Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Unabii, Jina la Yesu, Mungu anaokoa na Makwazo katika maisha ya mwanadamu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Unabii, Jina la Yesu, Mungu anaokoa na Makwazo katika maisha ya mwanadamu! 

Tafakari Jumapili 26 ya Mwaka B: Jina la Yesu: Mungu Anaokoa!

Katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 26 ya Mwaka B ningependa kujielekeza zaidi katika mambo makuu manne: Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani. Unabii kama karama ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jina la Yesu maana yake ni Mungu anaokoa. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na mwisho ni hatari ya makwazo katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 26 ya Mwaka B wa Kanisa. Katika tafakari hii, ningependa kujielekeza zaidi katika mambo makuu manne: Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani. Unabii kama karama ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jina la Yesu maana yake Mungu anaokoa. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na mwisho makwazo katika maisha! Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu.

Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akaanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na sababu za kichungaji akaamua Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani iadhimishwe Jumapili ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 26 Septemba 2021. Kauli mbiu inayonogesha maadhimisho haya ni “Kuelekea Sisi Kubwa Zaidi”, changamoto ya Kanisa ni kujenga umoja katika utofauti wake unaofumbatwa katika familia ya binadamu. Kanisa ni familia ya wabatizwa, inayoitwa na kutumwa kutoka nje ili kwenda kukutana na kondoo walijeruhiwa na kupotea, ili kuwapokea na kuwahudumia, tayari kujenga na kudumisha amani na utulivu, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya jamii!

Ubatizo ni kifungo cha Kisakramenti cha umoja uliopo kati ya watu waliozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, yaani Wakristo ambao wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Kumbe, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Wazo la Unabii linajitokeza kwenye Somo la kwanza Hes. 11: 25-29 na Injili ya Marko 9: 38-43; 47-48. Musa katika Agano la Kale alikuwa na nafasi muhimu sana, kwani alikuwa ni Nabii wa Mungu, kumbe, alikuwa ni kiongozi wa kiroho, aliyewatangazia Waisraeli mapenzi ya Mungu, lakini pia aliheshimiwa kama kiongozi wa kisiasa. Kinachojitokeza katika Somo la kwanza ni wivu katika kutoa unabii, au kuhubiri. Wakristo wanakumbushwa kwamba, Roho wa Mungu anatenda kadiri anavyotaka. Rej. Yn 3:8.

Hakuna mtu anayeweza kumbinafsisha Roho wa Bwana yaani "kumweka Roho wa Bwana, mfukoni na kumtumia kama unavyotaka". Karama mbalimbali ambazo waamini wamekirimiwa ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mitume wa Yesu walidhani kwamba, wanayo hati miliki ya Roho Mtakatifu na kwamba, walikuwa wametumwa kutenda kwa niaba ya Mungu! Kristo Yesu anahitimisha mjadala huu kwa kusema “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake.” Mk 9: 39-40. Kimsingi, Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya matendo yao adili na matakatifu.

“Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Flp 2:9-11. Ni katika jina la Kristo Yesu nguvu ya Mungu inayoganga, kuponya na kuokoa imejidhihirisha katika Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele katika historia ya wokovu! Katika Agano la Kale jina lilionesha utambulisho na utume wa mtu! IESVS kwa Lugha ya Kilatini; Iēsous Kwa Kigriki: Ἰησοῦς), na Kwa Kiharamayo: Yeshua Y'shua na hatimaye kwa Kiebrania: ישוע‎). Kumbe, Jina Yesu maana yake Mungu anaokoa. Kwa njia ya Jina la Yesu mwanadamu anakirimiwa maisha mapya. Kanisa la Mwanzo lilitenda miujiza mingi kwa njia ya Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umoja wa Kanisa. Rej. LG 48.

Kanisa linatambua kwamba, Injili ya Kristo ni chemchemi ya mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu inayopania kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na binadamu; maadili na utu wema; tunu msingi za maisha ya kifamilia, uhuru wa kidini na majiundo makini. Katika kipindi hiki cha mmong'onyoko wa tunu msingi za kiutu na kimaadili, Mama Kanisa anatumwa kuwa ni sauti ya kinabii, kwa kutangaza kweli kuhusu Mwenyezi Mungu anayeokoa na Binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wivu na hususani usiokuwa na mvuto wala mashiko ni kikwazo kwa mchakato wa uinjilishaji. Umoja na mshikamano; utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji. Uchoyo, ubinafsi na upendeleo ni kikwazo na huo kimsingi ni mwanzo wa uchu wa mali na madaraka. Kanisa lijenge utamaduni wa kusindikizana, ili kukoleza huruma, kuponya na kuwaweka watu huru sanjari na kuendelea kukua katika maisha ya Kikristo. Rej. EG 169.

Mababa wa Kanisa wanahimiza umuhimu wa kujali: utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuepuka makwazo. Kimsingi kwazo ni hali au tabia inayomwongoza mwingine kutenda ubaya, kwa kushawishi na hivyo anaharibu fadhila na ukamilifu. Tabia hii inaweza kumwingiza mtu katika kifo cha kiroho. Kwazo ni kosa kubwa kama kwa tendo au kwa kuacha kutenda mwingine anaongozwa kwa makusudi katika kosa kubwa. Ni kutokana na uzito wa kwazo hasa kwa watoto wadogo Kristo Yesu anatamka apizo hili: “Bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.” Mt. 18:8. Kumbe, yeyote anayetumia uwezo wake hivi anawaongoza wengine kutenda ubaya ana hatia ya kwazo na anawajibika kwa ajili ya ubaya uliohimizwa moja kwa moja au vinginevyo. Kumbe, tujitahidi kuchuchumilia na kuambata tunu msingi za maadili na utu wema. Rej. KKK 2284-2289.

Kwa ufupi kabisa kwazo linawaangusha wengine dhambini au kuwazuia kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Maadhimisho ya Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani yasaidie kujenga familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika umoja, upendo na mshikamano. Yesu Kristo anatibu, anaganga na kuokoa. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu. Tuepuke, tusijekuwa ni sababu ya makwazo kwa jirani zetu.

Liturujia J26
24 September 2021, 13:17