Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22 ya Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu na Mapokeo ya Kiyahudi: Upendo kwa Mungu na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22 ya Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu na Mapokeo ya Kiyahudi: Upendo kwa Mungu na jirani! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22: Amri za Mungu Na Mapokeo

Hatari nyingine ya kulinganisha Neno la Mungu na mapokeo ya zamani, iliwapotosha wengine kwani walidhani kutimiza mapokeo ilitosha sana katika kujenga mahusiano yao na Mungu. Wengine wakabaki kuwa watumwa wa mapokeo na hata kuliweka kando Neno la Mungu. Walikumbushwa kuwa walitakaswa sio kwa kutawadha maji ya ziwani au mtoni bali kwa kuzishika amri za Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Baada ya kutafakari kwa Dominika tano mfululizo sura ya sita ya Injili ya Yohane, leo Mama Kanisa anaturejesha tena kuendelea kuitafakari Injili ya Marko, ambayo tutaendelea kuitafakari kwa Dominika zote zilizobaki mpaka mwisho wa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Leo pote ulimwenguni tunapambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, na moja kati ya ushauri wa kitabibu ni ule wa kunawa mikono kila mara kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vitakasa mikono, ili kuepuka kujiambukiza na kuwaambukiza wengine na kirusi hatari cha Korona. Ni janga kubwa si tu nchini kwetu bali ni dunia nzima na kwa kweli hatuna budi kusikiliza ushauri huu wa kitabibu maana ni wao wenye utaalamu na ujuzi wa jinsi ya kulinda afya na uhai wetu. Sehemu ya Injili ya leo, kwa kweli inagusa moja kati ya mambo ya msingi kabisa katika dini ya Kiyahudi: kunawa au kutawadha, kwa Kiebrania inaitwa “netilat jadajim” Tofauti na ushauri wa kitabibu dhidi ya janga la UVIKO-19, kwao hilo ni swali la kidini na kiimani. Wakati sisi leo tunashauriwa kunawa mikono kwa maji tiririka au kwa vitakasa mikono kwa sababu za kiafya na kitabibu, kwa Wayahudi swala la kunawa au kutawadha mikono halikuwa haswa kwa ajili za kiafya na kitabibu kwa nafasi ya kwanza, bali kama tulivyosema ni zile za kidini na kiimani.

Kwa Wayahudi ulimwengu umegawanyika hatika sehemu kuu mbili zinazokinzana, yaani, ulimwengu safi na mwingine ni ule najisi. Ulimwengu safi ndio ule ambao kwao kuna nguvu zile za maisha na uhai, na ule najisi ndio ule unaofumbatwa na nguvu za giza na mauti. Kwa Wayahudi kitu kilicho najisi ni chochote kile, ambacho kwanza kimegusana au kuhusisiana na sanamu au ibada za miungu ya uongo, miungu ambayo haina uwezo wa kutoa uhai na uzima. “Kwa maana wao wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea. Wanasimulia jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha ibada za sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli.” (1Wathesalonike 1:9) Na kwao haikuishia katika kutenganisha vilivyo safi na vilivyo najisi, Wayahudi hata pale walipoingia katika nchi ya kipagani, hawakula mazao ya nchi ile ya kigeni kwa muda wa miaka mitatu, wakiamini waliacha kula mazao yale kwa misimu mitano ya miaka mitatu, ili kujiepusha na najisi ya nchi ile ya kipagani. (Walawi 19:23) “Mtakapofika katika nchi ya Kanaani na kupanda aina zote za miti ya matunda, matunda hayo hamtayala; hamtaruhusiwa kuyala kwa muda wa miaka mitatu”

Watu wa mataifa mengine au wapagani walikuwa sawa na hata waliitwa “mbwa” (Marko 7:27), na hata Yesu alitumia neno hilo kuwatambulisha wapagani. “Yesu akamwambia, tuwaache watoto washibe kwanza, kwa maana si halali kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Na taifa takatifu ni lile la Israeli. “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.” (Kumbukumbu la Torati 7:6). Na zaidi sana kwa Wayahudi mahali pakatifu zaidi ni hekaluni, mahali ambako ndio kuna utukufu wa Mungu, yaani, Shekinah. Hivyo, kwa Wayahudi kila mmoja anayegusana au kukaribiana na mpagani, au kushika au kugusa kitu amacho kiliguswa na mpagani, basi hilo lilitosha kumfanya kuwa najisi, na hivyo mwenye kuhitaji kujitakasa kwa kutawadha na kujiosha. Na Marabi walienda mbali zaidi katika kufundisha aina mbalimbali za najisi na pia kwa namna gani mmoja alipaswa kutawadha ili kurejea hali ya usafi.

Walifundisha pia hata aina ya maji yaliyopaswa kutumiwa kwa kujitakasa na hata ya kuoshea na jinsi ya kuosha vitu vilivyonunuliwa sokoni kabla ya kuweza kuanza kutumika. Na kila Myahudi alipaswa kuzijua na kuzishika kwa kichwa taratibu zote hizo za “netilat jadadim”, ndio ibada ya kunawa na kutawadha. Kuivunja mojawapo ya taratibu zile ilikuwa ni sawa na kukosa uaminifu kwa Mungu na sheria zake. Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, tunaona wahusika wakuu ni Yesu kwa upande mmoja, na Mafarisayo na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu. Na moja lililowastua ni kuona wanafunzi wa Yesu, wakila kwa mikono isiyonawiwa, ndio kusema wanafunzi wa Yesu hawashiki sheria na taratibu zile za kutawadha mikono kama ilivyotakuwa na dini yao ya Kiyahudi. “Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Kwa kweli kama tulivyotangulia kuona pale mwanzoni, swala la kunawa mikono halikuwa swala la kiafya bali la kimapokeo ya kidini zaidi. Kwao si tu walipaswa kuosha au kunawa mikono yao, bali mmoja anayekuwa amenawa alipaswa kukaa mbali na mpagani ili asinajisike.

Ni karibu sawa na leo tunaposhauriwa na wataalamu wa afya kukaa mbali na wengine ili kupeuka kuambukiza au kuambukizwa na wengine Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kwao kukaa mbali na Wapagani halikuwa swali la kiafya bali la kidini na kiimani, kwani waliamini ukigusana na mpagani basi nawe unanajisika na kupoteza utakatifu. Mafundisho makali ya namna hii yalitokana na mafundisho ya Marabi wao wa Kiyahudi. Marabi hata karibu wakawasadikisha kuwa mafundisho yao juu ya mapokeo ya kale yanakuwa na uzito sawa na Neno la Mungu. Mwenyezi Mungu anamwagiza Musa kuwaambia Aroni na wanawe, ukoo wa kikuhani juu ya ulazima kwao wa kutawadha mikono kabla ya kula nyama iliyotolewa sadaka hekaluni. “Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, utatengeneza birika la shaba la kutawadhia lenye tako la shaba, uliweke katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ndani yake. Aron ina wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu, kabla ya kuingia au kukaribia madhabahu ili kunitolea mimi Mwenyezi Mungu, tambiko zitolewazo kwa moto, watafanya hivyo wasije wakafa. Ni lazima wanawe mikono na miguu yao wasije wakafa. Hii itakuwa ni kanuni kwao daima, tangu Aron ina uzao wake, vizazi hata vizazi.” (Kutoka 30:17-21)

Lakini kati yao baadhi ya Wayahudi walianza nao kufanya haya maagizo yaliyowahusu makuhani hata majumbani kwao, na taratibu ikaanza kuonekana kuwa ni agizo la Mungu. Na Wayahudi walianza na hata kusali wakiwa wanatawadha kwa kusali maneno yafuatayo: “Utukuzwe wewe, Bwana Mungu mfalme wa ulimwengu, ambaye unatutakatifuza kwa sheria zako kwa jinsi ulivyotuagiza kutawadha mikono yetu.” Na hapa ndio tunaona kama tunavyosoma katika somo la kwanza la Dominika ya leo, (Kumbukumbu la Torati 4:2) “Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.” Ni baada ya kubadili mapokeo na kuyafananisha sawa na Neno na maagizo ya Mungu ndio hatari inapoanzia. Ni hapo tunaona mwanadamu anaona mahusiano na Mungu ni mzigo mzito usioweza kubebeka kirahisi na kumfanya kuwa mbali na Mungu. Mbele ya Mungu hakuna watu najisi na watu safi, kwani sisi sote ni watoto wake, Mungu haangalii kama sisi wanadamu tunavyoangalia na kuwatendea wengine.

Mtume Petro akiwa ndotoni anakumbushwa kuwa; “Usiite chochote alichokitakasa Bwana kuwa ni kichafu” (Matendo 10). Mtume Paulo naye kwa waraka wake kwa Wagalatia 3:28 anasema; “Hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanaume na mwanamke. Wote mmekuwa kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu.” Tunasoma pia kutoka Kitabu cha Hekima ya Sulemani 11:24; “Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba” Hatari nyingine ya kulinganisha Neno la Mungu na mapokeo ya zamani, iliwapotosha wengine kwani walidhani kutimiza mapokeo ilitosha sana katika kujenga mahusiano yao na Mungu. Wengine wakabaki kuwa watumwa wa mapokeo na hata kuliweka kando Neno la Mungu. Na ndio tunaona kati ya Wayahudi kulikuwa na kikundi cha Wamonaki wa Kumrani ambao waliwafundisha na kuwakumbusha watu kuwa kilichokuwa kinaweza kutakasa watu sio kwa kutawadha maji ya ziwani au mtoni bali kwa kuzishika amri za Mungu, ni kuwasaidia watu kutoka utumwa wa mapokeo na kuliweka kando Neno la Mungu.

Ni katika muktadha huu, tunaweza kusema kosa lenye heri, Yesu anatumia fursa ile kuwafundisha ni nini mapenzi ya Mungu, ni nini Mungu anataka kwa mwanadamu, sio kushika mapokeo na maagizo ya mwanadamu bali kwa kuwa na mahusiano ya ndani na Mungu, sio tena kwa kuangalia mambo ya nje nje bali ya ndani, yale ya moyoni kabisa mwa mwanadamu. Ni hapa Yesu ananukuu maneno ya Nabii Isaya: “Watu hawa huniheshimu kwa midomo ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo ya wanadamu.” (Isaya 6-7). Na hata katika Injili ya Matayo, Yesu pia anatumia maneno yenye kufanana na haya: “Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: Nataka huruma, wala si dhabihu. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.” (Mathayo 9:13 na 12:7) Na ndio Yesu leo anawabatiza jina wale wote wanaolinganisha mapokeo haya na Neno la Mungu kuwa ni “wanafiki”, ni sawa na kusema katika lugha ya leo watu wenye sura mbili, wasanii, waigizaji, wanaofunika sura zao kwa barakoa za kidini, barakoa za uchamungu, na kusahau yale yaliyo ya muhimu na ya msingi kabisa, upendo kwa Mungu na kwa jirani, wanaomwabudu Mungu kwa midomo yao na wakati mioyo yao ikiwa mbali na kinyume na Mungu kabisa.

Na hata nasi leo ndugu zetu, tunaweza kuwa katika hatari zile zile katika maisha yetu ya ufuasi, ya kuwa waamini wenye sura mbili, ya kuwa wasanii na kukosa kuwa wakweli mbele ya Mungu na Kanisa, watu wenye ndimi mbili, watu geugeu kwani maisha yetu yanakosa kuakisi Neno la Mungu, maisha yetu yanapokosa kuakisi Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu leo anataja kujiangalia na vilema vile kumi na viwilia ambavyo havitoki nje yetu bali ndani, na ndio mapambano yetu yanapaswa kuwa ya ndani, yale ya kiroho, yale ya kuangalia kila mara tunabaki kuwa na mahusiano mema na ya upendo kwa Mungu na kwa jirani au watu wengine wanaotuzunguka. Vilema anavyovitaja Yesu leo ni vile ambavyo mara nyingi tunakosa ujasiri wa kuviangalia na kujirekebisha, imani ya kweli na komavu ni ile inayojali daima mahusiano ya upendo kwa Mungu na kwa wengine. Niwatakie Dominika na tafakari njema.

25 August 2021, 15:02