Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho! 

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka B: Ekaristi: Chakula Cha Kiroho!

Masomo ya Jumapili ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa yanatualika na kutusisitiza kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuuelekea uzima wa milele mbinguni tukiambiwa kila mmoja wetu; “Amka, Inuka ule, maana safari hii ni ngumu kwako.” Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni chakula cha maisha ya kiroho!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatualika na kutusisitiza kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuuelekea uzima wa milele mbinguni tukiambiwa kila mmoja wetu; “Amka, Inuka ule, maana safari hii ni ngumu kwako.” Somo la kwanza la katika kitabu cha kwanza cha Wafalme (19:4-8); linatusimulia habari za kutoroka kwa Nabii Eliya kwa kukata tamaa kwa maovu yalikidhiri kwa watu wake kiasi cha kutamani kufa ndiyo maana akiwa chini ya mretemu anajiombea roho yake afe akisema; “Yatosha sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Eliya yuko katika hali hii kwa sababu ya ukatili wa Yezebeli na kuasi kwa Waisraeli. Malaika wa Bwana anamwimarisha na kumpa mkate uliookwa juu ya makaa ale na gudulia la maji anywe ili aendelee na safari hadi Horebu, mlima wa Mungu akimwambia; “Inuka, ule maana safari hii ni ngumu mno kwako. Naye akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu. Chakula hiki anachokula Eliya ni ashirio la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Kristo, chakula cha kiroho, kinachotupa nguvu katika safari ya kuelekea mbinguni kwa Mungu Baba.

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (4:30-5:2); linatukumbusha kuwa tulipobatizwa, Roho Mtakatifu alitutia muhuri, alama ya kufanywa kuwa wana wa Mungu. Tusimsikitishe Roho huyo wa mapendo akaaye ndani yetu kwa kufarakana kati yetu, bali tuvumiliane na kusameheana kwa moyo wote. Paulo anasema; “Msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kama harufu ya manukato.”

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:41-51); inatuambia kwa kuwa Wayahudi waliwafahamu wazee wake Yesu, waliona vigumu kumsadiki kuwa alitoka kwa Mungu. Yesu anakubali ugumu huo kwani wale tu wanaovutwa na Mungu watamsadiki na kuwa na uzima wa milele. Nasi tukimdadiki na kutimiza asemayo, tutakuwa na uzima huo. Sababu ya Wayahudi kumnung’unikia Yesu na kushindwa kumwamini ni fundisho lake juu ya mkate wa uzima, chakula kishukacho toka mbinguni, ndio mwili na Damu yake/Ekaristi Takatifu. Baada ya Yesu kusema; “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele na akasisitiza kuwa chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” basi wakasema; huyu siye Yesu ambaye twajua babaye ni Yusufu mseremala, na mamaye ni Maria? Sasa asemaje kuwa nimeshuka kutoka mbinguni? Yesu anawaambia wasinung’unike kwa maana sio kwa nguvu na uwezo wao wanaweza kumsadiki bali ni kwa neema na baraka za Mungu Baba zinazowafanya waweze pia kufufuliwa siku ya mwisho. Yesu anasisitiza kuwa; Yeye aaminiye yu-na uzima wa milele.

Ekaristi Takatifu, adhimisho la Misa ni adhmisho la Sadaka ya Msalaba. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unatufundisha kuwa; kila inapoadhimishwa Ekaristi kazi ya ukombozi wetu inakamilika. Kwa hiyo, tunaalikwa tuadhimishe Ekaristi Takatifu kila mara ili tupate ukombozi ambao Kristo alitutafutia msalabani ili tuweze kuishinda dhambi katika maisha yetu. Ekaristi Takatifu ni silaha ya kupambana na dhambi na nguvu za shetani. Ekaristi Takatifu ni namna ya Yesu kukaa kati yetu ndiyo maana anasema; “Tazama mimi niko pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari” (Mt. 28:19-20). Maisha ya hapa duniani yana magumu mengi; tunahitaji kuwa na ulinzi wa Mungu. Ekaristi Takatifu inatuunganisha na Kristo na kutufanya watoto wa Mungu. Tunapopokea Ekaristi Takatifu tunaungana na Kristo kwa namna ya ajabu. Kristo mwenyewe anasema; “aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Ekaristi Takatifu inatufanya tuwe watoto wa Mungu kwani tunampokea Kristo mwenyewe. Yohane anasema; “wale wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (Yn. 1:12).

Hii ni kwa sababu tunakuwa kile tunachokula. Tunapompokea Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai tunakuwa sehemu ya Mwili na Damu yake Kristo, tunakuwa na ukristo ndani mwetu, tunakuwa Krsito. Ekaristi Takatifu inatupa nguvu za kupambana na dhambi na tabia mbaya ndani mwetu kwa sababu tunakuwa na Roho wa Kristo aliyeshinda dhambi na mauti ndani mwetu. Wimbo wa katikati unatualika kumpokea Kristo ili tuuonje wema wa Bwana ukisema; “Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema.” Ekaristi Takatifu ni amana ya uzima wa milele ndiyo maana Yesu anasema; “Yule anilaye yu na uzima wa milele.” Ekaristi Takatifu inatushirikisha maisha ya kimungu kwani ni chakula cha kutupeleka mpaka ukamilifu wa maisha ya mbiguni ndiyo maana Yesu anasema; “anilaye mimi nitamfufua siku ya mwisho.” Nani asiyependa kwenda mbiguni? Inuka basi ule maana safari hii itakua ngumu kwako. Ekaristi Takatifu inatuunganisha sisi kwa sisi. Kama Ekaristi Takatifu inatufanya watoto wa Mungu basi inatufanya ndugu wa Kristo. Hivyo, sote ni ndugu. Ekaristi Takatifu licha ya kutuunganisha hivyo, inatusaidia kumuona mwenzako kuwa ndugu.

Ndiyo maana Paulo katika somo la pili anasema; “uchungu wote na hasira viondoke kwenu.” Ekaristi Takatifu ni mwanzo na mwisho wa maisha ya Mkristo. Neema za kuweza kuishi vema maisha ya nje tunazipata katika Ekaristi; maisha ya nje ni mwendelezo wa sadaka ya Ekaristi yanayokamilika katika adhimisho jingine la Ekaristi Takatifu tunapotolea hayo maisha kama sadaka. Hii inaendelea mpaka Kristo atakaporudi. Hivyo, basi tufanye hima kuvunja kuta zote zinazotuzuia kupokea Ekaristi Takatifu, tufanye hima kuipokea Ekaristi Takatifu. Tusiidharau Ekaristi takatifu kwani ndiyo amana ya uzima wa milele.

J 19 Mwaka B
05 August 2021, 16:16