Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Katekesi kuhusu Ndoa na familia Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Katekesi kuhusu Ndoa na familia 

Tafakari Jumapili 27 ya Mwaka B: Katekesi ya Ndoa na Familia!

Somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo (2:18-24); ni simulizi la kuumbwa kwa mwanadamu kulivyo tofauti na uumbaji wa viumbe vingine. Katika simulizi hili tunaona kuwa mwanamke ana hadhi na utu sawa na mwanaume kwa kuwa wote waameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu naye ni msaidizi wa mwanaume n asio mtumwa kwake. Yesu anakazia udumifu wa maisha ya ndoa!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ni katekesi inayotukumbusha asili yetu sisi wanadamu, asili ya maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo (2:18-24); ni simulizi la kuumbwa kwa mwanadamu kulivyo tofauti na uumbaji wa viumbe vingine. Katika simulizi hili tunaona kuwa mwanamke ana hadhi na utu sawa na mwanaume kwa kuwa wote waameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu naye ni msaidizi wa kweli wa mwanaume n asio mtumwa kwake kama tunavyosoma kuwa: “Bwana Mungu akasema; Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye.” Hii inatuonyesha kuwa upendo aliouweka Mungu kati ya Mume na Mke katika maisha ya ndoa yanapita aina zote za mapendo maana ni katika ubavu wa mwanamume akiwa usingizini, mwanamke amepatika kama tunavyosoma; “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha, akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu, Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.”

Naye Adamu alipomwona alisema; “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Hapa tunaona asili ya ndoa kuwa ni ya mume mmoja na mke mmoja kadiri ya mpango wa Mungu. Kinyume na hapo, tofauti zingine zinazojitokeza katika maisha ya ndoa ni ya ibilisi na lengo ni kupinga mpango wa Mungu, na matokeo yake yako wazi kuteseka kwa mwanadamu kwa kuishi na kufanya yaliyo kinyume na mpango wa Mungu. Somo la Pili la Waraka kwa Waebrania (2:9-11); linatufundisha kuwa Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu alipochukua umbo la mwanadmu katika fumbo la umwilisho na kuwa Mungu-Mtu, alizaliwa, akakua na kuishi katika familia ya kibinadamu. Katika utu wake alionekana kuwa mdogo kuliko Malaika, akaonja mateso na kifo kwa kumtii Mungu Baba yake kama tunavyosoma; “Ndugu, twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.”

Kwa sababu hiyo alipata utukufu na heshima za pekee hivi hata wanadamu wanaweza kukombolewa kwa njia yake; “Kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.” Hapa tunaona dhamani na umuhima wa familia katika maisha ya mwanadamu hata Mungu alipokuja kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti alikuja kwa kupitia katika familia ili kutuonyesha umuhimu na dhamani ya ndoa na maisha ya familia. Injili ilivyoandikwa na Marko (10:2-16); imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatufundisha kuwa katika ndoa ya kweli mume na mke ni mwili mmoja; hivi hawawezi kutengana. Sehemu hii ni jibu la Yesu kwa swali la Mafarisayo kuwa; “Je, ni halali kwa mwanamume kumwacha mkewe?” Swali lao limejaa hila maana ni la kumjaribu. Jibu la Yesu linawakumbusha mafundisho ya Mungu akirejea sherea alizowapa Musa akiwauliza; “Je, Musa aliwaauru nini?” Kwa jibu lao kuwa; “Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha”, Yesu anawaambia ni “kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao Musa aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, Mungu aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Wanafunzi wake nao hawakuelewa fundisho hilo, ndio maana wakiwa nyumbani wanamuuliza habari ya neno hilo.

Yesu anawaambia kuwa; “Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini.” Sehemu ya Pili inatueleza kuwa tukitaka kuingia katika ufalme wa Mungu lazima tuwe watulivu, waongofu na wanyenyekevu. Yesu anatoa fundisho hili baada ya wanafunzi wake kuwakataza watoto wadogo walioletwa kwake ili awaguse. Kitendo cha wanafunzi kuwakemea waliowaleta watoto kwake kilimfanya Yesu achukizwe sana na kuwaambia; “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyekubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.” Kumbe, tunaona wazi kuwa ndoa ya mume mmoja na mke mmoja ni mpango wa Mungu na mwanadamu kuishi katika familia ni mpango wa Mungu. Lakini hali ya maisha ya ndoa na familia nyakati zetu imegubikwa na changamoto nyingi mno. Wapo waliofunga ndoa na wanaishi vizuri. Tuwapongeze na kumshukuru Mungu. Ni ukweli kuwa mafanikio yao si kwamba hawana matatizo bali wanayavumilia kwa moyo wa sadaka na imani. Wapo waliofunga ndoa lakini ndoa zao ni za matatizo na wengine wameachana. Tuwaombee hao.

Wapo wale wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa na wamezaa watoto maana kitanda hakizai haramu. Wapo pia vijana na watu wazima wanaoishi peke yao hawajaolewa wala kuoa labda kwa kupenda au kutokupenda nao wana watoto. Hili nalo ni tatizo na changamoto kubwa katika jamii zetu. Tukumbuke kuwa hii ni hatari sana kwa malezi ya mtoto. Hali hii yaweza sababishwa na vitu vingi lakini hata hivyo haiwezi kuhalalishwa. Tufanye nini basi katika hali hii? Tukubali kuwa ndoa ni tunu kwa maisha ya mtu. Ndiyo maana Mungu anasema; “Si vema huyu mtu awe peke yake.” Kwa vijana; tuwasihi, tuwashauri, tuwafundishe na kuwaelimisha wahue uzuri na furaha ya ndoa na familia na ubaya wa kuishi kiholela. Ni wajibu wa wazazi kuwasaidie kujiandaa vyema kuingia katika maisha ya ndoa na familia na mtu sahihi na sio kupurukuka na kuolewa au kuoa kiholela. Pia wazazi kuwajibika kuwafundisha watoto madhara ya ngono au mapenzi kabla ya ndoa. Tabia hii sio tu ni dhambi kwa lenyewe bali pia linaleta ubaridi katika ndoa pindi mtu anapoolewa au kuoa maana hana chochote kipya anachotarajia katika ndoa.

Tukumbuke, anayefanya ngono au mapenzi kabla ya ndoa hana zawadi yoyote ya dhamani anayoitunza kwa ajili ya mwenzake wa ndoa na hivyo hana cha kujivumia kwa mume au mke wake maana atamwona yuko sawa tu na wengine aliowahikuwa nao. Wazazi kuwafundisha na kudumisha usawa, haki, heshima na ushirikiano kwa watoto. Pasiwepo Bwana na mtumwa katika maisha ya ndoa. Lakini pia tunapopigania usawa na haki tukumbuke kuwa “mke asiache kuwa mke na mme asiache kuwa mme” na kila mtu atimeze wajibu wake katika familia. Hili linapaswa kuambatana na sala na uaminifu. Kukosa uaminifu katika ndoa ni chanzo cha matatizo katika ndoa ambako kunaendana na uongo katika maisha. Moyo wa sadaka unahitajika katika maisha ya ndoa na familia. Hii inaambatana na kuamua kuachana na wengine. Wazazi mjifunze na tuwafundishe watoto “kuacha”, na kusema “inatosha.” Hapo atakuwa na ujasiri wa kumwacha baba na maman a kuambatana na mwenzake.

Tujifunze kutoka kwa Tobia ambaye ni mfano wa upendo wa dhati na wa kweli katika ndoa. Kabla kuoa Tobia alisali akisema: “Utukuzwe ee Mungu wa wazee wetu…ndiwe uliyesema: Si vizuri mwanamume kuwa peke yake; tumuumbe mtu wa kumsaidia aliye kama yeye. Kwa hiyo namchukua dada yangu Sara si kwa sababu ya tamaa ya mwili ila nafanya hivyo kwa dhamiri safi” (Tobiti 8: 5-7). Tobia alikuwa na upendo kwa Sara na si tamaa ya mwili. Upendo ni pale unapopendezwa na kupenda kila kitu ambacho mwenzako anachofanya. Tamaa ya mwili unapenda kitu kimoja. Katika upendo haufikirii hata siku moja kutengana. Katika tamaa ya mwili haufikirii hata siku moja kama mnaweza kuishi pamoja. Katika tamaa ya mwili kuwa naye tu katika chumba cha kulala na si kwingineko. Katika tamaa ya mwili kuugana ni; “Tukutane wiki ijayo wakati kama huu na chumba hiki na kitanda hiki.” Katika upendo unaandika na kutuma ujumbe wa mapendo. Katika tamaa ya mwili unaandika tu namba yake ya simu. Katika upendo macho yanakutana, tabasamu zinakutana na masikio yanakutana. Katika tamaa ya mwili ni ndimi tu zinakutana. Basi tuwaombee wana ndoa, ili waweze kuishi kwa upendo wa dhati na sio katika tamaa za mwili ili kutoka kwao wengine wajifunze dhamani na hadhi ya ndoa.

Jumapili 27 Mwaka B
30 September 2021, 16:52