Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 28 ya Mwaka B wa Kanisa: Malimwengu kisiwe kikwazo cha kutafuta na kuambata maisha ya uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 28 ya Mwaka B wa Kanisa: Malimwengu kisiwe kikwazo cha kutafuta na kuambata maisha ya uzima wa milele! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili 28 Mwaka B: Malimwengu na Uzima!

Ukarimu ni fadhila inayofukuza ndani ya roho ya mwanadamu uchoyo na ubinafsi. Ukarimu unamfanya mtu adumishe matumaini yake kwa Mungu. Tukumbuke kuwa kadiri unavyoweka matumaini yako katika malimwengu, ndivyo matumaini yako kwa Mungu yanavyopungua. Ndiyo maana kijana tajiri alipoambiwa auze alivyonavyo awasaidie maskini, akaondoka kwa huzuni!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatukumbusha kuwa; “Kupenda mno na kujihusisha kupita kiasi na mali ya dunia hii, ni pingamizi la kufika mbinguni”. Somo la kwanza la kitabu cha Hekima ya Sulemani (7:7-11); ni ushuhuda wa mfalme Sulemani kuwa “hekima” ni kitu bora zaidi kuliko kitu chochote duniani. Dhamani yake inashinda cheo chochote kile, utajiri na uzuri wote ule. “Hekima” hii ndiyo inayomuwezesha mwanadamu kumjua Mungu na kutimiza mapenzi yake. Hekima hii Sulemani anaishuhudia akisema; “Naliomba, nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu ikilinganishwa nayo; wala sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama udongo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo nikajiliwa mema yote ya jamii, na mikononi mwake mali isiyoweza kuhesabika.”

Kumbe, hekima ndiyo inayotusaidia tumjue, tumpende na tumtumikie Mungu na kwa namna hiyo tunapata neema na baraka zake zinazotuwezesha kuvipata na kuvitumia vitu alivyoviumba yeye kwa ajili ya sifa na utukufu wake ili kwavyo tuweze kutakatifuzwa na kustahilisha kuurithi uzima wa milele. Somo la Pili la Waraka kwa Waebrania (4:12-13); latufundisha kuwa Neno la Mungu ni ufunuo wa Mungu mwenyewe uliotufikia kwa njia ya Manabii wake na kwa namna ya pekee kwa njia ya Mwanae wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo. Neno hili lina nguvu ya wokovu, ni neno lenye uhai. Neno hili lina ukali wa kuangamiza kila aina ya ubaya na kutupatia uzima kwa kutujalia uwezo wa kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Kumbe somo hili linatuonyesha jinsi Neno la Mungu lilivyo la dhamani katika maisha yetu. Tujitahidi basi kulisoma, kulitafakari na kuliishi kwani ndilo chakula cha roho zetu, ndicho chakula kituleteacho uzima wa milele.

Katika Injili ilivyoandikwa na Marko (10:17-30); Yesu anatuangalisha na kututahadharisha na hatari ya utajiri. Lakini angalisho ni tahadhari juu ya tahadhari inayotolewa. Tahadhari hii ni kuwa Injili kamwe haikatazi kuwa na mali bali inatoa tahadhari kwa wale wanaoweka tumaini lao lote katika mali na kumuweka Mungu pembeni kuwa itakuwa vigumu kwao kuingia katika ufalme wa Mungu. Yesu anatoa tahadhari hii baada ya mtu mmoja kumwuliza; “Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” Yesu anaweka wazi hali ya binadamu kuwa sio ya ukamilifu akisema; “Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.” Kisha anatufundisha namna ya kuurithi uzima wa milele. Hatua ya kwanza ni kuzijua na kuzishika amri za Mungu. Hatua ya pili ni kuwatumikia wengine hasa walio wadogo hasa: wagonjwa, maskini wenye njaa na kiu. Ndiyo maana muuliza swali aliposema; Mwalimu, amri 10 za Mungu nimezishika tangu utoto wangu; Yesu alimpenda, akamwambia; Umepungukiwa na neno moja; “Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.”

Marko anasema; “Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kujilimbikizia mali nyingi kupita unachohitaji sio tu kunakuletea mkunjo wa uso na kuenenda kwa huzuni bali pia kunakufanya uingie kwa shida na taabu katika ufalme wa Mungu na wakati mwingine kuukosa kabisa! Mali inamfanya mtu aitegemee na kuiona ndiyo impayo uzima na kumsahau Mungu, Baba wa uzima na kumtumaini yeye ni kupata yote na uzima wa milele. Kumbe basi kilema cha kukumbatia mali za dunia hii ni kushindwa kuukumbatia ufalme wa Mungu. Kujilimbikizia mali zaidi ya unachohitaji ni kuwa na uchoyo wa hali ya juu sana. Mtu mchoyo anatumia karama zake zote na nguvu zake zote na uwezo wake wote ili kuufurahisha mwili wake na kuiacha roho itiayo uzima ikiangamia. Hali hii yaweza kumpata pia maskini kwa kuwa na tamaa ya mali, kiasi kwamba Mungu anakuwa hana nafasi kwake. Maskini na tajiri wote wanapaswa kupambana na kilema hiki. Kwanza kabisa kwa sala kwani bila sala hatuwezi kupiga hatua yoyote katika maisha ya kumpenda na kumtumikia Mungu na jirani kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Pili tukumbuke kuwa chochote tunachokihangaikia hapa duniani hakidumu tutakiacha kama anavyotuambia Mtume Paulo kuwa: “Maana hatukuleta kitu chohocte hapa duniani wala hatutachukua chochote.” Kumbe Mungu akikujalia mali maana yake amekuweka uwe mgawaji kwa wengine na sio kuendelea kuzirundika halafu mwisho unakufa na kuziacha. Kumbuka hizo ndizo ushahidi wako siku ya hukumu ya mwisho.

Kumbe basi, mali tulizojaliwa na Mungu tuzitumie kwa ukarimu kama anavyotuasa Mtume Paulo akisema: “Furahini na wenye kufurahi, na lieni na wenye kulia” (Rum 12:15). Ukarimu ni fadhila inayofukuza ndani ya roho ya mwanadamu pendo la ubinafsi. Ukarimu unahimiza kuwapenda wenzetu kwa kujizoesha kufanya matedo ya huruma ya kimwili na kiroho. Ukarimu unamfanya mtu adumishe matumaini yake kwa Mungu. Tukumbuke kuwa kadiri unavyoweka matumaini yako katika hazina za dunia, ndivyo matumaini yako kwa Mungu yanavyopungua ndiyo maana kijana tajiri alipoambiwa na Yesu auze alivyonavyo awasaidie maskini; “Yeye alikunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni.” Je, tusikiapo maneno ya Yesu Nenda kauze ulivyonavyo wape maskini, tunafanyaje? Tunakunja uso na kuondoka kwa huzuni au tunafurahi? Mama Theresa wa Calcutta aliwahi kusema: “wakati mnaendelea kujadili kiini na maelezo yatolewayo, nitapiga magoti kandoni mwa walemavu, maskini zaidi kati ya maskini na kushughulikia mahitaji yao. Ombaomba, mkoma, mlemavu, hawaitaji majadiliano na nadharia, wanahitaji upendo kwa matendo.” Huku ndiko kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni (Lk 6:36).

Ndiyo maana Yesu anasema; “kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi” (Mt. 25:40). Hivyo tuchote neema kwa kutenda matendo ya huruma kwa wenye kuhitaji msaada wetu. Toa kwa moyo kadiri ya uwezo wako ili maskini waweze kupata mahitaji yao msingi na Mungu atabariki kwa kile mtakachotoa kwa moyo. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema kuwa; “Ni katika kutoa ndipo tunapokea. Ni katika kusamehe ndipo tunasamehewa. Ni katika kufa tunazaliwa katika uzima wa milele”. Kumbukeni alichofanya yule mjane wa Serepta kwa kumhudumia Nabii Eliya (1Fal. 17:1–16), pipa lake la unga na chupa ya mafuta havikupungua. Nasi tukitoa kwa moyo, hatutapungukiwa na kitu kwani Bwana ndiye mchungaji wetu (Zab 23:1). Usidangayike kwa kukumbatia mali za dunia hii na kusahau kumtumikia Mungu. Tumia mali uliyonayo kwa ajili kuupata ufalme wa Mungu. Daima unapotoa kwa wahitaji kwa moyo, ndipo Mungu anapokujaza mara nyingi zaidi ya kile ulichotoa kwa moyo.  “Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni” (Marko 10:17-30).

Tafakari J28
06 October 2021, 15:29