Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27 Mwaka B: Upendo Katika Ndoa

Maandiko Matakatifu yanatuonesha kuwa ni katika mpango wa Mungu wa milele yote, kumuumba mwanaume na mwanamke. Wote wawili wanaumbwa kwa kufanana na kusaidiana. Ni mpango wa Mungu tangu awali wawili hawa kuhitajiana na ndio kujitoa kwa mapendo bila kujibakiza kwa ajili ya mwingine. Mwanadamu anakosa kukamilika anapokuwa peke yake. Upendo wa dhati!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! “Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye.” Ndio maneno ya Mungu mwenyewe ambayo leo tunayasikia katika somo la kwanza. Mwenyezi Mungu aliona kila alichokiumba kuwa ni chema na kizuri, lakini bado akamuangalia mwanadamu yule wa kwanza na kuona alikuwa anateseka na kutabika na upweke. Mwanadamu yule wa kwanza pamoja na kuwa katika bustani ile nzuri, pamoja na kuwa na ukaribu na Mungu aliye muumba wake, na kujaliwa uwezo wa kutawala viumbe vingine vyote, bado kulikuwa na kitu alichopungukiwa nacho, ni mmoja wa kufanana naye, mmoja anayepaswa kuwa msaidizi wake, mmoja wa kujadiliana na kuishi naye, huku akimpenda naye pia akipokea mapendo kutoka kwa mwingine. Hivyo, Mwenyezi Mungu anatambua tangu awali kuwa kuna bado kilichopungua kwa mwanadamu yule wa kwanza, nacho ndio upweke, kukosa msaidizi na mwingine wa kumpenda. Kwa mwanadamu, hivyo tunaona haitoshi kuwa na mali au vitu, pia hata kuwa na ukaribu na Mungu bali daima anauhitaji wa mwingine wa kufanana naye na msaidizi wake.

Somo letu la kwanza Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, halina tu lengo la kutuonesha jinsi alivyoumbwa mwanamke, bali zaidi sana kutuonesha mwanamke ni nani. Kwa nini basi Mungu ameumba mtu mume na mtu mke? Kwa nini mmoja anajisikia kutokukamilika kwa kubaki mwenyewe bila kuunganika na mwingine wa jinsia tofauti? Maandiko Matakatifu yanatuonesha kuwa ni katika mpango wa Mungu wa milele yote, kumuumba mtu mume na mtu mke. Ni mpango wa Mungu ambapo wawili hawa wanaumbwa kwa kufanana na kusaidiana. Ni mpango wa Mungu tangu awali wawili hawa kuhitajiana na ndio kujitoa kwa mapendo bila kujibakiza kwa ajili ya mwingine. Mwanadamu anakosa kukamilika anapokuwa peke yake. Mwanamke sio mtumwa wa mwanaume, sio kitu cha kutumika bali tunaona leo, anatambulishwa kwanza ni mmoja anayefanana na mwanaume, na zaidi sana anapewa sifa nyingine ya kuwa msaidizi wa mwanaume.  

Mwanamke ni “Kenegdò”, ni neno la lugha ya Kiebrania likimaanisha wa kufanana, hivyo Mwenyezi Mungu anamuumba mwanamke sio kutawaliwa au kuwa mtumwa wa mwanamme, kwani anamuumba anayefanana na mwanaume, ndio kusema tunaona anapewa thamani na utu sawa kabisa na mwanaume. Mwanamke ni msaidizi wa mwanaume, yafaa tutambue kuwa kuwa msaidizi haimaanishi kuwa wa hadhi ya chini, la hasha. Neno msaidizi kwa Kiebrania ni “Ezer”, ndio neno ambalo pia linatumika katika Maandiko Matakatifu kumtambulisha Mungu mwenyewe. Ni Mungu anayekuwa msaada wa kweli kwa mwanadamu. Mzaburi anaimba akisema; “Nami niliye maskini na mhitaji, Ee Mungu, unijie hima! Wewe ni msaada wangu na mwokozi wangu. Ee Bwana usikawie.” (Zaburi 70:6) Basi kama Mungu ndiye anakuwa msaidizi wetu katika maisha kwa maana ya kuwa msaada wetu, basi na mwanamke leo anatambulishwa na Mungu kama mmoja mwenye kutoa msaada na hivyo kamwe asionekane kuwa ni kiumbe wa hali na hadhi ya chini, bali mmoja aliumbwa kwa kufanana na mwanaume na pia anapewa jukumu la kuwa msaada kwa mwanaume.

Hivyo, mwanaume anakosa kuwa mkamilifu anapobaki mwenyewe bila msaidizi, bila mwanamke ambaye ameumbwa kwa kufanana naye. Upweke haundoki kwa kuoa au kuolewa, bali yafaa sana tutambue ni kwa kutambua kuwa mwingine ni wa kufanana nawe, mwingine ni msaidizi wako katika maisha. Kinyume na hapo mwanadamu anabaki katika upweke ule ule, kwa kushindwa kumpokea mwingine kadiri ya mpango wa Mungu tangu uumbwaji wa mwanadamu. Kamwe mahusiano ya watu wa ndoa hayapaswi kuona mwingine kama kitu hivyo kukitawala au kukitumia kwa masilahi yako binafsi, vinginevyo mmoja anarudi na kuendelea kuishi katika upweke na mateso na mahangaiko makubwa. “Je, ni halali mtu kumwacha mkewe ?’’ Ni swali linalotoka kwa Mafarisayo kwa Yesu, lakini ni swali lenye kushangaza kwani, kundi hili kama Wayahudi wengine wote hawakuwa na mashaka juu ya uhalali wa talaka. Mwinjili Marko anaingiza wazo juu ya fundisho hili muhimu katika maisha ya wafuasi wake Kristo, na Yesu anatumia fursa ya swali lile ili kutufundisha maana halisi ya amri ya Musa, Yesu hakuja kuifuta Agano la Kale bali kutufundisha maana yake na kulikamilisha.

"Pakiwa na mtu aliyemchukua mke na kuitimiza ndoa naye, lakini mke yule hampendezi machoni pake, kwa vile ameona kitu kisichofaa, basi amwandikie hati ya talaka akampe mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake… " (Kumbukumbu la Torati 24 :1) Baadhi ya Marabi walifundisha kuwa mwanaume angeweza kumwandikia talaka mkewe katika kesi za kukosa uaminifu tu katika ndoa yake, lakini wapo wengine waliofundisha kuwa mwanaume angeweza pia kumwandikia talaka mkewe na kumwacha hata kwa kukosa kupika vyema chakula, au pale mwanaume anapomuona mwanamke mwingine anayekuwa mzuri zaidi kuliko huyu wa sasa, hapo angeweza kumwacha mkewe kwa kumwandikia talaka na kumuona mwingine. Yesu leo anawageukia Mafarisayo na kuwaambia : « Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. " Neno la Kigiriki linalotumika ni  "sklerokardia", likiwa na maana ya ugumu wa moyo, yaani, ukosefu wa kumtii Mungu, kupenda dhambi na kufa kwa dhamiri. "Zitahirini nyoyo zenu msiwe na shingo ngumu" (Kumbukumbu la Torati 10 :16) Na ndio lugha ninayotumi mara nyingi katika takafari zetu juu ya umuhimu wa kukata au kubadili vichwa vyetu, ndio kukubali kuwaza na kufikiri na kutenda pamoja na Mungu, ndio kufikiri sio kwa mantiki ile ya kibinadamu bali ya Mungu mwenyewe. Na ndicho Yesu anachotualika leo, kurudi kuwaza na kufikiri kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu.

 Ndio kusema haukuwa mpango wa Mungu tangu awali juu ya uhalali wa talaka au kumwacha mwanamke wa ndoa. Yafaa kuangalia japo muktadha wa amri ile ya Musa mintarafu hati ya talaka. Musa anawaruhusu kuandika hati ya talaka, ni kwa nia na lengo ya kumlinda mwanamke katika mazingira ya Wayahudi. Kwani kabla ya amri hii ya Musa, mwanaume aliweza kumwacha mkewe bila hati, na ikiwa mwanamke yule aliolewa na mtu mwingine, mwanaume yule wa awali angeweza kumuundia kesi ya uzinifu, na kwa kadiri ya Wayahudi kosa la uzinifu lilimpasa mwanamke apigwe mawe mpaka kifo. Hivyo amri hii ya Musa ya kuandika hati ya talaka ilikuwa na nia na dhumuni la kumlinda mwanamke, la kumtetea mwanamke ambaye alionekana kuwa wa hadhi na hali ya chini kulinganisha na mwanaume. Ni amri yenye nia ya kumuweka mazingira salama mwanamke ili asibambikiwe kesi ya uzinifu. Hati ile ilikuwa inampa mwanamke yule uhalali wa kuwa huru na hivyo angeliweza kuolewa na mwanaume mwingine, na hivyo hati ya talaka daima alibaki nayo kwa ajili ya usalama wake endapo mwanaume wa awali angetaka kumuhujumu kwa kumtaka apigwe mawe hadi kifo.

Katika somo la Injili ya leo, Yesu anatualika kurejea tangu awali juu ya mpango wa Mungu mintarafu mtu mume na mtu mke. "Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe ; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe." Ni muunganiko wenye nguvu ya upendo kati ya mtu mume na mtu mke, ni muunganiko wa kukamilishana kwa hawa wawili, mwanamke anatokana na ubavu wa mwanaume, hivyo kila mmoja anamuhitaji mwingine ili kukamilika, kila mmoja anamuhitaji mwingine ili kuishi kwa amani na furaha, bila kurudi katika upweke ule aliokuwa nao mwanadamu kabla ya kuumbwa kwa mwanamke. Wimbo Ulio Bora unatuonesha nguvu ya upendo ule kwa kusema; "Kwa kuwa upendo una nguvu kama mauti." (Wimbo Ulio Bora 8 :6) Ndio muunganiko wenye nguvu isiyoelezeka, ni matunda ya upendo ya wawili kuwa mwili mmoja na kuishi kwa kutakiana mema daima, yaani kwa kupendana katika hali zote siku zote za maisha yao, kwani huo ndio mpango wa Mungu na si vinginevyo. Kwani upendo unatoka kwa Mungu mwenyewe, basi mwanadamu anapata kushirikishwa naye upendo ule wenye asili yake kwa Mungu mwenyewe.

"Zaeni, ongezekeni " (Mwanzo 1 :28) Marabi walifundisha kuwa amri ya kwanza ya Mungu kwa mwanadamu ndio hii ya kwenda kuzaana na kuongezeka. Na hata ikatiliwa mkazo kuwa ikiwa mwanamke ni tasa basi alipaswa kumruhusu mumewe kuzaa na mwanamke mwingine, kwani ni amri na agizo la Mungu. Lakini tunaona leo Yesu anaonesha ulio mpango wa Mungu kwa mwanadamu, anatupa katekesi mintarafu muunganiko wa mtu mume na mtu mke, yaani, ndoa takatifu. Muunganiko wa mtu mume na mtu mke, Yesu anatuonesha leo ni Mungu mwenyewe anayewaunganisha wawili hawa, na anazidi kutuonesha kuwa kadiri ya mpango wa Mungu, wawili hawa wanaunganishwa na Mungu na kuwa mwili mmoja. Yesu anatufundisha mpango wa Mungu mintarafu ndoa, ni muunganiko wa mapendo kwa maisha yote, ni muunganiko usioruhusu hata mara moja hati au uhalali wa talaka. Ndoa ni muunganiko wa upendo, na asili ya upendo ni Mungu mwenyewe.

Si tu hatuwasikii tena Mafarisayo katika somo la Injili ya leo, bali mwinjili anazidi kutuonesha hata wanafunzi wake wa karibu walilipokea kama fundisho gumu na hivyo nyumbani wakamwuliza juu ya neno au swali lile. Na jibu la Yesu linazidi kuonesha juu ya fundisho ambalo tayari ameshalitoa hapo awali. "Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake ; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini." Ni hapa Yesu anaonesha juu ya agizo hili kumgusa si tu mwanaume bali mwanamke pia, sio amri inayogusa upande mmoja bali kwa pande zote mbili. Yesu leo anakazia juu ya kurejea katika mpango wa Mungu tangu awali, ndio katazo la hati ya talaka. Ndoa ni muunganiko ambao unafanywa na Mungu mwenyewe na hivyo hakuna hata mmoja mwenye uhalali wa kutenganisha kile ambacho kimeunganishwa na Mungu. Na ndio tunaona katika Kanisa Katoliki hakuna sio tu msamiati bali hata kufikiri juu ya uhalali wa hati ya talaka kwani ni kinyume na mpango wa Mungu.

Katika sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, Yesu tena anarudia kutumia mfano wa mtoto katika kumfuasa. "Kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao." Ni mwaliko kwetu nasi kuwa na moyo na roho ile ya kitoto, ndio roho na moyo wa kujikabidhi bila mashaka kwenye mpango na mapenzi yake Mwenyezi Mungu katika maisha yetu, kulitii na kulishika Neno lake bila kuanza kufuata mantiki zetu za kibinadamu, ni kukubali kuongozwa daima na Mungu. Leo mwanadamu anapotoka kwa kuanza kuunda mpango wake, anakengeuka kwa kuacha kumsikiliza Mungu na kuanza kufuata njia zake, iwe katika maswala ya ndoa na hata mengine ya maisha ya siku kwa siku. Mwanadamu leo anachukua nafasi ile ya Mungu, kwa kujiumba yeye mwenyewe, kwa kuamua kuishi aonavyo inampendeza yeye, bali sisi, tulio wafuasi na rafiki zake Yesu Kristo, hatuna budi kutambua kuwa sisi ni viumbe na hivyo daima hatuna budi kuishi kadiri ya mpango wa Muumbaji wetu. Na ndio huu mwaliko wa kuwa kama watoto daima mbele ya Mungu na mpango wake kwetu, kwani daima tuna hakika Mungu anatupenda na hivyo njia zake ni kutuhakikishia maisha ya furaha milele na kinyume chake ni kuyaangamiza maisha yetu. Kamwe tusijione tu wakubwa mbele ya Mungu na hivyo kutaka kufanya kadiri tunavyopenda na kutaka sisi na si kadiri ya Neno na maagizo yake. Leo Yesu anawakumbusha si tu Mafarisayo na wale wanafunzi wake wa kwanza bali kila mmoja, ni Neno la Mungu ndio linapaswa kuongoza maisha yetu. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

30 September 2021, 11:29