Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka B: Katekesi Kuhusu Ekaristi Takatifu
Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.
UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika siku hii ya Bwana, Dominika ya 21 ya Mwaka B wa Kanisa. Katika Dominika hii Liturujia ya Neno la Mungu linahitimisha katekesi ya Bwana wetu Yesu Kristo juu ya Ekaristi Takatifu. Kwa ufupi kabisa: Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo. Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Katika Ekaristi tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Katika Ekaristi mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ekaristi ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na ule umoja wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Rej. KKK 1324-1327. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika: Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa; katika Meza ya huruma, upendo na huduma makini kwa watu wa Mungu. Waamini wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu wamwachie nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwamegea huruma na upendo wake kwa njia ya Neno na hatimaye, wokovu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba.
Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa uwepo angavu, endelevu na fungamani wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu anayetembea na waja wake hadi utimilifu wa dahali. Uwepo wake unafichika katika maumbo ya Mkate na Divai; Sakramenti ya Upendo na chakula safi cha wasafiri kuelekea mbinguni kwa Baba. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na ni Fumbo la Mwili wa Kristo linaloendelea kuboreshwa kwa njia ya: toba, wongofu wa ndani, unyenyekevu wa moyo, sala na upendo unaopyaishwa na kufumbatwa kwenye Jumuiya za Kikristo zilizotakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo. Mwaliko tunaopewa katika Dominika hii ni wa kufanya uamuzi makini wa kubaki na kushikamana na Kristo Yesu aliye uzima wetu. Tunaalikwa kuamua kuandamana na Kristo kwa imani na mapendo ya kweli kwake ambaye anatuongoza katika njia iletayo uzima. Tunaalikwa kuamua wenyewe kuonja na kuuona wema wa Bwana. Mfuasi wa kweli husimama ni Kristo siku zote na katika hali zote.
TAFAKARI: Katika Somo la kwanza Yoshua anawataka watu wa kabila zote za Israeli waamue kwa uhuru na utashi kamili ni nani wanataka kumtumikia. Yeye akiwa ni kiongozi wa watu hawa anaweka wazi msimamo wake kwao kwa kusema kuwa “yeye na nyumba yake watamtumikia Bwana.” Watu wa Israel kwa kumbuka wema wa Mungu, ishara kuu alizozifanya na yote aliyowatendea katika safari yao ya ukombozi kutoka Misri wanaazimia kutokumwacha Bwana na wananuia kumtumikia. Wanafanya uamuzi huo kwa uhuru na utashi wao wakisukumwa na upendo na imani kwa Mungu. Uamuzi wanaoufanya ndio msingi wa urafiki katika yao na Mungu. Na ikiwa wanasimamia hicho walichoamua basi wataishi katika agano la kweli na Mungu, yaani watakuwa kweli watu wake na yeye atakuwa Mungu wao mwenye kuwaokoa na kuwajalia uzima. Katika Somo la pili Mtume Paulo, kwa kutumia lugha ya mlinganisho, anaonesha muunganiko ulioko kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Anasifu upendo mkuu wa Kristo kwa Kanisa lake na jinsi ambavyo Kristo amejitoa kikamilifu kwa ajili yake ili apate kulitakasa, kulisafisha, kuliletea utukufu na kulikamilisha katika utakatifu.
Uamuzi huu wa Kristo kwa Kanisa lake unajengwa juu ya msingi wa upendo wa dhati alio nao kwake kama ilivyo kwa mume na mke. Kufikia hatua kama hii hakutokei kama jambo la nasibu bali ni maamuzi ya dhati yanayohusisha uhuru na utashi, imani, uaminifu na uthabiti. Sisi tukiwa ni viungo vya mwili wa Kristo tunaalikwa kufanya maamuzi thabiti ya kuambata na Kristo aliye Bwana wetu. Katika Injili Yesu anauliza swali msingi ambalo linaamua hatima ya uhusiano uliopo kati yake na wale ambao wameamua kuwa wanafunzi wake. Baada ya mafundisho mazito kuhusu uzima utokanao na mwili na damu yake Kristo, watu wengi wanarejea nyuma na wanaacha kuandamana na Kristo. Wanafanya hivyo kwa sababu neno lake Yesu limekuwa gumu kwao kupokeleka. Katika hatua hii Yesu anawataka wanafunzi wake kufanya uamuzi kwa uhuru na utashi kamili ikiwa wanataka kubaki nae au wangependa nao kwenda zao. Katika hatua hii Simoni Petro akamjibu, “Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” Huu ni uamuzi mzito ambao unadai imani thabiti na upendo wa kweli kwa Kristo. Si uamuzi ambao unaweza kufanywa na watu ambao wako tayari kumfuata Kristo pale tu mambo yanapokuwa rahisi.
KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika Dominika hii tunakumbushwa jambo moja msingi ya kwamba Mungu ametuumba kwa upendo mkubwa na ametujalia akili, uhuru na utashi wa kuamua nini tunataka katika maisha yetu sisi wenyewe. Hii ni moja ya zawadi kubwa kabisa tulizopokea kutoka kwa Mungu. Yeye mwenye kujua yote, hata mawazo yetu ametupa zawadi hii ya uhuru wa kuamua ambapo tunaweza kuamua hata kinyume cha vile anavyotaka yeye. Leo tunapewa nafasi ya kumshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa, lakini pia tunapewa fursa ya kutafakari ni namna gani tunaitumia zawadi hii. Jambo lingine muhimu linaloendana na ukweli huu ni kwamba tutawajibika kwa maamuzi tunayoyafanya katika maisha yetu. Katika maisha ni lazima kufanya maamuzi. Iwe ni katika mambo madogo au katika mambo makubwa tunafanya maamuzi kwa kila hatua katika maisha yetu. Hata pale ambao tunaacha kufanya maamuzi tayari tunakuwa tumeamua na tunawajibika kwa namna hiyo ya kutenda na kuenenda. Kwa sababu hiyo ni lazima kuamua kwa busara. Tunatambulika na tunajipambanua pia kwa maamuzi tufanyayo kila siku katika maisha yetu. Tunaitwa wema kwa sababu ya maamuzi tunayofanya kila siku kuhusu matendo yetu na kinyume chake ni sawa.
Tunaitwa Wakristo kwa sababu ya maamuzi tunayofanya kila siku kuhusu wito wetu katika njia ya utakatifu. Imani ni zawadi ya Mungu si shuruti lakini inachochewa na kukua kutokana na maamuzi tufanyayo kila siku. Watakatifu tunaowatazama kama mifano ya kuiga walifanya maamuzi na kubaki waaminifu kwa maamuzi yao na wametuachia mfano bora wa kuiga. Sisi nasi lazima tujue kupima vema yepi ni mambo mema na yepi ni mambo maovu. Tuamue kushika yaliyo mema na kuachana na yaliyo maovu, kielelezo makini cha dhamiri nyofu! Aidha, katika kufanya maamuzi tusitafute njia nyepesi. Maamuzi yetu yatazame daima lengo letu, yaani tunapoamua tuzingatie daima shabaha yetu, wapi tunataka kufika na lengo gani tunataka kutimiza. Wakati mwingine ili kufikia malengo tutafanya maamuzi magumu sana ambayo yatatudai hata sadaka kubwa. Lakini mwisho wa siku tutapata matunda bora. Hili ni jambo muhimu la kuzingatia katika maisha binafsi na katika jumuiya. Yeyote mwenye kutaka kupiga hatua ya mafanikio katika maisha yake lazima akubali kufanya maamuzi sahihi na asitafute njia nyepesi bali njia iliyo sahihi. Ndivyo tunavyodaiwa kufanya hata katika njia ya imani, njia ya ufuasi wetu kwa Kristo.
Kama tunataka kufika kule aliko yeye mwalimu wetu basi tuamue kuambatana naye na kusafiri naye katika njia yake, hata kama itatudai sadaka kubwa ili mradi tuna hakika ya kwamba mwisho tutajaliwa uzima wa milele. Zaidi ya hayo, kuamua ni kupokea wajibu. Haitoshi tu kusema nimeamua hivi kuhusu jambo fulani. Lazima tuwe tayari kuwajibika kwa maamuzi tunayoyafanya. Ni kwa namba hiyo pekee ndio tutaona matunda ya kuamua kwetu. Tusiseme tu kwa kinywa bali lazima tutekeleze kwa matendo. Haikutosha tu kwa watu wa Israeli kusema kuwa watamtumikia Mungu bali walipasika kuenenda kadiri ya ahadi yao na maamuzi yao. Ndio sababu walipokwenda kinyume waliingia katika madhira makubwa na walipobaki waaminifu waliuona mkono wa Mungu juu yao. Sisi nasi haitoshi tu kusema tumebatizwa, ni lazima tuwajibike kama wakrsito kweli. Mfuasi wa kweli husimama na Kristo katika hali zote. Maamuzi tufanyayo leo ndio yatakayoamua wapi tutakuwa kesho. Tuamue kwa busara, kwa imani na kwa upendo wa kweli kwa Mungu. Ninakutakia Dominika Njema.