Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27 Mwaka B: Injili ya Ndoa na Familia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu taasisi inayounda familia yaani ndoa takatifu kati ya Bwana na Bibi kadiri ya mpango wa Mungu. Tunaalikwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbalimbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Waamini wanaalikwa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo ya huruma kwa sababu Kristo Yesu ni chemchemi ya upendo wa ukweli unaowaunganisha wanadamu na Muumba wao!
Katika tafakari hii, ningependa kujielekeza zaidi kuhusu asili ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu na talaka ambayo ni changamoto pevu katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. “Agano la Ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti.” Ndoa ni kielelezo cha mapendo ya Mungu kwa mwanadamu yanayokazia umoja usiovunjika kama ilivyokuwa tangu asili yake kama tunavyosikia katika Injili toka mwanzo hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja. Rej. Mwa 2: 23 na KKK 1602 – 1605. Katika Injili Kristo Yesu anafundisha maana ya asili ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu. Ruhusa iliyotolewa na Musa ya kumwacha mke ilikuwa ni kibali kilichosababishwa na ugumu wa moyo. Kimsingi umoja wa ndoa ya mume na mke hauvunjiki. Rej. Mt 19:6. Kumbe, tunaweza kusema Talaka ambayo kwa sasa ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo ni matokeo ya dhambi.
Mila na desturi nyingi katika Agano la Kale zilitawaliwa na mfumo dume. Lakini leo hii, mambo yamebadilika sana kwa watu kujikita katika masuala ya haki na wajibu. Haya ni mambo yanayowafanya wanandoa kujitahidi kujenga ndoa ya kweli inayowaunganisha ili waweze kuwa mwili mmoja. Ili kuondokana na talaka za maneno, mawazo na matendo, kwanza kabisa kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusikilizana, kusamehe na kusahau, ili kudumisha uvumilivu na udumifu. Familia zinahamasishwa kuwa ni nyumba ya sala, msamaha, sadaka, furaha na ushiriki mkamilifu katika maisha ya kifamilia. Msamaha wa dhati unajenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya Mungu na wanandoa wenyewe. Unarejesha amani,utulivu wa ndani, ufanisi na upendo wa dhati. Msamaha wa kweli unawakumbusha wanandoa kwamba, wao ni binadamu wenye hisia na vionjo tofauti. Msamaha ni neema kutoka kwa Mungu. Wanandoa daima wasukumwe na ukarimu wa Kikristo, watafute wema, ustawi na mafao ya familia nzima!
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wanasema, wakati wanandoa wanapopatwa na matatizo katika mahusiano yao, lazima waweze kutegemea msaada na ufuatiliaji wa Kanisa. Sera na mikakati ya uchungaji wa mapendo na huruma, vinaelekea kurekebisha watu na mahusiano. Mang’amuzi huonesha kwamba, kwa msaada ufaao na kwa kitendo cha upatanisho, kwa neema, asilimia nyingi za migogoro ya kindoa zinapita kwa namna inayoridhisha. Kujua kusamehe na kujisikia kusamehewa ni mang’amuzi ya msingi katika maisha ya kifamilia. Msamaha kati ya wanandoa huwezesha kung’amua upendo ambao ni wa daima wala haupiti kamwe (Rej. 1Kor 13:8). Mara nyingine lakini, huonekana kuwa vigumu, kwa yule aliyepokea msamaha wa Mungu, kutoa msamaha wa kweli unaompa tena binadamu furaha na nguvu ya kuishi.
Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yananogeshwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Malengo makuu ni: kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka ili kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki, amani na ukarimu. Itakumbukwa kwamba, Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, uhai na upendo kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu.
Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana. Kanisa halina budi kukazia malezi na majiundo ya awali na endelevu kwa wanandoa ili hatimaye, waweze kuwa ni kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wanandoa wajibidiishe kujenga utamaduni wa kusikilizana kwa dhati, kuheshimiana na kuthaminiana katika safari ya maisha yao! Ninawatakia Dominika Njema, yenye amani, upendo na mshikamano wa dhati!