Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 28: Uzima wa Milele ni Zawadi ya Mungu
Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Mwinjili Marko haanzi Injili yake kwa kutueleza nini tunadaiwa kufanya au kutekeleza kama wafuasi wa Kristo mintarafu maadili, bali madai ya kimaadili ni kwa wale wanaokuwa wameelewa tayari nini maana ya kumfuasa Yesu Kristo, nini maana ya ufuasi wa kweli. Ndio kusema hata nasi hatuna budi katika kazi ya kuhubiri na kuwashirikisha wengine Habari Njema, kuwaonjesha kwa nafasi ya kwanza sio madai na namna ya kuishi imani yetu, bali maana na uzuri wa kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo, kuwasaidia kukutana kwa nafasi ya kwanza na Nafsi ya Yesu Kristo, ili wamjue na mwisho waweze kumpenda na kumtumikia kama wafuasi wake, kama wale wanaokuwa tayari kukata na kubadili vichwa vyao na kuvaa mantiki mpya ya Injili, mantiki ya mbinguni hali tungali bado hapa duniani. Dominika iliyopita, tulisikia juu ya mafundisho ya ndoa, na hapo Yesu anaturudisha nyumbani kuishi kadiri ya mpango wa Mungu tangu awali, na leo basi anatualika wanafunzi wake kutambua ulazima wa kwenda na kuuza yote na kuwapa maskini na mwisho tuweze kumfuata.
Tunakutana leo na kijana tajiri anayekimbia na kupiga magoti mbele ya Yesu na kumuuliza; “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuurithi uzima wa milele?” Tunastuka kwa ukweli kwamba mara nyingi waliomkimbilia Yesu na kuanguka mbele yake ni watu waliokuwa na mahangaiko na shida mbali mbali mathalani maladhi, mapepo, ulemavu na kadhalika, lakini leo Mwinjili Marko anatuonesha anayekwenda kwa Yesu tena kwa kukimbia anampa tena sifa za kuwa alikuwa kijana na tajiri. Ndio kusema kwa macho ya mantiki ya ulimwengu huu ni mtu aliyekuwa na mafanikio, iwe kwa umri wake kwani kila mmoja angetamani kubaki kuwa kijana, ndio umri wa kufurahia maisha kwa kiwango cha juu kabisa katika hali na nyanja mbali mbali, zaidi sana ni tajiri. Na ndio tamaa ya wengi kubaki na umri wa ujana na pia kuwa na mali, kuwa na mafanikio kadiri ya mantiki ya kidunia. Mtu yule pamoja na kuoneshwa kuwa alikuwa kijana, tajiri na mwenye nguvu na siha njema hata kuweza kumkimbilia Yesu, tunaweza kusema alitambua bado uhitaji mkubwa ndani mwake, kuwa amepungukiwa na kitu kikubwa na hivi hakuwa katika utulivu na amani ya ndani.
Kijana tajiri ni baada ya kutambua shimo tena tupu ndani mwake anaona ni Yesu pekee anayeweza kumsaidia kulijaza shimo lile, hali ile ya mashaka na kukosa amani ya kweli, na ndio anamkimbilia na kumuuliza kama Mwalimu tena anampa na sifa nyingine kumtofautisha na walimu wengine, na marabi wengine, anamtambua Yesu kama mwalimu mwema, kama mwalimu aliyeishi pia mafundisho yake kikamilifu na kiaminifu. Kijana tajiri, si tu alikuwa ni mtu aliyeshika amri, bali zaidi sana tunaonja alikuwa ni mtu mwenye uelewa sahihi wa kitaalimungu juu ya ukweli kuwa; Uzima wa milele sio haki au tunzo kwa mwanadamu baada ya kufanya vema, bali anatambua kuwa ni zawadi. Na ndio anatumia neno “kuurithi”, Urithi ni zawadi na sio mastahili wala malipo baada ya kazi njema na nzuri. Yote yatokayo kwa Mungu ni urithi, ni zawadi kwa mwanadamu; ardhi (Zaburi 135:12), Sheria (Zaburi 119:111), baraka, ahadi zake (Waebrania 6:12), Ufalme wa Mungu (Matayo 25:34), na hata Bwana aliye urithi wa Israeli (Zaburi 16:5). Hivyo yote ni mali ya Bwana na kwetu tunayapokea kama zawadi.
Pamoja na kutambua kuwa uzima wa milele ni urithi, ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini bado anaona naye kwa upande wake lazima afanye kitu au jambo fulani ili kuweza kuurithi, nifanye nini ili niweze nami kuurithi, ndio kusema anatambua umuhimu w anafasi yake ili kuurithi uzima wa milele. Mungu hamlazimishi mwanadamu asiyetaka kuurithi uzima wa milele, bali daima anautoa kwa yeyote yule anayekuwa tayari kuurithi uzima wa milele, hivyo nasi hatuna budi kuitikia wito na mwaliko wake katika kuuendea uzima wa milele, katika kufikia kilele cha lengo la maisha ya mkristo, kuunganika na Mungu milele yote. Unazijua amri? Ni swali chokozi na tafakarishi sio tu kwa kijana tajiri bali hata kwetu nasi leo tunaokuwa ni marafiki na wafuasi wake Yesu Kristo. Yesu leo anamtajia sehemu ya zile amri kumi za Mungu, na hasa zile zinazogusa mahusiano yetu na wengine, amri zinazotualika kumpenda mwingine na kumthamini mwingine. Ndio kusema Yesu anaona ndani ya kijana yule kile anachopungukiwa au kile kilichosababisha shimo tupu ndani mwake, ni kukosa upendo kwa jirani. Na ndio maana anajaribu kumkumbusha amri zile zinazohusu mahusiano yetu na wenzetu.
Hata hivyo, jibu la kijana tajiri linatuacha karibu vinywa wazi, kwani ni mmoja aliyezishika amri zile kiaminifu tangu utoto wake, tangu akiwa na umri ule wa kutambua mema na mabaya, ndio kusema alikuwa mtu mwenye kushika amri na dini yake kwa kiwango cha juu kabisa. Mtume Yohane katika Waraka wake wa kwanza anatuambia asemaye hana dhambi basi kweli haimo ndani mwake. (1Yohane 1:8) Marabi wa Kiyahudi walifundisha ili kuwa mwenye haki lazima kuzishika amri na kuziishi kiaminifu, na Yesu anamwangalia kijana tajiri na kumpenda. Mwinjili Marko mara nyingi si tu anatupa mafundisho ya Yesu bali hata hali yake anayokuwa nayo katika matukio kadha wa kadha, na leo anatuonesha Yesu alimkazia macho na kumpenda kijana yule. Kwa nini anamwangalia na kumpenda, kwani Yesu anaona tayari kijana huyu amepungukiwa na kitu kimoja cha mwisho ili aweze kukamisha mahusiano yake mema kwa Mungu na kwa jirani. Kijana tajiri anapaswa sasa kuvuka hatua ya mwisho kabisa, ndio kula mkia baada ya kumaliza kumla ng’ombe mzima. Ni mwaliko wa Yesu kwa kijana tajiri kukamilisha hatua ile muhimu kabisa ya mwisho ndio ya kwenda na kuuza yote aliyonayo nayo na kuwapa maskini na hapo atakuwa na hazina yake mbinguni na kisha arudi amfuate Yesu.
Yesu anamwalika kubadili kichwa chake, kuvaa sio mantiki ya dunia hii bali ile ya mbinguni, ndio ile ya kutojishikamanisha na mali za dunia hii, kuacha kuwa mtumwa wa mali na utajiri na vitu na badala yake kuvitumia sio kwa manufaa binafsi bali hasa kwa upendo na ukarimu kwa wengine wanaokuwa katika uhitaji. Si kwamba Yesu anatoa amri mpya, la hasha bali daima anatusaidia kupata maana inayokuwa kamili na timilifu ya amri za Mungu, anakuwa ni mwalimu wa kweli wa sheria tofauti na wale wengine wote. Ni mwaliko wa kutoka katika ubinafsi na umimi sio tu wa mali bali wa yote mengine tunayojaliwa katika maisha iwe ni akili au karama mbali mbali, muda, ujuzi na utaalamu, nguvu na uwezo wetu mbali mbali vyote leo tunaalikwa kuviuza na kuwapa maskini. Kuuza na sio kutupa, ndio kusema Yesu anatambua thamani ya mali na karama zetu mbali mbali, lakini zinakuwa na thamani mbele ya Mungu ikiwa tu tunazitumia sio kwa ajili yetu wenyewe kwa ubinafsi bali kama nilivyosema kwa upendo na ukarimu na wengine, ndio moyo wa kuwashirikisha wengine mema tuliyoyapokea kwa Mungu. Wakristo tunaalikwa kuwa watu wa shukrani daima, na ndio maana kila Dominika au kila siku tunaadhimisha Sadaka ya Misa Takatifu, ndio Ekaristi Takatifu ikiwa na maana ya Sala kuu ya shukrani. Hivyo maisha yetu hatuna budi kuwa ya shukrani kwa kuwashirikisha wengine yale tunayojaliwa na Mungu.
Mwaliko huu wa kwenda na kuuza na kuwapa maskini sio tu kwa watu ulani wanaochagua maisha fulani ndani ya Kanisa, bali ni kwa kila mbatizwa, ni kwa kila mfuasi wake Yesu Kristo, yaani mimi na wewe. Ni mwaliko wa kila siku kutoka na kwenda kuuza, kutoka katika umimi na ubinafsi wangu, kuuza yale yote ambayo yananikwamisha kukua kumwelekea Mungu kupitia upendo kwa jirani. Kila tunaposhindwa kumpenda jirani kwa kuona uso wa Mungu kwake, basi hapo tunakwama kukua katika safari yetu ya kiroho hata kama tunashika amri nyingine zote kama kijana tajiri tena hata iwe kwa uaminifu mkubwa kiasi gani. Mwinjili Marko anatuonesha kijana tajiri pamoja na kuwa mshika sheria na amri za Mungu anashindwa kufanya maamuzi magumu, hatua ile ya mwisho ili aweze kuurithi uzima wa milele. Kijana tajiri anafadhaika moyoni na ndio maana tangu mwanzoni hatajwi kwa majina yake bali kwa vigezo vya umri na utajiri wake, kijana tajiri yumo ndani ya kila mmoja wetu hasa pale tunaposhindwa kutoka na kuuza ubinafsi na umimi wetu, kila mmoja wetu ni vema akaingia ndani mwake na kujitathimini ni wapi amekuwa sawa na kijana tajiri, wapi tumeshindwa kuwa wafuasi wa kweli kwa kumwangalia mwingine na kumshirikisha yale mema ninayojaliwa au niliyojaliwa na Mungu?
Kijana tajiri anashindwa kutambua kuwa tumeumbwa kwa upendo na pia nasi tumetumwa ulimwenguni kuwapenda si tu watu wa karibu na jirani yetu bali watu wote bila masharti wala mipaka ya kibaguzi, na ni hapo tunakuwa na hakika ya furaha na amani ya ndani. Kijana yule anashindwa kuwa mkristo pamoja na kuwa mwaminifu katika kushika amri za Mungu. Kumbe kuwa mkristo lazima kupiga hatua sio ya kubaki katika amri kumi bali kutoka na kwenda na kuuza na kuwapa maskini. Kutoka na kuuza umimi na ubinafsi, kutoka na kumpenda Mungu kwa njia ya kumpenda jirani. Na ndio tunaona sehemu ya pili ya Injili ya Dominika ya leo, Yesu anatuonesha hatari ya utajiri, na hasa ugumu kwa tajiri kuurithi uzima wa milele. Yesu anatumia lugha ya picha ya ngamia kupita katika tundu la sindano. Wataalamu wetu wa Maandiko Matakatifu wanatuonesha neno ngamia inaweza kuwa na maana mbili tofauti. Neno la Kigiriki “kamelos”, likiwa na maana ya ngamia, na lingine “kamilos” likiwa na maana ya ile kamba kubwa na nene inayotumika kuwekea nanga meli au mtumbwi inapokuwa bandarini. Na tundu la sindano wengine wanajaribu kufananisha na mlango mdogo kabisa wa kuingilia jiji la Yerusalemu.
Yote katika yote, kwa maana yeyote ile tunayoweza kuona ni rahisi kwetu, bado Yesu anatuonesha ugumu wa kufanya maamuzi ya kuwa mfuasi wake wa kweli kweli. Ndio maamuzi ya kutoka na kwenda kuuza na kuwapa maskini, ndio maamuzi ya kukata na kubadili vichwa vyetu, yaani kuvaa mantiki ya Kimungu badala ya ile ya ulimwengu huu, ile ya umimi na ubinafsi, ili ya kutokuwajali wengine bali hata kuwatumia wengine kwa kijitajirisha na kujilimbikizia mali za dunia hii. Ni ngumu iwe ni ngamia au kamba ile kubwa na nene kupita katika tundu la sindano, ni ngumu kwa ngamia kupita katika kimlango kile kidogo ili kuingia Yerusalemu, kuingia katika Ufalme wa Mungu. Kama vile Yesu anavyotuambia hatuwezi kumtumikia Mungu na mali (Luka 16:13), ni mwaliko wa kutambua katika maisha ya mfuasi daima nafasi ya kwanza ni Mungu na kamwe isiwe kitu kingine chochote.
Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, pia Yesu anawafundisha kuwa yote yanawezakana kwa njia ya msaada wa Mungu mwenyewe. Nasi hatuna budi kutambua tunaweza kuurithi uzima wa milele kwa njia ile ya Mungu mwenyewe sio kwa nguvu au akili au juhudi zetu pekee bali daima hatuna budi kumtegemea Mungu. Petro anaingia na kuuliza na sisi je tulioacha yote na kukufuata. Na hapo Yesu anawageukia na kuwafundisha ikiwa wameacha yote nyuma, ikiwa wameacha haimaanishi kutowapenda na kuwajali bali kwa kumpa Mungu nafasi ya kwanza, kumpa nafasi ile anayostahili katika maisha yetu. Yesu hasemi kuacha na kutelekeza iwe ni familia zao, bali kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yao. Na ndicho walifanya mitume kwa kutoa maisha yao sio kwa kutelekeza familia zao bali kumpa Mungu nafasi anayostahili hata kwa kumwaga damu na maisha yao kwa ajili ya Injili. Nawatakia Dominika na tafakari njema.