Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma! 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka B wa Kanisa: Uongozi Ni Huduma!

Wazo kuu: Haki kama kielelezo cha uchaji wa Mungu; Hekima inayofumbatwa katika unyenyekevu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya mapendo kwa watu wa Mungu. Haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mwenyezi Mungu na jirani haki yao. Mababa wa Kanisa wanasema, haki kwa Mwenyezi Mungu huitwa fadhila ya Kimungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Wazo kuu linalojitokeza katika Liturujia ya Neno la Mungu ni: Haki kama kielelezo cha uchaji wa Mungu; Hekima inayofumbatwa katika unyenyekevu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya mapendo kwa watu wa Mungu. Haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mwenyezi Mungu na jirani haki yao. Mababa wa Kanisa wanasema, haki kwa Mwenyezi Mungu huitwa fadhila ya Kimungu. Haki kwa binadamu inakita mizizi yake katika amani, utu, heshima, usawa na maridhiano. Mtu mwenye haki atastawi kama mtende wa Lebanon, kwa sababu mawazo yake ni sahihi na anaonesha na kushuhudia kwa matendo yake unyofu wa moyo. Rej. KKK 1808.

Kristo Yesu ni mfano kamili wa mtu mwenye haki, kwani aliteswa, akafa na hatimaye akafufuka kwa wafu. Hivyo tunapaswa kutunza heshima na sifa njema ya jirani, kwani kumwondolea mtu sifa njema ni kosa dhidi ya fadhila ya haki na mapendo. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anatuambia kwamba, Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Rej. KKK 1716. Matunda ya haki ni: heshima, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, amani na utulivu. Mababa wa Kanisa wanasema amani si kutokuwako na vita wala shinikizo la usawa wa nguvu kati ya wapinzani. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo. Rej. KKK 2304.

Hekima ya Kikristo ni chemchemi ya amani, unyenyekevu, upole, huruma na ukweli. Imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki na kimsingi inapambwa na amani kama anavyosimulia Yakobo Mtume anavyosimulia katika Waraka wake kwa Watu wote. Yak 3:16-14: 3. Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, hekima ni karama na mwanga wa maisha ya kiroho. Ni nuru inayomwezesha mwamini kutafakari mambo ya kimungu kwa jicho la kimungu kwa moyo wa unyenyekevu kadiri ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Hekima ni karama inayoibuliwa kwa kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na mshikamano wa upendo.

Hekima ni karama inayomwezesha mwamini kutambua kwa furaha mpango wa Mungu katika mambo yote. Hekima ya maisha ya Kikristo ni neema ya Mungu na uwezo wa kutambua uwepo na uzuri wake unaowazunguka watu wake wote pasi na ubaguzi. Ulimwengu mamboleo una kiu ya kuona watu wakitolea ushuhuda wa karama hii. Huu ni mwaliko wa kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kutukirimia karama hii, ili kwa kufurahia katika Roho Mtakatifu, tuweze kuwa kweli ni wachamungu, yaani watu wa Mungu; tukiwa wazi kwa hekima na nguvu ya upendo unaoganga, kuponya na kuokoa! Huu ni wajibu wa kila mwamini kuhakikisha kwamba, ananogesha maisha yake kwa ushuhuda wa uwepo angavu na endelevu wa Mungu, ili kung’amua mema na mabaya katika maisha, tayari kuwaonjesha wegine upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani.

Tunahamasishwa na Mama Kanisa kukua, kukomaa na kudumu katika hekima ya Mungu, ili tuweze kutaalamika katika mambo ya Kimungu kwa kuwashirikisha pia jirani zetu. Hekina na ukweli wa Kikristo ni zawadi ya Roho Mtakatifu, vinginevyo ni patashika nguo kuchanika kutokana na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; magomvi na tamaa mbaya kama anavyokaza kusema Yakobo Mtume katika Somo la Pili. Uchu wa mali, madaraka na sifa ni kielelezo cha watu kumezwa na malimwwengu, hali inayochochewa na tamaa na wivu na matokeo yake wanakuwa ni rafiki wa dunia na kwa upande mwingine, wanakuwa ni adui wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu huwapinga wajikuzao, watu wanaopenda kujimwambafai bali huwapa neema wanyenyekevu wa moyo. Injili: Mk 9: 30-37. Katekesi kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu baada ya ungamo la imani la Mtakatifu Petro bado haikufua dafu wala kuzama katika akili na nyoyo za Mitume wa Yesu. Tunakumbushwa kwamba, Kristo Yesu alitekeleza kazi ya ukombozi kwa njia ya Fumbo la Msalaba, jambo ambalo halikuwa rahisi sana kwa wafuasi wake kuelewa kwa wakati huo, kwani mawazo yao yalijikita zaidi katika masuala ya kiulimwengu. Walitamani kuwa wakuu na kupokea heshima katika Ufalme wa Mungu. Lakini Kristo Yesu anakaza kusema, uongozi katika Kanisa unafumbatwa katika uaminifu, mateso na kifo.

Yesu mwenyewe alitumia fursa hii kuwaelewesha maana halisi ya kuwa ni mfuasi wake; kwa njia ya uaminifu, mateso na kifo. Ili kuweza kutekeleza haya kwa ukamilifu zaidi, kuna haja kwa wafuasi wa Kristo kujenga utamaduni wa kukaa karibu zaidi na Kristo kwa njia ya: Kufunga na Kusali; Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na matendo ya huruma. Wafuasi wa Kristo Yesu, wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni wito wa huduma inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa ukuu na utakatifu wa Mungu; kwa huruma na upendo unaofunuliwa na Kristo Yesu kwa waja wake na kilele chake ni Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Kwa ufupi kabisa, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo inayosimikwa katika hali ya upole, unyenyekevu na utu wema. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, daima wakijitahhidi kujivika hekima ya Kikristo ili kuwahudumia watu wa Mungu kwa unyenyekevu katika kweli na haki!

Liturujia J25
18 September 2021, 15:40