Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 23 ya Mwaka B wa Kanisa: Jipeni moyo msiogope! Shikamaneni ili kutangaza na kushuhudia: upendo, ukarimu na haki jamii! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 23 ya Mwaka B wa Kanisa: Jipeni moyo msiogope! Shikamaneni ili kutangaza na kushuhudia: upendo, ukarimu na haki jamii! 

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka B: Jipeni Moyo Msiogope: Ukarimu

Waamini tunakumbushwa wajibu wetu katika kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo sio tu kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu bali pia kufanya juhudi ya kuwasaidia waondokane na hali hiyo ya unyonge, umaskini, hofu na mashaka ili nao waweze kuishi kwa furaha na amani kuelekea mbinguni kwa Baba tukisema; “Jipeni moyo, msiogope”. Upendo

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 23 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha wajibu wetu kama wabatizwa katika kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo sio tu kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu bali pia kufanya juhudi ya kuwasaidia waondokane na hali hiyo ya unyonge, umaskini, hofu na mashaka ili nao waweze kuendelea na kusonga mbele kimaisha waishi kwa furaha na amani kuelekea mbinguni kwa Baba tukisema; “Jipeni moyo, msiogope”. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (35:4-7a); ni utabiri wa Nabii Isaya akiwa utumwani Babeli habari za kurudi kwa Waisraeli katika nchi yao ya ahadi na kwamba Mungu atawaadhibu maadui wao. Maneno ya Nabii Isaya ni mazito mno na ya faraja kubwa naye anasema; “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchem za maji.” Huko kukombolewa kwa Waisraeli toka utumwani Babeli ni mfano wa kukombolewa kwetu toka utumwa wa dhambi na shetani.

Somo la pili la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (2:1-5); latueleza ukweli kuwa mbele ya Mungu binadamu wote ni sawa wala hakuna upendeleo wowote kwake kati ya tajiri na maskini wote ni sawa. Yakobo anaonya na kukemea kuwa kusiwe na upendeleo kwa maswala ya imani kati ya waamini. Ndani ya sinagogi mtu tajiri na mwenye mavazi mazuri hana tofauti na mtu maskini, mwenye mavazi mabovu, maana mbele za Mungu wote ni sawa, wote wanamuhitaji Mungu kwa ajili ya uzima wao. Hivyo sio sahihi kumstahi aliyevaa mavazi mazuri na kumketisha manali pazuri na maskini kwa kuwa amevaa nguo zilizochanika anaambiwa asimame, au keti miguuni pa wengine. Kufanyo hivyo ni kuwa na hitilafu mioyoni, ni kuwa maamuzi yenye mawazo mabovu. Yakobo anatukumbusha kuwa Mungu huwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao. Hivyo basi tusiwapendelee matajiri kwa gharama za maskini. Kufanya hivyo ni kukosa imani na kuwa mbali na Mungu.

Injili ilivyoandikwa na Marko (7:31-37); ni simuliza la Yesu kumponya kiziwi akiwa safarini kutoka mipaka ya Tiro kupitia Sidoni kuelekea bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Katika kumponya kiziwi Yesu alifanya matendo saba; kwanza alimtenga na watu. Pili akatia vidole vyake masikioni. Tatu akatema mate. Nne akamgusa ulimi. Tano akatazama juu mbinguni kwa Mungu Baba ashirio la utimilifu wa utabiri wa nabii Isaya kuwa; “Mungu atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa” (Isaya 35: 4-7). Sita akaugua yaani akapumua kwa nguvu kwa kuguswa na matatizo na shida za mwingine na kumuonea huruma. Na saba akamwambia kiziwi; Efatha yaani funguka. Hapa tunapata chimbuko la moja ya matendo muhimu katika sakramenti ya ubatizo; tendo la mtoa huduma ya ubatizo kumgusa mpatizwa masikio na kinywa kwa kidole gumba akisema; “Bwana Yesu, aliyewafanya viziwi wasikie, na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya kikristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba.”

Matatizo ya kimaisha: uchumi mbaya, uhaba wa chakula, kukosa ajira au kazi zenye tija, manyanyaso kazini, matatizo ya kiafya, kufiwa na kubaki yatima, kubambikiziwa kesi au kutotendewa haki mahakamani, matatizo katika ndoa na katika mahusiano, kukosa watoto; haya yote yanayotutia hofu na wasiwasi. Tunahitaji sauti tunahitaji kuisikia tena sauti ya Nabii Isaya; “Jipeni moyo msiogope”. Lakini sauti tu ya jipeni moyo msiogope tu haitoshi, yahitaji ifuatane na matendo ya kusaidia kuondokana na shida na matatizo haya. Sauti ya “jipeni moyo usiogope” yapaswa kuwekwa katika matendo kuwasaidia wenye hofu na mashaka kwa moyo wa upendo na ukarimu, sio tu kwa kuwapatia misaada mbalimbali bali kuangalia mbali zaidi na kujiuliza “kwa nini tunao wahitaji katika jamii zetu, kwanini watu wana hofu na mashaka?” Sababu ni nyingi: uwepo wa mila, tamaduni, sheria na taratibu kandamizi na pendelevu ambazo ni za kiasili na za kihistoria.

Tufanye nini? Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika waraka wake wa kitume “Caritatis in Veritate” anatuasa kuwa ukarimu wetu uwe katika ukweli. Inawezekana wengine wamekuwa maskini kwa sababu sisi hatujawa wakweli katika ukarimu wetu. Tunatoa ukarimu pale usipohitajika au tunajifanya wakarimu pale tunapojua tutapata faida binafsi au tunakuwa na upendeleo katika kutoa misaada yetu. Huwezi kujifanya mkarimu kwa watoto wa “nyumba ndogo” wakati watoto wako mwenyewe wanalala njaa, hawaendi shule au wanarandaranda mitaani. Huwezi kusema u mkarimu kwa kumnunulia “nyumba ndogo” gari na kumjengea nyumba wakati mwenzio wa ndoa anahangaika peke yake na familia. Huwezi kujifanya mkarimu kwa kutunza nafasi ya kazi ya mtu ambaye hana vigezo kwasababu ni tajiri wakati mtoto wa maskini anayekujia kila siku na barua za maombi ya kazi humuajiri. Hivyo Yakobo anatuambia tusiwe na upendeleo. Wengine wamekuwa ombaomba kwa sababu haki yao imechukuliwa na walionacho zaidi. Inawezekana watu wamekuwa maskini, wanakosa huduma za kijamii kwa sababu viongozi wamekula rasilimali za umma na kujinufaisha wao wenyewe mbaya zaidi kwa kumwaga damu za waliopaswa kunufaika nazo ili wao waendelee kunufaika nazo.

Wito kwa viongozi tuwasaidie watu wetu kwa kutokomeza mila potofu, sheria na mifumo kandamizi na yenye upendeleo iliyogubikwa na rushwa ambayo kwayo wengi wananyimwa haki zao kwa manufaa ya wengine na hivyo wanaishi kwa hofu na mashaka. Wengine wameingia katika umaskini kwa sababu mila potofu na sheria kandamizi zinazowanyima uhuru na fursa za kujitegemea na kujiendeleza kimaisha. Tutende kaki kabla ya ukarimu. Hakuna ukarimu kama hakuna haki. Kama tukiwanyima watu fursa na nafasi za kujiendeleza kimaisha na hivyo tukawa sababu ya wao kuwa maskini hatuwezi kujifanya wakarimu kwao kwa kuwapatia misaada. Ndiyo maana Mtakatifu Ambrose aliwahi kusema kuwa; “Chochote unachompatia maskini kama msaada kutoka katika ziada uliyonayo sio tendo la huruma na ukarimu bali unamrudishia haki yake uliyomuibia”.   Kumbe tunaalikwa na kuaswa tuondoe utegemezi na tusijifanye sauti za wanyonge. Tuwafanye viziwi wasikie na bubu waseme. Tusijifanye kuongea kwa niaba yao, au kusikia kwa niaba yao “tuwafanye waongee, tuwafanye wasikie” kwa kuwapatia haki zao na fursa katika ajira ili wajiendeleze.

Haya yote yatawezekana kama tukiwa na viongozi wanaodhubutu kujitoa kwa moyo wote katika kweli na haki kwa ajili ya kuwatumikia na kuwahudumia watu wao. Hawa ndio viongozi wanaoweza kuwaaambia watu kwa vitendo; “Jipeni moyo msiogope”. Viongozi wenye huruma kwa watu na wenye maisha ya watu katika mioyo yao. Viongozi wanaotambua uhuru na haki kwa kila mtu. Viongozi wanaotunga sheria za haki zisizowakandamiza wanyonge. Viongozi wasio na ubinafsi wa kujali maslahi yao tu. Viongozi wasio na upendeleo wanaotoa fursa sawa kwa wote na kugawana pato la taifa kwa usawa bila kujali jinsia, ukabila, udini au uchama. Tumwombe Mungu atupatie moyo wa ukarimu, haki, na mapendo, kwa maana kutoka ndani ya mioyo yetu ndimo yanaweza kutoka mema au mabaya yategemea tumeijaza nini mioyo yetu (Marko 7: 15-23).

J 23 Mwaka
02 September 2021, 16:25