Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka B: Maneno ya Uzima wa Milele!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Leo katika sehemu ya somo la Injili, Yesu anahitimisha mafundisho yake marefu, ya kujitambulisha kwake, “Ego eimi”, yaani, “Mimi ndimi”, mkate ushukao kutoka mbinguni, mkate wa uzima wa milele. Ni mafundisho ambayo Yesu anayatoa akiwa katika Sinagogi la Kapernaumu. Ni moja ya mafundisho magumu si tu kwa makutano, bali kwa Wayahudi na hata leo tunaona hata kwa wanafunzi wake wa karibu. Kundi la kwanza, ndio lile la makutano waliomfuata Yesu kama mtenda miujiza, kama mmoja anayeweza kuwalisha na kushiba na hata kusaza, lakini mwisho Yesu anawaonesha ili kuwa wafuasi wake, hawana budi kumpokea Yeye mwenyewe kama mkate ulioshuka kutoka mbinguni, yaani kulipokea Neno lake. Kulishika na kulipokea Neno lake, ni mwaliko wa kubadili namna zao za kufikiri na kutenda, na hapo ndipo watapata uzima wa kweli na wa milele. Kundi la pili ndilo lile la Wayahudi, kwa maana sio ya taifa bali viongozi wa dini, ambao nao wanajikwaa kutokana na mafundisho ya utambulisho wa Yesu, anapojitanabaisha kama mmoja atokaye mbinguni, kama Mungu.
Na sehemu ya Injili ya leo, tunasikia kundi la tatu la wasikilizaji, baada ya makutano na Wayahudi, ajabu leo tunatajiwa kundi lingine nalo ndio la wanafunzi wa Yesu. Mwinjili Yohane anajaribu kuonesha kwa jumuiya yake aliyokuwa anaiandikia Injili hii na hata kwetu nasi leo, kujua maana halisi ya kumfuasa Yesu ni kuwa tayari kubadili vichwa vyetu, kuwa na namna mpya ya kufikiri na kutenda kadiri ya kweli za Injili, na kamwe sio kwa akili na mantiki zetu za kibinadamu. Mwitikio wa wasikilizaji wa mafundisho ya Yesu pale Kapernaumu pamoja na kuona muujiza ule wa kuwalisha watu wengi mikate bado tunaona ni hasi. “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?” Naomba hapa kwa kulisikia ina maana ya nani anayeweza kulielewa? Ni karibu na kusema anachozungumza kwetu hakiingii akili na wala akina mantiki wala hoja yenye mashiko. Ni mafundisho yanayokuwa ni sawa na jiwe lenye kuwapelekea kujikwaaa njiani, na ndio makwazo na wao wanakwazika.
“Neno hili ni gumu”, ni maneno yanayotupa mwitikio wa wasikilizaji wa makundi yote matatu, makutano waliofuata mikate, Wayahudi walioshika mapokeo na hata wanafunzi na wafuasi wake. Ni fundisho gumu la kumtambua Yesu kuwa ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, ni mkate wa uzima wa milele, anayejitoa Yeye mwenyewe yaani mwili na damu yake kwa ajili ya uzima wa milele. Ugumu haukuwa katika kulielewa tu neno lake, bali hasa madai yatokanayo na mafundisho yake, madai ya kuwataka kuunganisha maisha yao pamoja na ya Yesu Kristo, kuwa tayari kujitoa wazimawazima, kwao hili ni neno gumu, ni neno lisiloingia akilini na kuleta maana. Yesu anatutaka nasi leo kutokubaki kati kati bali kufanya maamuzi ya dhati na ya kweli katika kumfuasa yeye. Ukristo ni kuwa tayari kufanya maamuzi magumu, maamuzi ya kukubali kuishi sio tena kwa mantiki zetu, bali kuwa tayari kubadili vichwa, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, kuishi katika ya Injili na si kinyume chake, hakuna tena maamuzi ya mtumba, maamuzi ya pungufu unaongea, bali daima tunaalikwa bila kujibakiza kuishi kweli za Injili. Hi indio gharama ya ufuasi!
Hakuna tena nafasi ya kusema tunazikubali kweli baadhi za Injili, na nyingine basi tunaweza kuongozwa na mantiki ya soko la mitumba, pungufu unaongea.Na leo tunaona Yesu anatutaka sio tu kulipokea na kulishika Neno lake, bali zaidi anatutaka pia tuijongee meza ile ya upendo wake, ndio meza ya Ekaristi Takatifu. Ekaristi Takatifu sio mlo wa kawaida kama milo mingine tunayoweza kuwa nayo, bali ni Yesu halisi na kamili katika maumbo yale ya mkate na divai, ni Yesu anayejitoa sadaka na kuwa chakula chetu cha kiroho, ni Yeye anatualika kula mwili wake na kuinywa damu yake. Mwili na damu yake hapa sio lugha ya picha, bali ni kweli mwili na damu yake Bwana wetu Yesu Kristo. Na ndilo fundisho analotupa hata nasi leo, na ndio mwaliko kwa kila muumini wa kuijongea meza ya karamu ya upendo wa Kimungu kwetu. Hata baada ya kuona fundisho hili kuwa gumu, kutoeleweka vema si tu na makutano, Wayahudi na wanafunzi wake. Yesu bado haongozwi na ile mantiki ya soko la mitumba, ya pungufu unaongea, kwani Yesu hajaribu kulegeza au kubadili msimamo na mafundisho yake, bali zaidi sana anawaonesha mengine yanayoweza kuwa magumu mbele yao. “Je!
Neno hili inawakwaza? Itakuaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwa kwanza? Ndio kusema kama sasa Yesu angali yupo pamoja nao bado wanapata ugumu kumuelewa, je ikifika saa ile ambapo atakuwa amerejea katika utukufu wa mbinguni? Ndio kusema heri yao wasioona wakaamini na kusadiki. “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu” Ili kulipokea na kulielewa fundisho hili la Yesu, tunaalikwa kuingia katika ulimwengu wa kiroho na kuachana na mantiki na mitazamo ya kiulimwengu. Ni kukubali kuwa na kichwa kipya, sio tena kinachoangalia na kutenda kadiri ya mantiki ya kidunia bali ile ya Mungu mwenyewe. Hekima na akili za dunia hii haziwezi kutusaidia kufika katika mafumbo makubwa ya Kimungu bali ni kwa msaada wa neema za Mungu mwenyewe. “Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yanayotoka kwa Roho wa Mungu kwa sababu mambo hayo ni upuuzi kwake; na hawezi kuyaelewa kwa kuwa hayo yanaeleweka tu kwa msaada wa Roho”. (1 Wakorintho 2:14)
“Hakuna awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Na ndio Yesu anazidi kutuonesha kuwa imani ni zawadi, ni neema itokayo kwa Mungu, ni Mungu anayekuja na kukutana na mwanadamu, ili apate kuyatawala na kuyaongoza maisha yake, ili aweze kufikiri na kutenda sio tena kwa namna zetu bali kwa ile ya Mungu mwenyewe, kadiri ya kweli za Injili na si kinyume chake. “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.” Wanarudi nyuma kwa sababu za madai ya ufuasi, gharama za ufuasi, na ndio hata leo madai na gharama ni zile zile, ni daima ili tuwe kweli wanafunzi na wafuasi wake hatuna budi kuyabadili maisha yetu, kukubali kuongozwa na mantiki za Injili na sio zile za akili na matakwa yetu bali kadiri ya Mungu mwenyewe. Kuijongea meza yake na kuupokea mwili na damu yake, ni kukubali kuwa ndugu wa damu pamoja na Yesu Kristo, ni sawa na kusema hatuwezi kitu bila yeye, hatuwezi kupiga hatua katika maisha yetu ya kumwelekea Mungu bila msaada wake tunaoupata kwa kula mwili na damu yake.
Wakristo wa Karne ya nne wa Afrika ya Kaskazini walikamatwa pale walipokusanyika siku ya Dominika na kuadhimisha Ekaristi Takatifu. Alipoulizwa na liwali mmiliki wa nyumba ile aliyejulikana kama Emeritus, kuwa kwa nini aliruhusu watu kukusanyika nyumbani kwake, alijibu, kwa kuwa watu wale ni kaka na dada zake. Na hata Liwali aliposisitiza kuwa alipaswa kuwazuia watu wale kukusanyika nyumbani wake, Emeritus alijibu kwa Kilatini: “Quoniam sine dominico non possumus”, yaani ingawa sio tafsiri sisisi ni, “Bila siku ya Bwana (Dominika), hatuwezi kuishi” Kwao haikuwa swala la kuamua au hiari, bali Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ndio vitu vya msingi na lazima katika maisha yao. Na hi indio inapaswa kuwa mwitikio wetu nasi baada ya kulisikiza kwa mfululizo kwa Dominika karibu tano juu ya utambulisho wa Yesu kama mkate ushukao kutoka mbinguni na kama chakula cha uzima, hivyo nasi hatuna budi kuwa na hamu na shauku ya kuadhimisha kila Dominika meza ya Neno na ile ya Ekaristi Takatifu. Thenashara wanatoa jibu lenye kuhitimisha somo la Injili ya leo, jibu ambalo linapaswa kuwa la kila mmoja wetu kama nilivyoonesha simulizi hapo juu la jumuiya ya wakristo wa karne zile za mwanzoni kabisa mwa Ukristo. Hata baada ya makundi mengine kuliona fundisho hili ni gumu na kuamua kuachana na Yesu, Yesu anawageukia wanafunzi wake na kuwauliza kama nao wanataka kuondoka, kama nao hawapo tayari kubadili vichwa vyao na kumtambua Yesu kama mkate ulioshuka kutoka mbinguni, na kama chakula na kinywaji cha uzima wa milele.
Simon Petro anajibu kwa niaba ya wale wengine wote na hata nasi leo; “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe mtakatifu wa Mungu.” Jibu la Petro hakika halikutokana na ukweli kuwa alielewa vema fundisho lile la Yesu, bali kama anavyokiri amesadiki na ndio hata nasi leo ambapo wengi wanahoji na kuuliza juu ya Ekaristi Takatifu kuwa kama ni kweli ni mwili na damu yake Yesu, kama anavyojibu Mtakatifu Toma, kuwa hatuoni kwa macho yetu ya nyama bali kwa yale ya imani peke yake, ni fundisho linalotutaka kuwa na imani. Imani sio tunza au zao la kweli za kisayansi za kuweza kuthibitishwa katika maabara, bali ni kujikabidhi wazimawazima pasi kuwa na mashaka, na ndio inatutaka kuingia katika mahusiano ya upendo na uaminifu kwa Mungu na yale ambayo ametufunulia kwa njia ya Neno lake na Sakramenti yake. Imani inatudai kubadili vichwa vyetu na kufikiri na kutenda kadiri ya kweli za Injili, katika ya maongozi ya Mungu kwetu wanadamu. Nitawakie Dominika na tafakari njema.