Watakatifu ni rafiki wa Mungu na jirani zetu! Watakatifu ni rafiki wa Mungu na jirani zetu! 

Sherehe ya Watakatifu Wote! Watakatifu ni Rafiki wa Mungu na Jirani Zetu!

Utakatifu sio baada ya kifo bali ni leo yetu tungali bado duniani, katika familia yangu, mahali pangu pakazi na watu wanaonizunguka hawana budi kuambukizwa na harufu nzuri ya maisha yangu ya utakatifu. Utakatifu lazima uonekane katika maisha yetu kwa kukubali kweli kuongozwa na katiba ya maisha ya heri, yaani na Neno la Mungu. Utakatifu ni wito kwa wote na wala si wachache!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! “Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, hao ndio wanatoka katika dhiki iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo”. Ni maneno tunayoyasikia leo kutoka katika somo letu la kwanza kutoka Kitabu cha Ufunuo. Ni Kitabu kigumu kukielewa kwani inayotumika sana ni lugha ya picha, hivyo ili kupata ujumbe wake ni lazima kuelewa muktadha wa Kitabu. Tunapoangalia maisha yetu ya siku kwa siku, tunajiuliza kwa nini mwanadamu anasongwa na dhiki, huzuni, majonzi, mateso, madhulumu, ukosefu wa haki na kila aina ya uovu? Na uovu huu hauwakuti tu wale wanaokuwa mbali na Mungu bali hata na waaminio na rafiki wakubwa wa Mungu. Sura nne za Kitabu cha Ufunuo zinajaribu kuelezea ukweli huu unaosumbua sana mwanadamu (Ufunuo 5-8). Ndio sura zinazozungumzia ile mihuri saba. Bwana akiwa katika kile kiti cha enzi, mkononi mwake akiwa na kitabu cha historia kilichobeba majibu ya maswali haya ya msingi juu ya kwa nini dhiki, mateso na madhulumu kwa mwanadamu. Bahati mbaya sana kitabu kile kimefungwa na mihuri ile saba, na hakuna hata mmoja kati ya wale viumbe mwenye uwezo wa kukifungua kitabu hicho.  Na hata malaika wa Bwana anatangaza kwa sauti kuu; “Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?” (Ufunuo 5: 2)

Mwandishi wa Kitabu hiki ambaye ndiye aliyepata maono yale, analia na kuomboleza ili apate kujua siri zilizomo katika kitabu kile. “Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu” (Ufunuo 5:5) Ni Mwanakondoo yule aliyetolewa sadaka anavunja mihuri ile mmoja baada ya mwingine. Sehemu ya somo letu la kwanza la leo ni masimulizi ya kile kilichojiri baada ya kuvunjwa kwa ule mhuri wa sita. Malaika wanne waliowekwa ili kuilinda nchi na bahari waliwekwa katika pande kuu nne za dunia, ndio kusema Mungu anayeulinda ulimwengu mzima. Malaika mwenye muhuri wa Mungu Mwenyezi mikononi mwake akipanda kutoka maawio ya jua, ndio kusema kutoka upande wa Mashariki ya dunia. Ni Malaika anayetoa amri kuwa wasiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata watakapokwisha kuwatia mihuri watumwa wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao. Idadi ya wale waliotiwa mhuri ni watu mia na arobaini na nne elfu.  Ndio hesabu ya 12 x 12 x 1000. Katika Maandiko Matakatifu na hasa katika Vitabu vya Kiapokalipsia, ndio Vitabu vya Kiufunuo, idadi au namba daima zinabeba maana. Ni namba kamili, na si kweli kama wengine wanaopenda kusema ndio idadi ya watakatifu wote wa Mungu waliopo mbinguni. Ni namba inayoashiria si tu wale watakatifu waliopo mbinguni baada ya kumaliza safari yao hapa duniani, bali kwa kila mtakatifu wa Mungu hata wale wanaoishi waliopokea muhuri wa Mungu kwa sakramenti ile ya Ubatizo, kwani kwayo tunafanyika kuwa wana wa Mungu, tunapokea uzima kwani ni sakramenti inayotuunganisha na Mungu katika utakatifu, ni sakramenti inayotufanya kuwa watakatifu kwa kupokea neema ile ya utakatifu wa Mungu mwenyewe.

Kitabu cha Ufunuo kinatueleza kuwa hata hawa wanaopokea muhuri bado nao hawapokei upendeleo wa kutopitia dhiki ile, na madhulumu yale. Na wao wanasafiri katika dhiki na madhulumu ya kila aina sawa na wale wengine wasiopokea bado muhuri wa Mungu Mwenyezi.  Hawa waliopokea muhuri wapo huru wanapokea uhuru kutoka nguvu za yule muovu, kwani sasa wao wanakuwa ni watu wa miliki ya Mungu. Ni kwa muhuri wanatambulika sasa kuwa wao ni mali yake Mungu, ni wana wake Mungu, wanaingia hadhi mpya kwa kujiweka mikononi mwa Mungu. Hivyo wao ni watu huru kutoka utawala wake yule muovu. Hawa waliopokea muhuri sasa wanaangalia dhiki, madhulumu na mateso ya kila aina kwa jicho tofauti kabisa na wale wasiokuwa na muhuri wa Mungu. Hawa ni watu wapya na hivyo wanaangalia maisha kwa jicho jipya, wanaongozwa sio tena na mantiki ya dunia hii bali ile ya mbinguni. Ni wale wanaokuwa tayari kubadili vichwa vyao, wanaruhusu Mungu mwenyewe aongoze maisha yao. Kwao kuishi ni katika kuangalia yote kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Ni wazi wanateseka kama wengine iwe ni dhiki, mateso, madhulumu na mambo kama hayo, lakini wanabaki imara. Maradhi au magonjwa, maumivu, usaliti, madhulumu, kifo, na yote mabaya kwao hayana neno la mwisho kwani wana imani na matumaini katika maisha baada ya maisha ya hapa duniani, wana imani katika maisha ya umilele pamoja na Mungu.

Ni kwa ishara ya Mwanakondoo yule aliyetolewa sadaka, nao wanaona thamani katika mateso, dhiki, madhulumu na hata kifo ikibidi ikiwa ni katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Mwanakondoo anatolea maisha yake kwa kuwa anampenda mwanadamu, anamwaga damu yake ili kumkomboa mwanadamu. Mwandishi wa Kitabu cha Ufunuo hata baada ya kuona idadi hiyo ambayo tumejaribu kueleza hapo juu bado anaona tena; “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, , na mbele za Mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao…” Ndio kusema utakatifu sio mali ya watu wa mila au tamaduni au dini fulani tu, bali ni wito kwa kila mwanadamu, sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tunaitwa kuishi katika mahusiano na Mungu wetu, kila mmoja wetu bila kujali tofauti tunazoweza kuwa nazo. Kila mwanadamu anabeba sura na mfano wa Mungu na hivyo tunaalikwa sote kufanana na Mungu kwa maisha yetu, kuwa kweli wana wa Mungu, na rafiki zake katika maisha yetu. Vazi jeupe ni ishara ya cheo na hali yao mpya, ishara ya furaha na maisha mapya ya ukamilifu ndio utakatifu, maisha bila madoa ya dhambi, maisha ya urafiki na Mungu. Matawi ya mitende ndio ishara ya ushindi baada ya kubaki waaminifu kwa Kristo. Na mihuri katika mapaji ya nyuso zao, ndio ishara ya kuwa mali yake Mungu, wamejitoa kikamilifu kubaki wana wa Mungu katika maisha yao.

Hii ndio ile jumuiya ya watakatifu baada ya kumaliza safari ile ya dhiki na madhulumu, ni jumuiya ya Kanisa la washindi kule mbinguni.  Kama Mwanakondoo nao wamekuwa tayari kutolea maisha yao kwa upendo kwa Mungu na jirani. Katika macho ya wanadamu hapa duniani walionekana kuwa wameshindwa ila Mungu anawavalisha taji la ushindi kwa kuwakaribisha kumuona jinsi alivyo, kuishi furaha ya umilele pamoja na Mungu na malaika wake na watakatifu wake wote. Ufunuo huu si tu kwa ajili ya Wakristo wa mwisho wa karne ile ya kwanza baada ya kuwa walipitia dhiki na madhulumu makubwa, lakini pia ni ujumbe hata katika nyakati na siku zetu za leo. Leo kuishi imani yetu kiaminifu lazima kuwa tayari kupitia kila aina ya dhiki na madhulumu labda ya aina nyingine, lakini somo letu la leo linatupa faraja kwa kila mmoja wetu anayetamani kwa dhati kuwa mtakatifu, hatuwi watakatifu baada ya kifo, la hasha bali lazima tuishi urafiki na muunganiko na Mungu katika maisha yetu tukiwa tungali bado hapa duniani. Utakatifu ni kuishi maisha ya ujasiri katika fadhila, na fadhila kuu ndio ile ya kumpenda Mungu na jirani.

Somo la Injili ya leo, Mwinjili Mathayo anamwonesha Yesu akitoa hotuba yake ya kwanza mlimani. Mlimani katika lugha ya Kibiblia ni mahali ambapo mbingu inakutana na nchi, ni mahali pakukutana na Mungu, anapojifunua na kujidhihirisha kwetu. Na ndio tunaona hata Abrahamu, Musa na Eliya wanafanya mageuzi makubwa ya maisha yao ya kiroho katika milima, Moria, Horebu na Karmelo. Mwinjili Matayo leo anatuonesha Yesu akifanya hotuba yake ya kwanza kwa makutano akiwa mlimani. Hivyo, mlima katika Maandiko Matakatifu sio tu mahali pa juu Kijiografia, bali ina maana ya Kitaalimungu ni mahali pakukutana na Mungu. Pamoja na hayo yafaa tangu mwanzo kutambua kuwa Mwinji Mathayo hamaanishi hasa mlima kwa maana ya sehemu kijiografia, bali zaidi sana tupate ujumbe na maana yake kitaalimungu. Zaidi ya maana ya kijiografia, mlimani katika Maandiko Matakatifu inamaanisha hasa muda au nafasi ile ya kukutana na Mungu na hasa kulipokea Neno na mapenzi yake. Na ndio tunaweza kusema saa ya mlimani ni saa ile muhimu kabisa katika safari yetu ya kumfuasa Kristo, ndio saa ya kukutana na Mungu na kubadili maisha yetu kwa kuanza kuishi maisha mapya, maisha ya urafiki na Mungu, maisha ya kuongozwa sio na vichwa vyetu bali na mantiki ya Neno la Mungu.

Yesu anatoka sehemu ya tambarare anapanda mlimani, ni sawa na kusema kujitenga na malimwengu, ni kujitenga na mantiki za dunia hii na anawaongoza wanafunzi wake na makutano kupanda mlimani, kuanza maisha mapya, maisha ya kukubali sasa kuongozwa na mantiki ya mbinguni.  Kupanda mlimani ni kukubali kuongozwa sio kwa jicho na mitazamo ya kidunia bali ile ya Mungu mwenyewe. Ni kukubali kubadili vichwa, katika dunia hii nini chenye thamani na bora kabisa ni afya njema, familia nzuri, mafanikio kielimu, kiuchumi na hata kijamii, akaunti ya pesa iliyonona, marafiki na wajuani na kadhalika na kadhalika. Labda leo tunaposherehekea sikukuu ya watakatifu wote, ni vema kujiuliza; ni mara ngapi mimi nimetamani kwa dhati kuwa mtakatifu, utakatifu sio kuogopa moto wa milele baada ya kifo, narudia tunakuwa watakatifu sio baada ya kifo, la hasha, bali wakati tungali hapa duniani. Utakatifu sio baada ya kifo bali ni leo yetu tungali bado duniani, katika familia yangu, mahali pangu pakazi na watu wanaonizunguka hawana budi kuambukizwa na harufu nzuri ya maisha yangu ya utakatifu. Utakatifu lazima uonekane katika maisha yetu kwa kukubali kweli kuongozwa na katiba ya maisha ya heri, yaani na Neno la Mungu.

Mama Kanisa anawatangaza Wenyeheri na hata Watakatifu wale watoto wake waliojitahidi wangali hapa duniani kuishi maisha ya Heri zile nane anazotufundisha leo Yesu. Hivyo kama nasi tunatamani kwa dhati ya moyoni kuwa watakatifu hatuna budi kukubali kuziishi heri hizi za mlimani. “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao” Ni moja kati ya heri ambayo lazima nikiri tunaipa mara nyingi tafsiri potofu kabisa. Mwinjili Matayo anaiweka heri walio maskini wa roho, tofauti na Mwinjili Luka anayesema heri maskini. (Luka 6:20) Wapo wanaodhani umaskini unaozungumziwa hapa ni wa mali, au vitu au elimu na mambo ya namna hiyo ya kuishi katika ufukara wa kupindukia, na kama ndivyo labda tujitahidi tuwe maskini na mafukara ili tuupate ufalme wa mbinguni. Hiyo ni tafsiri hasi na inayopotosha, kwani tunasoma katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 4:34-35 “Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake”. Ni kuuvaa utu mpya, nao ndio ule wa kumuona mwingine ni kaka na dada yangu, ndio kushiriki maisha ya Kristo Mfufuka, Kristo anayejitoa mwenyewe kuwa zawadi kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Kristo hatoi pesa wala mali bali anatualika katika kila adhimisho la Misa Takatifu anaposema twaeni Mwili wangu mle wote, twaeni Damu yangu mnywe nyote, ndio huo wito ambao nasi tunaalikwa kuuishi katika maisha yetu kama wafuasi wake Kristo Mfufuka.

Tunasoma katika sura ile ya nne ya Kitabu cha Matendo ya Mitume, Anania na Safia mke wake wanaoshindwa kuwa wakarimu kwa kuwashirikisha wengine mali zao, ni kishawishi hata nyakati zetu. Ni mara ngapi nimekuwa mnyimi na mchoyo katika kuwashirikisha wengine mema niliyojaliwa na Mungu? Leo tunaishi katika nyakati sio za kuelewa ukweli huu walioushi wakristo wale wa Kanisa la mwanzo. Baba Mtakatifu Fransisko anatuonya kwani tunaishi ulimwengu wa udikteta wa teknolojia, ndio ulimwengu wa kununua na kutumia, ndio ulimwengu wa kuwa na kila toleo jipya iwe ni vifaa vya kieletroniki kama simu na kompyuta, magari, nyumba, nguo, mavazi, viatu na kadhalika na kadhalika. Ulimwengu sio wa kujitoa sisi wenyewe kama zawadi bali kuweza kutumia vingi na vizuri iwezekanavyo kwa manufaa yetu binafsi. Tunaishi ulimwengu wa ponda raha kwani kifo kinakuja! Wapo pia wanaosema maskini wa roho ni wale ambao pamoja na kumiliki mali au vitu, lakini hawajaruhusu kuwa watumwa wa mali au vitu kwa kujishikamanisha navyo, bali wanaojua kutumia mali zao kwa upendo na wale wasiojaliwa mengi. Mantiki ya ulimwengu huu ndio ile ya kushindwa kupanda juu mlimani na kufuata ile ya Mungu, kwa kuona haki ni kila mmoja kubaki na iliyo yake. Ni kushindwa kutambua kuwa yote niliyo nayo si mali yangu, mimi ni mlinzi tu, ni wakili tu kwani vyote ni mali ya Mungu. Zaburi 24:1 “Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi Mungu; ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake”

Ni mantiki hii ya kusahau kuwa sisi sio wamiliki bali ni waangalizi tu wa mali ya Mungu tunajikuta tunaishia katika vishawishi vya kujilimbikizia, kumiliki kwa gharama zozote zile, na ndio tunaona tunaishi katika ulimwengu wa vita, mapambano, husuda, wizi, ufisadi, rushwa, wivu na kadhalika na kadhalika. “Kwa maana kupenda sana pesa ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi” 1Timotheo 6:10 Mfano wa mwaliko wa harusini ndio unaoeleza vema kuwa sisi sote ni waalikwa tu kwenye harusi ya mwana wa mfalme, hakuna hata mmoja wetu ndiye mwenye harusi, bali sisi sote kama anavyotukumbusha Baba Mtakatifu Francisko kuwa sisi sote ni ndugu, ni kaka na dada. Kila mmoja wetu anaalikwa kushiriki na wengine furaha ya ile karamu ya harusi, tunaalikwa kushiriki bila malipo wala gharama, ndio neema ya Mungu kwetu, ni neema inayotutaka sisi kuwa tayari kushiriki karamu ile kwa kuvaa vazi la harusi, kwa kukubali kuongozwa na mantiki ya Neno la Mungu na kamwe sio na mantiki zetu za dunia hii. Tunakosa vazi la harusi kila mara tunaposhindwa kubadili vichwa, kukataa makusudi kuisikiliza na kuifuata mantiki ya Mungu mwenyewe, tunayoipata kwa kuliishi Neno lake.

Kila anayetamani kuwa mtakatifu basi hana budi kufuata mantiki hii mpya ya Kristo mwenyewe; “Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho” Luka 14:33 Sio kwamba Yesu leo anatutaka tuwe maskini hohehahe, la hasha, bali anaongeza heri walio maskini wa roho. Ndio wale wanaokuwa na roho huru bila kujishimakanisha na mali au vitu na hivyo kutumia yale yote wanayokuwa nayo kadiri ya mpango wa Mungu, wakitambua kuwa mali na vitu vyote ni vya Mungu na wao wamewekwa kuwa waangalizi wa mali hizo na hivyo hawana budi kutumia yote katika kuudhihirisha upendo wao kwa Mungu na jirani. Maskini sio yule asiyekuwa na kitu bali ni yule asiyeweka moyo au roho yake kutawaliwa na vitu, kuwa mtumwa wa mali au vitu. Bali anayejua kutumia mali zake kwa ukarimu na kamwe sio kwa kuongozwa na roho ya uchoyo au ubinafsi, anayekuwa huru na ile roho ya bwana makusanya, mtu anayetaka kila kitu kiwe chake na kwa ajili yake tu kana kwamba hakuna mwingine anayekuwa muhitaji pembeni yake. Na ndipo tunaona mmoja anaweza kuwa maskini hohehahe kabisa lakini anakosa kuwa maskini wa roho. Hivyo sifa ya kuwa maskini wa roho haitegemei wingi au uchache wa mali au vitu ninavyo miliki. Wapo matajiri wakubwa kabisa na kwao tunaonja umaskini wa roho, kama vile wapo pia maskini wakubwa na kwao hatuoni ile roho ya umaskini kwa kuruhusu kutawaliwa na ubinafsi na umimi na uchoyo.

Heri wenye huzuni. Huzuni hii sio ile ya kawaida kwa mfano mtu aliyepoteza mali zake au kuibiwa au kufiwa. Ni huzuni kwa kuona ulimwengu unaenda kinyume na mpango wa Mungu, wa kufanya ulimwengu mpya wenye kuishi kadiri ya Injili, Upendo kwa Mungu na jirani. Ni jukumu letu kuufanya ulimwengu mpya, nibaki mwenye huzuni kwa vile ulimwengu unakwenda kinyume na kweli za Injili. Heri wapole. Hata hapa upole anaozungumzia Yesu Kristo, sio ule wa kusema mimi sifanyi kitu kwa vile sitaki kuumiza au kuwaudhi wengine, hivyo kubaki bila kufanya kitu katika kuunda ulimwengu mpya. Mpole ni yule anayefanya kitu kuujenga ulimwengu mpya ila kwa hekima na busara kama Kristo mwingine. Ni yule anayeishi kwa kutenda ila kwa namna na jinsi ya Kristo anayetualika kujifunza kwake aliye mpole na mnyenyekevu. Heri wenye njaa na kiu ya haki. Haki anayozungumzikia Yesu Kristo ni ile ya Kimungu, yaani wanadamu wote kuishi kama ndugu na kusameheana, na kamwe asionekana mtu kuwa yeye ndio mmiliki wa ulimwengu, bali sote ni wana wa Mungu na ametukabidhi ulimwengu tuishi kindugu na kwa kumsikiliza Yeye pekee.Heri wenye rehema. Ni hao wasiofunga macho kwa ndugu anayeteseka, badala yake kutaka kufanana na Mungu mwenye huruma na rehema. Heri wenye moyo safi, ndio hao wenye kuweka imani yao kwa Mungu pekee na kamwe wanabaki bila kugawanyika katika maisha yao.

Heri wapatanishi, ni hao wenye kufanya kila wawezalo kujenga ulimwengu mpya wenye amani ya kweli kwa kila mwanadamu. Heri wenye kuudhiwa, kila atayepokea kweli za Injili na hasa maisha ya heri kwa hakika atapingana na mtazamo wa ulimwengu wa zamani. Ila kwa ufupi wapendwa sisi tunaalikwa na Kristo mwenyewe kuziishi heri hizi katika maisha yetu ila nasi tuweze kupata heri ya kweli, yaani kuwa kati ya wateule wake Mwenyezi Mungu. Ni mwaliko wa kuishi upendo wa Kimungu katika maisha yetu ya siku kwa siku, na huo ndio utakatifu, kujaribu kuishi kweli hizi. Ni vema kutokukata tamaa kwani watakatifu sio wale wasio na dhambi au kuanguka katika maisha yao, bali ni wale waliojaribu kila siku kusimama baada ya kuanguka na kumwelekea Mwenyezi Mungu. Utakatifu ni mwito na mwaliko wa kumwelekea Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yetu, ni mwaliko wa kusimama kila tuangukapo kwa kuwa tunampenda Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko anatualika pia kwa maneno haya; Mwenyezi Mungu hachoki kamwe kutusamehe bali ni sisi tunachoka kumrudia Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha. Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, tuitwe wana wa Mungu na ndio watakatifu. Sisi ni wana wa Mungu, watu wa Taifa lake, wateule, watakatifu wake. Tuzidi kumwomba neema na baraka zake ili tuzidi kufananisha maisha yetu na maisha ya Mungu kwa utakatifu na wema. Sherehe njema ya Watakatifu wote.

28 October 2021, 15:21