Tafakari: Kristo Yesu Ni Nuru ya Mataifa na Wokovu wa Ulimwengu!
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Injili ya domenika hii yahusu uponywaji wa Bartimayo kipofu na Yesu kama ishara wazi ya kutimia kwa utabiri wa Manabii juu ya ujio wa Masiha maana kadiri ya maandiko matakatifu, kumwezesha kipofu kuona ilikuwa ishara wazi ya kufika kwa Masiha. “Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa…” (Isa 35:5), “Bwana huwafumbua macho waliopofuka…” (Zab 146:8), “Vipofu watapata kuona…” (Mt 11:5). Katika Injili tunakutana na matukio matano ambapo vipofu waliponywa: Vipofu wawili ambao Yesu aliwaponya mara tu baada ya kumfufua Binti Jairo (Mt 9:27-31), Yesu anamponya mtu aliyekuwa bubu na kipofu: “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona” (Mt 12:22); Kipofu wa Betsaida ambaye baada ya kuponywa akasema “naona watu kama miti, inakwenda,” na uponyaji ulipokamilika, “akaona vyote sawasawa” (Mk 8:22-26), na Bartimayo wa Yeriko kadiri ya Injili Pacha (Mt 20: 29-34, Mk 10:46-52, Lk 18:35-43). Yesu anamponya mtu aliyezaliwa kipofu aliyeishi huko Yerusalemu: ambaye wanafunzi wa Yesu walihoji “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?” Yesu akajibu, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake, bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake (Yn 9:1ff). Tunaweza kusema kuwa kuponywa kwa vipofu ni kuanza kutimia kwa utabiri kuwa Yesu Kristo ni Masiya anakuja kutukomboa kutoka utumwa na upofu wa dhambi.
Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Yeremia (31:7-9); ni utabiri/uaguzi wa Nabii Yeremia juu ya ujio wa Masiha ambaye kupitia yeye Mungu atawaponya wagonjwa na vipofu. Utabiri huu Yeremia anautoa kwa watu waliobaki Yerusalemu wakati wa uhamisho wa Babeli ndiyo maana anasema; “Mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme; Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli.” Kipindi cha uvamizi na kuchukuliwa mateka watu wengine waliachwa na majeraha na mavunjiko mbalimbali. Yeremia anawafariji kwa kuwaahidi kuponywa kwako. Utabiri huu pia unawahusu wale walioko uhamishoni Babeli kuwa nao watarudishwa ndiyo maana Yeremia anasema; “Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni Baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.” Licha ya kuwa utabiri huu ulitimia kwa kurudi kwa wana wa Israeli kutoka uhamishoni Babeli, lakini ulikuwa ni maanadalizi ya ujio wa Kristo kama tunavyoona katika Injili Yesu akimponya Bartimeyo kipofu.
Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (5:1-6); ni maelezo na ufafanuzi kuhusu uhusiano uliopo kati ya ukuhani wa Yesu na ule wa Agano la Kale. Somo hili linatueleza kuwa Kuhani ambaye ni mpatanishi kati ya Mungu na watu, inampasa kuwa na hali ya ubinadamu ili, aonje udhaifu wa kibinadamu, ili aweze kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu. Hii ndio sababu ya Yesu Kristo, Kuhani wetu Mkuu kuchukua mwili wa kibinadamu katika Fumbo la umwilisho ili ashiriki hali yetu ya kibinadamu, aonje uhalisia wa mahangaiko yetu na kutupa uwezo nasi wa kushiriki katika ukuhani wake katika kuwafanya watu wamjue, wampende na wamtumie Mungu na mwisho kufika kwake mbinguni. Kumbe basi kuhani anatwaliwa katika wanadamu, anawekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu; kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu wake. Tukumbuke kuwa hadhi na heshima hii hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe, ila yeye aitwaye na Mungu. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu ndiyo maana maandiko matakatifu yanasema; “Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa na kukufanya kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.”
Injili ilivyoandikwa na Marko (10:46-52); ni simulizi la mwujiza wa Yesu kumponya Bartimayo kipofu huko Yeriko. Muujiza huu unadhihirisha kuwa Yesu ni Masiya aliyetabiriwa katika Agano la Kale. Huyu kipofu alikuwa mwombaji aliyeketi kando ya njia. Naye aliposikia kuwa Yesu Mnazareti anapita, alipaza sauti akisema; “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu”. Watu walimkemea ili anyamaze, lakini yeye hakunyamaza wala kukata tamaa bali alizidi kupaza sauti; “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.” Yesu anasimama na kuamuru aitwe. Waliokuwa wanamkemea wanamwambia; “Jipe moyo; inuka, anakuita.” Akatupa vazi lake, akaruka kwa shangwe, akamwendea Yesu. Yesu akamwambia; Wataka nikufanyie nini? Akasema; Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia; “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona. Hapa tunaona kuwa ni imani ndiyo iliyomponya Bartimayo upofu wake. Imani ni kama darubini. Imani hushinda upeo wa macho yetu, huweza kuona yanakoshidwa kuona macho. Imani haiangalii mambo ya sasa tu, bali hata yajayo ambayo kwa sasa hayapo bayana. Hivyo imani ni chanzo cha uvumilivu, chanzo cha subira na chanzo cha unyenyekevu. Imani inapokosekana hupelekea kukata tamaa na kutojishughulisha na chochote. Ndiyo maana kazi na mambo mengi katika maisha hufanyika yakitanguliwa na imani. Mfano, mkulima hulima na kupanda mbegu akiamini mvua itanyesha, mbegu zitamea, zitakua na kuzaa naye atavuna na kufanikiwa kimaisha. Kumbe imani ndiyo inayofanya maisha yasonge mbele.
Sala ya Bartimayo kipofu ni fupi mno; “Bwana nataka nipate kuona.” Ni sala itokayo ndani kabisa mwa mtima wa moyo wake. Yeye alitaka kuona. Neno kuona katika mazingira haya lina maana ya kuona kwa macho. Kipofu anaomba apewe uwezo wa kuona vitu kwa macho. Lakini zaidi sana ni uponyaji wa kiroho, kupata kuona udhaifu wake wa kiroho. Kumbe tunawezakuwa vipofu wa kutoona udhaifu na kasoro zetu. Tukajiona tu wakamilifu. Lakini jinsi tunavyoshindwa kutambua uovu na dhambi zetu na kuomba msamaha kwa Mungu ndivyo tunavyozidi kuishi maisha ya huzuni, mafadhaiko, msononeko na kukosa amani na furaha. Bartimayo anatualika tumlilie Yesu na kumwambia: “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.” Tukiomba hivyo kwa imani; jibu la Yesu ni kuwa; “Imani yako imekuponya”. Tukumbuke kuwa, ukiwa katika dhambi unakuwa kama kipofu; hauoni uzuri wa maisha. Saikolojia inatueleza kuwa mtu anapotenda dhambi kwa mara ya kwanza anakuwa na hofu, woga na wasiwasi mkubwa mno hivyo anaitenda kwa kujificha madhalani usiku, tena nako mtu anajificha. Lakini akishaizoea, haoni haya tena maana amepoteza mizani ya maadili na kukatika mshipa wa aibu na haya. Kumbe basi tuogope kuzoea dhambi.
Kama kuna dhambi yoyote inayokusumbua; “Jipe moyo, inuka, Yesu anakuita utoke huko ulikozama na anakuuliza; “Wataka nikufanyie nini?” Sema bila kuogopa; “Bwana nipate kuona tena.” Bwana nitoe katika dhambi hii. Bwana nitoke katika uovu huu. Nyumba ndogo imekufanya kipofu hata humuoni mwenzako wa ndoa mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Ubinafsi umekufanya kipofu hata huoni matatizo ya wengine sema; “Bwana nipate kuona.” Pombe imekufanya kipofu huoni mahitaji ya familia yako, sema; “Bwana nipate kuona.” Tamaa za ujana zimekufanya kipofu huoni mwelekeo wa maisha, sema; “Bwana nipate kuona.” Ufisadi umekufanya kipofu huoni wanaoteseka kwa ajili yako, sema; “Bwana nipate kuona.” Umetafuta mchumba kwa muda mrefu bila mafanikio. Usike tamaa mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona”. Umetafuta kazi mda mrefu bila mafanikio, usiogope. Mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Biashara imekwama, usirudi nyuma mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Umeugua muda mrefu na umekosa matibabu, mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Ndoa na familia yako imejaa malumbano na matatizo hakuna furaha wala amani, mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Umesubiri kwa muda mrefu upandishwe cheo bila mafanikio, usikate tamaa mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Jibu la Yesu daima ni hili; “Imani yako imekuponya.”
Ni kwa uhakika ukiwa na imani yote uombayo Mungu atakupatia. Ili Yesu asikie kilio chetu sisi nasi tunapaswa kusikiliza vilio vya wengine kwa maana kipimo kile kile tuwapimiacho wengine ndicho tutakachopimiwa. Yawezekana kila siku tunasikia vilio vya wengine vya kuomba msaada, vilio vya kutaka kufarijiwa, vilio vya kuomba mwanga lakini tunajifanya viziwi, hatusikii wala kugeuka kuwasaidia. Tutambue kuwa kufanyahivyo ni ujeuri na ukatili mbaya sana. Tujifunze kutoa faraja kwa wanaolia na kuwaambia: “Jipe moyo; inuka. Tujifunze kufumbua macho yetu na mioyo yetu kwa wahitaji wanaopiga kelele kama Bartimayo wakihitaji msaada na sio kuwafunga mdomo na kuwanyamazisha wasisikike bali tuwatie moyo ili nao waweze kuishi kwa furaha. Lakini tutambue kuwa ili uombe kuona lazima kwanza ujitambue kuwa u-kipofu. Mafarisayo walikataa kwamba wao si vipofu. Yesu akawaambi; “kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia lakini ninyi mwasema: “Sisi tunaona”, na hiyo yaonyesha mna hatia bado” (Yn 9:41). Tumwombe Yesu atusaidie tujikubali tunapokosea na tukiendee kitubio ili atusamehe na kuturudishia neema zake zitakazotusaidia kuona njia ile iendayo uzimani kwa Mbinguni kwa Baba.