Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Muhtasari wa Amri Kuu za Mungu ni upendo kwa Mungu na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Muhtasari wa Amri Kuu za Mungu ni upendo kwa Mungu na jirani! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili 31 Mwaka B: Amri Kuu Ni Upendo!

Ningependa kugusia kidogo tu kuhusu ushirika wa watakatifu, lakini nitazama zaidi kwenye Amri za Mungu ambazo Kristo Yesu amezifupisha kwa kukazia upendo kwa Mungu na jirani. Mama Kanisa anaungama Ushirika wa Watakatifu. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu ambayo kimsingi ni hazina ya pamoja. Ni ushirika katika imani, Sakramenti za Kanisa, karama na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 31 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Kutokana na sababu za kichungaji, ili kuweza kuwashirikisha waamini wengi katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote, baadhi ya majimbo yanasherehekea Dominika tarehe 31 Oktoba 2021. Katika tafakari hii, ningependa kugusia kidogo tu kuhusu ushirika wa watakatifu, lakini nitazama zaidi kwenye Amri za Mungu ambazo Kristo Yesu amezifupisha kwa kukazia upendo kwa Mungu na jirani. Mama Kanisa anaungama Ushirika wa Watakatifu. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu ambayo kimsingi ni hazina ya pamoja. Ni ushirika katika imani, Sakramenti za Kanisa, karama na mapendo. Upendo hautafuti mambo yake binafsi. Mababa wa Kanisa wanasema, lililo dogo kati ya matendo yetu, ambalo limefanywa katika upendo, huleta faida kwa wote katika mshikamano huu na watu wote walio hai au waliokufa, ambao una msingi wake katika ushirika wa watakatifu. Kila dhambi huudhuru ushirika huo!

Wakristo wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwani huu ni mwaliko na wito kwa wote na wala si kwa kundi la watu wachache ndani ya Kanisa. Changamoto hii imetiliwa mkazo kwa namna ya pekee kabisa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa. Lengo ni kuyatakatifuza malimwengu.  Mtakatifu Paulo Mtume anapoawaandikia Wakorintho: 1 Kor. 1: 1-2 anawakumbusha kwamba wao wametakatifuzwa kwa njia ya Yesu Kristo, katika: maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanafanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, wakiwa na haki na wajibu unaoambatana na wito huu. Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wanauvua utu wa kale uliochakaa kwa njia ya dhambi na kuanza kujivika utu mpya ili kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Amri 10 za Mungu zinazowezwa kufupishwa kwa kukazia upendo kwa Mungu na jirani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, hali inayomtuma kuanzisha Agano na binadamu, kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu mwenyewe, changamoto kwa waamini kuonesha imani yao kwa Mwenyezi Mungu. Mtume Paulo anatukumbusha akisema “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.” Rum 13:8-10. Kristo Yesu anatoa mkazo wa pekee kwa upendo kwa Mungu na jirani, ili kuwaachia wengine nafasi ya kuonja upendo huu, kama kielelezo makini cha utimilifu wa Sheria ulioletwa na Kristo Yesu! Rej. KKK 2196. Sheria mpya ni neema ya Roho Mtakatifu inayotimiza Ahadi, Amri na Sheria! Hii ndiyo Sheria ya mapendo. Mababa wa Kanisa wanakaza kusema, kwa hiyo, upendo kwa Mungu na kwa jirani ndio muhuri aliotiwa kila mfuasi wa kweli wa Kristo Yesu. Tena utakatifu wa Kanisa hutukuzwa kwa namna ya pekee kwa njia ya mashauri ya aina nyingi ambayo Kristo Yesu amewapatia wafuasi wake katika Injili ili wayashike! Rej. LG 42.

Ni katika muktadha huu, Amri za Mungu zinakuwa ni ukweli mfunuliwa unaokita mizizi yake katika maisha ya mwamini yanayofumbatwa katika upendo, hamu ya kutenda mema, kiu ya kufurahia maisha; hamu ya kupata amani, wema, uzuri, unyenyekevu pamoja na kuwa na kiasi katika maisha! Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu katika mchakato wa kujenga na kuimarisha jamii inayosimikwa kwenye msingi wa: haki, usawa na mapendo; jamii inayotamani kushibishwa kwa ukweli, utu na maadili mema. Kuna mmong'onyoko mkubwa wa kimaadili na kiutu unaotokana na ukanimungu na tabia ya binadamu ya kutaka kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake. Amri 10 za Mungu ni mwongozo makini unaowaelekeza wale wanaotafuta amani, haki, utu na heshima ya binadamu. Hii ni njia ya uhuru wa kweli unaomwongoza mwanadamu kuchagua jambo jema na kulikumbatia na sheria ya Mungu ambayo imeandikwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Ni changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kama ilivyokuwa wakati wa Waisraeli pale Mlimani Sinai kuonesha uaminifu kwa Mungu anayewajalia uhuru wa kweli.

Amri za Mungu zinamwonesha mwanadamu uhuru wa kweli kwa kuondokana na utumwa unaowafunga watu wengi katika uchoyo na ubinafsi wao kwa kuwachangamotisha kuishi kwa kuwaheshimu wengine ili kushinda kishawishi cha kupenda mali, madaraka na sifa ucharwa! Watu wajifunze kuwa wakweli, waaminifu na waadlifu; wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Amri 10 za Mungu ni changamoto kwa binadamu kuwa mwaminifu kwake yeye mwenyewe huku akitembea katika heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu. Amri hizi ni sheria ya upendo inayojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho na mwaliko wa kumpenda Mungu na jirani kama unavyojipenda mwenyewe, ufafanuzi makini uliotolewa na Kristo Yesu, kwa kuonesha mambo msingi ambayo mwanadamu anapaswa kuyapatia kipaumbele cha pekee katika maisha yake! Amri hizi ni kielelezo cha utambulisho na mafungamano na Mwenyezi Mungu na jirani yake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, moyo wa shukrani ni msingi wa imani na utii kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemkirimia mwanadamu yote na kwamba, anamtaka kumwabudu Muumba wake peke yake badala ya kuabudu “miungu wa kuchongwa”. Hawa ni miungu wanaomtumbukiza mwamini katika utumwa badala ya kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, aliyewawezesha kuwa waana wa Baba wa milele! Huu ni mchakato wa baraka na ukombozi; kwani mwamini anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwamba na wokovu wake, hatatikisika kamwe. Tafakari ya maisha katika mwanga wa Amri za Mungu inamwonesha mwamini kuwa ni mtu wa shukrani, huru, mkweli, anayebariki, mkomavu, mlinzi na mtunza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mwaminifu, mkarimu mambo ambayo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake ya kila siku na hivyo kujiona kuwa mbele ya Kristo Yesu, kila siku ya maisha! Ninakutakia maadhimisho mema ya Dominika ya Bwana na maandalizi mema ya Sherehe ya Watakatifu wote.

Liturujia J31
29 October 2021, 15:47