Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa: Uongozi ndani ya Kanisa unapaswa kuanza kuchukua mtazamo mpya wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Tafakari ya neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa: Uongozi ndani ya Kanisa unapaswa kuanza kuchukua mtazamo mpya wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 29: Uongozi ni Huduma Makini!

Masomo ya dominika hii yanatufundisha kuwa sifa kuu ya kiongozi ni kuwatumikia watu aliokabidhiwa kuwaongoza. Yesu anasema; Anayetaka kuwa mkubwa, kuwa kiongozi na awe mtumishi. Uongozi si kutumikiwa bali ni kuwatumikia watu. Nabii Isaya (53:10-11): Huu ni utabiri wa Nabii Isaya wa ujio wa “mtumishi wa Bwana” atakayetolea nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi za watu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatufundisha kuwa sifa kuu ya kiongozi ni kuwatumikia watu aliokabidhiwa kuwaongoza. Yesu anasema; Anayetaka kuwa mkubwa, kuwa kiongozi na awe mtumishi. Uongozi si kutumikiwa bali ni kuwatumikia watu. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (53:10-11); ni utabiri wa Nabii Isaya wa ujio wa “mtumishi wa Bwana” atakayetolea nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi za watu. Mtumishi huyu ataona uzao wake, ataishi siku nyingi na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake. Yeye ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Mtumishi huyu ni mwenye haki, naye atawafanya wengi kuwa wenye haki. Mtumishi huyo wa Bwana ni Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, nafsi ya pili ya Mungu aliyechukua mwili kwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yeye kwa mateso, kifo na ufufuko na wake, amewafanya wengi kuwa wenye haki, watoto wateule wa Mungu. Nasi kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya na kuwa watu wa haki mbele za Mungu. Ni wajibu wetu kutenda haki kwani kwa njia Yesu tumefanywa kuwa watu wa haki. Huku ndiko kuwa viongozi wa wengine katika kuwasaidia nao wawe watu wa haki.

Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (4:14-16); laeleza matunda yaliyoletwa na mtumishi wa Bwana yaani Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ndiye Kuhani Mkuu na wa kweli- ambaye kwa mateso, kifo na ufufuko wake ametuwezesha na anatualika kukisogelea kiti cha Mungu kwa moyo mwepesi. Yesu Kristo Kuhani mkuu yuko mbinguni, ili nasi tuweze kufika aliko yeye sharti tuyashike maagano yetu. Anayajua madhaifu yetu maana hata yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, lakini kwa kuwa alikuwa mkamilifu yeye hakutenda dhambi. Mtume Paulo anatutia moyo na kutihimiza kuwa; “Tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji,” ili mwisho wa yote tuufikie uzima wa milele mbinguni aliko Mwokozi wetu Yesu Kristo. Injili kama ilivyoandikwa na Marko (10:35-45); ni mawaidha na mafundisho ya Yesu ya namna tunavyopaswa kuishi ili tuweze kuurithi uzima wa milele. Yesu anatueleza kuwa wanaopata nafasi ya kuingia mbinguni ni wale wanaotoa uzima wao kwa ajili ya Kristo. Pili ni Mungu Baba peke yake ndiye aliye na mamlaka na uwezo wa kumketisha yeyote yule mkono wa kuume au kushoto kwa Yesu. Tena, utumishi ni alama ya ukubwa katika Kanisa la Kristo.

Mafundisho haya Yesu anayatoa baada ya mitume Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, kumwomba kuketi, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto, katika utukufu wake. Mawazo ya wana wa Zebedayo ni ya kisiasa. Wao walimwona Yesu kama kiongozi wa kisiasa anaenda kuunda dola yake yenye nguvu hivyo wakatamani kuwekwa katika mamlaka ya juu. Ombi hili kwa Yesu sio sahihi ndio maana anawaambia; “Hamjui mnaloliomba”. Kwa maana nyingine Yesu anawaambia; Mimi naelekea msalabani. Licha ya kuwa wanasema kuwa wanaweza kukinywea kikombe na kubatizwa ubatizo wa Yesu, lakini Yesu anawaambia kuhusu habari za kuurithi uzima wa milele ni mpango wa Mungu. Tamaa hii haikuwa ya Yakobo na Yohane tu, hata mitume wengine pia waliitamani nafasi hiyo ndiyo maana waliposikia waliwakasirikia Yakobo na Yohane. Ndipo sasa anawapa za usoni akiwaambia kuwa; “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza kwenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

Fundisho hili la Yesu ni juu ya Uongozi na Kiongozi bora. Uongozi ni utumishi. Ombi la Yakobo na Yohane kwa Yesu linahusu kukaa: “Utujalie tukae mmoja mkono wako wa kulia na mmoja mkono wako wa kushoto katika utukufu wako.” Wanataka wakae. Haja yao ni kukaa na kustarehe katika utukufu. Uongozi sio kukaa ni kutumikia. Wapo waliochoka na kazi za kuajiriwa hivyo wanakimbilia siasa ili wawe viongozi wakae wastarehe. Yakobo na Yohane wanatafuta upendeleo wa kuwa viongozi. Mwinjili Luka (9:46) anasema; “Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi.” Yakobo na Yohane baada ya kushindwa katika mjadala huo kuwaridhisha wenzao kuwa wanafaa kuwa viongozi wao wanaamua kwenda moja kwa moja kwa Yesu ili awafanyie upendeleo. Tusitafute vyeo kwa upendeleo. Yawezekana kwa kuwa Zebedayo Baba yao alikuwa tajiri nao pengine walikuwa na pesa na mali walijiona kuwa maarufu na kuwa wao ndio wanaostahili kuwa viongozi hata kwa rushwa ndiyo maana wanasema; “Tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.” Ni kana kwamba wanasema; “Utufanyie lolote tutakalokuomba kama ni pesa tutakupatia.”

Uongozi na kiongozi sio swala la upendeleo. Mtu kukaa mkono wa kulia au kushoto ni kazi ya Mungu na watapewa wale wanaostahili. Ni kweli Kristo alizungumzia Ufalme wa Mbinguni lakini inatuonyesha kuwa kumfanya mtu kiongozi ni kazi ya Mungu na wanapewa wale wanaostahili si kwasababu wana chochote, ni matajiri ndio wapewe upendeleo wa kuwa viongozi. Kiongozi anapaswa kuwa tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya wale anaowaongoza. Kiongozi bora yuko tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya wale anaowaongoza. Kiongozi bora yuko tayari kuteseka kwa ajili ya watu wake. Kiongozi bora yuko tayari kuchubuliwa, anakubali kuhuzunishwa na kutukanwa kwasababu anatetea haki za watu wake na kuzisimamia. Kiongozi bora yuko tayari kukinywea kikombe cha kupambana na maovu katika jamii yake. Somo hili pia latufundisha kuwa katika maisha usitafute vitu vya kupendelewa. Utapoteza uhuru wako kwa yule anayekupendelea. Tutafute maendeleo katika maishi kwa kupambana kwa njia halali. Kiongozi bora ana huruma, anachukuliana na watu wake katika unyonge wao na hivyo kuwainua mpaka kwenye utukufu.

Kiongozi bora yuko tayari mapenzi ya “Bwana yatafanyika kwa mkono wake.” Kiongozi bora ni mcha Mungu, anatambua kuwa Mungu anamtumia katika kutimiza mapenzi yake. Sifa hizi ni kwa kila kiongozi kuanzia ngazi ya familia, jumuyia, kanisa, maofisini, sehemu za kazi na zaidi sana viongozi wa siasa. Tumshukuru pale tunapokuwa na viongozi wenye sifa hizi, viongozi ambao wanafanya kazi yao vizuri, viongozi wanaotumika na si wanaotumikiwa. Nasi kila mmoja katika nafasi yake ajitahidi kutumikia na sio kutumikiwa kwani ni katika kutumika tunastahilishwa kuurithi uzima wa milele mbinguni.

Tafakari J29
14 October 2021, 15:48