Tafakari ya Neno la Mungu: Kristo Yesu Ni Masiha na Kuhani Mkuu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Ningependa kujielekeza zaidi kwa Kristo Yesu ambaye ni Kuhani Mkuu! Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu! Mwaliko kwetu sisi waamini kumlilia Kristo Yesu kama alivyofanya Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo, ili aweze kutuponya na upofu wa imani, kwa pamoja tuweze kutembea katika umoja; ili tuweze kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu adili na matakatifu! Ujio wa Masiha wa Bwana ni ufunuo wa uwepo angavu na endelevu wa huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya dhambi na udhaifu wa binadamu kama tunavyosoma kutoka katika Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Yeremia 31:7-9.
Kuhani alikuwa ni mpatanishi kati ya Mungu na binadamu. Kristo Yesu ni ukamilifu wote wa Kikuhani. Utume wa kimisionari ndilo wazo ambalo Mama Kanisa anapenda tulivalie njuga katika tafakari ya Jumapili 30 ya Mwaka wa Kanisa. Uponyaji ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu mwenye rehema. “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu...” Ebr. 4: 1-4.
Mapadre ndio Makuhani wa Agano Jipya wanaopaswa kuonesha mshikamano wa utu wa kibinadamu na heshima kwa watu wa Mungu, hususan maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii. Padre ni kiongozi anapaswa kuonesha upole na unyenyekevu. Atambue kwamba, ameitwa na kuteuliwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi Makuhani wapo kwa ajili ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Padre ni chombo makini cha kuinjilisha, kutakatifuza na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni huduma inayotekelezwa Altareni kwa kuadhimisha Mafumbo la Kanisa na hivyo kunogesha mchakato wa ushiriki wa waamini katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kama mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu unavyokazia. Unabii, Sakramenti na Utume; ni kielelezo cha maisha ya Kristo Yesu kama yanavyofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, ili kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni chemchemi ya Sakramenti zote za Kanisa. Mapadre kama Makuhani wa Agano Jipya wanawajalia waamini karama za Roho Mtakatifu na maisha mapya ya kiroho. Rej. Yn 6:63.
Kwa ufupi, Padre ni mtu kamili aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo yanayomhusu Mungu, akijitahidi kufungua hazina ya moyo wake, ili kuonesha huruma kwa ulimwengu na magumu yanayowasonga watu wa Mungu katika maisha yao. Ni mtu ambaye anapaswa kuwa ni mwaminifu na mtiifu kwa amri na maagizo ya Mungu. Fadhila ya utii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia inaonekana kana kwamba, imepitwa na wakati. Padre, anapaswa kujitoa kwa Mungu bila ya kujibakiza. Kristo Yesu anaoneshwa kama Masiha aliyetegemewa na Waisraeli, tangu Agano la Kale na akawa ni chemchemi ukombozi wa mwanadamu katika Agano Jipya na la Milele. Yesu anatimiza utabiri wa kinabii, uliotolewa katika Agano la Kale, lakini mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anamuunganisha Kristo Yesu kama Mfalme, Mwana wa Mungu na Kuhani mkuu kwa mfano wa Melkisedeki. Kutokana na mwelekeo huu, Upadre unakuwa ni daraja linalomuunganisha mwanadamu na Mwenyezi Mungu, katika kazi ya uumbaji na ukombozi ili hatimaye, kuuona mwanga na maisha ya kweli.
Injili kama ilivyoandikwa na Marko: 10: 46-52. Marehemu Abate Alcuin Nyirenda, OSB., aliwahi kusema, “Timayo” kwa lugha ya Kiebrania lina maana mbili: Mosi, ni heshima, hadhi, ukuu, kufanikiwa na kuthaminiwa katika maisha ya ulimwengu huu. Kwa hiyo Mwana wa Timayo au Bartimayo ni mtu anayefanana na baba yake katika heshima, yaani mwana au mtoto wa yule anayetafuta heshima, hasahasa heshima katika vitu vya ulimwengu huu. Maana nyingine ya Timayo ni uchafu, yaani Mwana wa uchafu. Maana hii ndiyo inayoweza labda kuelezeka hapa linaposisitizwa jina hilo. “Mwana wa Timayo, Bartimayo,” yaani kile kionekanacho machoni pa jamii nzima kuwa ni cha maana, cha ukuu, cha hadhi, na cha heshima, kumbe, kwa kweli ni uchafu na takataka, kwani vitu hivyo vya hadhi ndivyo vinavyotupofusha macho tusiweze kuona njia ya kweli. Yawezekana hata sisi ni wana wa ukoo wa Timayo.” Anaitwa kwa maneno matatu ya kutia moyo: “Jipe moyo; inuka, anakuita.” Kwa lugha ya Kigiriki ni “Tharsei” maana yake jikaze, uwe na furaha, changamka. Halafu “Egeirai” ni inuka, amka achana na maisha ya zamani. “Phonei” maana yake anakuita.
Mama Kanisa anatualika kuanza kutembea na kumwendea Kristo Yesu anayepita katikati ya viunga vya maisha yetu kwa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na kwa njia ya watu wote wa Mungu tunaokutana nao katika maisha. Yohane na Yakobo Wana wa Zebedayo, walikuwa na imani haba, wakataka kuambata na kumezwa na malimwengu. Leo, Mama Kanisa anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa. Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu”. Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti, kiasi cha kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake. Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu.
Tunaadhimisha Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anafafanua kuhusu: Uhusiano na mafungamano ya Kristo Yesu na wafuasi wake na binadamu katika ujumla wake, ambayo yamewawezesha kufunuliwa Injili na Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia uzoefu wa Mitume wa Yesu wanaoshuhudia upendo, huruma na msamaha ulioneshwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Anaelezea matatizo na changamoto zilizojitokeza kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo katika mwanzo wa safari yao ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Tunakumbushwa kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Kumbe, asiwepo hata mmoja anayetengwa na huruma na upendo wa Kristo Yesu, Ufunuo wa Uso wa Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu katika majuma kadhaa imetusaidia kutafakari mazingira ya kukamatwa kwa Yohane Mbatizaji, Tamko na Katekesi kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kama kielelezo cha huruma, upendo na wokovu wa Mungu. Imegusia kuhusu umuhimu wa kuwa na imani thabiti; Ubatizo na kikombe cha mateso, kwa kumwonesha Kristo Yesu kuwa ndiye yule Mtumishi wa Mungu aliyetabiriwa kwenye Agano la Kale. Sasa yuko safarini kuelekea Yerusalemu ili kukabiliana na Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Huu ni wakati wa kumlilia na kumwita, ili aweze kutuponya upofu wetu wa imani, ili hatimaye, tuweze kufuatana naye kwenye chemchemi ya visima wa wokovu. Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la milele, kumwendee kwa imani na matumaini katika shida na mahangaiko yetu, kama alivyokuwa Bartimayo Mwana wa Timayo!