumpokea Yesu kama mkate wa uzima, kwa njia ya Neno lake na Sakramenti zake na zaidi sana katika Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi, ndio Ekaristi Takatifu. Ni kwa Yesu tunaalikwa kuupata uzima wa kweli, ndio uzima wa milele, hakika na furaha isiyo na mwisho, ni ile ya kuunganika na mantiki ya Mungu mwenyewe iwe tunaishi duniani na hata baada ya kufa. Mfuasi wa kweli, au mmoja anayekubali kuongozwa na neema za Mungu ndiye yule anayajibidisha kila siku za maisha yake kujimwilisha Neno la Yesu Kristo, kuishi Injili, kuwa Habari Njema inayotembea na kumtangaza Kristo kuwa kweli ni Mtu kweli na Mungu kweli!
Kwa bahati mbaya hata katika ulimwengu mamboleo, bado wapo wengi ambao wanabaki kumtambua Yesu kama mtenda miujiza tu, mtu mwenye karama ya ajabu, anayestahili heshima na kustaajabiwa, mwalimu wa njia za haki na amani, mwana wa Yusufu Mseremala, na kushindwa kufika katika imani ya kumwona kama Mwana pekee wa Mungu. (Yohane 1:14). Na wanashindwa kuamini kuwa ni njia ya Yesu Kristo, Mungu anaukomboa ulimwengu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohane 3:16) Labda tunaweza kujiuliza kwa nini ugumu, kwa nini wengine wanajikwaa kwa fundisho hili la kumtambua Yesu kama chakula cha kweli na cha uzima wa milele? Jibu la swali hili linajibiwa pia katika sehemu ya Injili ya Dominika ya leo. “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Kumtambua Yesu kama Mwana wa Mungu, kama mkate wa uzima, sio matokeo ya juhudi zetu za kibinadamu au akili zetu bali ni matunda ya neema za Mungu kwa mwanadamu.
Ni wale tu wanaoruhusu neema hiyo kufanyakazi ndani mwao, hao kwa hakika hawatajikwaa bali watafikia imani katika Mwana pekee wa Mungu, aliye kweli chakula cha uzima wa milele, kinyume chake ni kubaki kumuona kama mwana wa Yusufu na Mariamu tu, mmoja aliyewahi kuishi katika historia ya mwanadamu. Mungu hana upendeleo kwani kila mmoja anajaliwa neema hizi, ila Mungu anaheshimu uhuru wetu kila mmoja wetu katika kupokea mantiki yake ya Kimungu katika maisha ya mwanadamu. Ni Mungu anakuja na kukaa kati yetu, anayejifunua kwetu, lakini kila mmoja anabaki na uhuru wa kuamua kuchagua uzima au mauti, na ndio kusema Mungu hamwangamizi mwanadamu bali ni mwanadamu anayaangamiza na kuyapoteza maisha yake kwa kukataa mpango na chakula cha uzima wa kweli na wa milele. Ni mwaliko kwetu kila mara kumruhusu Roho wa Mungu aongoze maisha yetu, atufundishe kweli yote ili mwishoni tuweze kuzijua kweli za mbinguni. Ili mwishoni tuweze kuwa na hakika ya uzima wa milele. Neno lake halina budi kumwilika katika maisha yak ila mfuasi, ni kwa njia ya Neno lake, kila mmoja wetu anakuwa na hakika ya uzima wa milele pamoja na masakramenti yake na hususani Ekaristi Takatifu, kwani ni Yesu Kristo mzima na kamili katika maumbo yale duni ya mkate na divai. Niwatakie tafakari na Dominika njema!