Tafuta

Kanisa linatangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kanisa linatangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. 

Imani ya Kanisa: Yesu Aliteswa, Akafa na Kufufuka Kwa Wafu!

Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro Mtume: Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Hii ndiyo imani inayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda wenye mashiko!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Marko anatuonesha kila mara Yesu yupo safarini na wanafunzi wake, ambao nao walimfuata na kuamini wapo na mtu mwenye haiba isiyokuwa ya kawaida. Marafiki wanaunganishwa sio tu na upendo bali na upendo unaokuwa ni matunda na matokeo ya kukutana, kufahamiana kwa karibu na kwa undani. Hivyo hata marafiki za Yesu wa karibu kabisa ambao ni mitume, ni matarajio yetu kuwa walipata kumfahamu kwa karibu huyu wanayemfuata, huyu wanayesafiri na kwenda naye mahali mbali mbali akifundisha na hata kutenda miujiza iliyowastaajabisha wengi. Mwinjili Marko anatuonesha kuwa hata Mitume au marafiki wa karibu kabisa wa Yesu bado walikuwa hawajamuelewa na kumfahamu vema Bwana na Mwalimu wao. Katika Injili ya Marko tangu mwanzoni anatuonesha swali ambalo walijiuliza si tu makutano bali hata kati ya wanafunzi wa Yesu: “Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” (Marko 1:27) Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, “Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?” (Marko 4:41)

Tunaweza kuona swali juu ya utambulisho wa Yesu likijirudia tena na tena, wote waliomsikiliza na kushuhudia makuu aliyoyatenda walibaki na swali juu ya utambulisho wake. Na ndio tunaona sehemu ya Injili ya leo, Yesu anakuja na swali lile lile ambalo mwanzoni walikuwa wanajiuliza makutano na hata rafiki na wafuasi wake wa karibu, yaani Mitume, makasisi na makuhani wale wa kwanza kabisa. Mtihani na swali lile, Yesu analitoa walipokuwa katika mji wa Kaisaria Filipo, mji uliokuwa unakaliwa na wapagani, ni hapo Yesu alimua kwenda pamoja na wanafunzi wake. Ni huko pia Yesu anataka kufundisha na kutenda ishara za kuonesha Umungu na ukuu wake. Ni huko pia Yesu anataka kuujenga ufalme wa Mungu. Ni huko Yesu anatoa mtihani wa kwanza kwa wanafunzi wake juu ya utambulisho wake, kuona kama kweli wamemtambua kuwa kweli ni Masiha wa Mungu, kuwa ni Mungu kati yao. Swali au mtihani wa Yesu unagusa makundi makubwa mawili, kwanza ni watu wengine au makutano; “Watu huninena mimi kuwa ni nani?”, ambalo kwa hakika ni swali rahisi kwani ni maoni na mitazamo ya watu wengine, lakini swali la pili linachangamotisha na linakuwa gumu zaidi kwani sasa anawageukia rafiki zake wa karibu, sasa anawageukiwa na kutaka kusikia kile wanachokijua wao n asio wengine kama swali la awali. “Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?”

Jibu la upande wa kwanza wa swali la Yesu juu ya mitazamo ya watu, tayari Mwinjili Marko anatuonesha mara kadhaa katika Injili yake. “Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake. Wengine walisema, Mtu huyu ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale. Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.” (Marko 6:14-16) Hivyo, tunaweza kuona tayari mtazamo wa watu na hata wa Herode juu ya Yesu kama anavyotuonesha mapema kabisa Mwinjili Marko, na ndilo jibu la swali la kwanza. Yesu anawageukia na wao, wale ambao ameambatana na kusafiri na kuishi nao maisha ya siku kwa siku, watu ambao kwa hakika tungelitegemea wawe na jibu linalokuwa sahihi zaidi. Ni mbele kidogo Yesu aliwageukia na kuwakemea kwa kushindwa hata nao kumtambua; Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa?  Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki.” (Marko 8:17-18).

Mtume Petro leo anaonesha kumtambua na kumuelewa na hivyo anajibu kwa niaba ya wengine wote; “Wewe ndiwe Kristo.” Ni ungamo la imani la kwanza la Mitume na rafiki wa karibu kabisa wa Yesu. Na hata katika Injili ya Mathayo tunaona baada ya ungamo hili, Yesu pia anasema; “Na Yesu akamwambia, Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona, kwa maana si mwanadamu aliyekufunulia hili, bali ni Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu ambalo hata nguvu za kuzimu haziwezi kulishinda.” (Matayo 16:17-18). Mwinjili Marko badala yake anazidi kutuonesha kuwa hata baada ya ungamo la imani la Petro kwa niaba ya wafuasi wengine wote, Yesu anawaonya wasimwambie mtu habari zake, wasimwambie mtu juu ya utambulisho wake kuwa ni Kristo, kuwa ni Masiha wa Mungu, ndiye mpakwa mafuta wa Mungu. Ni hapa tunajiuliza juu ya usiri wa Masiha kama tulivyoona na kutafakari mara kadhaa katika Injili ya Marko. Ni hapa tunapata jibu la kwa nini kila mara Yesu anawaonya na kuwakataza juu ya kuwashirikisha wengine juu ya utambulisho wake, juu ya Umasiha wake. Ni kweli Mtume Petro anatoa jibu linalokuwa sahihi kabisa, lakini ni jibu ambalo bado hajapata kuelewa nini maana ya Yesu kuwa Masiha, Kristo, kuwa mpakwa mafuta wa Mungu, bado Petro anawaza na kufikiri katika namna isiyokuwa sahihi, isiyoendana na mpango wa Mungu, bali ni ile inayoongozwa na mantiki ya dunia hii. Bado Petro na hata mitume wanashindwa kufika na kuelewa mantiki na mpango wa Mungu.

Na ni hapa tunaona hata baada ya kutoa jibu ambalo tungeliweza kusema ni sahihi, lakini Yesu anatumia fursa hii kuwafundisha, ndio kusema anatambua kuwa bado hawajaweza kufaulu mtihani aliouweka mbele yao. Mwalimu hana sababu ya kufanya masahihisho au kurudia tena kipindi au somo ambalo amejiridhisha pasi na mashaka kuwa wanafunzi wake wote wameelewa vema somo lile. Ndio kusema Yesu anatambua kuwa bado wanafunzi wake hajapata kulielewa vema somo lile na hivyo anaanza kuwafundisha, anaanza tena mwanzo somo ambalo tungetemea kuwa walishalielewa na kufuzu vema. Mwinjili Marko anawaandikia Injili yake waamini au Wakristo wa Kanisa la Roma, ni tangu mwanzo anawakumbusha na kuwasisitiza wapate kuelewa Kristo wanayemwamini na kumfuasa ni nani haswa, ni mwenye utambulisho upi. Kishawishi na mtazamo potofu anaokuwa nao Petro na hata wale mitume wengine, ni hatari inayoweza kuwepo hata kati yetu leo. Yesu anatambua kuwa bado wanafunzi wake hawajaelewa sababu hasa za kumfuasa Yeye, za kuacha nyumba, familia na hata kazi na mali zao ili waweze kumfuasa. Fundisho la Yesu leo si tu lilikuwa gumu kwa wasikilizaji wake wa nyakati zile bali hata nasi kwetu leo; “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Ni hapa Yesu anawafunulia kwa mara nyingine juu ya utume wake, juu ya kazi inayoakisiwa na ukweli kuwa ni Masihi, kuwa ni Kristo ni katika mateso, kifo na ufufuko.

Hakika halikuwa fundisho rahisi lenye kueleweka kirahisi na ndio tunaona Petro kwa niaba ya wengine na hata nasi leo, kwa Petro bado aliongozwa na mantiki ya mafanikio, ya ushindi, ya kutokukubali kirahisi kushindwa, ni mantiki na falsafa ya dunia hii. Kwake kilele cha mafanikio hakipo katika mateso na kifo bali katika kupambana kwa kufa na kupona, ni kuona mafanikio kadiri ya mtazamo wa dunia hii. “Nenda nyuma yangu, shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” Nini maana ya maneno haya ambayo kwa kweli yanaonekana kuwa ni makali kabisa kutoka kwa Yesu. Ndio kusema Yesu anamkumbusha Petro kutambua kwanza nafasi yake mintarafu mahusiano yake na Masiha. Petro amefanya kosa la kutangulia mbele, kuchukua nafasi ambayo si yake, nafasi ya mbele ni ya Kristo mwenyewe. Lakini pia anamuita “shetani”, na hapa ni vema tukaelewa wazi kwani Mwinjili Marko anatuonesha mara moja kwa nini aliitwa jina lile, ni kwa kuwa alikuwa haendani kadiri ya mipango ya Mungu, kwani anakuwa kinyume na Mungu. Na hata nasi tunapokuwa kinyume na mpango wa Mungu hapo tunapingana na Mungu, hapo tunakuwa mbali na Mungu, hapo tunayaangamiza maisha yetu. Neno shetani kwa Kigiriki ni “diaballein”, likiwa na maana sisisi ya muharibifu, anayegawanya au kufarakanisha, muongo na msingiziaji. Shetani ni yule anayekuwa mbali na kweli, ambao ni Mungu mwenyewe, anayeharibu maisha yetu na kutuweka mbali na upendo na urafiki na Mungu.

“Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake…” Mwinjili Marko anatuonesha kuwa fundisho lile halikuwa kwa ajili ya mitume peke yao na ndio maana anatuonesha kuwa pia Yesu alinena na mkutano, ndio kusema ni fundisho kwa jumuiya nzima ya Kanisa, ni fundisho kwa kila mbatizwa wa nyakati na mahali na zama zote. Ni hapa Yesu anatufundisha na kutuonesha nini maana ya kuwa mfuasi wake, gharama ya kuwa mfuasi wa Kristo. Ni gharama sio ya mitume peke yao bali yak ila mbatizwa, na ndio kiini na maana ya ufuasi wetu. “Mtu yeyote akitaka kunifuata na AJIKANE mwenyewe, AJITWIKE na MSALABA wake, anifuate.” Ni mwaliko kwa kila mmoja, lakini ni mwaliko wenye madai, ni mwaliko wenye gharama kwetu. Kujikana mwenyewe, ndio kusema kuachana na umimi, kujifikiria mimi, ni kuanza kuongozwa sio tena na mantiki ya dunia au ulimwengu huu bali ile ya Mungu mwenyewe. Mfuasi wa kweli ni yule anayempenda kwanza Mungu na jirani bila masharti, bila kujitafuta wala kuangalia manufaa yake binafsi.

Ajitwike Msalaba wake, labda hapa pia tunaweza kubaki na maswali kwani lengo la maisha ya ufuasi au ya Kikristo sio mateso kwa hakika bali upendo. Msalaba ulikuwa ni hukumu ya watumwa, watu wasiokuwa wenye utaifa wa Kirumi. Hivyo kujitwika msalaba ni mwaliko wa kukubali kuwa na hadhi ya watumwa, kukubali kujivua utukufu na heshima na kuona maisha yetu yanapata maana tu kwa kuwa wadogo na tayari kuwatumikia wengine kama ambavyo Kristo Yesu alivyojishusha na kuwa mtumishi wetu. (Wafilipi 2:7-8). Msalaba ni ishara ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Mungu ambaye amekuwa wa kwanza kutupenda, ameshuka na kuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu aliye mdhambi na mkosefu. Unifuate, ndio kusema kushiriki misheni ile ya Kristo, ni kukubali kuongozwa sio tena na mantiki au falsafa za dunia hii bali na ile ya Injili, ile ya Neno la Mungu mwenyewe, yaani, Logos. Mwinjili Marko leo anatuonesha sifa za mfuasi wa kweli wa Bwana wetu Yesu Kristo ni yule anayeshiriki kikamilifu njia ile ile ya Kristo mwenyewe. Njia ya kuwa mdogo na hivyo mtumwa, njia ya kukubali kuwa mtumishi kwa wengine, na ndio njia ya upendo kwa Mungu na kwa jirani. Sisi ni Wakristo kwa kuwa tunakubali kuongozwa na mantiki ya Kristo mwenyewe. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

08 September 2021, 08:50