Askofu Lazarus Vitalis Msimbe Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania: Atoa Daeaja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 19 kutoka katika Mashirika ya Kitawa 5, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania: Atoa Daeaja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 19 kutoka katika Mashirika ya Kitawa 5, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro. 

Majandokasisi 19 Kwa Mkupuo Wapewa Daraja ya Ushemasi wa Mpito Morogoro!

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S wa Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania kwa mara ya kwanza tangu awekwe wakfu kama Askofu Jimbo ametoa Daraja takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 19 kutoka katika Mashirika matano yanayosomesha wanafunzi wao kwenye Chuo Kikuu Kishiriki cha Yordan, Jimbo Katoliki la Morogoro. Shemasi ni mhudumu wa Neno na shuhuda wa Huduma!

Na Angela Kibwana, - Morogoro, Tanzania.

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza na kuhubiri Injili; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa niaba ya Kanisa! Mashemasi wapya wanakumbushwa kwamba, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo, wameandaliwa vyema: kiutu, kiakili, kiroho na kichungaji ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika maisha ya watu wanaowazunguka.

Mashemasi wapya watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hivi karibuni, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S wa Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania kwa mara ya kwanza tangu awekwe wakfu kama Askofu Jimbo ametoa Daraja takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 19 kutoka katika Mashirika matano yanayosomesha wanafunzi wao kwenye Chuo Kikuu Kishiriki cha Yordan, Jimbo Katoliki la Morogoro. Amewataka kwa namna ya pekee, Mashemasi wapya kutangaza na kuhubiri Injili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko na wala si kwa nguvu ya hoja. Watambue kwamba, wanapaswa kuwashirikisha wengine Habari Njema ya Wokovu, ili hatimaye hata wao waweze kuokoka!

Maktaba zimejaa vitabu vingi vya falsafa na taalimungu! Kumbe si maandishi tu yanayoweza kumwongoa mtu, bali ushuhuda wa wema, matendo adili na manyoofu. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe amewashukuru na kuwapongeza wakuu wa mashirika na walezi mbalimbali waliochangia hadi Mashemasi wapya kufikia hatua hii. Amewataka Mashemasi wawe ni watu wa: Sala, waendelee kuboresha maisha yao kwa tafakari makini ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mashemasi wapya wamemshukuru Askofu Lazarus Vitalis Msimbe na kumwahidi kwamba, watajitahidi kumfahamu Mungu si kwa hoja bali kwa imani timilifu!

Ushemasi Morogoro
29 October 2021, 17:26