Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Malumbano ya Mitume wa Yesu kuhusu ukuu! Yesu anakazia huduma ya upendo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Malumbano ya Mitume wa Yesu kuhusu ukuu! Yesu anakazia huduma ya upendo! 

Tafakari Jumapili 25 Mwaka B: Malumbano Ya Mitume Kuhusu Ukuu!

Mwinjili Marko anatusaidia kuona kuwa bado Mitume walikuwa mbali na utume wa Kristo, ni hatima ya Bwana na Mwalimu wao. Na hata walipofika Kapernaumu Yesu anawauliza; “Mlishindania nini njiani?” Ni swali lenye katekesi ndani mwake, ni fursa hii anaitumia tena Yesu kuwapa fundisho lingine juu ya maana ya Kristo, Mpakwa mafuta wa Mungu, yaani Masiha wa Mungu. Huduma!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya Dominika ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa tulikutana na ungamo la imani la Mtume Petro; “Wewe ndiwe Kristo”. Ni jibu sahihi kabisa lakini kwa bahati mbaya sana si tu mtume Petro bali hata na wale mitume wengine wote bado walikuwa na picha tofauti kabisa na kile alichokuwa anawafundisha Bwana na Mwalimu wao. Taifa la Israeli lilikuwa chini ya utawala wa Kirumi, na hivyo kwao walikuwa wanamtarajia Masiha anayekuja ili kuwakomboa kutoka utawala ule wa Kipagani na wa kigeni, ni Masiha anayekuja kuwa mtawala wao kama wanavyokuwa watawala wengine wa dunia hii. Mwinjili Marko anatuonesha kwa mara nyingine tena Yesu anawafundisha wanafunzi wake juu ya hatima yake atakapofika huko Yerusalemu, yaani mbele yake ni mateso, kifo na siku ya tatu atafufuka. Akiwa safarini, Yesu anarudiarudia mara tatu juu ya fundisho hili gumu, ndio kusema ni fundisho muhimu kwa wanafunzi wake. Pamoja na kurudiarudia mara tatu tunaona bado mitume walikuwa mbali na ukweli huo, walikuwa bado na mawazo tofauti kabisa na misheni yake Kristo.

Ni baada ya kumtambua na kukiri kuwa Yesu ni Kristo, mitume wanamtegemea Masiha anayekuwa mtawala, na hivyo hata kati yao wakaanza kuulizana na kujadiliana juu ya nafasi za kila mmoja wao, nani atakuwa nani katika serikali na utawala wa Yesu? Hivyo yakazuka malumbano baina yao, kila mmoja anajiona kuwa na nafasi ya heshima na labda yenye masilahi kwa kila mmoja wao. Ni katika muktadha huo, Yesu leo anawafundisha tena kwa mara ya pili juu ya hatima yake huko Yerusalemu; “Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka.” Labda tunaweza kujiuliza Yesu anaposema “yuaenda kutiwa katika mikono ya watu”, na nani anayeenda kumtia katika mikono ya watu? Mara nyingi tunafikiri ni Yuda Iskariote anayemsaliti Yesu, lakini kwa kweli ni kitendo kinachoonesha ni Mungu mwenyewe anayemtoa mwanae wa pekee ili awe sadaka ya ukombozi wa mwanadamu na ulimwengu mzima. Ni kitendo cha upendo usio na kujibaki wa Mungu mwenyewe kwa mwanadamu na kwa kila kiumbe. Anayependa anajitoa bila kujibakiza kwa yule anayempenda, habaki ndani mwake bali anatoka na kujikabidhi mzima mzima kwa yule anayempenda na ndio tunaona kitendo cha Mungu anayejitoa bila kujibakiza kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu.

“Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.” Ndio hali wanayokuwa nayo mitume mintarafu fundisho hili la mateso, kifo na ufufuko wake Kristo. Ni gumu kwao kwani bado mawazo na fikra zao zilikuwa ni zile zenye kuakisi mantiki ya ulimwengu huu, ukubwa na utawala wa dunia hii. Mitume walishindwa kukata vichwa vyao ili kuongozwa na kuivaa mantiki ya mbinguni, ile ya Mungu mwenyewe. Kama tulivyotangulia kuona hapo juu bado mitume wanafikiri kuwa Kristo anaenda kuwa mtawala kama watawala wa dunia hii, anayeenda kuchukua nafasi ya heshima na sifa na hivi hata nao pia watashiriki kwa kupewa nafasi na vyeo mbali mbali katika utawala wake. Ni hapo wanajadiliana baina yao juu ya nafasi na vyeo watakavyokuwa navyo baada ya kufanya mapinduzi ya utawala wa kigeni wa Kirumi huko Yerusalemu.

“Mwalimu. Twataka utufanyie tutakachokuomba…utujalie sisi kuketi, mmoja mkono wako wa kulia na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.” Mawazo ya namna hii hayakuwa kichwani kwa wale mitume wawili tu, yaani wana wa Zebedayo, Yakobo na Yohane bali kwa mitume wote. (Marko 10:35-37). Ni fundisho gumu kwao, kwani haikuwa inaingia akilini iweje Mungu aruhusu mteule wake, auawe kwenye mikono ya watu? Ni kama Elifazi alivyomshauri rafiki yake Ayubu; “Fikiri mwenyewe, je, mtu asiye na hatia hupotea? Tangu lini watu wema wakaangamizwa? Bali mimi kila mara nimeona hivi: Wapandao maovu na wenye kusia mateso, huvuna hayo hayo.” (Ayubu 4:7-8) Na hata Mzaburi pia anasema: “Nilikuwa kijana, sasa mimi ni mzee, lakini sijamwona mnyofu ameachwa wala watoto wake wakiomba mkate.” (Zaburi 37:25) Na hata baada ya kulisikia fundisho lile kwa mara ya pili tena wakiwa wenyewe tu na Bwana na Mwalimu wao, bado Mitume walishindwa kulielewa fundisho lile gumu na hivyo kushindwa hata kuuliza swali. Bado hawakuwa tayari kupokea fundisho juu ya mateso na msalaba na kifo na ufufuko. Ni fundisho lenye makwazo kwao, ni jiwe la kujikwaa kwao, ni fundisho gumu kwa akili zetu za kibinadamu.

Mwinjili Marko anatusaidia kuona kuwa bado Mitume walikuwa mbali na utume wa Kristo, ni hatima ya Bwana na Mwalimu wao. Na hata walipofika Kapernaumu Yesu anawauliza; “Mlishindania nini njiani?” Ni swali lenye katekesi ndani mwake, ni fursa hii anaitumia tena Yesu kuwapa fundisho lingine juu ya maana ya Kristo, Mpakwa mafuta wa Mungu, yaani Masiha wa Mungu. Mijadala ya nani mkubwa, ipo sio tu katika ulimwengu wa kisiasa na kijamii bali hata katika jumuiya zetu za Kanisa, iwe nyumba za watawa, iwe ni katika jumuiya za mapadre, iwe ni kati ya maaskofu au makardinali na  kadhalika. Ni mashindano yanayokuwepo katika maisha yetu ya siku kwa siku, lakini leo Yesu anatualika kusogea karibu yake ili atufundishe jinsi ya kuwa kweli wafuasi na wanafunzi wake. Ilikuwa ni kawaida kama ya Marabi mijadala juu ya ukubwa na hivyo nafasi za heshima, iwe mezani, kwenye masinagogi, njiani na hata sehemu zenye mikusanyiko mikubwa, watu hawa kila mara walihitaji kuwa na nafasi yao ya heshima, nafasi ya pekee inayoakisi vyeo na ukubwa wao. Na hata marabi walifundisha kuwa paradiso pia kulikuwa na ngazi au nafasi saba, hivyo watakatifu kila mmoja ilitegemea na utakatifu wake, kila mmoja ana nafasi yake kwani zile nafasi saba hazifanani.

“Akaketi chini, akawaita wale Thenashara…” Kuketi chini, Yesu hapa anachukua tena nafasi kama ya Marabi, nafasi ya kuwa mwalimu, kwani Marabi walipokuwa wanatoa fundisho muhimu na kubwa iliwapasa kuketi na ndio kitendo anachokifanya Yesu leo. Si tu anaketi bali pia anawaita, kuwaita maana yake walikuwa mbali bado naye, mbali katika kuwaza na hata kufikiri, anawaalika kubadili vichwa vyao, kukata vichwa vile vinavyoongozwa na mantiki ya dunia hii ili kuvaa kichwa kipya, ndio kile kinachowaza na kufikiri kadiri ya mantiki ya Mungu mwenyewe. “Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.” Ni fundisho muhimu na kubwa kwa kila mfuasi wake Yesu Kristo na ndio tunaona Wainjili wanarulirudia mara sita juu ya kuwa wadogo na watumishi wa wengine. Mwinjili Marko anatuonesha pia kuwa fundisho hili Yesu alilitoa alipokuwa nyumbani. Nyumba hapa inaashiria jumuiya nzima ya wabatizwa, yaani Kanisa. Ni fundisho kwa kila mbatizwa, kwa kila mmoja wetu anayetaka kuwa mfuasi na mwanafunzi wake Bwana wetu Yesu Kristo. “Lakini ninyi sivyo!

Bali aliye mkubwa wenu awe kama mdogo wenu, na kiongozi awe kama mtumishi.” (Luka 22:26-27) Kila mmoja wetu kwa nafasi zetu mbali mbali tunaalikwa kutoa huduma kwa upendo na unyenyekevu na hivyo asiwepo hata mmoja wetu wa kunyanyua mabega kwani ni kinyume na maisha ya ufuasi wa kweli. Ni kweli ni kishawishi cha kibinadamu cha kujiona wa muhimu au mkubwa kuliko wengine, lakini sisi tunaotaka kuwa wafuasi wa Yesu Kristo tunaalikuwa kuongozwa na mantiki ya Kimungu, ndio ile ya udogo, ile ya utumishi, ile ya unyenyekevu daima. “Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia…” katika muktadha wa Kiyahudi, watoto walipuuzwa kwani ni viumbe wasio na ukomavu na hivyo hakuna aliyemtia maanani mtoto mdogo. Yesu anamtwaa mtoto na kumkumbatia na ndio anamtumia kutoa fundisho lile muhimu kabisa. Yesu anamtumia mtoto kama kielelezo cha maisha ya kila mwanafunzi na mfuasi wake, kwa kila mbatizwa. Mtazamo hasi juu ya watoto walikuwa nao hata wanafunzi wa Yesu, na ndio tunaona Mwinjili Marko 10:13-16 juu msimamo wa Yesu kwa watoto; “Watu walimletea watoto wadogo ili awaguse, wafuasi wake wakawakemea. Lakini Yesu alipoona hayo aliudhika akawaambia, waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, asiyeupokea ufalme wa Mungu kama watoto, hatauingia kamwe. Kisha kawakumbatia na kuwawekea mikono, akawabariki.”

Ni kutoka kwa watoto tunajifunza udogo, jinsi wanavyojikabidhi kwa imani kwa wazazi wao, jinsi wanavyopenda bila kusubiri faida au manufaa binafsi. Leo tunaishi katika ulimwengu wenye ushindani mkubwa si tu kiuchumi, au kisiasa bali hata kijamii na kidini. Ni ulimwengu ambapo kila mmoja ili aonekane amefanikiwa basi lazima kujichukulia nafasi yenye tija, nafasi ya kwanza, nafasi ya heshima. Utu wa mtu hautokani tena na ukweli wa kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bali kwa kile unachokuwa nacho, au nafasi unayokuwa nayo. Na ndio leo Yesu anatualika sisi wanafunzi wake kuwa kama watoto wadogo, kuwa na moyo wa mtoto mdogo mbele ya Mungu, ndio moyo wa imani isiyo na mashaka, ndio moyo usiokuwa na ubinafsi wala kujitafuta. “Mtu akimpokea mtoto mmoja kwa jina langu, anipokea mimi, na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma”. Ni wito kwetu sote kuwa walinzi wa watoto wadogo wadogo, kwa bahati mbaya sana leo tunasikia madhulumu ya watoto wadogo si tu kutoka kwa watu wasioamini bali hata kwa watumishi wa Kanisa tena wa ngazi za juu kabisa. Ni vema katika Dominika ya leo kutambua kuwa kila mmoja wetu leo anaalikwa na Kristo kuwa kama kristo mwenyewe aliyewakumbatia watoto na kuwabariki, aliyewapenda na kuwalinda watoto wadogo. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwalinda wale wote wasiokuwa na uwezo wa kujisemea na kujitetea, kuona kila mmoja anaishi kama mwana kweli wa Mungu, kujali utu wa wengine. Nitawakie tafakari na Dominika njema.

Tafadhali mshirikishe ni jirani yako, kama sehemu ya kuinjilishana!

16 September 2021, 16:55