Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 28: Hekima, Neno & Utajiri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Tunaungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya uzinduzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana, na kumtegea Mungu masikio yetu, ili kutambua uwepo wake wa daima na hivyo kuwa tayari kupokea ujumbe wake anapopita na kutembea kati yetu! Mchakato wa Awamu ya Kwanza unayahusu Makanisa Mahalia na Taasisi zote za Kanisa yaani kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022. Katika tafakari ya Neno la Mungu, leo ningependa kujielekeza zaidi katika fadhila ya Hekima, ili kuweza kumfahamu, kumpenda, kumtumikia Mungu na hatimaye, kufika kwake Mbinguni. Hekima ya Mungu imefunuliwa katika Kazi ya Uumbaji na katika Maandiko Matakatifu. Kristo Yesu ni nguvu na Hekima ya Mungu. Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, lina ukali kuliko upanga wenye makali kuwili. Kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha. Haitoshi kuzifahamu Amri za Mungu na Maagizo yake. Sheria na Maongozi ya Mungu yawe ni dira ya maisha adili na matakatifu. Utajiri kisiwe ni kikwazo cha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Wale walioacha yote na kuamua kumfuasa Kristo Yesu na Injili yake, watapata maradufu, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele!
Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Hekima ya Sulemani. Hek. 7:7-11. Mfalme Sulemani anasema naliomba, nikapewa ufahamu, nalimwita Mungu akanijalia roho ya hekima. Hekima ni kati ya Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu ambayo wanakirimiwa waamini wakati wanapopokea na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara. Lakini, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni nguvu na hekima ya Mungu. Rej. KKK 272. Kimsingi mwanadamu anashiriki hekima na wema wa Mwenyezi Mungu anayempa mamlaka juu ya matendo yake na uwezo wa kujitawala kuhusu kweli na wema. Sheria ya maumbile inaonesha maana adili ya asili inayomwezesha mtu kupambanua kwa njia ya akili yaliyo mema na yaliyo mabaya, ukweli na uwongo! Rej. KKK 1954. Hekima ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa imefunuliwa na kujidhihirisha katika kazi ya Uumbaji na Maandiko Matakatifu, lakini zaidi ni kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, watu wote wanaweza kutambua hekima ya Mungu kwa njia ya kazi ya uumbaji hata kama hawajui kusoma wala kuandika. Kwa Wayahudi hekima ya binadamu inajidhihirisha katika Sheria inayopata chimbuko lake katika falsafa! Hekima ya Kimungu ni chanzo cha uhuru, usalama, upendo, amani na utulivu! Hekima ikiambatana na busara mambo yanakwenda vyema!
Somo la Pili kutoka katika Waraka kwa Waebrania: Ebr 4:12-13. Ni ufunuo wa jinsi ambavyo mwanadamu amekengeuka na matokeo yake akajichumia dhambi na majanga. Leo Mama Kanisa anatualika kulipatia Neno la Mungu uzito wa pekee kwa kulisoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yetu, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo thabiti wa maisha. Imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia ni sehemu ya mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa katika kazi ya Uumbaji na katika Maandiko Matakatifu na kilele chake ni Kristo Yesu! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wameliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira na mwanga katika mapito ya maisha yao hapa duniani. Hii ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na kwenye Vyama vya Kitume katika ngazi mbalimbali!
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio “APERUIT ILLIS” yaani: “ALIWAFUNULIA AKILI ZAO” ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu itakayokuwa inaadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa. Dominika hii itakuwa ni: kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Neno la Mungu lina utajiri mkubwa na amana ya kufundishia. Ni muhtasari wa maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya imani na ukweli wa maisha na Fumbo la Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Neno la Mungu linafafanua historia ya wokovu, linabainisha maisha ya kiroho na kanuni ya Fumbo la Umwilisho. Neno la Mungu linatenda kazi ndani ya yule anayelisikiliza kwa makini, kiasi cha kumwajibisha kuwashirikisha wale wote anaokutana nao, ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya watoto wa Mungu. Neno la Mungu ni chemchemi ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma kwa akina Lazaro wanaoendelea kuteseka sehemu mbalimbali za dunia hata katika ulimwengu mamboleo, changamoto na mwaliko wa “kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo”, ili kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Injili kama ilivyoandikwa na Marko 10: 17-30. Haitoshi kuzifahamu Amri na Maagizo ya Mungu, bali zinapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha adili na Mtakatifu. Kristo Yesu anatoa muhtasari wa Amri za Mungu kwa upendo kwa Mungu na jirani. Anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye ukamilifu wa wema na utakatifu wote wa maisha na mengine yote yanabubujika kutoka kwake! Ili kijana aweze kujichotea wema na furaha ya kweli katika maisha; Mosi, ni kuwatendea mema jirani kama sehemu ya utekelezaji wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Kristo Yesu alitambua pia udhaifu wa yule kijana tajiri na kumtaka kupiga hatua moja mbele kwa kujiondoa katika haki kwa sababu ya kutenda mema na kujikita katika sadaka ya maisha. “Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Mk 10:21. Mkazo ni neno “Njoo Unifuate.” Kumfuasa Kristo Yesu katika maisha ni chemchemi ya furaha ya kweli na sadaka inayotolewa inang’oa vikwazo vyote. Kwa bahati mbaya, kijana tajiri alikuwa ameelemewa sana, kiasi cha kutaka kuwahudumia Mabwana wawili, yaani Mungu na mali! Ndiyo maana yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
Waamini wavutwe na Uso wa huruma na upendo wa Kristo Yesu, unaowaokoa kutoka katika vishawishi vya uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka unaoweza kuwatumbukiza katika utamaduni wa kifo na ugonjwa wa sonona! Mali, utajiri na anasa si mambo yanayomfanya mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha. Karama, mapaji, mali na utajiri mbalimbali vikusaidie kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kweli na Mungu pamoja na huduma kwa Mungu na jirani. Mitume wa Yesu na wale wote walioacha yote kwa ajili ya Kristo Yesu na Injili yake watakapata maradufu pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele! Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican kwa ufupi kabisa Hekima ya Mungu imejifunua katika kazi ya Uumbaji na utimilifu wake ni katia Maandiko Matakatifu; Kristo Yesu ni nguvu na hekima ya Mungu. Neno la Mungu ni muhtasari wa maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya imani na ukweli wa maisha na Fumbo la Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Neno la Mungu linafafanua historia ya wokovu, linabainisha maisha ya kiroho na kanuni ya Fumbo la Umwilisho.