Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili ya 31 Mwaka B: Amri za Mungu! Upendo!

Furaha ya kweli hupatikana katika kuzishika na kuziishi Amri za Mungu. Hizi tumepewa ili zitusaidie kuishi maisha adilifu na yanayompendeza Mungu na jirani na mafundisho ya Kanisa yanatufafanulia namna ya kuzishika na kuziishi vyema amri za Mungu kwa kuwa anatupenda. Utekelezaji wa amri za Mungu humpatia mtu uhuru, furaha na amani ya kweli, utulivu na msamaha!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika hali ya kibinadamu tunaweza kufikiri kuwa amri 10 za Mungu, amri za Kanisa pamoja na maagizo na mafundisho yake yasingalikuwepo maisha yangekuwa mazuri na ya kupendeza zaidi. Ukweli ni kwamba furaha ya kweli hupatikana katika kuzishika na kuziishi Amri za Mungu. Hizi tumepewa ili zitusaidie kuishi maisha adilifu na yanayompendeza Mungu na jirani na mafundisho ya Kanisa yanatufafanulia namna ya kuzishika na kuziishi vyema amri na maagizo ya Mungu kwa kuzisuta dhamiri zetu. Huu ndio ujumbe wa masomo ya dominika hii kuwa Mungu ametupa amri zake kwa kuwa anatupenda. Masomo haya yanatukumbusha kuwa utekelezaji wa amri 10 za Mungu humpatia mtu uhuru, furaha na amani ya kweli, utulivu na mshikamano. Tunapokengeuka na kutokuzishika amri hizi, tunakosa amani na furaha, tunakuwa watumwa wa maisha yetu na hisia zetu.

Somo la kwanza la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (6:2-6). Hiki ni kitabu cha mwisho kati ya vitabu 5 vya Sheria/Torati ya Musa, ambavyo Wayahudi wanaviheshimu kama vitabu vitakatifu sana vya maandiko matakatifu, kwa kuwa vinabeba maagizo ya Mungu hasa amri 10 ambazo ndizo mwongozo wa maisha yao, limebeba mausia ya Musa kwa Waisraeli namna wanavyopaswa kumcha Mungu na kuzishika Amri zake siku zote za maisha yao.  Katika kuzishika amri za Mungu kuna ahadi zinazoambata nazo; kuwa na siku nyingi duniani, maisha marefu na yenye heri, usitawi katika familia, pamoja na kuwa na watoto na vitukuu vingi. Mapokeo yanasimulia kuwa Waisraeli katika kuhakikisha wanazishika vyema amri za Mungu, walizigeuza kuwa sala inayoitwa “shema Israeli au sikiliza ee Israeli, ambayo kila mtoto myahudi alipoanza kujifunza kuongea aliifundishwa na kuisali mara mbili kwa siku. Sala hii inasema; “Sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena uyaandike katika miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kumb 6:4-9).

Kumbe, kutokana na maagizo haya, waisraeli waliindika sala hii “sikiliza ee Israeli” kwenye vitambaa wakayatengenezea vishada mfano wa “skapulari” au “hirizi” kama ishara ya sala iletayo usalama na kuviweka kwenye vikasha vidogo na kuvivaa mbele ya uso wao ili kuwakumbusha kila wakati wajibu wao kwa Mungu. Kadiri ya kitabu cha Hesabu (15:37-39), wanaume wa Kiyahudi ili kuzikumbuka amri za Mungu walivivaa vishada vyenye amri hizi katika ncha za nguo zao. Bila shaka Yesu kama Myahudi alizivaa na ndiyo maana yule mwanamke aliyetokwa na damu kwa muda mrefu alitamani kugusa pindo la nguo ya Yesu ili apate kupona (Lk 8:44, Mt 9:20-21. Mk 5:28). Wapo waliofanya hivyo kinafiki ndiyo maana Yesu aliwakemea Mafarisayo kwa kupanua hirizi zao na kuongeza matamvua yao kama ishara ya uaminifu wao kwa amri za Mungu (Mt 23:5). Kumbe somo hili inatukumbusha kuwa kuzishika amri za Mungu ni kuzuri kwani ndio msingi wa kuishi kwa furaha na amani.

Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (7:23-28); ni ufafanuzi uliopo kati ya ukuhani wa Agano la Kale na wa Agano jipya kuwa; Makuhani wa Agano la Kale walikuwa wengi na walikufa, na ukuhani wao ukaisha. Lakini makuhani wa Agano Jipya wanaoshirikishwa ukuhani wa Yesu aliye Kuhani mkuu, ukuhani wao ni wa milele. Kama ukuhani wa Yesu ulivyo naye anatuombea daima kwa Mungu kama tunavyosoma; “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliye kamili hata milele.” Kumbe, basi somo hili linatukumbusha kuwa Kristo ndiye kuhani wetu Mkuu na wa milele na mapadre wanashirikishwa ukuhani huu wa Kristo ili kupitia kwao tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na sadaka ya Yesu Msalabani kila inapoadhimishwa sadaka ya Misa Takatifu.

Injili kama ilivyoandikwa na Marko (12:28-34); ni mafundisho ya Yesu juu ya amri iliyo kuu kuliko zote: Amri kuu ya mapendo. Amri hii ndiyo msingi wa maisha ya mwanadamu hapa duniani kwa ajili ya uzima wa milele. Kipimo cha maisha ya kikristo ni kumpende jirani kama unavyojipenda mwenyewe kwa nguvu ile ile kama kumpenda Mungu. “Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Amri zote mbili zinakwenda pamoja, ili kwamba mmoja asipompenda jirani hampendi Mungu kwani twampenda Mungu kwa kumpenda jirani. Kuzishika na kuziishi amari hizi “kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa karibu na ufalme wa Mungu. Kipindi Yesu alinazaliwa Viongozi wa Dini ya Kiyahudi walifanya amri za Mungu kuwa ngumu kuiishi kwani walizinyambulisha na kuzifanya kuwa 613. Kwa watu wa kawaida ilikuwa ni mzigo usiobebeka. Hivyo, kulikuwepo malumbano yasiyoisha juu ya kufahamu ni amri ipi ilikuwa kuu na muhimu. Ndiyo maana mmojawapo wa waandishi anamuuliza Yesu; “Mwalimu ni amri ipi iliyo kuu na ya kwanza?” Yesu alijibu swali hili kwa kunukuu aya mbili za Maandiko Matakatifu. Kwanza ni; “Sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote (Kumb 6:4-5).

Na pili ni; “Umpende jirani yako kama nafsi yako. Mimi ndimi Bwana, “(Wal 19:18). Yesu anaziweka Amri hizi mbili kuwa na usawa au ukuu uleule. Ndiyo kusema upendo kwa jirani ni maelezo yetu ya upendo kwa Mungu. Hii ndiyo amri mpya kama alivyosema Yesu; “Amri mpya nawapa mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (Yn 13:34). Tukumbuke kuwa kumpenda jirani ni kutambua kuwa sisi sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na tumekombolewa sote kwa damu ya Kristo msalabani kutoka utumwa wa dhambi na mauti ili tuurithi ufalme wa mbinguni. Hivyo tunapaswa kuwajali wote katika mahitaji ya kiroho na kimwili, kwa namna ya pekee, yatima, wafungwa na wakimbizi, wagonjwa na maskini. Kumbe basi kuwasaidia wenzetu walio katika shida mbalimbali, kufurahi na wenye kufurahi na kusikitika na wenye kusikitika na kuwasamehe wanapotukosea, ni wajibu tunaojitwika tunaposali sala ya “Baba yetu” ndiko kumpenda Mungu na jirani na kuwa karibu na ufalme wa Mungu. Na kufanya hivyo ndio kuuishi ukristo wetu na tunapata mastahili ya kuurithi uzima wa milele.

Tafakari J31
28 October 2021, 16:17