Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 21 ya Mwaka B wa Kanisa: Ekaristi Takatifu Zawadi ya Imani: Huduma na Uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 21 ya Mwaka B wa Kanisa: Ekaristi Takatifu Zawadi ya Imani: Huduma na Uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! 

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka B: Imani, Huduma na Uaminifu kwa Yesu!

Masomo ya dominika ya 21 ya Mwaka B wa Kanisa yanatuasa kuwa na msimamo mmoja katika maisha na msimamo ulio wa maana na wenye tija ni kuwa upande wa Mungu, ni kumtumikia Mungu tukifuata maongozi ya Yesu Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Hivyo tunaalikwa kufanya uamuzi wa kumfuata na kumtumikia Mungu. Ekaristi Takatifu, Huduma na Uaminifu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa kuwa na msimamo mmoja katika maisha na msimamo ulio wa maana na wenye tija ni kuwa upande wa Mungu, ni kumtumikia Mungu tukifuata maongozi ya Yesu Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Hivyo tunaalikwa kufanya uamuzi wa kumfuata na kumtumikia Mungu. Somo la kwanza la katika kitabu cha Yoshua (24:1-2a, 15-18); linahusu kufanya maamuzi katika maisha na kuwa msimamo unaoeleweka, kuepuka undumilakuwili na kutangatanga. Joshua anawaambia Waisraeli kuwa hawawezi kuendelea na maisha yasiyo na msimamo. Anawataka wafanye maamuzi na wachague kati ya kumtumikia Mungu aliyewaokoa toka utumwani Misri na kuwapa nchi takatifu au miungu mingine ile ambayo baba zao waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba miungu ya wale Waamori ambao wanakaa katika nchi yao. Lakini yeye ameshachagua msimamo wake na anauweka wazi akisema; “Mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana”. Waisraeli wanachagua kumtumikia Bwana, Mungu wa kweli wakisema; “Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine.” Wakaweka msimamo wao wazi wakisema; “Sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye Mungu wetu.” Huu ukawa msimamo wa Taifa la Israeli.

Swali kwetu; Je, sisi tunamtumikia Mungu wa kweli aliyetuumba na kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo au tunaitumikia miungu mingine? Kama tunaishi katika dhambi tujue wazi tunatumikia miungu mingine. Lakini kama tunahofu ya kutenda dhambi na tukianguka dhambini tunahuzunika na kumuomba Mungu msamaha katika sakramenti ya kitubio basi tuko upande wa Mungu na Mungu daima atabaki nasi siku zote naye atatuokoa na taabu zetu zote. Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (5:21-32); latueleza ukamilifu wa ndoa ya kikristo kwa mfano wa mapendo ya Kristo kwa Kanisa lake. Kama vile Kristo alipendavyo na kuishi daima na Kanisa (taifa la Mungu), vivi hivi inawapasa watu wa ndoa kupendana na kuishi pamoja daima hali wakinyenyekeana katika kichwa cha Kristo. Paulo anaufananisha muungano na uaminifu kati ya Mungu na watu na muungano na uaminifu wa watu wa ndoa. Jinsi watu wa ndoa wanavyoungana ndivyo na sisi tunavyoungana na Kristo kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Hali kadhalika, uaminifu wanaopaswa kuwa nao watu wa ndoa ndio tuanopaswa kuwa nao kwa Kristo. Kama ambavyo wana ndoa hawafurahii wenzi wao wa ndoa kuwadanganya kwa kukosa uaminifu, ndivyo ambavyo Mungu anavyochukizwa tunapomuasi na kuumikia miungu mingine.

Maneno ya mausia ya Mtume Paulo ni mazito mno yafaa kuyasikiliza jinsi yalivyo. Mtume Paulo anasema; “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na hila wala kunyanzi lolote, bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayechukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.”

Injili ilivyoandikwa na Yohane (6:60-69); nayo yatueleza habari za kufanya maamuzi magumu katika kuchagua hatima na mstakabali wa maisha yetu. Katika sehemu hii ya Injili tunaona wanafunzi na wafuasi wengine walimwacha Yesu sababu waliona vigumu kumsadiki alipowafundisha kuhusu Ekaristi Takatifu, kuhusu kuula mwili wake na kuinywa damu yake wakisema; “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisiikia?” Yesu alitambua manung’uniko yao akawaambia; “Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” Katika hali hii ya kunung’unika na kurudi nyuma kwa wafuasi, Yesu anawageuzia kibao mitume wake kumi na wawili na kuwadai nao waamue kunyoa au kusuka, kumfuata au kumwacha akiwaambia; “Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Simoni Petro anamjibu kwa niaba ya wenzake akisema; “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” Nasi yatupasa kufanya maamuzi magumu kumfuata Yesu ili tupate uzima wa milele au kumuacha ili tuangamie milele.

Katika kuamua kumtumikia Mungu kila mmoja yuko huru. Kila mtu ana uhuru kamili katika kuchagua kumtumikia Mungu au kutomtumikia. Lakini uhuru huu ni uhuru wa kuwajibika. Kila mmoja anawajibika kwa uchaguzi wake. Mungu daima anaheshimu uhuru wa kila binadamu. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati aliwaambia Waisraeli: “Leo hii nawapeni uchaguzi kati ya mema na mabaya; kati ya uhai na kifo…kati ya Baraka na laana. Basi chagueni uhai ili mpate kuishi” (30:15-20). Kwa hiyo, katika masuala ya Imani tusiwe watu wa kulalamika; hulazimishwi kumtumikia Mungu. Unachohitaji ni kupima matokeo ya kumtumikia na ya kukataa kumtumika na kufanya uamuzi binafsi na kuwa tayari kukabiliana na matokeo ya uamuzi wako. Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kutufanya tumwache Kristo na mafundisho yake. Kubwa zaidi ya zote ni kutoelewa kwa undani mafundisho yake yanayotolewa na Kanisa labada kwa ya kutoyasoma na kuyatafakari maandiko matakatifu. Lakini pia kutotambua kuwa imani si suala la akili tu bali ni kufungua macho ya mioyo yetu ili kumuona mkuu wa uzima wa milele na kumfuata ili kuupata uzima huo.

Ndiyo maana Petro alisema; “Twende kwa nani Bwana; wewe unayo maneno ya uzima wa milele.” Sio kwamba Petro aliyaelewa fundisho la Yesu kwa undani wake bali aliamini na kufungua moyo wake na kumruhusu Yesu aingie ndani ya maisha yake. Kutokuelewa kwa undani anachofundisha Yesu hakuondoi ukweli wa mafundisho yake. Si kwamba hatupaswi kuelewa kabisa bali ni kuamini na kuelewa tunachoweza kuelewa na tusipoelewa tunatambua kuwa hatukuelewa lakini kutoelewa kwetu ni kwa sababu ya asili na udhaifu wetu si kutoeleweka kwa mafundisho. Pale tunaposhindwa kuelewa ni vyema kupiga magoti na kusema; “Nasadiki”. Imani yetu inapojengeka juu ya vitu kiasi kwamba tunampenda Mungu ili tupate tunachohitaji; tukikikosa tunarudi nyuma kiimani na kuigeukia miungu mingine. Tufuate msimamo wa Petro na Yoshua wa kubaki upande wa Mungu ili aweze kutuponya kama wimbo wa katikati unavyotuusia kuwa; “Mateso ya mwenye haki ni mengi; lakini Bwana humponya nayo yote”. Basi tuseme kama Habakuk (3:17) kwamba; “hata kama mitini isipochanua maua; hata kama zabibu hazitazaa zabibu; hata kama mizeituni isipozaa zeituni; hata kama mashamba yasipotoa chakula; hata kama kondoo wakitoweka mazizini; mimi nitaendelea kumfurahia Mungu wangu.”

Ni vyema kufahamu na kukumbuka daima kuwa; Misimamo au mafundisho ya Kanisa ambayo ni ufunuo wa Mungu kwa wanadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu hayatabadilika kwa watu kulalamika au kutoyaelewa. Wakati mwingine mafundisho ya Kanisa juu ya Imani hasa juu ya maadili ya kuheshimu uhai wa binadamu, na kuzuia au kutoa mimba, ndoa ya mume na mke mmoja na mahitaji mbalimbali ya kupokea Sakramenti yanaonekana kuwa magumu au kuwa kinyume cha mazoea na matarajio au mila za watu. Mara nyingi watu wasioelewa wanalilaumu Kanisa wakisema; “haliendani na wakati au halisikilizi matakwa ya watu.” Ukweli ni kuwa Kanisa linapofundisha ukweli halitaubadilisha ukweli huo eti kwa sababu watu wamepiga kelele. Kristo mwenye aliwaambia; “Ukweli ni kwamba lazima mle mwili wangu na kuinywa damu yangu ili mpate uzima wa milele.” Kwamba inaendana na mila au mazoea yenu haijalishi. Kama mnataka kunikimbia, kimbieni lakini sibadilishi msimamo huo maana ndio ukweli. Basi, tujitahidi kuelewa mafundisho ya Kanisa na kuwa wanyenyekevu kuyapokea. Aidha pale unaposimamia ukweli au haki fulani, usitetereke au kulegeza misimamo ili kujifanya rafiki wa watu. Kinachohitajika ni kuwaeleza watu ukweli huo kulingana na mazingira yao. Watakulaumu au watalilaumu Kanisa lakini tujue kuwa: “Uovu utamwua asiye haki; Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake; wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao” (Zab.33:1-2,15-22). Tuamue leo kumtumikia Mungu na kuitupilia mbali miungu mingine kwani haina tija kwa maisha ya uzima wa milele.

J21 Mwaka B
19 August 2021, 15:16