Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Wivu na makwazo ni changamoto katika mchakato wa kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Wivu na makwazo ni changamoto katika mchakato wa kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 26 Mwaka B: Wivu na Makwazo!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 26 ni mwendelezo wa kuishi vema kwa upendo ili kuepuka tamaa mbaya na wivu, ili kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu kwa kuishi maisha ya mfano mwema ili mwisho wa yote kupewa tuzo mbinguni katika uzima wa milele na Mungu Baba aliyetujalia zawadi zote za kiroho na kimwili.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Vifungu vya Neno la Mungu vinavyotuongoza katika tafakari hii. I. Hes. 11:25-29; II. Yak. 5:1-6; III. Mk. 9:38-43, 45, 47-48. Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni mwendelezo wa fundisho la masomo ya dominika ya 25B kuhusu kuishi vema kwa upendo katika jumuiya, kuepuka tamaa mbaya na wivu, ili kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu kwa kuishi maisha ya mfano mwema ili mwisho wa yote kupewa tuzo mbinguni katika uzima wa milele na Mungu Baba aliyetujalia zawadi zote za kiroho na kimwili. Somo la kwanza la Kitabu cha Hesabu (11:25-29); linatueleza kuwa Musa na wasaidizi wake walifaulu kuwaongoza Waisraeli toka utumwani kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Mwanzoni roho wa Mungu alikuwa juu ya Musa peke yake. Baadae Mungu alitwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu Musa na kuitia juu ya wazee sabini waliokuwa katika hema ya kukutana naye nao wakapokea kipaji cha unabii, wakaweza kutabiri, lakini mara moja tu. Eldadi na Medadi waliosalia kambini roho ile iliwashukia nao wakatabiri kambini. Musa alipoona hivyo alifurahi.

Lakini Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujani wake, aliposikia habari za Eldadi na Medadi kutoa unabii kambini alimwambia Musa; “Ee bwana wangu Musa, uwakataze.” Musa alimjibu; “Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake.” Onyo hili la Musa kwa Yoshua ni fundisho kwa wale wanaoona wivu pale neema na baraka za Mungu zinapowashukia wengine wakifikiri kuwa wao ndio wanaostahili tu kuzipokea neema na baraka zitokazo kwa Mungu. Mungu hana upendeleo anamjalika kila mtu kadiri ya mpango wake ili awasaidie na wengine waweza kutambua mpango wake wa watu wote kuwa watakatifu.

Somo la Pili la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (5:1-6); linatoa maonyo juu ya utajiri wa dhuluma. Matajiri na makabila wanaowanyonya wengine, wanakosa haki mbele ya Mungu na wataadhibiwa sana. Yakobo anasema; “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Maneno ya Yakobo ni kama rungu la kumuua nyani ambalo haliangalii usoni bali yanausema ukweli jinsi ulivyo: “Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.” Maonyo haya yanatutahadharisha na mali zitokanazo na dhuluma. Basi tujiepushe nazo tusije nasi tukalia na kupiga yowe kwa maumivu makali.

Injili ilivyoandikwa na Marko (9:38-43, 45, 47-48); imebeba mawazo makuu matatu: Wazo la kwani ni onyo Yesu kwa mitume kuwa wasimkataze mtu anayetoa pepo kwa jina lake kwa wivu sababu tu hafuatani nao. Yohane alitoa taarifa kwa Yesu akisema; “Mwalimu tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.” Yesu akamjibu: “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.” Wazo la pili ni maonyo makali ya Yesu kwa wanaowapotosha na kuwaingiza wengine dhambini akisema; “Na yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.” Tatu Yesu anafundisha kuhusu makwazo yatokayo nafsini mwa mtu na kusababisha makwazo kuwa sharti yang’olewe: “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate, ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kutupwa katika jehanum ukiwa na miguu miwili. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe ulitupe, ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kutupwa katika jehanum ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki ukiwa na macho mawili.”

Makemeo haya ni kuonyesha ubaya wa wivu na dhambi za makwazo. Wivu unakwamisha maendeleo, unaleta uhasama na chuki. Hivyo tuukwepe. Mazingira ya dhambi nayo tuyakwepe, tuyaogope kwa hofu na tetemeko. Wivu ni hasira itokanayo na wema na maendeleo ya mwingine. Mtu mwenye wivu anakasirika akiona mwingine anaendelea zaidi yake. Mwingine anaumia akiona Mungu amewatendea wema wengine ambao si wa jamii yake. Yoshua alikasirika kuona Eldadi na Medadi wakitabiri kama Musa, akaumia moyoni. Yohana alikasirika kuona asiyeambatana na Yesu anaponya na kukemea pepo. Pengine alipenda uwezo huo uwe wao peke yao. Nasi pia tunaweza kuwa na mawazo kama ya Yoshua na Yohane. Tutambue na kukumbuka daima kuwa; Wema wa Mungu hauna mipaka. Tusichukie tukiona wale walio tufauti nasi wakipendelewa na Mungu, wakiwa wema au wakitenda wema. Tungetamani watu wote wawe wema. Wao wakifanikiwa haituzuii sisi kufanikia. Jumapili iliyopita, Yakobo alitukataza kuwa na wivu na tamaa mbaya kwa sababu tabia za namna hizo husababisha vita, chuki na mafarakano katika jumuiya.

Tujihadhari, tusiwanyanyase wengine kwa mali tulizonayo. Tusiwafanyisha wengine kazi bila kuwalipa wanachostahili tukaenda kujistarehesha kwa anasa kwa kutumia jasho lao, hakika hukumu iko mbele yetu. Tujifunze kuwa watu wa haki. Yule mfanyakazi wa ndani usiyemlipa mshahara wake, akimlilia Bwana atasikia kilio chake naye atakulipa kwa uovu huo. Watoto yatima, tukiwaibia urithi wao wakamlilia Bwana, atasikia kilio chao na kutulipa kwa uovu huo. Mliokula rasilimali za umma kwa ufisa watu wakakosa huduma bora za kijamii, mahakimu na watoa ushahidi wa uongo mahakamani ili kumnyima haki mnyonge, matajiri mnaowadharau wengine kwa sababu ni maskini, wasomi mnaowadharua waiosoma kumbukeni kuwa wakimlilia Mungu atawasikiliza na kuwalipa kwa uovu wenu. Mfanye nini basi? Lieni na kupiga yowe mkauache uovu wenu ili mpone na hasira na hukumu ya Mungu. Tujifunze kutenda haki. Tusiwadharau wengine. Tuwe wakarimu hatutakosa thawabu maana Yesu anasema; “Atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji hatakosa thawabu yake”. Wema tunaoutenda kwa kuwasaidia wengine katika shida zao, hatutakosa kupewa thawabu.

Maneno ya Yesu; “Lolote jema mlilowatendea hawa wadogo, mlinitendea mimi” ni ukweli wa nyakati zote. Yesu anatudai jambo dogo sana; “tuwape watu kikombe cha maji”. Wasaidie kwa chakula walio na njaa, wafariji wanaoteseka, wagonjwa, waliofiwa, wasio na matumaini, wanaodai haki zao “waambie walio na hofu jipeni moyo.” Tumia nafasi uliyonayo katika jamii kuboresha maisha ya watu hutakosa thawabu yako. Tusiwe sababu ya wadogo kutenda dhambi maana adhambu yake ni “kufungiwa jiwe la kusaga na kutupwa baharini”. Tusiwe sababu ya wengine kuharibikiwa bali tuwe mfano mwema wa kuigwa hasa kwa watoto na vijana. Tukumbuke kuwa dhambi huanza na hisia (kusikia, kunusa, kugusa, kuona). Basi tuvikata viuongo hivyo ndiko kuvinyima mapendeleo yake ili visitupeleke pabaya. Tukumbuke kuwa; Mtaka yote kwa pupa hukosa yote. Mshika mbili moja humponyoka. Mpanda farasi wawili hupasuka msamba. Tukifanikiwa kuyaisha haya njia ya kwenda mbinguni i wazi kwetu.

Tafadhali mshirikishe pia na jirani yako, utamu wa tafakari ya Neno la Mungu inapendeza sana!

J26 Mwaka B
22 September 2021, 14:07