Tafakari Jumapili 25 Mwaka B: Hekima na Unyenyekevu wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 25 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni maonyo juu ya tamaa mbaya ambayo ni chanzo cha vurugu, machafuko na malumbano kwanza kwa mtu binafsi ndani ya moyo wake, halafu kati ya mtu na mtu, na familia, na jumuiya, na kanisa, na taifa na ulimwengu kwa ujumla. Ili kuepuka haya madhara yatokanayo na tamaa mbaya sharti kuishi kwa kuongozwa na hekima itokayo juu kwa Mungu ambayo kwayo inatujalia amani, upendo, utulivu na moyo wa utumishi na kutufanya kuwa wana wa Mungu na waridhi wa uzima wa milele. Somo la kwanza la kitabu cha Hekima ya Sulemani (2:12, 17-20); latujuza namna alivyochukuliwa mtu mchamungu katika Agano la Kale aliitwa “mwana wa Mungu”. Lakini mtu huyu mchamungu alichukiwa na waovu maana matendo yake mema yaliwasuta na kuzishitaki dhamiri zao ovu na kuumia mioyoni mwao ndivyo wanvyoshuhudia wakisema; “Zaidi ya hayo tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu, atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu.”
Kwa kuwa ndani ya mioyo yao yamejaa mawazo maovu, Waovu hawa wanapanga maovu kwa mtu mwema wakisema; “Haya na tuone kama Mungu atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.” Tunaona wazi katika somo hili utabiri wa namna Yesu Kristo mtu mwema na mwenye haki atavyotendwa kwa jeuri na watu waovu na kuuawa kifo cha aibu msalabani ili atukomboe sisi watu waovu na wadhambi kutoka utumwa wa shetani na mauti. Ndio kusema Yesu ni hekima halisi iliyoshuka kutoka mbinguni kutufunua mpango wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Hata nyakati zetu, mtu mwema anaendelea kuteseka na kuhangaika mahangaiko mengi yanayopangwa na waovu kwa sababu ya matendo yake mema. Tujiulize ni mara ngapi tumepanga mipango ya kuumiza mtu mwema? Mara ngapi tumeshiriki katika mateso ya watu wengine kisa tu maneno na matendo yao mema yanaenda kinyume na yetu. Tuombe hekima ya Mungu ikae ndani mwetu ili ituepushe na mipango miovu ya kuwaumiza watu wema na hivyo nasi tujifunze kuwa wema.
Somo la pili la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (3:16-4:3); linafundisha namna mkristo anavyopaswa kuishi kwa hekima ya kikristo. Hekima hii ina sifa hizi; ni safi, ya amani, ya upole, iko tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki wala haina hila yoyote. Ikikosekana hii hekima matokeo yake ni; vita, mapigano wivu, ugomvi, machafuko, kila tendo baya na tamaa zisizofaa miongoni mwa wakristo kama anavyosema; “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Katika Injili ilivyoandikwa na Marko (9:30-37); Yesu anatabiri mara ya pili mateso, kifo na ufufuko wake akisema; “Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka.” Huu ni utabiri wa kutimia kwa utabiri uliotolewa katika somo la kwanza juu ya kifo cha mtu mwema.
Licha ya kuwa wanafunzi wake hawakuelewa fundisho hili, hata hivyo hakuna aliyedhubutu kumuuliza anachomaanisha maana walijaa woga, hofu na mashaka maana kila mmoja alitamani awe mkubwa kwa wenzake. Yesu alitambua mawazo yao. Walipofika Kapernaumu anawauliza; “Mlishindania nini njiani?” Hakuna aliyedhubutu kujibu. Marko anasema; “Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa.” Yesu akawaweka kitako na kuwapa somo akiwaambia; “Mtu atakayekuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote…Mtu akimpokea mtoto mdogo kwa jina langu, anipokea mimi, na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.” Mtu mwema, mwana wa Mungu, anayeishi kwa hekima ya Mungu ni mtumishi wa wengine. Mtu huyu mwema akubali kuteseka maana waovu hawatampenda maana matendo yake mema yanazisuta dhamiri zao ovu na tamaa zao mbaya.
Tamaa mbaya inatufanya tushikane koo maana inaleta mashindano na mapigano. Mwenye tamaa mbaya ya madaraka, ya mali na umaarufu atafanya kila jitihada kutimiza tamaa yake mbaya hata ikibidi kuwanyang’anya wengine haki ya kuishi. Tamaa mbaya inatufanya tuwe na wivu na hata uadui na watu wengine na hata kupelekea kutenda dhambi zingine mbaya zaidi. Tukumbuke kuwa tamaa mbaya inaaza taratibu katika mawazo ya mtu, ukiipalilia inatawala mawazo yako na kukufanya uifikirie kila wakati hata ukilala unaota unachokiwaza. Ukiamka unafanya mipango yoyote ili kutimiza tamaa yako mbaya ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wote wanaoweza kuleta kipingamizi katika kutimiza tamaa yako mbaya na hivyo sala yako inakuwa daima “tamaa yangu itimizwe” na sio mapenzi ya Mungu yatimizwe. Yakobo anasema Mungu hawezi kujibu sala ya namna hiyo maana ni sala mbaya. Sala nzuri inayosikilizwa na Mungu ni sala isiyogubikwa na tamaa mbaya na ubinafsi.
Ili tuweze kuondokana na tamaa mbaya sharti tukubali kuongozwa na Hekima ya Kikristo ambayo yatoka juu na ina umungu ndani yake. Mitume walikuwa wanabishana kwa sauti walipokuwa peke yao. Lakini walipoulizwa na Yesu walikuwa wanabishania nini hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kusema mawazo yake kwa sababu yalikuwa mabaya. Nasi tukiona tunaongozwa na tamaa mbaya tuende mbele ya Yesu ili tamaa hiyo isisikike. Tusitafute mafanikio kwa kufuata hekima za kibinadamu na itikadi za kiulimwengu maana matokeo yake ni majuto ambaye daima ni mjukuu. Tutafute mafanikio katika Hekima ya mbinguni ambayo ni ya upole, haing’ang’anii sheria na haki kwa gharama yoyote. Mwenye hekima hii: yuko tayari kusamehe hata kama sheria inamruhusu kulalamika. Yuko tayari kuachilia haki yake ikibidi kwa ajili ya amani. Yuko tayari kufanya huruma zaidi ya haki. Hekima hii iko tayari kuwasikiliza wengine. Anayetaka ukubwa au uongozi lazima awe tayari kusikiliza mawazo ya wengine hata kama yako kinyume cha mawazo yake. Hekima hii inazaa matunda mema; amani, uvumilivu na kusamehe, haina fitina wala unafiki.
Tukitaka kuishi vema katika jumuiya zetu lazima tuwe wazi. Maneno tunayoongea mbele za wenzetu yalingane na mawazo tunayofikiri, pia yalingane na maneno tutakayosema juu yao hata kama wao hawapo. Tumwombe Mungu atuepushe na tamaa mbaya na ubinafsi, atujalie unyenyekevu tusijione watu wa maana zaidi ya wengine, tutambue kuwa maisha ni zaidi ya umaarufu, mali na mamlaka au madaraka, maisha ni zaidi ya kujulika, maisha ni zaidi ya tamaa za mwili, maisha ni zaidi ya malumbano. Basi tuitafute kwa bidii Hekima itokayo juu ili ituwezeshe kuishi kwa amani na furaha na mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele.