Bartimayo Kipofu Mfano Hai wa Kanisa la Kisinodi: Kusikiliza!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Ni kwa nadra sana kwenye Injili tunakutana na majina ya watu walioponywa na Yesu Kristo, na hata kutajwa kwa eneo au mahali ambapo muujiza umetendeka. Hata hivyo Mwinjili Marko leo, anatutajia ubini wa yule kipofu, ndiye Bartimayo, maana yake ni mwana wa Timayo. Muujiza ule ulitendeka katika mji wa kale kabisa ndio ule wa Yeriko. Sehemu ya Injili ya Dominika ya leo, ni hitimisho la sehemu ile ambayo Yesu anajaribu kuwaonesha wanafunzi na wafuasi wake lengo la safari yake ya kuelekea Yerusalemu na pia madai ya gharama ya ufuasi: Upendo usiojitafutia faida, usiojibakisha wala kujipendelea, kutokujishikamanisha na mwishowe kuabudu mali, kuwa mtumishi na mdogo, kuwatumikia wengine bila kusubiri malipo au faida binafsi na kadhalika na kadhalika. Muujiza huu unahitimisha sehemu ile ambayo Yesu anawafundisha madai na gharama ya ufuasi. Mwinjili Marko leo anatuonesha kuwa Yesu anakaribia kufika kilele cha safari yake, ndio mji ule wa Yerusalemu. Baada ya kusafiri kutoka katika mji wake wa Galilaya, na kupita bonde lote la Mto Yordani, na sasa amefika katika mji mkongwe kabisa, yaani, Yeriko. Kutoka Yeriko kufika Yerusalemu ni umbali wa kilometa 27 tu, hivyo anatuonesha jinsi gani Yesu sasa anakaribia kufika kilele cha safari yake, akiwa pamoja na wanafunzi wake. Baada ya kumaliza bonde lile la Mto Yordani, sasa Yesu anabakiwa na sehemu fupi ambayo ni milima ya kupanda kuelekea Yerusalemu, mji ulio juu kabisa.
Uwepo wa mkutano mkubwa, ni ukweli kuwa kipindi cha Pasaka ya Kiyahudi, mahujaji wengi walikuwa wanasafiri kwenda kutolea sadaka zao hekaluni, ndio Yerusalemu. Hata hivyo, kwa upande mwingine, bado tunabaki na maswali juu ya uwepo wa mkutano mkubwa, kwani tayari Yesu alishajifunua na kuwafundisha kile kinachomsubiri Yerusalemu, sio ushindi na utawala wa kisiasa bali ni kukataliwa, kutolewa ili ateswe na kufa, na kisha siku ya tatu kufufuka. (Marko 10:38) Mbele yake ni kikombe kile cha mateso na kifo, ndio ubatizo ule wa kutolea Mwili na Damu yake kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu mzima. Hakika tunaweza kusema si tu makutano hawakuelewa neno lile gumu, bali hata wanafunzi wake wa karibu, yaani, mitume nao pia walikuwa mbali kulielewa fundisho hilo juu ya hatima yake pale Yerusalemu. Bado akilini na vichwani mwao wanasubiri kwa hamu na shauku kubwa nafasi na sehemu za heshima baada ya Yesu kuwa mkombozi wao wa kisiasa na kiutawala mara afikapo Yerusalemu. Hali yao inafanana kabisa na wale wenye upofu, bado hawajapata mwanga wa kuweza kuwaangazia akili na mioyo yao, hivyo walibaki bado wakitembea gizani.
Hawakuwa tayari kufungua mioyo na akili zao ili kuweza kulipokea na kulielewa fundisho lile juu ya mateso, kifo na ufufuko. “Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa? Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii?” (Marko 8:17-18). Bado mitume na hata makutano walibaki na mioyo na akili zilizoshupaa. Na ndio tunaona katika Injili ya Marko, Yesu anajaribu kuwaponya upofu ule wa ndani kabisa, kuwaalika kubadili vichwa vyao, namna zao za kufikiri na kutenda, kuwataka kuongozwa na mantiki mpya, sio ile ya dunia hii bali ile ya Mungu mwenyewe. Kama ambavyo anamponya kipofu wa Bethsaida, vivyo hivyo pia Yesu anataka kuwaponya na wanafunzi na wafuasi wake. (Marko 8:22-26). Na sasa Yesu akiwa pamoja na wanafunzi wake, anafika katika mji ule wa kale kabisa wa Yeriko, na hapo anatenda muujiza wake wa mwisho kabla ya kuanza kupanda kuelekea Yerusalemu. Wakati wa Sikukuu za Pasaka, kwa desturi Wayahudi walifanya matendo ya huruma, mathalani kuwapatia misaada ya ukarimu kwa wahitaji, ili nao waweze kusherehekea na kufurahia sikukuu zile za Pasaka. Hivyo maskini na wenye ulemavu na wahitaji wengine, nyakati za sikukuu walitoka katika miji na vijiji na kukaa barabarani, mahali ambapo mahujaji walipita ili nao waweza kupata chochote.
Na kati ya hao, ndio Mwinjili Marko anatuonesha leo kuwa alikuwepo pia kipofu mmoja anayetambulishwa kwa jina la ubini wake, ndio Bartimayo, yaani, Mwana wa Timayo. Muujiza huu wa uponywaji wa Bartimayo, tunakutana nao katika Injili zote pacha. Mwinjili Marko anatupa simulizi hili, sio tu kama tukio na simulizi la kawaida, bali linalobeba ujumbe wa Kitaalimungu ndani mwake. Bartimayo, ni kielelezo cha kila mfuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, anayekuwa tayari kuililia huruma yake, ili aweze kuona tena na kutembea katika nuru na mwanga wa kweli, kwa kuongozwa na Neno lake. Bartimayo alikuwa mwombaji kipofu, na Mwinjili anatuambia, alikuwa ameketi kando ya njia. Labda yafaa leo tuangalie na kutafakari maneno hayo na hasa juu ya kuketi. Sio kuketi kwa kawaida bali Mwinjili Marko anajaribu kutuonesha kuwa hakuwa na uwezo wa kuishi maisha yake katika ukamilifu. Hakuwa na uwezo wa kutembea na kujitafutia mkate wake wake wa kila siku, zaidi ya kupewa pia sifa nyingine hasi, alikuwa mwombaji. Dominika mbili mfululizo zilizopita, kule Roma kwanza na baadaye pia majimboni pote ulimwenguni, imezinduliwa rasmi Sinodi ya Maaskofu yenye ujumbe mama; KANISA LA KISINODI-Ushirika/Umoja, Ushiriki na Utume, yaani umisionari ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Kanisa la Kisinodi ni lile linalotembea, ni lile lisilobaki limeketi pembeni mwa njia, bali linalokuwa njiani daima, linalokuwa njia kama Yesu mwenyewe alivyo Njia, Ukweli na Uzima. (Yohane 14:6). Na ndio mwaliko kwa kila mmoja wa kutoka katika ile ya kuketi, hali ya kutokufanya lolote katika maisha yetu, bali tunaalikwa kuililia huruma ya Yesu ili atuponye na kila aina ya upofu, kila aina ya kikwazo kinachotuzuia kupiga hatua katika safari ya mahusiano yetu na Mungu na jirani.
Kanisa la Kisinodi, ndilo Kanisa linaloakisi pia Kanisa lile la mwanzo kabisa, kama anavyotuonesha Mwinjili Marko mara nyingi kuwa Yesu alikuwa njiani, na hakuwa peke yake bali na wanafunzi wake, alisafiri na kutembea nao, alishirikiana nao katika hali zote. Na ndio mwaliko wa Sinodi ya maaskofu juu ya Kanisa la Kisinodi, tunaalikwa kusafiri pamoja kama Kanisa, lakini sio peke yetu bali na Mungu mwenyewe katika Nafsi Tatu. Kanisa la Kristo daima linatanguliwa na kuongozwa na Mungu Roho Mtakatifu, anayebaki nasi katika hali ya kutoonekana kwa macho ya nyama. Bartimayo anafanya maamuzi leo, anatambua uduni na hali yake nyonge, lakini zaidi sana, anatambua sio mahujaji na matajiri wenye pesa, wanaoweza kumuondolea hali ile duni, bali ni Yesu mwana wa Daudi. Bartimayo anaomba rehema, anaomba huruma ya Mungu. Kipofu mwombaji, anatambua hali yake na pia anatambua mahali sahihi pakupata tiba sahihi kwa shida yake. Hivyo, anakuwa ni fundisho kwetu, kila mara kutambua hali zetu na ndani kabisa zinazotukwamisha kuishi maisha kweli ya ufuasi, maisha kweli ya Ukristo wetu, hivyo tiba sahihi daima ni kuikimbilia huruma ya Mungu.
Bartimayo, anasikia habari za Yesu akipita, na hapo anatambua ni kwa Yesu tu anaweza kupokea uponyaji wake. Kipofu huyu mwombaji anashinda vizuizi na vipingamizi vyote, watu wanamkemea ili anyamaze, lakini tunasikia alizidi kupaza sauti yake. Hata nasi katika maisha yetu ya kukua kiroho kuna vikwazo vingi katika kumfikia na kukutana na Yesu, lakini, tunaambiwa leo hatuna budi kujbidisha, hatuna budi kuomba neema ya ujasiri ya kuzidi kupambana ili tutoke katika hali zile duni na mbaya. Watu wanamzuia: Ndio kusema watu wale wanajimilikisha Yesu, wanakuwa kinyume na dhana ya Kanisa la Kisinodi, Kanisa ambalo linatualika sisi sote kutembea pamoja bila kujali hali zetu, bila kumbagua na kumwacha nyuma au pembeni yeyote, bali sote tutembee pamoja na Yesu Kristo. Hivyo, tunazidi kuona tangu mwanzoni Yesu anatutaka wanafunzi wake kuwa na Kanisa la Kisinodi, ndio Kanisa linalojumuisha wote na kuwaunganisha katika ushirika, wakidumu katika kushikiana, ili kwa pamoja tuweze kutoka na kutekeleza misheni yetu kama Wakristo, mashuhuda wa kweli za Injili sio tu kwa maneno bali kwa maisha yetu ya siku kwa siku.
Na ndio Baba Mtakatifu anatuonya pia kila mmoja wetu katika kutembea pamoja kama Kanisa la Kisinodi, tusiwe vikwazo vya kuwafanya wengine washindwe kukutana na Yesu. Kuepuka kishawishi cha kuhodhi Kanisa, kuhodhi matakatifu, kwani kila mmoja wetu kwa nafasi yake ni bawabu, ni mtumishi na mlinzi wa hazina za mbinguni. Ni mwaliko wa kututaka kila mmoja wetu kuwa macho na kishawishi hicho, kishawishi ambacho mara nyingi kinawafanya wengine kuwa au kubaki pembeni mwa njia, na badala yake, tuwe msaada wa kuwaleta wengine kwenye ushirika, tukishirikiana nao katika utume wetu wa kuwa wamisionari katika nyakati na ulimwengu wetu. Si tu watu wale walikuwa enzi zile za Bartimayo, bali hata katika enzi na nyakati zetu. Kipo kishawishi cha kudhani, mimi ni wa muhimu zaidi, mimi ndio kila kitu na kwa kweli tuseme ni kishawishi cha kuchukua nafasi ya Mungu. Wa lazima na bila Yeye hatuwezi kitu ni Mungu pekee, ambaye daima anatualika kutafakari na kukubali kuongozwa naye, kwani ni Yeye anatualika daima tutembee kwa pamoja. “Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, jipe moyo; inuka, anakuita.” Ni maneno ya wale wanaotambua nini maana ya kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, nini maana ya kuwa Mkristo. Ndio wale wanaotambua nini maana ya kutembea kwa pamoja kama Kanisa la Kisinodi. Ni wale wanaokuwa tayari kuguswa na kusikiliza kwa upendo shida na mahangaiko ya wengine iwe katika familia, jumuiya, mahali pakazi na kadhalika na kadhalika.
Si tu wanasikiliza wenye shida bali zaidi sana wanatenga muda wa kuongea na kuwapa faraja na moyo na hata kuwaongoza ili waweze nao kukutana na Yesu. Ni wale wasiohodhi Kristo wala Kanisa lake, bali wanatambua wito wao wa kuwa watumishi wa wengine, wa kuwa msaada wa wengine ili nao waweze kuingia katika Njia na kutembea pamoja na Yesu na Kanisa lake. “Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.” Ndio maneno ya faraja kubwa ambayo kila mmoja wetu angependa kuyasikia kutoka kwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu, ni maneno ambayo mimi na wewe tunaalikwa kuwa baraka kwa wengine, kuwa faraja na kuwakaribisha wengine wanaokuwa mbali ili nao waweze kuingia katika ushirika, ushiriki na misheni ya Kanisa la Kisinodi. Mwinjili Marko anatuonesha kipofu yule mwombaji, Bartimayo anatupa vazi lake na kuruka na kumwendea Yesu. Kwa kweli tunabaki na maswali na mshangao kwani sio namna ya mtu mwenye ulemavu wa upofu, kwani tungetarajia kuona akijivika vema vazi lake na hata kungojea msaada wa watu wenye kuona ili wapate kumuongoza kwa Yesu.
“Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua.” (Kutoka 22:26) Vazi au joho kwa Wayahudi ndio kitu pekee alichomiliki mtu maskini na duni. Bartimayo anatupa vazi lake, anatupa labda na pesa chache alizopewa na mahujaji waliokuwa njiani kuelekea Yerusalemu, ndio kusema Mwinjili Marko anatupa fundisho la Kiteolojia, ni baada ya kutambua na kugundua kilicho na thamani kabisa sio tena vazi lake wala pesa, bali ni kwenda na kuambatana na kutembea pamoja na Yesu Kristo anayepanda kwenda Yerusalemu. Anatupa vazi lake, katika Kanisa la mwanzo, wakatekumeni siku ya Ubatizo wao walivua mavazi yao ya zamani na kuvishwa mavazi mapya, ndio kusema kuachana na maisha ya zamani na kuanza maisha mapya. Na ndio Bartimayo anatualika nasi kutupa vazi lile linalotuweka katika hali duni na mbali na Mungu na Kanisa, kila aina ya kikwazo kinachotutenga na upendo na huruma ya Mungu kwetu. Kutupa yale yote yanayotukwamisha kutembea pamoja kama Kanisa la Kisinodi. Bartimayo kabla alikuwa ameketi ila baada ya kukutana na Yesu anainuka na kutembea. Ndio mwaliko kwetu sisi leo tunaposafiri katika tafakari yetu ya Kanisa la Kisinodi, ni Kanisa linaloalikwa kujitafakari na linapotammbua uduni wake basi hatuna budi kutupa vazi lile na kutoka katika hali zetu za kubweteka na kuridhika na badala yake kuanza kutembea tena, kwani Kanisa daima linaalikwa kutembea kuelekea sio tena Yerusalemu ya duniani bali ile ya mbinguni.
Hii ni safari ambayo inatutaka tutembee kwa pamoja katika umoja wa ushirika, kila mmoja akishiriki kikamilifu, katika utume wa kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Kanisa la Kisinodi linasafiri na kutembea kwa pamoja kwa kupeana moyo na kuhurumiana ili sisi sote tuweze kufika kilele cha safari yetu, ndio Utakatifu, ndio muunganiko na Mungu wa milele yote. Nawatakia Dominika na takakuri njema na maandalizi mema ya Sherehe ya Watakatifu wote.