Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka B: Kristo Yesu Ni Faraja na Matumaini
Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 23 ya mwaka B wa Kanisa. Ugonjwa na mateso yamekuwa daima kati ya matatizo mazito sana yanayoweka maisha ya mwanadamu katika majaribu. Katika ugonjwa mtu anapata mang'amuzi ya kutokuwa na uwezo, ya mipaka yake na kikomo chake. Kila ugonjwa unaweza kutufanya tuchugulie kifo. Huruma ya Kristo Yesu kwa wagonjwa na kazi zake za kuponya ni ishara angavu kwamba, Mwenyezi Mungu amewajia watu wake na kwamba, ufalme wa Mungu umekaribia. Kristo Yesu alikuwa na uwezo wa kuponya na kusamehe dhambi, kielelezo cha upendo na dhamana ya Mama Kanisa katika kufariji. Katika Sakramenti za Kanisa, Kristo Yesu anaendelea kuwagusa waja wake, ili kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao! Rej. KKK 1500-1503. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatualika kutafakari ukweli ya kwamba Mungu ni Baba ni wa watu wote. Yeye hambagui yeyote bali anawaita na kuwapokea wote kwake kama wana wake. Hivyo basi, sisi nasi tunaalikwa kuchukuliana kama ndugu na kama watoto wa Baba mmoja. Tunaalikwa kupendana na kutendeana mema na kwa kuiga mfano wa Kristo mwenyewe tunaalikwa kuwapokea watu wote basi ubaguzi. Tukifanya hivyo Mungu atatukuzwa kweli kati ya watu na sisi tutatakatifuzwa.
TAFAKARI: Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Isaya ni neno la matumaini kwa wale wenye moyo wa hofu. Ni neno la faraja ya kwamba Mungu ni wokovu wa watu wake. Yeye ndiye huwainua watu kutoka katika hali yao ya unyonge, mahangaiko na huzuni na kuwajaza tena furaha na amani. Nabii Isaya anatangaza ujumbe huu kwa watu wa Mungu walioko utumwani, na anawataka wawe na moyo wa matumaini na wala wasiogope kwa sababu Mungu wao anakuja kuwaokoa. Nabii Isaya anayatamka haya kwa sababu anamtambua Mungu kuwa Baba wa huruma na upendo ambaye anawajali watu wake. Hivyo, mbali na kutoa neno la matumaini na faraja kwa watu wa Mungu, somo hili linatangaza pia uweza wa Mungu, ukuu wake na tabia yake ya upendo kwa watu wake. Katika somo la pili, Mtume Yakobo anawaasa wote walio na imani kwa Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, wasiwe na upendeleo. Anawaonya waepuke dhambi ya ubaguzi na anawaalika waoneshe upendo na kuwatendea wote kwa usawa.
Anawaonya dhidi ya dhambi ya ubaguzi kwa sababu ni kinyume cha tabia ya Mungu aliye Baba wa wote na inakinzana na mwito wa kikristo wa kuwapenda watu wote. Kwa maneno mengine mtume Yakobo anawaambia wale wenye imani katika Kristo Yesu ya kwamba imani ya kweli inajidhihirisha katika namna wanavyowatendea wengine. Matendo yanayoongozwa na imani ya kweli hayatambagua yeyote kwa sababu ni myahudi au myunani, mfungwa au mtu huru, maskini au tajiri, bali yanafungua mlango na kuwapokea wote kama wana wa Mungu. Katika Injili Yesu anaendelea na kazi yake ya kutangaza Habari Njema ya Ufalme wa Mungu. Anaendelea na ziara yake kutoka mji mmoja hadi mwingine na anakutana na watu ambao anawagusa kwa maneno na matendo yake ya kimungu. Anafanya yote pasipo kumbagua mtu bali anawapokea wote wanaomwendea kwa imani. Kama asemavyo mtume Paulo, Yesu alijishusha na kuwa yote kwa watu wote. Maskini, tajiri, watoza ushuru na wenye dhambi, vipofu, viwete, wenye ukoma na hata waliokuwa wazima wote walikuwa na nafasi katika moyo wake. Yesu alimpokea kila mmoja na hakumbagua yeyote. Anamponya kiziwi na kudhihirisha ukuu na upendo wa Mungu. Tendo hili linawavuta wengi kumfuata na kuimba sifa zake.
KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, masomo ya Dominika hii yanatupa neno la faraja na matumaini katika maisha yetu. Tunapopitia nyakati ngumu za mateso na mahangaiko, sababu yetu ya kuendelea kuwa na matumaini ni imani katika Mungu anayeokoa, Mungu asiyetuacha katika mahangaiko yetu bali huja na kutukomboa. Mungu wetu ni Baba wa upendo na mwenye kutupokea sote kama watoto wake. Je, tunapopitia magumu ni msaada gani tunaoanza kuufikiria? Pamoja na mengi tunayoweza kuyatumia kujikwamua katika mateso yetu tusimsahau Mungu. Neno la nabii Isaya katika somo la kwanza ni faraja kwetu pia. Aidha, masomo ya Dominika hii yanazungumza moja kwa moja kwetu sisi tulio wafuasi wake Kristo na yanatukumbusha wajibu tulio nao wa kuleta chachu ya mabadiliko katika maisha ya watu. Mungu ambaye amejifunua kwetu kwa njia ya Kristo Yesu, anadhihirisha uwepo wake kwa njia ya matendo yetu mema.
Tunamsadiki Mungu aliye Baba wa wote na asiyembagua yeyote. Je, sisi tulio wafuasi wa Kristo tunatafunwa na dhambi ya ubaguzi. Katika karne ya kwanza ya Ukristo, ili kuleta umoja wa waamini wote, jumuiya za kikristo zilipambana sana na shida ya ubaguzi. Baadhi, pamoja na kuamini walijiona kuwa ni bora zaidi ya wengine. Ni kwa sababu hiyo mtume Yakobo anawakemea. Lakini uhalisi wa ubaya wa jambo hili haufichiki hata katika nyakati zetu. Tunatafunwa na ubaguzi kuanzia katika familia zetu, jumuiya zetu na jamii kwa ujumla. Tunayo daima maelekeo na tabia za kuwaweka watu na kuwatendea kadiri ya makundi ambayo sisi tumeyatengeneza. Kwa macho yetu tunawaona wengine kuwa ni bora zaidi na wengine kuwa ni dhalili. Je, tunawapokea na kuwatendea vema wanaoonewa? Watu wenye njaa, wafungwa, wagonjwa, wageni, yatima, wajane na wenye kupitia madhira mbalimbali katika maisha wanapata faraja yoyote wanapokuja kwetu? Katika sehemu zetu za kazi tunawahudumiaje watu?
Ukristo wetu una maana ikiwa tunakuwa sababu ya faraja na matumaini kwa wengine. Tunapaswa kukumbuka ya kwamba sisi tumeitwa kuwa chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu (Mt 5:13-16). Ni ladha gani tunaleta katika maisha ya watu? Kwa matendo yetu tunalifukuza giza la upendeleo na ubaguzi? Yesu ametupa mfano mzuri wa kufuata. Kila alipokwenda aliyagusa maisha ya watu kwa namna chanya na akafuatwa na wengi kwa sababu walionja faraja na tumaini kwake. Sisi tulio wafuasi wake tumepewa mfano ili tutende vile alivyofanya yeye. Tuwe vyombo vya upendo wa Mungu kwa watu. Tuwe njia ya kujenga familia ya kidugu ulimwenguni kote ambako upendeleo na ubaguzi vitakaa mbali nasi. Tukumbuke ya kwamba watu wote ni mali yake Mungu na wale wanaoonewa Mungu anawapigania na kuwainua kutoka katika unyonge wao. Sisi tutafute kuwa watenda kazi pamoja na Mungu kwa kushiriki katika kuwatendea wote kwa wema kama wana wa Baba mmoja. Ninakutakia Dominika njema.